Uaminifu Endelevu na Thabiti
Kuamini katika Bwana kunajumuisha kuamini katika muda Wake na kunahitaji subira na uvumilivu ambao unadumu kupita dhoruba za maisha.
Kijana wetu Dan aliugua sana kwenye misheni yake huko Afrika na alipelekwa kwenye hospitali yenye rasilimali chache. Tuliposoma barua yake ya kwanza kwetu baada ya ugonjwa wake, tulitegemea kwamba angekuwa amekata tamaa, lakini badala yake aliandika, “hata nilipokuwa nimelala kwenye chumba cha dharura, nilihisi amani. Sijawahi kamwe kuwa na furaha endelevu na thabiti katika maisha yangu.”
Wakati mimi na mke wangu tuliposoma maneno haya, tulizidiwa na mhemko. Furaha Endelevu na Thabiti. Kamwe hatujawahi kusikia furaha ikielezewa hivyo, lakini maneno yake yalikuwa kweli. Tulijua kwamba furaha aliyoielezea haikuwa starehe tu au sununu iliyoinuliwa bali amani na shangwe ambayo huja tunapojisalimisha kwa Mungu na kuweka uaminifu wetu Kwake katika mambo yote.1 Sisi pia tumekuwa na nyakati hizo katika maisha yetu ambapo Mungu alizungumza amani katika nafsi zetu na kutusababisha tuwe na tumaini katika Kristo hata wakati maisha yalipokuwa magumu na yasiyo na uhakika.2
Lehi anafundisha kwamba kama Adamu na Hawa hawangeanguka, “wangeishi katika hali ya kitoto, bila shangwe, kwani hawakufahamu dhiki; …
“Lakini tazama, vitu vyote vimetendwa kwa hekima ya yule ajuaye vitu vyote.
“Adamu alianguka ili wanadamu wawe; na wanadamu wapo ili wapate shangwe.”3
Katika njia inayoonekana kama kweli, mateso na huzuni hutuandaa kupata uzoefu wa shangwe ikiwa tutaamini katika Bwana na mpango Wake kwa ajili yetu. Ukweli huu unaelezewa vizuri na mshairi wa karne ya 13: “Sorrow prepares you for joy. Kwa nguvu nyingi inafagia kila kitu nje ya nyumba yako, ili kwamba shangwe mpya iweze kupata nafasi ya kuingia. Inatikisa majani ya njano kutoka kwenye tawi la moyo wako, ili kwamba majani mazuri, ya kijani yaweze kukua kwenye nafasi yao. Inachimbua mizizi iliyooza, ili kwamba mizizi mipya iliyojificha pembeni ipate mahala pa kukua. Huzuni yoyote inayotikisa kutoka moyoni mwako, na mambo mazuri yatachukua nafasi yake.”4
Rais Russell M. Nelson alifundisha, “Shangwe ambayo Mwokozi anaitoa [kwetu] … ni ya kudumu, akituhakikishia kwamba ‘mateso yetu yatakuwa kwa muda mfupi’ [Mafundisho na Maagano 121:7] na yatatakaswa kwa ajili yetu.”5 Majaribu yetu na mateso yanaweza kutoa nafasi kwa shangwe kuu.6
Habari njema ya injili si ahadi ya maisha yasiyo na huzuni na masumbuko bali maisha yaliyojaa lengo na maana—maisha ambayo huzuni yetu na mateso yetu yanaweza “kumezwa katika shangwe ya Kristo.”7 Mwokozi alitangaza, “Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”8 Injili Yake ni ujumbe wa matumaini. Huzuni iliyoambatana na tumaini katika Yesu Kristo hubeba ahadi ya shangwe ya kudumu.
Tukio la safari ya Wayaredi kwenda nchi ya ahadi linaweza kutumika kama sitiari ya safari yetu kupitia maisha ya duniani. Bwana alimuahidi kaka wa Yaredi na watu wake kwamba “angetangulia mbele [yao] katika nchi ambayo ni bora kuliko nchi zote duniani.”9 Aliwaamuru kujenga mashua, na kwa utiifu walienda kuzijenga kulingana na maelekezo ya Bwana. Hata hivyo, wakati kazi ikiendelea, kaka wa Yaredi alianza kuwa na wasiwasi kwamba usanifu wa Bwana kwa ajili ya mashua haukua wa kutosheleza. Alilia:
“Ee Bwana, nimefanya kazi ambayo uliniamuru, na nimetengeneza mashua kama vile ulivyoniongoza.
“Na tazama, Ee Bwana, ndani zao hamna mwangaza.”10
“Ee Bwana, utakubali tuvuke haya maji mengi kwenye giza?”11
Je, umewahi kuimimina nafsi yako kwa Mungu kwa njia sawa na hiyo? Unapojitahidi kuishi kama Bwana anavyoamuru na matarajio ya haki hayafikiwi, je, umewahi kujiuliza ikiwa unapaswa kupita maisha haya katika giza?12
Kaka wa Yaredi kisha alielezea haja nyingine kubwa kuhusu uwezo wao wa kuendelea kuishi ndani ya mashua. Alilia, “Na pia tutaangamia, kwani ndani yao hatuwezi kupumua, isipokuwa tu hewa iliyomo ndani yao.13 Je, ugumu wa maisha umewahi kufanya iwe vigumu kwako kupumua na kukufanya ujiulize jinsi unavyoweza kupitisha siku, acha hata kurudi nyumbani kwako mbinguni.
Baada ya Bwana kufanya kazi na kaka wa Yaredi kutatua kila moja ya wasiwasi wake, kisha akaelezea, “Hamuwezi kuvuka hiki kilindi kikubwa isipokuwa niwatayarishie [njia] dhidi ya mawimbi ya bahari, na pepo ambazo zimevuma, na mafuriko ambayo yatakuja.”14
Bwana aliweka wazi kwamba hatimaye Wayaredi wasingefika nchi ya ahadi bila Yeye. Hawakuwa na mamlaka, na njia pekee wangeweza kuvuka kilindi kikubwa ilikuwa ni kuweka uaminifu wao Kwake. Uzoefu huu na mafunzo kutoka kwa Bwana ilionekana kuongeza imani ya kaka wa Yaredi na kuimarisha uaminifu wake katika Bwana.
Gundua jinsi maombi yake yalivyobadilika kutoka kwenye maswali na wasiwasi kuwa madhihirisho ya imani na uaminifu.
“Ninajua, Ee Bwana, kwamba una uwezo wote, na unaweza kufanya chochote upendacho kwa faida ya binadamu; …
“Tazama, Ee Bwana, unaweza kufanya hivi. Tunajua kwamba unaweza kuonesha mbele uwezo wako mkuu, ambao unaonekana mdogo katika macho ya watu.”15
Imeandikwa kwamba Wayaredi kisha “walijipakia kwenye … mashua, na kuanza mwendo kuelekea baharini, wakimtegemea Bwana Mungu wao awalinde.”16 Kutegemea humaanisha kuamini au kujisalimisha. Wayaredi hawakuingia kwenye mashua kwa sababu walijua kwa hakika jinsi ambavyo mambo yangeenda katika safari yao. Walijipakia kwa sababu walikuwa wamejifunza kuamini katika nguvu ya Bwana, wema, na rehema, na hivyo walikuwa radhi kujisalimisha wao na shaka au hofu ambazo wangekuwa nazo kwa Bwana.
Karibuni mjukuu wetu Abe alikuwa anaogopa kupanda wanyama wa carousel ambao huenda chini na juu. Alipendelea mmoja ambaye hatembei. Bibi yake mwishowe alimshawishi kwamba ingekuwa salama, kwa hiyo, akiwamwamini bibi yake, alimpanda. Kisha alisema kwa tabasamu kubwa, “Sihisi salama, lakini niko salama.” Labda hivyo ndivyo Wayaredi walivyohisi. Kumwamini Mungu kunaweza daima kusionekane kuwa salama mwanzoni, lakini shangwe hufuata.
Safari haikuwa rahisi kwa Wayaredi. “Mara nyingi walizikwa chini ya vilindi vya bahari, kwa sababu ya milima ya mawimbi ambayo iliwaangukia.”17 Bado imeandikwa kwamba “upepo haukukoma kamwe [kuwasukuma] kuelekea ile nchi ya ahadi.”18 Jinsi ilivyo vigumu kuelewa, hasa kwenye nyakati katika maisha yetu wakati pepo kinzani zina nguvu na bahari zina ghasia, tunaweza kupata faraja katika kujua kwamba Mungu katika wema Wake usio na mwisho daima anatusukuma kuelekea nyumbani.
Kumbukumbu inaendelea, “walisukumwa mbele; na hakuna mnyama mkubwa wa baharini ambaye angewavunja, wala nyangumi ambaye angewaharibu; na walikuwa na mwangaza daima, hata wakiwa chini ya maji au juu ya maji.”19 Tunaishi katika ulimwengu ambapo mawimbi ya mnyama mkubwa ya kifo, ugonjwa wa mwili na akili, na majaribu na mateso ya kila aina yanatuvunja. Bado, kupitia imani katika Yesu Kristo na kuchagua kumwamini Yeye, sisi pia tunaweza kuwa na mwangaza daima iwe juu ya maji au chini ya maji. Sisi tunaweza kuwa na hakikisho kwamba Mungu kamwe haachi kutusukuma kuelekea nyumbani kwetu mbinguni.
Wakati wakitupwa huko na kule ndani ya mashua, Wayaredi “waliimba nyimbo za sifa kwa Bwana; … na [walimshukuru] na kumsifu Bwana siku yote nzima; na usiku ulipofika, hawakukoma kumsifu Bwana.”20 Walihisi shangwe na kutoa shukrani hata katikati ya mateso yao. Walikuwa bado hawajafika nchi ya ahadi, lakini walikuwa wakishangilia katika baraka zilizoahidiwa kwa sababu ya uaminifu wao endelevu na thabiti Kwake.21
Wayaredi walisukumwa mbele juu ya maji siku 344.22 Je, unaweza kufikiria hilo? Kuamini katika Bwana kunajumuisha kuamini katika muda Wake na kunahitaji subira na uvumilivu ambao unadumu kupita dhoruba za maisha.23
Hatimaye, Wayaredi “walitua kwenye ukingo wa nchi ya ahadi. Na baada ya kuweka miguu yao juu ya ukingo wa nchi ya ahadi walisujudu chini juu ya nchi, na wakajinyenyekeza mbele ya Bwana, na machozi ya shangwe yakatiririka mbele ya Bwana, kwa sababu ya wingi wa wororo wa rehema yake juu yao.”24
Ikiwa tu waaminifu katika kutunza maagano yetu, sisi pia siku moja tutafika salama nyumbani na tutasujudu mbele za Bwana na kutiririsha machozi ya shangwe kwa wingi wa huruma Zake ororo katika maisha yetu, ikijumuisha huzuni ambayo ilitoa nafasi kwa ajili ya shangwe zaidi.25
Ninashuhudia kwamba tunapojiweka kwa Bwana na kwa uaminifu endelevu na thabiti kuamini katika Yesu Kristo na malengo Yake matakatifu katika maisha yetu, Yeye atatutembelea kwa hakikisho, atazungumza amani katika nafsi zetu, na kutusababisha “kutumainia ukombozi wetu kwake.”26
Ninashuhudia kwamba Yesu ndiye Kristo. Yeye Ndiye kiini cha shangwe yote.”27 Neema Yake yatosha, na ni mkuu kuokoa.28 Yeye ni nuru, uzima, na tumaini la ulimwengu.29 Yeye hatatuacha tupotee.30 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.