2010–2019
Nguvu ya Kumshinda Adui
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


Nguvu ya Kumshinda Adui

Je, tunapataje amani, kukumbuka sisi ni nani, na kushinda U tatu za adui?

Akina Kaka na akina dada, nawashukuruni kwa yote mnayofanya kuwa, na kuwasaidia wengine kuwa, wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo na kufurahia baraka za hekalu takatifu. Asanteni kwa wema wenu. Ninyi ni wa kupendeza; ninyi ni wazuri.

Ni sala yangu kwamba tutatambua uthibitisho wa ushawishi wa Roho Mtakatifu tunapoelewa kikamilifu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” linasema: “Wanadamu wote—wanaume na wanawake—wameumbwa katika mfano wa Mungu. Kila mmoja ni mwana au binti mpendwa wa kiroho wa wazazi wa mbinguni, na, kwa hivyo, kila moja ana asili takatifu na takdiri.”1 Sisi ni “roho teule ambazo zilihifadhiwa ili kuja katika kipindi cha utimilifu wa nyakati kushiriki katika kuweka misingi ya kazi kuu ya siku za mwisho,”2 Rais Russell M. Nelson alitangaza: “Mlifundishwa katika ulimwengu wa roho kuwaanda kwa ajili ya chochote na kila kitu ambacho mngekabiliana nacho kipindi cha wakati huu wa siku hizi za mwisho (ona M&M 138:56). Fundisho hilo linadumu ndani yenu!”3

Ninyi ni wana na mabinti wateule wa Mungu. Mna nguvu ya Kumshinda Adui. Adui, hata hivyo, anafahamu ninyi ni kina nani. Anajua juu ya urithi wenu mtakatifu na anatafuta kuzuia uwezekano wenu wa kidunia na kimbingu kwa kutumia U tatu:

  • Udanganyifu

  • Uvurugaji wa mawazo

  • Ukatishaji tamaa

Udanganyifu

Adui alitumia kifaa cha udanganyifu katika siku za Musa. Bwana alitangaza kwa Musa:

“Na, tazama, wewe u mwanangu. …

“Nina kazi kwa ajili yako, … nawe u mfano wa Mwanangu wa Pekee.”4

Muda mfupi baada ya ono hili adhimu, Shetani alijaribu kumdanganya Musa. Maneno aliyoyatumia yanapendeza: “Musa, mwana wa mtu, niabudu mimi.”5 Udaganyifu haukuwa tu katika kumtaka amwabudu Shetani bali pia katika njia aliyomwelezea Musa kama mwana wa mtu. Kumbuka, Bwana ndiyo kwanza alikuwa amemweleza Musa kwamba alikuwa mwana wa Mungu, aliyeumbwa kwa mfano wa Mwana wa pekee.

Adui alikuwa mkali katika jaribu lake la kumjaribu Musa, lakini Musa alimpinga, akisema, “Ondoka kutoka kwangu, Shetani, kwa maana ni Mungu huyu mmoja tu nitakayemwabudu, ambaye ndiye Mungu wa utukufu.”6 Musa alikumbuka yeye alikuwa ni nani—mwana wa Mungu.

Maneno ya Bwana kwa Musa yanahusika kwako na kwangu. Tumeumbwa kwa mfano wa Mungu mwenyewe, na ana kazi kwa ajili yetu kufanya. Adui hujaribu kudaganya kwa kutufanya tusahau sisi ni akina nani hasa. Kama hatuelewi sisi ni nani, basi ni vigumu kutambua nani tunaweza kuwa.

Uvurugaji wa mawazo

Adui pia hujaribu kutuvuruga mawazo ili kutuweka mbali kutoka kwa Kristo na njia yake ya agano. Mzee Ronald A. Rasband alishiriki yafuatayo: “Mpango wa adui ni kutuvuruga mawazo ili kututoa kwenye ushahidi wa kiroho, wakati mataminio ya Bwana ni kutuelimisha na kutushirikisha katika kazi Yake.”7

Katika siku zetu, kuna vitu vingi vya kutuvuruga mawazo, ikijumuisha Twitter, Facebook, michezo mbalimbali, na mengine mengi. Maendeleo haya ya tekinolojia ni ya kupendeza, lakini kama hatuko waangalifu, yanaweza kutuvuruga mawazo tushindwe kukamilisha uwezekano wetu mtakatifu. Kuyatumia kwa njia ya kufaa kunaweza kuleta nguvu ya mbinguni na kuturuhusu kushuhudia miujiza pale tunapojitahidi kukusanya Israeli iliyotawanyika pande zote mbili za pazia.

Na tuwe waangalifu na tusiwe wa kawaida katika matumizi yetu ya tekinolojia.8 Daima tukitafuta njia ambazo tekinolojia inaweza kutuleta karibu zaidi na Mwokozi na kuturuhusu kukamilisha kazi Yake wakati tunapojiandaa kwa ajili ya Ujio Wake wa Pili.

Ukatishaji tamaa

Mwisho, adui anatamani sisi tukate tamaa. Tunaweza kukata tamaa wakati tunapojilinganisha na wengine au kuhisi hatuishi kufikia matarajio, ikijumuisha ya kwetu wenyewe.

Nilipoanza programu yangu ya udaktari, nilihisi kukata tamaa. Programu iliruhusu wanafunzi wanne tu mwaka ule, na wanafunzi wengine walikuwa wenye akili sana. Walikuwa na alama za juu zaidi kwenye mtihani na uzoefu mkubwa zaidi wa kazi kwenye nafasi kubwa katika utawala, na walionesha matumaini katika uwezo wao. Baada ya wiki zangu mbili za mwanzo katika programu, hisia za kukata tamaa na hofu zikaanza kunishika, karibu kunishinda.

Niliamua kwamba kama nilitaka kumaliza programu hii ya miaka minne, ni lazima nimalize kusoma kitabu cha Mormoni kila muhula. Kila siku niliposoma, nilitambua tangazo la Mwokozi kwamba Roho Mtakatifu angenifundisha mambo yote na angeleta mambo yote kwenye kumbukumbu zangu.9 Kilihakikisha kwa mara nyingine mimi ni nani kama mwana wa Mungu, kilinikumbusha kutokujilinganisha na wengine, na kilinipa kujiamini katika jukumu langu takatifu ili kufanikiwa.10

Rafiki zangu wapendwa, tafadhali msimruhusu yeyote kuiba furaha yenu. Usijilinganishe na wengine. Tafadhali kumbuka maneno ya upendo ya Mwokozi: “Amani Nawaachieni, amani yangu nawapa: sivyo kama ulimwengu utowavyo, niwapavyo mimi. Msifadhaike, mioyoni mwenu wala msiogope.”11

Hivyo tunalifanyaje hilo? Je, tunapataje amani hii, kukumbuka sisi ni nani, na kushinda U tatu za adui?

Kwanza, kumbuka kwamba amri ya kwanza na iliyo kuu ni kumpenda Mungu kwa moyo wetu, uwezo, akili, na nguvu.12 Vyote ambavyo tunafanya havina budi kupewa hamasa na upendo wetu Kwake na kwa Mwanaye. Tunapokuza upendo wetu Kwao kwa kutii amri Zao, uwezo wetu wa kujipenda wenyewe na kuwapenda wengine utaongezeka. Tutaanza kuhudumia familia, marafiki, na majirani kwa sababu tutawaona jinsi Mwokozi anavyowaona—kama wana na mabinti za Mungu.13

Pili, ombeni kwa Baba katika jina la Yesu Kristo kila siku, kila siku, kila siku.14 Ni kupitia sala ndipo tunaweza kuhisi upendo wa Mungu na kuonesha upendo wetu Kwake. Kupitia maombi tunaonesha shukrani na kuomba nguvu na ujasiri wa kuweka mapenzi yetu kuwa chini ya yale ya Mungu na kuongozwa na kuelekezwa katika mambo yote.

Ninawatia moyo “kuomba kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, ili muweze kujazwa na upendo huu, … ili muweze kuwa wana [na mabinti] wa Mungu; ili wakati atakapoonekana tutakuwa kama yeye.”15

Tatu, soma na jifunze Kitabu cha Mormoni kila siku, kila siku, kila siku.16 Kujifunza kwangu Kitabu cha Mormoni huwa bora zaidi ninaposoma nikiwa na swali mawazoni mwangu. Tunaposoma tukiwa na swali, tunaweza kupata ufunuo na kugundua kwamba Nabii Joseph Smith alisema ukweli wakati alipotangaza, “Kitabu cha Mormoni [ni] kitabu kilicho sahihi kuliko vitabu vyote duniani, … na mwanaume [au mwanamke] atamkaribia Mungu zaidi kwa kufuata mafunzo yake, zaidi ya kitabu kingine.”17 Kitabu cha Mormoni kina maneno ya Kristo na kinatusaidia kukumbuka sisi ni kina nani.

Mwisho, kwa moyo wa sala pokea sakramenti kila wiki, kila wiki, kila wiki. Ni kupitia maagano na ibada za ukuhani, ikijumuisha sakramenti, kwamba nguvu za Mungu zinadhihirika katika maisha yetu.18 Mzee David A. Bednar alifundisha: “Ibada ya sakramenti ni mwaliko mtakatifu na unaorudiwa kwa ajili ya kutubu kwa dhati na kufanywa upya kiroho. Kitendo cha kupokea sakramenti, ndani yake na chenyewe, hakileti msamaha wa dhambi. Lakini tunapojitayarisha kwa dhamira na kushiriki katika ibada hii takatifu kwa moyo uliovunjika na roho iliyopondeka, basi ahadi ni kwamba tunaweza daima kuwa na Roho wa Bwana pamoja nasi.”19

Tunapopokea sakramenti kwa unyenyekevu, tunakumbuka mateso ya Yesu katika bustani ile takatifu inayoitwa Gethsemane na dhabihu Yake juu ya msalaba. Tunaonesha shukrani kwa Baba kwa kumtuma Mwana Wake wa Pekee, Mkombozi wetu, na kuonesha utayari wetu kutii amri Zake na daima kumkumbuka Yeye.20 Kuna uelewa wa kiroho unaohusishwa na sakramenti—ni wa kibinafsi, ni wenye nguvu, na unahitajika.

Rafiki zangu, ninaahidi kwamba tunapojitahidi kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote, kuomba katika jina la Yesu Kristo, kujifunza Kitabu cha Mormoni, na kwa moyo wa sala kupokea sakramenti, tunakuwa na uwezo, kwa nguvu za Bwana, kushinda matendo ya udanganyifu ya adui, kupunguza kuvurugwa kimawazo ambako kunapunguza uwezekano wetu mtakatifu, na kuzuia kukata tamaa ambako kunapunguza uwezo wetu wa kuhisi upendo wa Baba yetu wa Mbinguni na Mwana Wake. Tutakuja kuelewa kikamilifu sisi ni kina nani kama wana na mabinti za Mungu.

Akina kaka na akina dada, ninashiriki nanyi upendo wangu na kutangaza kwenu ushahidi wangu kwamba ninajua Baba wa Mbinguni yu hai na Yesu ndiye Kristo. Ninawapenda Wao. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni ufalme wa Mungu duniani. Tuna kazi takatifu ya kuikusanya Israeli na kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Masiya. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha