Kwenye Mawingu na Jua, Bwana, Kaa Nami!
Ninashuhudia kwamba “kwenye mawingu na jua” Bwana atakaa nasi, kwamba “mateso yetu [yanaweza] kumezwa kwenye shangwe ya Kristo.”
Mojawapo ya nyimbo zetu pendwa unaelezea ombi “Kwenye Mawingu na Jua, Bwana, Kaa Nami!”1 Niliwahi kuwa ndani ya ndege pale ilipokaribia dhoruba kali. Kwa kutazama dirishani, ningeweza kuona moshi mzito wa mawingu chini yetu. Miale ya jua likichwea iliakisi nje ya mawingu, yakiisababisha kuangaza kwa mng’aro mkali. Punde, ndege ilishuka kupita mawingu mazito, na ghafla tulifunikwa katika giza nene ambalo lilituziba kabisa kwenye nuru kuu tuliyoshuhudia dakika chache kabla.2
Mawingu meusi yanaweza pia kujitengeneza katika maisha yetu, ambayo yanaweza kutuziba kwenye nuru ya Mungu na hata kutusababisha kujiuliza ikiwa nuru ile bado ipo kwetu. Baadhi ya mawingu hayo ni ya msongo, wasiwasi, na aina zingine za mateso ya hisia na akili. Yanaweza kuharibu jinsi tunavyojifikiria sisi, wengine, na hata Mungu. Yanaathiri wanawake na wanaume wa umri wote katika kila kona ya ulimwengu.
Kadhalika lenye madhara ni wingu lisilo na hisia la kushuku ambalo linaweza kuwaathiri wengine ambao hawajapata uzoefu wa changamoto hizi. Kama vile sehemu yoyote ya mwili, ubongo unaathiriwa na magonjwa, kiwewe na kukosa usawa wa kikemikali. Wakati akili zetu zinapoteseka, ni sahihi kutafuta msaada kutoka kwa Mungu, kutoka kwa wale wanaotuzunguka, na kutoka kwa wataalamu wa afya ya tiba ya akili.
“Wanadamu wote—wanaume na wanawake—wameumbwa katika mfano wa Mungu. Kila mmoja ni mwana au binti mpendwa wa kiroho wa wazazi wa mbinguni, na, … kila mmoja ana asili takatifu na takdiri.”3 Kama Wazazi wetu wa Mbinguni na Mwokozi wetu, tuna mwili4 na tunapata mhemko.5
Dada zangu wapendwa, ni kawaida kuhisi huzuni au woga mara moja moja. Huzuni na wasiwasi, ni hisia za asili za mwanadamu.6 Hata hivyo, ikiwa daima tuna huzuni na ikiwa maumivu yetu yanazuia uwezo wa kuhisi upendo wa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye na ushawishi wa Roho Mtakatifu, basi tunaweza kuwa tunaugua msongo, wasiwasi, au hali nyingine ya hisia.
Binti yangu wakati mmoja aliandika: “Kuna kipindi … [wakati] nilipokuwa na huzuni nyingi muda wote. Daima nilidhani kwamba huzuni ilikuwa jambo la kuonea aibu, na kwamba ilikuwa ishara ya udhaifu. Hivyo nilitunza huzuni yangu mimi mwenyewe. … Nilijihisi nisiye na thamani kabisa.”7
Rafiki alilielezea kwa njia hii: “Tangu utoto wangu, nimekuwa nikipambana na vita isiyoisha na hisia za kukosa tumaini, giza, upweke, na hofu na hisia kwamba nimevunjika au nina mapungufu. Nilifanya kila kitu kuficha maumivu yangu na kamwe kutotoa msukumo kwamba nilikuwa chochote bali mwenye kufanikiwa na imara.”8
Rafiki zangu wapendwa, inaweza kutokea kwa yeyote kati yetu—hasa wakati, kama waaminio katika mpango wa furaha, tunajiwekea mizigo isiyo ya lazima kwa kudhani tunapaswa kuwa wakamilifu sasa. Mawazo kama hayo yanaweza kuwa ya kuchosha. Kufikia ukamilifu ni mchakato ambao utatokea kote katika maisha yetu ya duniani na ya baadaye—na kupitia tu neema ya Yesu Kristo.9
Kinyume chake, tunapozungumza kuhusu changamoto zetu za hisia, tukikubali hatuko wakamilifu, tunawapa wengine nafasi ya kushiriki mahangaiko yao. Kwa pamoja tunatambua kuna tumaini na hatuhitaji kuteseka peke yetu.10
Kama wafuasi wa Yesu Kristo, tumefanya agano na Mungu kwamba “tuko tayari kuchukuliana mizigo” na “kuomboleza na wale wanaoomboleza.”11 Hii inaweza kujumuisha kuwa na taarifa kuhusu ugonjwa wa hisia, kutafuta nyenzo zinazoweza kusaidia kukabili mahangaiko haya, na hatimaye kujileta sisi na wengine kwa Kristo, ambaye ni Mponyaji Mkuu.12 Hata kama hatujui jinsi ya kujihusisha na kile wengine wanachopitia, kuthibitisha kwamba maumivu yao ni halisi kunaweza kuwa hatua muhimu ya kwanza katika kupata uelewa na uponyaji.13
Kwa baadhi ya hali, chanzo cha msongo au wasiwasi kinaweza kutambulika, wakati nyakati zingine inaweza kuwa vigumu kutambua.14 Bongo zetu zinaweza kuteseka kwa sababu ya mfadhaiko15 au uchovu wa kuduwaza,16 ambao wakati mwingine unaweza kuboreshwa kupitia marekebisho kwenye mlo, usingizi, na mazoezi. Mara zingine, matibabu au dawa chini ya uelekezi wa mtaalamu mwenye ujuzi vinaweza pia kuhitajika.
