2010–2019
Kusimamia Ahadi na Maagano Yetu
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


Kusimamia Ahadi na Maagano Yetu

Ninawaalika mfikirie kuhusu ahadi na maagano mnayofanya na Bwana, pamoja na wengine, kwa uadilifu mkubwa, mkijua ya kwamba neno lako ni kifungo chako.

Wapendwa akina kaka na akina dada, tunapohitimisha kikao hiki, kila mmoja wetu na aweke moyoni mwake ushahidi uliotolewa leo juu ya kweli za injili ya Yesu Kristo. Tumebarikiwa kuwa na wakati huu mtakatifu pamoja ili kuimarisha ahadi yetu kwa Bwana Yesu Kristo kwamba sisi ni watumishi Wake na Yeye ni Mwokozi Wetu.

Umuhimu wa kufanya na kutunza ahadi na maagano unanielemea akilini mwangu. Ni muhimu kiasi gani kwako kutimiza ahadi yako? kuaminiwa? kutenda kile ulichosema utatenda? Kujitahidi kuheshimu maagano yako matakatifu? kuwa muadilifu? Kwa kuwa wakweli kwenye ahadi zetu kwa Bwana na kwa wengine, tunatembea katika njia ya agano kurudi kwa Baba yetu wa Mbinguni na tunahisi upendo Wake katika maisha yetu.

Mwokozi wetu, Yesu Kristo, ni mfano wetu mkuu wakati linapokuja suala la kufanya na kushika ahadi na maagano. Alikuja duniani akiahidi kufanya mapenzi ya Baba. Alifundisha kanuni za injili kwa maneno na kwa matendo. Alilipia dhambi zetu ili tuweze kuishi tena. Ametimiza kila moja ya ahadi Zake.

Je, hilo linaweza kusemwa kwa kila mmoja wetu? Hatari ni zipi ikiwa tutadanganya kidogo, kuteleza kidogo, au kutofuatilia misimamo yetu? Vipi ikiwa tutaacha maagano yetu? Je, wengine watakuja kwa Kristo kutokana na nuru ya mfano wetu? Je, neno lako ndiyo kifungo chako? Kutimiza ahadi si mazoea; ni sifa ya kuwa mfuasi wa Yesu Kristo.

Daima akijali kuhusu udhaifu wetu katika maisha ya duniani, Bwana aliahidi, “Changamkeni, na msiogope, kwani Mimi Bwana nipo pamoja nanyi, na nitasimama karibu yenu.”1 Nimehisi uwepo Wake wakati nilipohitaji kuondolewa shaka, faraja, au nguvu kubwa zaidi ya kiroho au uvuvio, na nimenyenyekezwa na ninashukuru kwa ajili ya wenza Wake mtakatifu.

Bwana amesema, “Kila mtu atakayeziacha dhambi zake na kuja kwangu, na kulilingana jina langu, na kuitii sauti yangu, na kushika amri zangu, atauona uso wangu na kujua kuwa Mimi ndiye.”2 Hiyo ndiyo pengine ahadi Yake kuu.

Nilijifunza umuhimu wa kutimiza ahadi zangu katika ujana wangu. Mfano mmoja kama huu ni wakati niliposimama wima kukariri Kiapo cha Maskauti. Uhusiano wetu na Maskauti Wavulana wa Marekani, wakati sasa unapokaribia mwisho, daima utakuwa urithi muhimu kwangu na kwa Kanisa hili. Kwa chama cha Maskauti, kwa wanaume na wanawake wengi ambao wametumikia kwa bidii kama viongozi wa Maskauti, kwa akina mama—sifa halisi ziwaendee wao—na kwa wavulana ambao wameshiriki katika Uskauti, tunasema, “Asanteni.”

Katika kikao hiki, nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, na Mzee Quentin L. Cook wametangaza mabadiliko ambayo yatafokasi upya umakini wetu kwa vijana na kufungamanisha taasisi zetu na ukweli uliofunuliwa. Kwa kuongezea, Jumapili iliyopita, Rais Nelson na Rais M. Russell Ballard walifafanua programu mpya ya Watoto na Vijana wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa ajili ya Kanisa zima. Ni juhudi ya ulimwenguni kote ambayo imefokasi kwa Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili wameungana katika mwelekeo huu mpya, na mimi binafsi ninashuhudia kwamba Bwana ametuongoza katika kila hatua. Ninafurahi kwa ajili ya watoto na vijana wa Kanisa kupata uzoefu wa fokasi hii iliyofungamanishwa kwao kote nyumbani na kanisani—kupitia kujifunza injili, huduma na shughuli, na maendeleo binafsi.

Dhamira ya vijana kwa mwaka ujao, 2020, inazungumzia ahadi ya juu ya Nefi ya “kwenda na kutenda.” Aliandika, “Na ikawa kuwa mimi, Nefi, nilimwambia baba yangu: Nitaenda na kutenda vitu ambavyo Bwana ameamuru, kwani ninajua kwamba Bwana hatoi amri kwa watoto wa watu, isipokuwa awatayarishie njia ya kutimiza kitu ambacho amewaamuru.”3 Ingawa ilitamkwa kitambo sana, sisi tulio Kanisani tunasimamia ahadi hiyo leo.

“Kwenda na kutenda” inamaanisha kuinuka juu ya njia za dunia, kupokea na kufanyia kazi ufunuo binafsi, kuishi kwa haki ukiwa na tumaini na imani katika siku zijazo, kufanya na kushika maagano ya kumfuata Yesu Kristo, na hivyo basi kuongeza upendo wetu Kwake, Mwokozi wa ulimwengu.

Agano ni ahadi ya pande mbili baina yetu na Mungu. Kama waumini wa Kanisa, tunafanya agano wakati tunapobatizwa kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo, kuishi jinsi alivyoishi. Kama wale waliobatizwa katika maji ya Mormoni, tunaahidi kuwa watu Wake, “kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine, ili iwe miepesi; … kuomboleza na wale wanaoomboleza; … kuwafariji wale ambao wanahitaji kufarijiwa, na kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote.”4 Kuhudumiana kwetu Kanisani kunaakisi msimamo wetu wa kuheshimu ahadi hizo.

Tunaposhiriki sakramenti, tunafanya upya agano hilo la kujichukulia juu yetu jina Lake na kufanya ahadi za nyongeza za kuwa bora zaidi. Mawazo na matendo yetu ya kila siku, yote makubwa na madogo, yanaakisi msimamo wetu Kwake. Ahadi Yake takatifu kwetu ni, “Na ikiwa mtanikumbuka daima Roho wangu atakuwa pamoja na nyinyi.”5

Swali langu leo ni je, tunasimamia ahadi na maagano yetu, au wakati mwingine ni misimamo isiyo kamili, iliyowekwa kikawaida na hivyo kuvunjwa kwa urahisi? Tunaposema kwa mtu fulani, “Nitakuombea,” tunafanya hivyo? Tunapoweka msimamo, “Nitakuwepo kukusaidia,” tutakuwepo? Tunapojipa wajibu wa kulipa deni, tunafanya hivyo? Tunapoinua mikono yetu kuwaidhinisha waumini wenzetu katika wito mpya, ikimaanisha kutoa msaada, tunafanya hivyo?

Jioni moja katika ujana wangu, mama yangu aliketi pamoja nami kwenye kitanda chake na kuzungumza kwa unyenyekevu kuhusu umuhimu wa kuishi Neno la Hekima. “Ninajua kutokana na uzoefu wa wengine, miaka mingi iliyopita,” alisema, “upotevu wa mambo ya kiroho na wepesi wa kuhisi ambao huja kwa kutofuata Neno la Hekima.” Aliniangalia moja kwa moja machoni mwangu, na nilihisi maneno yake yakipenya moyoni mwangu: “Niahidi, Ronnie, leo [aliniita Ronnie], kwamba daima utaishi Neno la Hekima.” Kwa dhati nilifanya ahadi hiyo kwake, na nimeishikilia kwa miaka hii yote.

Msimamo huo umenisaidia sana wakati nilipokuwa katika ujana wangu na katika miaka ya baadaye wakati nilipokuwa miongoni mwa wafanyabiashara ambapo vileo vilikuwa kwa wingi. Nilifanya uamuzi mapema wa kufuata sheria za Mungu, na kamwe sikuhitaji kufikiria upya juu ya hilo. Bwana amesema, “Mimi, Bwana, ninafungwa wakati ninyi mnapofanya ninayosema; lakini msipofanya ninayosema, ninyi hamna ahadi.”6 Anasema nini kwa wale ambao wanaishi kwa kutii Neno la Hekima? Kwamba tutapata ahadi ya afya, nguvu, hekima, ufahamu, na malaika wa kutulinda.7

Miaka kadhaa iliyopita, mimi na Dada Rasband tulikuwa katika Hekalu la Salt Lake kwa ajili ya kuunganishwa kwa mmoja wa mabinti zetu. Tulipokuwa tumesimama nje ya hekalu na binti mdogo ambaye hakuwa amefikia umri wa kuhudhuria ibada, tulizungumzia umuhimu wa kuunganishwa katika hekalu takatifu la Mungu. Kama vile mama yangu alivyokuwa amenifundisha miaka mingi awali, tulimwambia binti yetu, “Tunakutaka kwa usalama uunganishwe hekaluni, na tunataka utuahidi ya kwamba wakati utakapompata mwenza wako wa milele, utafanya miadi naye ya kuunganishwa hekaluni.” Alitupatia ahadi yake.

