2010–2019
Mabinti Wapendwa
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


2:3

Mabinti Wapendwa

Katika kiini cha yote tunayofanya kwa Wasichana ni hamu yetu ya kuwasaidia kupata imani isiyotikisika katika Bwana Yesu Kristo.

Dada zangu wapendwa, ni furaha kuwa nanyi! Tunashuhudia mmiminiko wa ufunuo ambao unainua na kusisimua nafsi.

Tunapoanza, ningependa kuwatambulisha kwa baadhi ya marafiki; ni wasichana wa kipekee katika talanta, tamaduni, na hali ya binafsi na kifamilia. Kila mmoja wao, kama vile ninyi nyote, amekonga moyo wangu.

Bella

Kwanza, kutana na Bella. Anasimama imara kama msichana pekee katika tawi lake huko Iceland.

Josephine

Kutana na Josephine mwenye bidii kutoka Afrika, ambaye ameweka msimamo mpya wa kujifunza Kitabu cha Mormoni kila siku. Anagundua nguvu na baraka ambazo huja kutokana na tendo hili rahisi, la uaminifu.

Ashtyn

Na hatimaye, kutana na rafiki yangu mpendwa Ashtyn, msichana wa kipekee ambaye alifariki baada ya kupambana kwa miaka sita dhidi ya saratani. Ushuhuda wake imara wa Upatanisho wa Yesu Kristo bado unajirudia katika moyo wangu.

Ninyi nyote ni wasichana wa kusifika. Ninyi ni wa kipekee, kila mmoja akiwa na vipawa na uzoefu wake mwenyewe lakini mkifanana katika njia muhimu na za milele.

Ninyi hasa ni mabinti wa kiroho wa Wazazi wa Mbinguni, na hakuna chochote kinachoweza kuwatenga kutoka upendo Wao na upendo wa Mwokozi wenu.1 Unaposogea karibu Naye, hata kwa kupiga hatua za kitoto kwenda mbele, utagundua amani ya kudumu ambayo hutulia ndani ya nafsi yako kama mfuasi mwaminifu wa Mwokozi wetu, Yesu Kristo.

Rais Russell M. Nelson, nabii wetu mpendwa, ameomba kwamba nishiriki baadhi ya marekebisho yenye uvuvio ambayo yatawasaidia “kujenga uwezo [wenu] binafsi mtakatifu”2 na kuzidisha ushawishi wenu wa uadilifu. Nitazungumzia maeneo manne ya marekebisho usiku huu.

Dhima ya Wasichana

Kwanza, katika kiini cha yote tunayofanya kwa Wasichana ni hamu yetu ya kuwasaidia kupata imani isiyotikisika katika Bwana Yesu Kristo3 na ufahamu hakika wa utambulisho wenu mtakatifu kama binti wa Mungu.

Usiku huu, ningependa kutangaza rejeleo kwenye dhima ya Wasichana. Ninaomba muweze kuhisi Roho Mtakatifu akishuhudia ukweli wa maneno haya wakati ninaposoma dhima mpya:

Mimi ni binti mpendwa wa Wazazi wa Mbinguni,4 mwenye asili takatifu na takdiri ya milele.5

Kama mfuasi wa Yesu Kristo,6 ninajitahidi kuwa kama Yeye.7 Ninatafuta na kufanyia kazi ufunuo binafsi8 na kuwahudumia wengine katika jina Lake takatifu.9

Nitasimama kama shahidi wa Mungu wakati wote na katika vitu vyote na mahali popote.10

Ninapojitahidi kustahili kwa ajili ya kuinuliwa,11 ninathamini zawadi ya toba12 na kutafuta kuwa bora kila siku.13 Kwa imani,14 nitaimarisha nyumba na familia yangu,15 kufanya na kushika maagano matakatifu,16 na kupokea ibada17 na baraka za hekalu takatifu.18

Gundua kuhama kutoka “sisi” kwenda “mimi.” Kweli hizi zinahusika kwako binafsi. Wewe ni binti mpendwa wa Wazazi wa Mbinguni. Wewe ni mfuasi wa agano wa Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Ninawaalika kujifunza na kutafakari maneno haya. Ninajua mnapofanya hivyo, mtapokea ushuhuda wa ukweli wake. Kuelewa kweli hizi kutabadilisha jinsi unavyozikabili changamoto. Kujua utambulisho na lengo lako kutakusaidia kufunganisha mapenzi yako na ya Mwokozi.