Madhara ya ugonjwa wa akili na hisia ambayo hayakushughulikiwa yanaweza kupelekea kwenye ongezeko la kujitenga, kutokuelewana, mahusiano kuvunjika, kujidhuru, na hata kujiua. Ninalijua hili vizuri, kwani baba yangu mwenyewe alikufa kwa kujiua miaka mingi iliyopita. Kifo chake kilikuwa cha kushtusha na cha kuvunja moyo kwangu na kwa familia yangu. Imenichukua miaka kupambana kushinda huzuni yangu, na ilikuwa hivi karibuni nilipojifunza kwamba kuzungumzia kujiua katika njia sahihi husaidia hasa kuzuia kuliko kuhimiza.17 Sasa kwa wazi nimejadili na watoto wangu kuhusu kifo cha baba yangu na kushuhudia uponyaji ambao Mwokozi anaweza kutoa kwenye pande zote za pazia.18
Kwa huzuni, wengi wanaoteseka kutokana na msongo mkali hujiweka mbali na Watakatifu wenzao kwa sababu wanahisi hawaendani na baadhi ya tabia za kufikirika. Tunaweza kuwasaidia kujua na kuhisi kwamba wao hakika wako pamoja nasi. Ni muhimu kutambua kwamba msongo si matokeo ya udhaifu, wala si daima matokeo ya dhambi.19 “Unasitawi katika siri lakini unasinyaa katika huruma.”20 Kwa pamoja, tunaweza kuvunja mawingu ya kutenga na kunyanyapaa ili mzigo wa aibu uinuliwe na miujiza ya uponyaji iweze kutokea.
Wakati wa huduma Yake duniani, Yesu Kristo aliponya wagonjwa na walioteseka, lakini kila mtu alipaswa kuonesha imani Kwake na kutenda ili kupokea uponyaji Wake. Baadhi walitembea umbali mrefu, wengine walinyoosha mikono yao kugusa vazi Lake, na wengine ilibidi wapelekwe Kwake ili waweze kuponywa.21 Linapokuja suala la uponyaji, je sote hatumuhitaji Yeye kwa kiasi kikubwa? “Si sisi wote ni waombaji?”22
Acha tufuate njia ya Mwokozi na kuzidisha huruma yetu, kupunguza tabia yetu ya kuhukumu, na kuacha kuwa wakaguzi wa hali ya kiroho ya wengine. Kusikiliza kwa upendo ni mojawapo ya karama kuu tunazoweza kutoa, na tunaweza kusaidia kubeba au kuinua mawingu mazito ambayo yanawasonga wapendwa wetu na marafiki23 ili kwamba, kupitia upendo wetu, wanaweza kwa mara nyingine kumhisi Roho Mtakatifu na kupokea nuru itokayo kwa Yesu Kristo.
Ikiwa daima umezungukwa na “ukungu wa giza,”24 mgeukie Baba wa Mbinguni. Hakuna ambacho umepitia kinaweza kubadili ukweli wa milele kwamba wewe ni mtoto Wake na kwamba Anakupenda.25 Kumbuka kwamba Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wako, na Mungu ni Baba yako. Wanaelewa. Pata taswira Yao karibu yako, wakisikiliza na kutoa msaada.26 “[Wao] watakufariji katika magumu yako.”27 Fanya kila uwezalo na amini katika upatanisho wa neema ya Bwana.
Mapambano yako hayakutambulishi, bali yanaweza kukuadilisha wewe.28 Kwa sababu ya “mwiba katika mwili,”29 unaweza kuwa na uwezo wa kuhisi huruma zaidi kwa wengine. Kadiri utakavyoongozwa na Roho Mtakatifu, shiriki hadithi yako ili uweze “kuwasaidia wadhaifu, kuinyoosha mikono iliyolegea, na kuimarisha magoti yaliyo dhaifu.”30
Kwa wale kati yetu wanaohangaika sasa au kumsaidia mtu anayehangaika, acha tuwe tayari kufuata amri za Mungu ili tuweze daima kuwa na Roho Wake pamoja nasi.31 Acha tufanye “vitu vidogo na rahisi”32 ambavyo vitatupatia nguvu ya kiroho. Kama Rais Russel M. Nelson alivyosema: “Hakuna kinachofungua mbingu kama vile muungano wa usafi uliozidishwa, utii kamili, kutafuta kwa bidii, kufurahia kila siku maneno ya Kristo katika Kitabu cha Mormoni, na muda uliopangwa kwa kazi ya hekaluni na historia ya familia.”33
Acha sote tukumbuke kwamba Mwokozi wetu, Yesu Kristo, “[amejichukulia] juu yake unyonge [wetu], ili moyo wake ujae rehema, kulingana na mwili, ili ajue … jinsi ya kutusaidia [sisi] kulingana na unyonge [wetu].”34 Alikuja “kuwaganga waliovunjika moyo, … kuwafariji wote waliao; … kuwapa taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito.”35
Ninashuhudia kwenu kwamba “kwenye mawingu na jua” Bwana atakaa nasi, “mateso yetu [yanaweza] kumezwa kwenye shangwe ya Kristo,”36 na “ni kwa neema kwamba tunaokolewa, baada ya kutenda yote tunayoweza.”37 Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo atarudi duniani “na uponyaji katika mabawa yake.”38 Hatimaye, Yeye “atafuta kila chozi katika macho [yetu]; na hakutakuwepo huzuni … tena.”39 Kwani wote “watakaokuja kwa Kristo, na kukamilishwa ndani yake,”40 “jua halitashuka tena; … kwa kuwa Bwana atakuwa nuru [yetu] ya milele, na siku za kuomboleza [kwetu] zitakoma.”41 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.