Utakatifu na Mpango wa Furaha
Furaha kuu huja kutokana na utakatifu mkuu binafsi.
Wapendwa akina kaka na dada zangu, nimeomba kwa ajili ya nguvu ili kuwasaidia katika utafutaji wenu binafsi wa furaha. Wengine wanaweza kujiona tayari wana furaha ya kutosha, hata hivyo hakika hakuna ambaye angeweza kukataa ofa ya furaha zaidi. Mtu yeyote angetamani kukubali hakikisho la ofa ya furaha ya milele.
Hicho ndicho kile Baba wa Mbinguni; Mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo; na Roho Mtakatifu wametoa kwa kila mtoto wa kiroho wa Baba wa Mbinguni ambaye sasa anaishi, ataishi, au aliyewahi kuishi katika dunia hii. Ofa hiyo wakati mwingine inaitwa mpango wa furaha. Uliitwa hivyo na nabii Alma wakati akimfunza mwanaye, ambaye alikuwa amenaswa kwenye huzuni ya dhambi. Alma alijua kwamba uovu kamwe hauwezi kuwa furaha kwa mwanaye—au kwa mtoto yeyote wa Baba wa Mbinguni.1
Alimfundisha mwanaye kwamba kuongezeka katika utakatifu ilikuwa ndiyo njia pekee ya furaha. Aliweka wazi kwamba utakatifu mkuu zaidi unawezekana kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo ukitutakasa na kutufanya wakamilifu.2 Ni kwa imani tu katika Yesu Kristo, toba endelevu, na kushika maagano ndipo tunaweza kupata furaha ya kudumu tunayotamani kuipata na kuihifadhi.
Sala yangu kwa leo ni kwamba niweze kuwasaidia kuelewa kwamba furaha kuu inakuja kutokana na utakatifu binafsi ili kwamba mtende kulingana na imani hiyo. Kisha nitashiriki kile ninachokijua mwenyewe kuhusu kile tunachoweza kufanya ili kustahili zawadi hiyo ya kuwa watakatifu zaidi.
Maandiko yanatufundisha kwamba miongoni mwa vitu vingine, tunaweza kutakaswa au kuwa watakatifu zaidi tunapoonesha imani katika Kristo,3 kuonesha utiifu wetu,4 kutubu,5 kutoa dhabihu kwa ajili Yake,6 kupokea ibada takatifu, na kushika maagano yetu tuliyoweka Naye.7 Kustahili kwa ajili ya kipawa cha utakatifu kunahitaji unyenyekevu,8 upole,9 na uvumilivu.10
Uzoefu mmoja wa kutaka utakatifu zaidi ulikuja kwangu nikiwa katika Hekalu la Salt Lake. Niliingia hekaluni kwa mara ya kwanza nikiwa nimeambiwa machache tu juu ya nini cha kutarajia. Niliona maneno kwenye jengo: “Utakatifu kwa Bwana” na “Nyumba ya Bwana.” Nilihisi hisia kubwa ya matarajio. Bado nilijiuliza ikiwa nilijiandaa kuingia.
Mama na baba yangu walitangulia mbele yangu tulipoingia hekaluni. Tuliombwa kuonesha vibali vyetu vya hekaluni, kuthibitisha ustahiki wetu.
Wazazi wangu walimjua yule mtu kwenye dawati la vibali. Kwa hivyo walikaa kidogo kuongea naye. Nilitangulia peke yangu hadi kwenye eneo kubwa ambapo kila kitu kilikuwa kinang’aa kwa weupe. Nilitazama juu kwenye dari iliyokuwa juu sana ilionekana kama anga la wazi. Katika wasaa ule, msukumo wa wazi ulinijia kwamba niliwahi kuwa hapo kabla.
Lakini kisha, nilisikia sauti nyororo sana—haikuwa yangu mwenyewe. Maneno yaliyosemwa kwa upole yalikuwa haya: “hujawahi kuwa hapa awali. Unakumbuka wakati kabla ya kuzaliwa kwako. Ulikuwa mahali patakatifu kama hapa. Ulihisi Mwokozi alikuwa karibu kuja mahala ambapo ulisimama. Na ulihisi furaha kwa sababu ulitamani kumwona Yeye.”
Uzoefu ule katika Hekalu la Salt Lake ulidumu kwa muda tu. Hata hivyo kumbukumbu yake bado huleta amani, shangwe, na furaha tulivu.
Nilijifunza masomo mengi siku hiyo. Moja lilikuwa kwamba Roho Mtakatifu anazungumza katika sauti ndogo, tulivu. Naweza kumsikia wakati kuna amani ya kiroho katika moyo wangu. Analeta hisia ya furaha na hakikisho kwamba ninakuwa Mtakatifu zaidi. Na hilo daima huleta furaha niliyohisi katika nyakati hizo za mwanzo katika hekalu la Mungu.
Umeona katika maisha yako mwenyewe na katika maisha ya wengine muujiza wa furaha ukija kutokana na kukua kwa utakatifu, kuwa zaidi kama Mwokozi. Katika wiki za hivi karibuni, nimekuwa pembeni ya vitanda vya watu ambao wangeweza kukutana na kifo kwa imani kamili katika Mwokozi na nyuso za furaha.
Mmoja alikuwa mtu aliyezungukwa na familia yake. Yeye na mke wake walikuwa wakizungumza kwa utulivu wakati mimi na mwanangu tulipoingia. Nilikua nimewajua kwa miaka mingi. Nilikua nimeona Upatanisho wa Yesu Kristo ukifanya kazi katika maisha yao na katika maisha ya wanafamilia wao.
Kwa pamoja walikuwa wamechagua kusimamisha juhudi za matibabu za kuongeza muda wa maisha yake. Palikuwa na hisia za ukimya wakati akizungumza nasi. Alitabasamu wakati alipoelezea shukrani kwa ajili ya injili na faida zake za utakaso kwake na kwa familia aliyoipenda. Aliongelea miaka yake ya furaha ya huduma hekaluni. Kwa ombi la mtu huyu, mwanangu alimpaka mafuta yaliyowekwa wakfu kichwani. Mimi nikafunga upako. Nilipofanya hivyo, nilipata msukumo dhahiri kumwambia kwamba muda si mrefu angemwona Mwokozi wake, uso kwa uso.
Nilimuahidi kwamba angehisi furaha, upendo, na idhinisho la Mwokozi. Alitabasamu kwa upendo wakati tukiondoka. Maneno yake ya mwisho kwangu yalikuwa “Mwambie Kathy ninampenda.” Mke wangu, Kathleen, kwa miaka mingi alivihimiza vizazi vya familia yake kukubali mwaliko wa Mwokozi wa kuja Kwake, kufanya na kushika maagano matakatifu, na hivyo kustahili kwa ajili ya furaha ambayo huja kama matokeo ya utakatifu huo mkuu.
Mtu huyu alifariki masaa kadhaa baadaye. Wiki kadhaa baada ya kufariki kwake, mjane wake alituletea mimi na mke wangu zawadi. Alitabasamu wakati tukizungumza. Alisema kwa furaha, “Nilitarajia kwamba ningehisi huzuni na upweke. Ninahisi furaha sana. Unafikiri hiyo ni sawa?”
Kwa kujua jinsi alivyompenda mumewe na jinsi wote wawili walivyokuja kumjua, kumpenda, na kumtumikia Bwana, nilimwambia kwamba hisia zake za furaha zilikuwa zawadi iliyoahidiwa kwa sababu yeye, kwa huduma yake ya uaminifu, alifanywa mtakatifu zaidi. Utakatifu wake ulikuwa umemstahilisha kwa ajili ya furaha hiyo.
Baadhi ya wanaosikiliza leo wanaweza kuwa wanajiuliza: “Je! Kwa nini sihisi amani na furaha iliyoahidiwa kwa wale ambao wamekuwa waaminifu? Nimekuwa mwaminifu katika dhiki za kutisha, lakini sihisi furaha.”