Amani na mwongozo vitakuwa vyako pale unapomfuata Yesu Kristo.

Madarasa ya Wasichana

Eneo la pili la mabadiliko linaathiri madarasa ya Wasichana. Mzee Neal A. Maxwell alisema, “Mara nyingi kile watu wanachohitaji sana ni kupata hifadhi kutokana na dhoruba za maisha katika kimbilio la kustahili.”19 Madarasa yetu lazima yawe kimbilio dhidi ya dhoruba, mahala salama pa upendo na kustahili. Katika juhudi ya kujenga umoja mkuu, kuimarisha urafiki, na kuzidisha ile hisia ya kustahili kuwa kati ya Wasichana, tunafanya baadhi ya marekebisho kwenye muundo wa darasa.

Kwa zaidi ya miaka 100, wasichana wamekuwa wakigawanywa kwenye madarasa matatu. Kwa kuanza mara moja, tunawaalika viongozi wa Wasichana na maaskofu kwa sala kufikiria mahitaji ya kila msichana na kuwapanga kulingana na hali mahususi za kata. Hapa ni baadhi ya mifano ya jinsi hili linavyoweza kuonekana.

  • Ikiwa una Wasichana wachache, ungeweza kuwa na darasa moja la Wasichana wote wakikutana pamoja.

  • Pengine una kundi kubwa la wasichana wa miaka 12 na kisha kundi dogo la wasichana ambao ni wakubwa. Unaweza kuamua kuwa na madarasa mawili: Wasichana wa miaka 12 na Wasichana wa miaka 13–18.

  • Au ikiwa una kata kubwa yenye wasichana 60 wanaohudhuria, unaweza kuwa na madarasa sita, moja kwa kila umri, yakipangwa kulingana na miaka.

Bila kujali mpangilio wa madarasa yenu, ninyi wasichana ni muhimu katika kujenga umoja. Kuweni nuru kwa wale wanaowazunguka. Kuweni chanzo cha upendo na ulinzi mnaotumaini kupata kutoka kwa wengine. Kwa sala moyoni mwenu, endeleeni kufikia na kuwa nguvu ile ya wema. Mnapofanya hivyo, maisha yenu yatajazwa ukarimu. Mtakuwa na hisia nzuri zaidi kwa wengine na mtaanza kuona wema wao kama malipo.

Majina ya Madarasa ya Wasichana

Tatu, kwa mpangilio huu mpya wa darasa, madarasa yote yatarejelewa kwa jina linalounganisha la “Wasichana.”20 Tutapumzisha majina ya “Beehive,” “Mia Maid,” na “Laurel.”

Kuimarisha Urais wa Darasa

Eneo la mwisho ninalotamani kuzungumzia ni umuhimu wa urais wa darasa. Bila kujali jinsi madarasa ya Wasichana yalivyopangiliwa, kila darasa linapaswa kuwa na urais wa darasa!21 ni kwa muundo mtakatifu kwamba wasichana wanaitwa kuongoza katika ujana wao.

Jukumu na lengo la urais wa darasa limeimarishwa na kufafanuliwa kwa uwazi. Kazi ya wokovu ni mojawapo ya majukumu haya muhimu, hasa katika maeneo ya kuhudumu, kazi ya umisionari, kurudisha kwenye kushiriki kikamilifu, na kazi ya hekalu na historia ya familia.22 Ndiyo, hivi ndivyo tunavyoikusanya Israeli23—kazi tukufu kwa wasichana wote kama washiriki wa jeshi la vijana la Bwana.

