Msimamo Thabiti kwa Yesu Kristo
Mungu anatualika kutupa njia zetu za zamani mbali kabisa na ufiko wetu na kuanza maisha mapya katika Kristo, tukionesha msimamo wetu kwa kufanya na kushika maagano.
Aprili iliyopita, nilikuwa na fursa ya kuweka wakfu Hekalu la Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.1 Maneno hayawezi kuelezea furaha ambayo mimi na watakatifu wa Kongo tulihisi kwa kuona hekalu likiwekwa wakfu nchini kwao.
Wale wanaoingia katika Hekalu la Kinshasa wanaona mchoro halisi uliopewa jina Maporomoko ya Maji ya Kongo.2 Kiupekee unawakumbusha wanaoenda hekaluni juu ya msimamo thabiti unaohitajika ili kujikita kwa Yesu Kristo na kufuata njia ya agano ya mpango wa Baba wa Mbinguni. Maporomoko ya maji yanayoonekana kwenye picha huleta kumbukumbu juu ya utamaduni ambao ulikuwa wa kawaida zaidi ya karne moja iliyopita miongoni mwa waongofu wa kale katika Ukristo huko Kongo.
Kabla ya uongofu wao, waliabudu vitu visivyo na uhai, wakiamini kwamba vitu hivyo vilikuwa na nguvu za ajabu.3 Baada ya uongofu, wengi walifanya hija kwenye moja kati ya maporomoko mengi ya maji kando ya Mto Kongo, kama vile maporomoko ya maji ya Nzongo.4 Waongofu hawa walitupa miungu yao ya kipindi cha nyuma katika maporomoko ya maji kama ishara kwa Mungu na kwa wengine kwamba walikuwa wametupa tamaduni zao za kale na kumkubali Yesu Kristo. Kwa kunuia hawakutupa vitu vyao kwenye maji yaliyotulia, yenye kina kifupi; walivitupa ndani ya maji yanayotiririka ya maporomoko makubwa, ambapo vitu visingeweza kupatikana tena. Matendo haya yalikuwa ni ishara ya msimamo mpya lakini thabiti katika Yesu Kristo.
Watu katika sehemu zingine na wa umri tofauti walionesha msimamo wao kwa Yesu Kristo katika njia sawa na hizo.5 Watu katika Kitabu cha Mormoni wanaojulikana kama Waanti-Nefi-Lehi “walizika silaha zao za uasi,” wakizizika chini mchangani” kama “Ushuhuda kwa Mungu … kwamba kamwe hawangetumia silaha [zao] tena.”6 Kwa kufanya hivyo, waliahidi kufuata mafundisho ya Mungu na kamwe hawakurudi nyuma katika msimamo wao. Tendo hili lilikuwa ni mwanzo wa kuwa “waongofu kwa Bwana” na kamwe kutoanguka.7
Kuwa “mwongofu kwa Bwana” humaanisha kuacha mwelekeo mmoja wa matendo, unaoongozwa na mfumo wa imani za zamani, na kushikilia mwelekeo mpya uliojikita katika mpango wa Baba wa Mbinguni na katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Badiliko hili ni zaidi ya kukubali tu kimawazo mafundisho ya injili. Linatengeneza utambulisho wetu, kuubadili uelewa wa maana ya maisha, na kupelekea kwenye kutobadilika kwa uaminfu kwa Mungu. Matamanio binafsi ambayo ni kinyume na kujikita kwa Mwokozi na kufuata njia ya agano hufifia na nafasi yake kuchukuliwa na uamuzi wa kujiweka chini ya mapenzi ya Baba wa Mbinguni.
Kuongoka kwa Bwana huanza na msimamo thabiti kwa Mungu, ukifuatiwa na kufanya msimamo huo kuwa sehemu ya sisi tulivyo. Kuufanya sehemu ya maisha yetu msimamo huo ni mchakato wa maisha yote ambao unahitaji uvumilivu na toba endelevu. Hatimaye, msimamao huu unakuwa sehemu ya sisi tulivyo, ukijumuishwa katika nafsi zetu, na daima kuwa katika maisha yetu. Kama vile tusivyoweza kusahau jina letu bila kujali ni kipi kingine tunakifikiria, kamwe hatusau msimamo ambao umeandikwa mioyoni mwetu.8
Mungu anatualika kutupa njia zetu za zamani mbali kabisa na ufiko wetu na kuanza maisha mapya katika Kristo, tukionesha msimamo wetu kwa kufanya na kushika maagano. Hii hutokea wakati tunapokuza imani katika Mwokozi, ambayo huanza kwa kusikia ushuhuda wa wale ambao wana imani.9 Kisha, imani huongezeka wakati tunapotenda katika njia ambayo hutuweka imara zaidi Kwake.10
Sasa, ingekuwa vyema ikiwa ongezeko la imani lingesambazwa kama mafua au kikohozi. Kisha, “chafya ya kiroho” ingeweza kujenga imani kwa wengine. Lakini haifanyiki katika njia hiyo. Njia pekee ambayo imani hukua ni kwa mtu kutenda kwa imani. Matendo haya mara nyingi husukumwa na mialiko iliyotolewa na wengine, lakini hatuwezi “kukuza” imani ya mwingine au kutegemea wengine kukuza ya kwetu. Ili imani yetu ikue, lazima tuchague matendo yanayokuza imani kama vile kusali, kujifunza maandiko, kushiriki sakramenti, na kutumikia wengine.