Hata Nabii Joseph Smith alikutana na mtihani huu. Aliomba msaada wakati alipofungwa jela huko Liberty, Missouri. Alikuwa amekuwa mwaminifu kwa Bwana. Alikuwa amekua katika utakatifu. Walakini alihisi alikuwa amenyimwa furaha.
Bwana alimfundisha somo la uvumilivu ambalo sisi sote tutalihitaji wakati fulani, na labda kwa muda mrefu, katika majaribio yetu hapa duniani. Hapa ni ujumbe wa Bwana kwa nabii Wake mwaminifu na mwenye kuteseka:
“Na kama utatupwa ndani ya shimo, au katika mikono ya wauaji, na hukumu ya kifo ikapitishwa juu yako; kama utatupwa kilindini; kama mawimbi makali yatakula njama dhidi yako; kama upepo mkali utakuja kuwa adui yako; kama mbingu zitakusanya giza, na vitu vyote vya asili vikiungana ili kuzingira njia yako; na juu ya yote, kama mataya yale ya jahanamu yataachama kinywa wazi kwa ajili yako, fahamu wewe, mwanangu, kwamba mambo haya yote yatakupa wewe uzoefu, na yatakuwa kwa faida yako.
“Mwana wa Mtu amejishusha chini yao wote. Je, wewe u mkuu kuliko yeye?
“Kwa hiyo, shikilia njia yako, na ukuhani utabakia nawe; kwa kuwa mipaka yao imewekwa, hawawezi kuivuka. Siku zako zinafahamika, na miaka yako haitahesabika kuwa michache; kwa hiyo, usiogope mwanadamu awezacho kukutenda, kwani Mungu atakuwa pamoja nawe milele na milele.”11
Hilo lilikuwa somo la kuelekeza sawa na ambalo Bwana alimpa Ayubu, ambaye alilipa gharama nzito ili kuruhusu Upatanisho kumfanya kuwa mtakatifu zaidi. Tunajua ya kuwa Ayubu alikuwa mtakatifu, kutokana na utangulizi tulio nao juu yake: “Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu.”12
Kisha Ayubu akapoteza utajiri wake, familia yake, na hata afya yake. Unaweza kukumbuka kuwa Ayubu alipata shaka kuwa utakatifu wake mkuu, uliopatikana kwa dhiki nyingi, ulikuwa umemstahilisha kwa ajili ya furaha kuu. Ilionekana kwa Ayubu kuwa utakatifu ulikuwa umeleta huzuni.
Lakini Bwana alimpa Ayubu somo la masahihisho sawa na lile Alilompa Joseph Smith. Alimruhusu Ayubu kuona hali yake ya kuumiza moyo kwa macho ya kiroho. Alisema:
“Basi jifunge viuno kama mwanamume; maana nitakuuliza neno, nawe niambie.
“Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! Sema, kama ukiwa na ufahamu.
“Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua? Au ni nani aliyenyosha kamba juu yake?
“Misingi yake ilikazwa juu ya kitu gani? Au ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni;
“Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, Na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha?”13
Kisha, baada ya Ayubu kutubu kwa kumwita Mungu si mtenda haki, Ayubu aliruhusiwa kuona majaribu yake katika njia ya juu na takatifu. Alikuwa ametubu.
“Ndipo Ayubu akamjibu Bwana, na kusema,
“Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.
“Ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa? Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, Mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua.
“Sikiliza, nakusihi, nami nitanena: Nitakuuliza neno, nawe niambie.
“Nilikuwa nimesikia habari zako kwa kusikia kwa masikio: bali sasa jicho langu linakuona.
“Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu Katika mavumbi na majivu.”14
Baada ya Ayubu kutubu na hivyo kuwa mtakatifu zaidi, Bwana alimbariki zaidi ya yote aliyopoteza. Lakini pengine baraka kubwa kwa Ayubu ilikuwa kuwa na ongezeko katika utakatifu kupitia dhiki na toba. Alikuwa amestahilishwa kuwa na furaha tele katika siku ambazo alikuwa bado hajaishi.
Utakatifu mkuu hauji tu kirahisi kwa kuuomba. Utakuja kwa kufanya kile kinachohitajika kwa ajili ya Mungu kutubadilisha.
Rais Russell M. Nelson ametoa kile kinachoonekana kwangu kuwa ushauri bora zaidi wa jinsi ya kutembea kwenye njia ya agano kufikia utakatifu mkuu. Alionesha njia wakati alipohimiza:
“Pata uzoefu wa nguvu ya kuimarisha ya toba ya kila siku—ya kufanya na kuwa bora zaidi kila siku.
“Tunapochagua kutubu, tunachagua kubadilika! Tunamruhusu Mwokozi kutubadilisha kuwa toleo zuri zaidi letu wenyewe. Tunachagua kukua kiroho na kupokea shangwe—shangwe ya ukombozi katika Yeye. Tunapochagua kutubu, tunachagua kuwa zaidi kama Yesu Kristo!”
Rais Nelson aliendelea kututia moyo katika juhudi zetu za kuwa watakatifu zaidi: “Bwana hatarajii ukamilifu kutoka kwetu wakati huu. … Lakini anatarajia sisi tuongezeke katika kuwa watakatifu. Toba ya kila siku ndiyo njia ya kuelekea utakatifu.”15
Rais Dallin H. Oaks, katika hotuba ya mkutano uliopita, alinisaidia pia kuona wazi zaidi jinsi tunavyokua katika utakatifu na jinsi tunavyoweza kujua kwamba tunasogea kuuelekea. Alisema: “Tunawezaje kufikia hali ya kiroho? Je! Tunapataje kiwango hicho cha utakatifu ambapo tunaweza kuwa na ushirika wa kila mara wa Roho Mtakatifu? Je, tunawezaje kuona na kutathmini vitu vya ulimwengu huu kwa mtazamo wa umilele?”16
Jibu la Rais Oaks linaanza na imani kubwa katika Yesu Kristo kama Mwokozi wetu mpendwa. Ambayo inatuongoza kutafuta msamaha kila siku na kumkumbuka Yeye kila siku kwa kutii amri zake. Imani hiyo kubwa katika Yesu Kristo inakuja tunaposherehekea neno lake kila siku.
Wimbo “More Holiness Give Me” unapendekeza njia ya kusali kwa ajili ya msaada wa kuwa watakatifu zaidi. Mwandishi kwa busara anapendekeza kuwa utakatifu tunaotafuta ni zawadi kutoka kwa Mungu mwenye upendo, itolewayo baada ya muda fulani, baada ya kufanya yote tunayoweza. Mnakumbuka aya ya mwisho:
Usafi zaidi nipe,
Nguvu zaidi za kushinda,
Uhuru zaidi kutoka kwenye mawaa ya dunia,
Kutamani zaidi nyumbani.
Kufaa zaidi kwa ufalme,
Kuweza kutumika zaidi,
Kubarikiwa zaidi na mtakatifu—
Zaidi, Mwokozi, Kama wewe.17
Bila kujali hali zetu binafsi, popote ambapo tunaweza kuwepo katika njia ya agano kuelekea nyumbani, acha sala zetu kwa ajili ya utakatifu zaidi zijibiwe. Ninajua kuwa sala yetu inapojibiwa, furaha yetu itaongezeka. Inaweza kuja taratibu, lakini itakuja. Nina uhakika huo kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo na Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo.
Ninashuhudia kwamba Joseph Smith alikuwa nabii wa Mungu, kwamba Rais Russell M. Nelson ni nabii wetu anayeishi leo. Mungu Baba anaishi na anatupenda. Yeye anatutaka turudi nyumbani Kwake katika familia. Mwokozi wetu mpendwa anatualika tumfuate Yeye kwenye safari yetu huko. Wao wameandaa njia. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.