Amri Mbili Kuu
Lazima tujaribu kutii amri kuu zote mbili. Ili kufanya hivyo tunatembea mstari mwembamba sana kati ya sheria na upendo.
Dada zangu wapendwa katika injili ya Yesu Kristo, ninawasalimu kama wenye jukumu takatifu la malezi ya familia ya milele. Rais Russell M. Nelson ametufundisha, “Kanisa hili lilirejeshwa ili kwamba familia ziweze kuundwa, kuunganishwa, na kuinuliwa milele.”1 Fundisho hilo lina maana muhimu kwa watu ambao hujitambulisha kama msagaji, shoga, mwenye jinsia mbili, au asiyekubali jinsia yake, kwa kawaida wakijulikana kama LGBT.2 Rais Nelson pia ametukumbusha kwamba si “lazima daima tukubaliane na kila mmoja ili kumpenda kila mmoja.”3 Mafundisho haya ya kinabii ni muhimu kwa ajili ya mijadala ya familia ya kujibu maswali ya watoto na vijana. Kwa sala nimetafuta uvuvio wa kuzungumza na umati huu kwa sababu mnaathiriwa kipekee kwa maswali haya, ambayo moja kwa moja au vinginevyo huathiri kila familia katika Kanisa.
I.
Ninaanza na kile Yesu alichofundisha kwamba ni amri mbili kuu.
“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.
“Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.
“Na ya pili yafanana nayo, Mpende jirani yako kama nafsi yako.”4
Hii humaanisha tumeamriwa kumpenda kila mtu, kwani fumbo la Yesu wa Msamaria mwema hufundisha kwamba kila mtu ni jirani yetu.5 Lakini ari yetu ya kutii amri hii ya pili lazima isitusababishe kusahau ya kwanza, kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote, roho na akili. Tunaonesha upendo huo kwa “[kutii] amri [Zake].”6 Mungu anatuhitaji tutii amri Zake kwa sababu ni kwa kupitia tu utii huo, ukijumuisha toba, tunaweza kurudi kuishi katika uwepo Wake na kuwa wakamilifu kama Yeye alivyo.
Katika hutoba yake ya karibuni kwa vijana wakubwa wa Kanisa, Rais Russel M. Nelson alizungumzia kile alichokiita “muunganiko imara kati ya upendo wa Mungu na sheria Zake.”7 Sheria inayohusika kikamilifu zaidi kwenye suala linalohusiana na wale wanaojitambulisha kama LGBT ni sheria ya Mungu ya ndoa na mwenza wake sheria ya usafi wa kimwili. Zote ni muhimu katika mpango wa wokovu wa Baba yetu wa Mbinguni kwa ajili ya watoto Wake. Kama Rais Nelson alivyofundisha, “sheria za Mungu zinapewa motisha kikamilifu kwa upendo Wake usio na mwisho kwetu na hamu Yake kwetu kuwa vyote tunavyoweza kuwa.”8
Rais Nelson alifundisha: “Nchi nyingi … zimerasimisha ndoa ya jinsia moja. Kama waumini wa Kanisa, tunaheshimu sheria za nchi … , ikijumuisha ndoa ya kiserikali. Ukweli ni kwamba, hata hivyo, kwamba hapo mwanzo … ndoa ilitakaswa na Mungu! Na mpaka leo inaamuliwa na Yeye kama kuwa kati ya mwanamume na mwanamke. Mungu bado hajabadili maana Yake ya ndoa.
Rais Nelson aliendelea: “Mungu pia hajabadili sheria Yake ya usafi wa kimwili. Vigezo vya kuingia hekaluni havijabadilika.”9
Rais Nelson alitukumbusha sote kwamba “agizo letu kama Mitume si kufundisha kingine bali ukweli. Agizo hilo halitupatii sisi [Mitume] mamlaka ya kurekebisha sheria takatifu.”10 Hivyo, dada zangu, viongozi wa Kanisa wanapaswa daima kufundisha umuhimu wa kipekee wa ndoa kati ya mwanamume na mwanamke na sheria ya usafi wa kimwili inayohusika.
II.
Kazi ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni kujihusisha kikamilifu na kuwaandaa watoto wa Mungu kwa ajili ya ufalme wa selestia, na zaidi hasa kwa utukufu wake wa juu, kuinuliwa au uzima wa milele. Takdiri hiyo ya juu inawezekana tu kupitia ndoa ya milele.11 Uzima wa milele hujumuisha nguvu za uumbaji zenye asili katika muunganiko wa mwanaume na mwanamke12—kile ambacho ufunuo wa siku hizi unauelezea kama “mwendelezo wa uzao milele na milele.”13
Katika hotuba yake kwa vijana, Rais Nelson alifundisha, “Kuishi kwa sheria za Mungu kutakuweka salama pale unapokua kuelekea hatma ya kuinuliwa.”14—hiyo ni, kuwa kama Mungu, ukiwa na maisha ya kuinuliwa na uwezekano wa kiungu wa Wazazi wetu wa Mbinguni. Hiyo ndiyo takdiri tunayotamani kwa wote tunaowapenda. Kwa sababu ya upendo huo, hatuwezi kuacha upendo wetu uchukue nafasi ya amri na mpango na kazi ya Mungu, ambayo tunajua itawaletea wale tunaowapenda furaha yao kuu.
Lakini kuna wengi tunaowapenda, ikijumuisha baadhi ambao wana injili ya urejesho, ambao hawaamini au wanachagua kutofuata amri za Mungu kuhusu ndoa na sheria ya usafi wa kimwili. Vipi kuhusu wao?
Mafundisho ya Mungu yanaonesha kwamba sisi sote ni watoto Wake na kwamba Ametuumba ili tupate furaha.15 Ufunuo wa siku hizi unafundisha kwamba Mungu ametoa mpango kwa ajili ya uzoefu wa maisha ya duniani ambapo wote wanaweza kuchagua utiifu ili kutafuta baraka Zake za juu au kufanya chaguzi ambazo zinaongoza kwenye mojawapo ya falme za utukufu wa chini.16 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Mungu kwa watoto Wake wote, falme hizo ndogo bado ni za kupendeza kuliko wanadamu wenye kufa wanavyoweza kufikiri.17 Upatanisho wa Yesu Kristo unafanya haya yote yawezekane, kwani Yeye “anamtukuza Baba, na kuokoa kazi zote za mikono yake.”18
III.
Nimezungumza juu ya amri ya kwanza, lakini vipi kuhusu ya pili? Ni kwa jinsi gani tunatii amri ya kuwapenda jirani zetu? Tunatafuta kuwashawishi waumini wetu kwamba wale wanaofuata mafundisho na matendo ya usagaji, ushoga, jinsia mbili, au kutokubali jinsia wanapaswa kuchukuliwa kwa upendo Mwokozi wetu aliotuamuru kuuonesha kwa jirani zetu wote. Hivyo, wakati ndoa ya jinsia moja ilipotangazwa kuwa halali huko Marekani, Urais wa Kwanza na Akidi ya Kumi na Wawili walitangaza: “Injili ya Yesu Kristo hutufundisha kuwapenda na kuwatendea watu wote kwa ukarimu na ustaarabu—hata wakati tunapokuwa hatukubaliani. Tunathibitisha kwamba wale wanaojileta kwenye sheria au mamlaka ya mahakama kuruhusu ndoa ya jinsia moja hawapaswi kuvunjiwa heshima.”19
Zaidi, hatupaswi kuwatesa wale ambao hawashiriki imani na misimamo yetu.20 Kwa majuto, baadhi ya watu wanaokumbana na maswala haya wanaendelea kuhisi waliotengwa na kukataliwa na baadhi ya waumini na viongozi katika familia, kata na vigingi vyetu. Lazima sote tujitahidi kuwa wakarimu zaidi na wastaarabu zaidi.
IV.
Kwa makusudi fulani hatuelewi, kwamba tuna changamoto tofauti katika uzoefu wetu wa maisha haya. Lakini tunajua kwamba Mungu atamsaidia kila mmoja wetu kushinda changamoto hizi ikiwa kwa dhati tunatafuta msaada Wake. Baada ya kuteseka na kutubu kwa kwenda kinyume na sheria tulizofundishwa, sote tunapewa takdiri kwa ajili ya ufalme wa utukufu. Hukumu kuu na ya mwisho itafanywa na Bwana, ambaye pekee ana ufahamu, hekima, na neema inayohitajika kumhukumu kila mmoja wetu.
Kwa sasa, lazima tujaribu kutii amri kuu zote mbili. Ili kufanya hivyo tunatembea mstari mwembamba sana kati ya sheria na upendo—kutii amri na kutembea njia ya agano, wakati tukiwapenda jirani zetu tukiwa njiani. Safari hii inatuhitaji kutafuta uvuvio wa kiungu juu ya nini cha kuunga mkono na cha kupinga na jinsi ya kupenda na kusikiliza kwa utiifu na kufundisha katika mchakato huo. Safari yetu inahitaji kwamba tusilegeze kamba juu ya amri bali tuoneshe kipimo kikamilifu cha uelewa na upendo. Safari yetu lazima iwafikirie watoto ambao hawana uhakika na maelekezo ya jinsia zao, lakini inapinga kubandikana majina kwa sababu, kwa watoto wengi, kutokuwa na uhakika huko kunapungua umuhimu kadiri muda unavyoenda.21 Safari yetu hupinga kuasajiliwa nje ya njia ya agano, na hukataa kuunga mkono yeyote anayeongoza watu mbali kutoka kwa Bwana. Katika hili lote tunakumbuka kwamba Mungu anaahidi tumaini na furaha na baraka kuu kwa wote wanaotii amri Zake.
V.
Akina mama na akina baba na kila mmoja wetu tunawajibika kufundisha amri kuu zote mbili. Kwa wanawake wa Kanisa, Rais Spencer W. Kimball alielezea wajibu huo katika unabii huu mkuu: “Wingi wa ukuaji mkubwa ambao unakuja kwenye Kanisa katika siku za mwisho utakuja kwa sababu wengi wa wanawake wema wa ulimwengu … watavutwa kuja Kanisani kwa idadi kubwa. Hii itatokea kwa kiasi kwamba wanawake wa Kanisa wataonesha uadilifu na ufasaha katika maisha yao na kwa kiasi kwamba wanawake wa Kanisa wanaonekana wa kipekee na tofauti … tofauti na wanawake wa ulimwengu. … Hivyo itakuwa kwamba mifano ya wanawake wa Kanisa itakuwa nguvu kubwa katika ukuaji wa idadi na kiroho wa Kanisa katika siku za mwisho.”22
Akizungumza kuhusu unabii huo, Rais Russell M. Nelson alitangaza kwamba “siku ile Rais Kimball aliyoiona ni leo. Ninyi ndiyo wanawake aliowaona!”23 Kidogo kiasi gani sisi ambao tulisikia unabii ule miaka 40 iliyopita tulitambua kwamba kati ya hao ambao wanawake wa Kanisa hili wanaweza kuwaokoa wangekuwa rafiki zao wapendwa na familia zao ambao kwa sasa wanashawishiwa na vipaumbele vya ulimwengu na uharibifu wa kishetani. Ombi na baraka yangu ni kwamba mtafundisha na kutenda ili kutimiza unabii huo, katika jina la Yesu Kristo, amina.