Wakati imani yetu katika Yesu Kristo inakua, Mungu anatualika kuweka ahadi pamoja Naye. Maagano haya, kama zilivyo ahadi hizi zinazojulikana, ni madhihirisho ya uongofu wetu. Maagano pia hutengeneza msingi imara kwa ajili ya ukuaji kiroho. Wakati tunapochagua kubatizwa, tunaanza kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo11 na kuchagua kutambulishwa pamoja Naye. Tunaweka ahadi kuwa kama Yeye na kukuza sifa kama zake.
Maagano hutukita kwa Mwokozi na hututia nguvu tuwapo katika njia ambayo huelekea kwenye nyumba yetu mbinguni. Nguvu ya maagano hutusaidia kubakia wenye badiliko kuu la moyo, kukuza uongofu wetu kwa Bwana, na kupokea kikamilifu mfano wa Kristo katika mwonekano wetu.12 Lakini msimamo usio kamili kwenye maagano yetu hautatuhakikishia chochote.13 Tunaweza kujaribiwa kufanya udanganyifu, kutupa tamaduni zetu za kale katika maji yaliyotulia, au kuzika silaha zetu za uasi mishikio yake ikibaki nje. Lakini msimamo usio wa kweli kwenye maagano yetu hautafungua mlango kwenye nguvu ya kutakasa ya Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.
Msimamo wetu wa kushika maagano haupaswi kuwa na masharti au kubadilika kulingana na mabadiliko ya hali katika maisha yetu. Uendelevu wetu kwa Mungu lazima uwe kama Mto Kongo unaotegemewa ambao unatiririka karibu na Hekalu la Kinshasa. Mto huu, tofauti na mito mingine mingi ulimwewnguni, hutiririka kwa mwaka mzima14 na kumimina karibu galoni milioni 11 (Lita milioni 41.5) za maji kwa sekunde kwenye Bahari ya Antlantiki.
Mwokozi aliwaalika wanafunzi Wake kuwa wa kutegemewa na imara kwa jinsi hii. Alisema, “Sasa, amueni vitu hivi mioyoni mwenu, kwamba mtatenda vitu hivi ambavyo nitawafundisha, na kuwaamuru.”15 Msimamo “uliofanyiwa uamuzi” wa kushika maagano yetu huruhusu utambuzi kamili wa ahadi ya Mungu ya shangwe ya kudumu.16
Watakatifu wengi wa siku za Mwisho wameonesha kwamba “wamefanya uamuzi” katika kushika maagano yao na Mungu na wamebadilika milele. Acha niwaambie kuhusu watu watatu kama hao—Kaka Banza Mucioko, Dada Banza Régine, na Kaka Mbuyi Nkitabungi.
Mnamo mwaka 1977 akina Banza waliishi Kinshasa katika nchi ya Zaire, ambayo sasa inajulikana kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Walikuwa wakiheshimika sana katika jumuiya yao ya Kiprotestanti. Kwa sababu ya vipaji vyao, kanisa lao lilipanga kwa ajili ya familia yao changa kwenda Uswisi kusoma na lilitoa udhamini wa chuo kikuu.
Wakati wako Geneva, katika basi kuelekea shuleni, Kaka Banza mara nyingi aliona jengo dogo la ibada likiwa na jina “Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.” Alijiuliza, “Je, Kristo ana watakatifu kwa sasa, katika siku za mwisho?” Hatimaye aliamua kwenda na kuona.
Kaka na Dada Banza walikaribishwa kwa upendo katika tawi. Waliuliza baadhi ya maswali endelevu waliyokuwa nayo kuhusu uhalisia wa Mungu, kama vile, “kama Mungu ni roho, sawa na upepo, je, inawezekanaje sisi kuumbwa kwa mfano Wake? Je, anawezaje kukaa katika kiti cha enzi?” Walikuwa hawajawahi kupokea jibu la kuridhisha mpaka wamisionari walipofafanua mafundisho ya urejesho katika somo fupi. Wakati wamisionari walipoondoka, akina Banza waliangaliana na kusema, “Je, huu tuliosikia si ukweli?” Waliendelea kuja kanisani na kukutana na wamisionari. Walijua kwamba kubatizwa katika Kanisa lililorejeshwa la Yesu Kristo kungekuwa na matokeo. Wangenyimwa udhamini wao wa chuo kikuu, viza zao zingefutwa, na wao pamoja na watoto wao wawili wadogo wangetakiwa kuondoka Uswisi. Walichagua kubatizwa na kuthibitishwa mnamo Oktoba 1979.
Wiki mbili baada ya ubatizo, Kaka na Dada Banza walirudi Kinshasa kama muumini wa kwanza na wa pili wa Kanisa katika nchi yao. Waumini katika Tawi la Geneva, waliendelea kuwasiliana nao na kuwasaidia kuwa na muunganiko na viongozi wa Kanisa. Akina Banza walitiwa moyo kusubiri kwa uaminifu muda ulioahidiwa wakati Mungu atakapoanzisha Kanisa lake huko Zaire.
Wakati huo, kama mwanafunzi toka Zaire, Kaka Mbuyi, alikuwa masomoni huko Ubelgiji. Alibatizwa mnamo mwaka 1980 katika kata ya Brussels. Punde baada ya hapo, alitumikia kama mmisionari huko Uingereza. Na Mungu alitenda miujiza Yake. Kaka Mbuyi alirudi Zaire kama muumini wa tatu wa Kanisa katika nchi yake. Kwa ruhusa ya wazazi, Kanisa lilifanya mikutano katika nyumba ya familia yake. Mnamo Februari 1986 ombi lilipelekwa serikalini kwa ajili ya utambuzi rasmi wa Kanisa. Saini za raia watatu wa Zaire zilihitajika. Watia saini watatu wenye furaha kwa ajili ya ruhusa walikuwa Kaka Banza, Dada Banza, na Kaka Mbuyi.
Waumini hawa waaminifu waliujua ukweli walipousikia; walifanya agano kwenye ubatizo ambalo liliwafanya wajikite kwa Mwokozi. Wao kistiari walikuwa wametupa tamaduni zao za kale katika maporomoko ya maji yenye kasi bila kuwa na nia ya kuzichukua tena. Njia ya agano kamwe haikuwa rahisi. Mchafuko wa kisiasa, kukosa mawasiliano ya mara kwa mara na Viongozi wa Kanisa, na changamoto zilizotokana na kujenga jamii ya Watakatifu zingeweza kuwadhoofisha watu wenye msimamo usio thabiti. Lakini kaka na Dada Banza na Kaka Mbuyi walistahimili katika imani yao. Walikuwepo wakati wa uwekaji wakfu wa Hekalu la Kinshasa, miaka 33 baada ya kutia saini ombi ambalo lilipelekea utambuzi rasmi wa Kanisa huko Zaire.
Akina Banza wako hapa leo katika Ukumbi wa Mkutano. Wamesindikizwa na wana wao wawili, Junior na Phil, na wakwe, annie na Youyou. Mnamo 1986, Junior na Phil walikuwa ni watu wawili wa kwanza kubatizwa Kanisani huko Zaire. Kaka Mbuyi anaangalia matangazo haya kutoka Kinshasa pamoja na mke wake, Maguy, na watoto wao watano.
Waasisi hawa wanaelewa maana na matokeo ya maagano ambayo kwayo waliletwa kwenye “uelewa wa Bwana Mungu wao, na kufurahia katika Yesu Kristo Mkombozi wao.”17
Je tunakitaje nafsi zetu kwa Mwokozi na kubakia waaminifu kama hawa na makumi elfu wengine wa Watakatifu wa Kongo ambao waliwafuata na mamilioni ya wengine ulimwenguni kote? Mwokozi alitufundisha jinsi ya kufanya hivyo. Kila wiki tunashiriki sakramenti na kufanya agano na Baba yetu wa Mbinguni. Tunaahidi kuunganisha utambulisho wetu na ule wa Mwokozi kwa kuwekea ahadi utayari wetu wa kujichukulia juu yetu jina Lake, Kumkumbuka daima, na kutii amri Zake.18 Kwa dhati kujiandaa kwa ajili ya na kwa kustahiki kufanya maagano haya kila wiki hutuweka thabiti kwa Mwokozi, hutusaidia kutafakari kwa kina msimamo wetu,19 na kwa nguvu kutusukuma katika njia ya agano.
Ninawaalika kuweka msimamo katika mchakato wa maisha yote wa ufuasi. Fanya na shika maagano. Tupeni tamaduni zenu za zamani katika maporomoko ya maji yenye kina kirefu, yenye kasi. Zikeni kikamilifu silaha zenu za uasi pasipo kuacha mishikio ikichomoza nje. Kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo, kufanya maagano kwa nia ya dhati ya kuyaheshimu kwa uthabiti kutabariki maisha yako milele. Utakuwa zaidi kama Mwokozi wakati daima unapomkumbuka Yeye, Kumfuata, na Kumpenda. Ninashuhudia kwamba Yeye ni msingi imara. Yeye ni wa kutegemewa, na ahadi Zake ni za uhakika. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.