Kama mnavyojua, katika kila ngazi ya Kanisa, Bwana anaita urais ili kuongoza watu Wake. Wasichana, kuwa mshiriki wa urais wa darasa inaweza kuwa fursa yenu ya kwanza kushiriki katika mpangilio huu wenye uvuvio wa uongozi. Viongozi watu wazima, fanyeni wito wa urais wa darasa kuwa kipaumbele na kisha ongozeni bega kwa bega pamoja nao, mkiwashauri na kuwaongoza ili waweze kufanikiwa.24 Bila kujali kiwango cha uzoefu wa uongozi wa urais wa darasa, anzia pale walipo na wasaidie kukuza ujuzi na ujasiri ambao utawabariki wao kama viongozi. Kuweni karibu nao, lakini msichukue madaraka. Roho atakuongoza pale unapowaongoza.

Chloe

Kuelezea jukumu muhimu la wazazi na viongozi kama washauri, acha niwasimulie hadithi. Chloe aliitwa kutumikia kama rais wa darasa. Kiongozi wake wa ukuhani mwenye busara alimtia moyo kutafuta usaidizi wa Bwana katika kupendekeza majina kwa ajili ya urais wake. Chloe aliomba na kupokea uvuvio wa nani wa kuwapendekeza kama washauri wake haraka sana. Alipoendelea kutafakari na kuomba kuhusu katibu muhtasi, Roho mara kwa mara alivuta fokasi yake kwa msichana ambaye alimshangaza—mtu ambaye alikuja kanisani au kwenye shughuli mara chache sana.

Akihisi hofu kwa ushawishi, Chloe alizungumza na mama yake, ambaye alielezea kwamba mojawapo ya njia tunazoweza kupokea ufunuo ni kupitia mawazo yanayojirudia. Kwa ujasiri mpya, Chloe alihisi alipaswa kumpendekeza msichana huyu. Askofu alitoa wito, na msichana alikubali. Baada ya kutawazwa, katibu muhtasi huyu mzuri alisema, “Unajua, sikuwahi kuhisi kana kwamba nilikuwa na sehemu au nilihitajika popote. Sikuhisi kama nilikuwa nafaa. Lakini kwa wito huu, ninahisi kana kwamba Baba wa Mbinguni ana lengo na sehemu kwa ajili yangu.” Wakati Chloe na mama yake walipoondoka kwenye mkutano, Chloe alimgeukia mama yake na kusema, kwa machozi machoni mwake, “Ufunuo ni halisi! Ufunuo kweli unafanya kazi!”

Urais wa darasa, mmeitwa na Mungu na kuaminiwa kuongoza kundi la mabinti Zake. “Bwana anakujua. … Yeye amekuchagua.”25 Wewe umetawazwa na yule mwenye mamlaka ya ukuhani; hii inamaanisha unapofanya majukumu ya wito wako, unafanyia kazi mamlaka ya ukuhani. Una kazi muhimu ya kufanya. Kuwa makini na fanyia kazi uvuvio wa Roho Mtakatifu. Unapofanya hivyo, unaweza kutumikia kwa ujasiri, kwani hautumikii peke yako!

Marais wa darasa, tunahitaji busara yenu, sauti, na nguvu kwenye baraza jipya la vijana la kata ambalo Mzee Quentin L. Cook amelitangaza leo. Ninyi ni sehemu muhimu ya suluhisho kwenye kukidhi mahitaji ya kaka na dada zenu.26

Mabadiliko haya katika mpangilio wa darasa na uongozi yanaweza kuanza punde kata na matawi yanapokuwa tayari lakini yanapaswa kufanya kazi ifikapo January 1, 2020.

Dada zangu wapendwa, ninatoa ushuhuda kwamba marekebisho haya niliyoyazungumzia leo ni maelekezo yenye uvuvio kutoka kwa Bwana. Wakati tunapotekeleza kwa bidii marekebisho haya, hebu tusipoteze uelekeo wa lengo letu: kuimarisha azma yetu ya kumfuata Yesu Kristo na kuwasaidia wengine kuja Kwake. Ninashuhudia kwamba hili ni Kanisa Lake. Jinsi gani nina shukrani kwamba Yeye anaturuhusu kuwa sehemu muhimu ya kazi Yake takatifu.

Ninaomba kwamba Roho yuleyule ambaye ameongoza marekebisho haya atawaongoza mnaposonga mbele kwenye njia ya agano. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.