Picha
Binti wa Mzee Rasband pamoja na mumewe

Tangu hapo ametueleza kwamba mazungumzo yetu na ahadi yake vimemlinda na kumkumbusha “kile kilicho muhimu zaidi.” Baadaye alifanya maagano matakatifu wakati alipounganishwa na mume wake hekaluni.

Rais Nelson amefundisha: “Sisi … tunaongeza nguvu za Mwokozi katika maisha yetu wakati tunapofanya maagano matakatifu na kuyashika maagano hayo kwa usahihi. Maagano yetu yanatuunganisha na Yeye na kutupatia nguvu za kiungu.”8

Wakati tunapotunza ahadi tulizoahidiana, tunakuwa na uwezo mkubwa wa kushika ahadi zetu kwa Bwana. Kumbuka maneno ya Bwana: “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.”9

Tafakari pamoja na mimi kuhusu mifano ya ahadi katika maandiko matakatifu. Amoni na wana wa Mosia katika Kitabu cha Mormoni waliazimia “kuhubiri neno la Mungu.”10 Wakati Amoni alipokamatwa na majeshi ya Walamani, alipelekwa kwa Lamoni Mfalme wa Walamani. Yeye alimuahidi mfalme, “Nitakuwa mtumishi wako.”11 Wakati wavamizi walipokuja kuiba kondoo wa mfalme, Amoni alikata mikono yao. Mfalme alishangazwa sana, alisikiliza ujumbe wa Amoni wa injili na aliongoka.

Ruthu, katika Agano la Kale, alimuahidi mama mkwe wake, “Wewe uendako, nitakwenda.”12 Alitimiza ahadi yake. Msamaria mwema, katika fumbo la Agano Jipya, alimuahidi mwenye nyumba kuwa ikiwa angemtunza msafiri aliyejeruhiwa, “Chochote utakachogharimia zaidi, mimi nitakaporudi, nitakulipa.”13 Zoramu, katika Kitabu cha Mormoni, aliahidi kwenda nyikani pamoja na Nefi na kaka zake. Nefi alielezea, “Wakati Zoramu alitupatia kiapo, hofu yetu kumhusu ikakoma.”14

Na kuhusu ile ahadi ya kale “iliyofanywa kwa mababa” kama ilivyoelezwa katika maandiko kwamba “mioyo ya watoto itawageukia baba zao”?15 Katika maisha yetu kabla ya kuja duniani wakati tulipochagua mpango wa Mungu, tuliahidi kusaidia katika kukusanya Israeli pande zote mbili za pazia. “Tuliingia katika ubia na Bwana,” Mzee John A. Widtsoe alieleza miaka mingi iliyopita. “Kufanyia kazi mpango kukawa wakati huo si tu kazi ya Baba, na kazi ya Mwokozi, bali pia kazi yetu.”16

“Kukusanyika ni kitu cha muhimu zaidi kinachofanyika duniani leo,” Rais Nelson amesema wakati akisafiri kote ulimwenguni. “Tunapozungumza kuhusu kukusanya, kiurahisi tunasema kanuni hii ya kweli: Kila mmoja wa watoto wa Baba yetu wa Mbinguni, katika pande zote za pazia, anastahili kusikia ujumbe wa injili ya urejesho ya Yesu Kristo.”17

Kama mtume wa Bwana Yesu Kristo, ninahitimisha kwa mwaliko na ahadi. Kwanza, mwaliko: Ninawaalika mfikirie kuhusu ahadi na maagano mnayofanya na Bwana, pamoja na wengine, kwa uadilifu mkubwa, mkijua ya kwamba neno lako ni kifungo chako. Pili, ninawaahidi, mnapofanya hili, Bwana atathibitisha maneno yenu na kuruhusu matendo yenu mnapojitahidi kwa bidii isiyotikisika kujenga maisha yenu, familia zenu, na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Atakuwa pamoja nanyi, kaka zangu na dada zangu wapendwa, na mnaweza, kwa kujiamini, kutazamia “kupokelewa mbinguni, ili hapo [ninyi] mpate kukaa na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho … kwani Bwana Mungu ameyazungumza hayo.”18

Juu ya haya ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha