2010–2019
Shangwe ya Watakatifu
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


Shangwe ya Watakatifu

Shangwe huja kwa kutii amri za Kristo, kwa kushinda huzuni na udhaifu kupitia Yeye, na kwa kuhudumu jinsi Yeye alivyohudumu.

Nabii Enoshi wa Kitabu cha Mormoni, mjukuu wa Lehi, aliandika uzoefu mmoja ambao ulitokea mwanzoni mwa maisha yake. Akiwa anawinda peke yake msituni, Enoshi alianza kutafakari mafundisho ya baba yake, Yakobo. Alielezea, “Maneno ambayo nilikuwa nimezoea kumsikia baba yangu akizungumza kuhusu uzima wa milele, na shangwe ya watakatifu, yakapenya ndani ya moyo wangu.”1 Katika njaa ya kiroho ya nafsi yake, Enoshi alipiga magoti kusali, sala ya ajabu ambayo ilidumu siku nzima mchana na usiku, sala iliyomletea ufunuo muhimu, hakikisho, na ahadi.

Kuna mengi tunayoweza kujifunza kutoka kwenye uzoefu wa Enoshi, lakini leo kinachokuja kwenye fikra zangu ni kumbukumbu ya Enoshi ya baba yake akizungumza mara nyingi juu ya “shangwe ya watakatifu.”

Katika mkutano huu miaka mitatu iliyopita, Rais Russell M. Nelson alizungumza kuhusu shangwe.2 Miongoni mwa vitu vingine alisema:

“Shangwe tunayohisi inahusiana kwa kiasi kidogo na hali za maisha yetu na inahusiana na kila kitu na fokasi ya maisha yetu.

“Wakati fokasi ya maisha yetu ipo katika mpango wa Mungu wa wokovu … na Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kuhisi shangwe bila kujali nini kinatokea—au hakitokei—katika maisha yetu. Shangwe huja kutoka Kwake na kwa sababu Yake. … Kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho, Yesu Kristo ni shangwe!”3

Watakatifu ni wale walioingia kwenye maagano ya injili kwa njia ya ubatizo na wanajitahidi kumfuata Kristo kama wafuasi Wake.4 Hivyo, “shangwe ya watakatifu” inaashiria shangwe ya kuwa kama Kristo.

Ningependa kuzungumzia shangwe ambayo huja kwa kutii amri Zake, shangwe ambayo huja kwa kushinda huzuni na udhaifu kupitia Yeye, na shangwe ya asili katika kutumikia jinsi Yeye alivyotumikia.

Shangwe ya kutii Amri za Kristo.

Tunaishi katika zama za maisha ya anasa wakati wengi wanahoji umuhimu wa amri za Bwana au kuamua tu kuziachilia mbali. Si mara chache, watu wanaokiuka maagizo ya kimungu kama sheria ya usafi wa kimwili, kiwango cha uaminifu, na utakatifu wa Sabato wanaonekana kufanikiwa na kufurahia vitu vizuri vya maisha, wakati mwingine zaidi hata ya wale ambao wanaojitahidi kutii. Wengine huanza kujiuliza ikiwa juhudi na dhabihu zinafaa. Watu wa kale wa Israeli walilalamika:

“Kumtumikia Mungu hakuna faida: na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi?

“Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.”5

Subiri, asema Bwana, hadi “katika siku ile niifanyayo hazina yangu. … Ndipo mtapambanua … kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia.”6 Waovu wanaweza “kuwa na shangwe katika matendo yao kwa kipindi fulani,” lakini mara nyingi ni ya muda.7 Furaha ya Watakatifu ni ya kudumu.

Mungu huona vitu kwa mtazamo wake wa kweli, na Yeye anashiriki mtazamo huo pamoja nasi kupitia amri zake, akituongoza vyema kuzunguka mashimo na makorongo ya maisha haya kuelekea shangwe ya milele. Nabii Joseph Smith alielezea: “Wakati amri Zake zinatufundisha, ni katika mtazamo wa umilele; kwa maana tunatazamwa na Mungu kana kwamba tulikuwa katika umilele; Mungu hukaa katika umilele, na hatazami vitu jinsi sisi tunavyotazama.”8

Sijakutana na mtu yeyote ambaye alipata injili baadaye katika maisha ambaye hakutamani ingekuwa mapema. “Oo, chaguzi mbaya na makosa ningeweza kuyazuia,” watasema. Amri za Bwana ni mwongozo wetu kwa chaguzi nzuri na matokeo ya furaha. Jinsi gani tunapaswa kufurahi na kumshukuru Yeye kwa kutuonesha njia hii nzuri zaidi.

Picha
Dada Kamwanya

Kama kijana, Dada Kalombo Rosette Kamwanya kutoka D.R. Kongo, sasa akihudumu katika Misheni ya Cote d’Ivoire Abidjan Magharibi, alifunga na kuomba kwa siku tatu ili kupata mwelekeo ambao Mungu alimtaka achukue. Katika ono la ajabu la usiku, alioneshwa majengo mawili, kanisa na kile anachotambua sasa kilikuwa hekalu. Alianza kutafuta na punde alipata kanisa aliloliona katika ndoto yake. Kibao kilisema, “Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.” Dada Kamwanya alibatizwa na kisha mama yake na kaka zake sita. Dada Kamwanya alisema, “Nilipoipokea injili, nilijihisi kama ndege aliyenaswa ambaye alikuwa ameachiliwa. Moyo wangu ulijawa na shangwe … Nilipata uhakika kwamba Mungu ananipenda.”9

Kutii amri za Bwana kunatuwezesha kikamilifu na kwa urahisi zaidi kuhisi upendo Wake. Njia nyembamba na iliyosonga ya amri huongoza moja kwa moja kwenye mti wa uzima, na mti na tunda lake, tamu na “la kupendeza zaidi ya vitu vyote,”10 ni mfano wa upendo wa Mungu na hujaza nafsi “kwa shangwe tele.”11 Mwokozi alisema:

“Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.

“Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.”12

Shangwe ya Kushinda kupitia Kristo

Hata wakati tunapotii amri kwa uaminifu, kuna majaribu na majanga ambayo yanaweza kuingilia shangwe yetu. Lakini tunapojitahidi kushinda changamoto hizi kwa usaidizi wa Mwokozi, inahifadhi vyote shangwe tunayohisi sasa na shangwe tunayoitarajia. Kristo aliwahakikishia wafuasi Wake, “Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”13 Ni kwa kumgeukia Yeye, kumtii Yeye, kujitoa kwetu Kwake kwamba majaribu na huzuni hugeuzwa kuwa shangwe. Ninataja mfano mmoja.

Mwaka 1989, Jack Rushton alikuwa akihudumu kama rais wa Kigingi cha Irvine California huko Marekani. Wakati wa likizo ya familia kwenye pwani ya California, Jack alikuwa akileleza majini wakati wimbi lilipomzamisha kwenye mwamba, kuvunja shingo yake na kujeruhi vibaya uti wake wa mgongo. Jack baadaye alisema, “Mara nilipojigonga, nilijua nimepooza.”14 Asingeweza tena kuzungumza au hata kupumua mwenyewe.15

Picha
Familia na marafiki wakiwasaidia akina Rushton

Familia, marafiki, na washiriki wa kigingi waliungana na Kaka Rushton na mke wake, Jo Anne, na, miongoni mwa mambo mengine, walirekebisha sehemu ya nyumba yao kuwezesha kiti cha magurudumu cha Jack kupita. Jo Anne akawa mtoa huduma mkuu wa Jack kwa miaka 23 iliyofuata. Akirejelea matukio ya Kitabu cha Mormoni ya jinsi Bwana alivyowatembelea watu wake katika mateso yao na kufanya mizigo yao kuwa miepesi,16 Jo Anne alisema, “mara nyingi nashangazwa katika wepesi wa moyo ambao ninahisi katika kumtunza mume wangu.”17

Picha
Jack na Jo Anne Rushton

Mabadiliko kwenye mfumo wake wa upumuaji yalirejesha uwezo wa Jack wa kuzungumza, na ndani ya mwaka, Jack aliitwa kama mwalimu wa Mafundisho ya Injili na Baba Mkuu wa kigingi. Wakati ambapo angetoa baraka ya baba mkuu, mwenye ukuhani mwingine aliweka mkono wa Kaka Rushton juu ya kichwa cha mtu anayepokea baraka na kuushikilia mkono wake na kiganja chake wakati wa baraka. Jack alifariki Siku ya Krismasi mwaka 2012, baada ya miaka 22 ya huduma ya uaminifu.

Picha
Jack Rushton

Wakati mmoja akiwa kwenye mahojiano, Jack alitoa angalizo: “Matatizo yatakuja katika maisha yetu yote; ni sehemu tu ya kuwa hapa duniani. Na watu wengine wanafikiri kwamba dini au kuwa na imani katika Mungu kutakulinda wewe kutokana na mambo mabaya. Sidhani kama hiyo ni hoja. Nadhani hoja ni kwamba kama imani yetu ni imara, kwamba wakati mambo mabaya yanatokea, ambayo yatatokea, tutaweza kukabiliana nayo. … Imani yangu kamwe haikutikisika, lakini hilo halina maana kwamba sikuwa na msongo. Nadhani kwa mara ya kwanza katika maisha yangu, nilikuwa nimesukumwa mpaka kwenye kikomo, na kwa kweli kulikuwa hakuna mahali pa kugeukia, na hivyo nilimgeukia Bwana, na hadi leo, ninahisi wingi wa shangwe.”18

Hii ni siku ambayo wakati mwingine mashambulizi yasiyo na huruma katika mitandao ya kijamii na kutoka kwa mtu dhidi ya wale wanaotafuta kuonesha kiwango cha Bwana katika mavazi, burudani, na usafi wa kimwili. Mara nyingi ni vijana wadogo na vijana wakubwa miongoni mwa Watakatifu, pamoja na wanawake na akina mama, ambao wanabeba msalaba huu wa dhihaka na mateso. Si rahisi kuinuka juu ya udhalimu huo, lakini Kumbuka maneno ya Petro: “Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo, ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia: kwa upande wao alinenwa mabaya, bali kwa upande wenu ametukuzwa.”19

Katika Bustani ya Edeni, Adamu na Hawa walikuwa ”katika hali ya kitoto, bila shangwe, kwani hawakufahamu dhiki.”20 Sasa, kama viumbe wanaowajibika, tunapata shangwe katika kushinda huzuni ya aina yoyote, iwe ni dhambi, jaribu, udhaifu, au kikwazo kingine chochote kwenye furaha. Hii ndiyo shangwe ya kuhisi maendeleo katika njia ya ufuasi; shangwe ya “kupokea msamaha wa … dhambi, na kupata amani katika dhamira”;21 shangwe ya kuhisi nafsi ya mtu ikipanuka na kukua kupitia neema ya Kristo.22

Shangwe ya Kutumika kama Kristo Anavyotumika

Mwokozi anapata shangwe katika kuleta kutokufa kwetu na uzima wa milele.23 Katika kuzungumzia Upatanisho wa Mwokozi, Rais Russell M. Nelson alisema:

“Jinsi ilivyo katika vitu vyote, Yesu Kristo ni mfano wetu wa mwisho, ‘ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba’ [Waebrania 12:2]. Fikiria hayo! Ili Yeye aweze kuvumilia uzoefu wa kuteseka uliowahi kuvumiliwa duniani, Mwokozi wetu alifokasi kwenye shangwe!

“Na nini ilikuwa shangwe ambayo iliwekwa mbele Yake? Hakika ilijumuisha shangwe ya kutusafisha, kutuponya, na kutuimarisha; shangwe ya kulipia dhambi za wote watakaotubu; shangwe ya kutuwezesha mimi na wewe kurudi nyumbani—safi na wenye kustahili—kuishi na Wazazi wetu wa Mbinguni na familia zetu za Mbinguni.”24

Vile vile, shangwe “iliyowekwa mbele yetu” ni shangwe ya kumsaidia Mwokozi katika kazi Yake ya ukombozi. Kama uzao na watoto wa Ibrahimu,25 tunashiriki katika kubariki familia zote za duniani “kwa baraka za Injili, ambazo ni baraka za wokovu, hata za uzima wa milele.”26

Maneno ya Alma yanakuja akilini:

“Hii ni furaha yangu, kwamba labda niwe chombo kwenye mikono ya Mungu kuleta roho moja kwa toba; na hii ndiyo shangwe yangu.

Na tazama, ninapoona wengi wa ndugu zangu wametubu kweli, na kumkubali Bwana Mungu wao, ndipo moyo wangu hujaa na shangwe. …

“Lakini mimi sijawi shangwe tu kwa kufanikiwa kwangu pekee, lakini shangwe yangu imejaa zaidi kwa sababu ya kufanikiwa kwa ndugu zangu, ambao wamekuwa kwenye nchi ya Nefi. …

“Sasa, ninapofikiria mafanikio ya hawa ndugu zangu roho yangu inabebwa, hata kama imetenganishwa kutoka kwa mwili, vile ilikuwa, kwani shangwe yangu ni kubwa sana.”27

Matunda ya huduma yetu kila mmoja kwa mwingine katika Kanisa ni sehemu ya shangwe “iliyowekwa mbele yetu.” Hata katika nyakati za kuvunjika moyo au dhiki, tunaweza kuhudumu kwa uvumilivu kama tumefokasi kwenye shangwe ya kumpendeza Mungu na kuleta nuru, faraja, na furaha kwa watoto Wake, kaka na dada zetu.

Wakati nikiwa nchini Haiti mwezi uliopita kwa ajili ya kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Port-au-Prince, Mzee David na Dada Susan Bednar walikutana na dada kijana ambaye mume wake alikuwa ameuawa siku chache kabla katika ajali ya kutisha. Walilia pamoja naye. Hata hivyo siku ya Jumapili mwanamke huyu mpendwa alikuwa mahali pake kama mhudumu wa kukaribisha katika huduma za uwekaji wakfu, akiwa na tabasamu la ukarimu kwa wote walioingia hekaluni.

Ninaamini kuwa “shangwe ya watakatifu” inakuja kwa kujua kuwa Mwokozi anatetea teto lao,28 “na hakuna yeyote ambaye anaweza kuona shangwe [itakayojaza] nafsi zetu [wakati] [tunapomsikia Yesu] akituombea kwa Baba.29 Pamoja na Rais Russell M. Nelson, ninashuhudia kwamba shangwe ni karama kwa Watakatifu waaminifu “ambao wamevumilia misalaba ya ulimwengu”30 na ambao “kwa makusudi wanajaribu kuishi maisha mema, kama ilivyofundishwa na Yesu Kristo.”31 Shangwe yenu na iwe timilifu, ninaomba katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha