2010–2019
Kujitwika Msalaba Wetu
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


2:3

Kujitwika Msalaba Wetu

Kujichukulia juu yenu misalaba yenu na kumfuata Mwokozi humaanisha kuendelea kwa imani kwenye njia ya Mwokozi na kutojiingiza katika tabia za kidunia.

Wapendwa akina kaka na akina dada, tumepokea mafundisho ya kupendeza kutoka kwa viongozi wetu kwa kipindi cha siku hizi mbili zilizopita. Ninashuhudia kwenu kwamba ikiwa tutajitahidi kutumia mafundisho haya yenye msukumo na ya wakati wa kufaa katika maisha yetu, Bwana, kupitia neema yake, atatusaidia kila mmoja wetu kubeba msalaba wetu na kuifanya miepesi mizigo yetu.1

Akiwa ujirani na Kaisaria Filipi, Mwokozi alifunua kwa wanafunzi Wake kile ambacho angeteseka mikononi mwa wazee, wa makuhani wakuu, na waandishi huko Yerusalemu. Aliwafundisha mahususi kuhusu kifo Chake na Ufufuo Wake mtukufu.2 Kwa wakati ule, wanafunzi Wake hawakuelewa kikamilifu wito Wake mtakatifu duniani. Petro mwenyewe, wakati aliposikia kile Mwokozi alichosema, alimvuta kando na kumkemea, akisema, “Hasha, Bwana: hayo hayatakupata.”3

Ili kuwasaidia wanafunzi Wake kuelewa kwamba uaminifu kwenye kazi Yake unajumuisha kujishusha na kuteseka, Mwokozi alitangaza waziwazi:

“Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.

“Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza: na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataipata.

“Kwani atafaidiwa nini mtu, akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?”4

Kupitia tangazo hili, Mwokozi alisisitiza kwamba wale wote walio tayari kumfuata Yeye wanahitaji kujikana na kuzuia tamaa zao, hamu, na matamanio, wakitoa dhabihu kila kitu, hata maisha ikiwa itahitajika, wakiwa wamejinyenyekeza kabisa kwenye mapenzi ya Baba—kama vile Yeye alivyofanya.5 Hii ni, kwa kweli, gharama inayotakiwa kulipwa kwa ajili ya wokovu wa nafsi. Yesu kwa lengo maalumu na kisitiari alitumia alama ya msalaba kuwasaidia wanafunzi Wake kuelewa vyema kile ambacho dhabihu na uaminifu kwa kusudi la Bwana ingemaanisha. Picha ya msalaba ilijulikana vyema kati ya wanafunzi Wake na wakazi wa Himaya ya Rumi kwa sababu Warumi waliwalazimisha wahanga wa kusulubiwa kubeba msalaba wao au boriti la msalaba hadharani kwenda mahali ambapo mauaji yao yangetokea.6

Ilikuwa ni baada ya Ufufuko wa Mwokozi kwamba akili za wanafunzi zilifunguliwa kuelewa yote yaliyokuwa yameandikwa kumhusu Yeye7 na kile ambacho kingehitajika kwao tangu wakati ule na kuendelea.8

Kwa namna hiyo hiyo, sisi sote, akina kaka na akina dada, tunahitaji kufungua mioyo yetu na akili zetu ili kuelewa kikamilifu zaidi uhusiano wa kujichukulia juu yetu misalaba yetu na kumfuata Yeye. Tunajifunza kupitia maandiko kwamba wale wanaotamani kujichukulia juu yao msalaba wao wanampenda Yesu Kristo kiasi kwamba wanajinyima ubaya wote na kila tamaa ya ulimwengu na kutii amri Zake.9

Azimio letu kutupilia mbali yote ambayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu na kutoa dhabihu vyote tunavyoombwa kutoa na kujitahidi kufuata mafundisho Yake kutatusaidia kustahimili kwenye njia ya injili ya Yesu Kristo—hata mbele ya dhiki, udhaifu wa nafsi zetu, au shinikizo la kijamii na falsafa za ulimwengu ambazo ni kinyume na mafundisho Yake.

Kwa mfano, kwa wale ambao bado hawajapata mwenza wa milele na wanaweza kuwa wanahisi upweke na kukosa tumaini, au kwa wale waliopata talaka na kuhisi kutengwa na kusahaulika, ninawahakikishia kwamba kukubali mwaliko wa Mwokozi wa kujichukulia juu yenu misalaba yenu na kumfuata humaanisha kuendelea kwa imani katika njia ya Bwana, kuendeleza mpangilio wa heshima, na kutojiingiza katika tabia za kiulimwengu ambazo hatimaye zitaondoa tumaini letu katika upendo na rehema za Mungu.

Kanuni hiyo hiyo inahusika kwa wale kati yenu ambao mnapitia mvuto wa jinsia moja na kuhisi kukata tamaa na kutosaidika. Na pengine kwa sababu hii baadhi yenu mnahisi kwamba injili ya Yesu Kristo siyo kwa ajili yenu tena. Ikiwa ni hivyo, ninataka kuwahakikishia kwamba daima kuna tumaini katika Mungu Baba na katika mpango Wake wa furaha, katika Yesu Kristo na dhabihu Yake ya upatanisho, na katika kuishi amri Zao zenye upendo. Katika hekima Yake, nguvu, haki na rehema kamilifu, Bwana anaweza kutuunganisha kuwa Wake, kwamba tuweze kuletwa kwenye uwepo Wake na kupata wokovu wa milele, ikiwa tutakuwa imara na wasiotikisika katika kutii amri10 na daima kuenenda katika kazi njema.11

Kwa wale waliofanya dhambi nzito, kukubali mwaliko sawa na huu humaanisha, kati ya mambo mengine, kujinyenyekeza mbele za Mungu, kushauriana na viongozi husika wa Kanisa, na kutubu na kuacha dhambi zako. Mchakato huu pia utawabariki wote wanaopigana dhidi ya uraibu wa kudhoofisha, ikijumuisha madawa ya kulevya, pombe, na ponografia. Kuchukua hatua hizi kunakuleta karibu na Mwokozi, ambaye hatimaye anaweza kukuweka huru kutokana na hatia, huzuni, na utumwa wa kiroho na kimwili. Kwa kuongezea, unaweza pia kutamani kutafuta msaada wa familia, rafiki zako, na wataalamu wa tiba na ushauri.

Tafadhali usikate tamaa baada ya kushindwa kunaofuatia na kujifikiria kama asiyeweza kuacha dhambi na kushinda uraibu. Hutaweza kuvumilia kuacha kujaribu na baadaye kuendelea katika udhaifu na dhambi! Daima jitahidi kufanya kwa uwezo wako wote, ukionesha kupitia matendo yako hamu ya kusafisha chombo cha ndani, kama ilivyofundishwa na Mwokozi.12 Wakati mwingine suluhisho kwa baadhi ya changamoto huja baada ya miezi mingi ya juhudi endelevu. Ahadi inayopatikana katika Kitabu cha Mormoni kwamba “ni kwa neema kwamba tunaokolewa, baada ya kutenda yote tunayoweza,”13 inahusika katika hali hizi. Tafadhali kumbuka kwamba zawadi ya Mwokozi ya neema “si lazima iwe na kikomo cha muda kwenye ‘baada’ ya kutenda yote tunayoweza. Tunaweza kupokea neema Yake kabla, wakati, na baada ya muda wakati tunapotumia juhudi zetu wenyewe.”14

Ninashuhudia kwamba tunapojitahidi daima kushinda changamoto zetu, Mungu atatubariki kwa baraka za imani ya kuponywa na za kutendeka kwa miujiza.15 Atafanya kwa ajili yetu kile ambacho hatuna uwezo wa kukifanya wenyewe.

Kwa kuongezea, kwa wale wanaohisi uchungu, hasira, kuchukizwa, au kufungwa kwenye huzuni kwa kitu unachohisi hukustahili, kujitwika msalaba na kumfuata Mwokozi humaanisha kujitahidi kuweka kando hisia hizi na kumgeukia Bwana ili aweze kutuweka huru kutokana na hali hii ya akili na kutusaidia kupata amani. Kwa bahati mbaya, kama tuking’ang’ania hisia hizi hasi, tunaweza kujikuta tukiishi bila ushawishi wa Roho wa Bwana katika maisha yetu. Hatuwezi kutubu kwa ajili ya watu wengine, lakini tunaweza kuwasamehe—kwa kukataa kushikiliwa mateka na wale waliotudhuru.16

Maandiko yanafundisha kwamba kuna suluhisho kwa hali hizi—kwa kumwalika Mwokozi wetu kutusaidia kubadili mioyo yetu ya mawe kwa mioyo mipya.17 Kwa hili kutokea, tunahitaji kuja kwa Bwana tukiwa na udhaifu wetu18 na kutafuta usaidizi na msamaha Wake,19 hasa kipindi cha wakati mtakatifu ambapo tunapokea sakramenti kila Jumapili. Acha tuchague kutafuta msamaha Wake na kupiga hatua muhimu na ngumu kwa kuwasamehe wale ambao wametuumiza ili kwamba majeraha yetu yaweze kuanza kupona. Ninawaahidi kwamba kwa kufanya kwenu hivyo, usiku wenu utajazwa na faraja ambayo huja kutokana na akili iliyotulia kwa Bwana.

Akiwa ndani ya Jela ya Liberty mnamo 1839, Nabii Joseph Smith aliandika waraka kwa waumini wa Kanisa uliokuwa na unabii ambao una matumizi makubwa katika mazingira na hali hizi. Aliandika, “Enzi zote na tawala, himaya na nguvu, zitafunuliwa na kuwekwa juu ya wote ambao wamestahimili kwa ujasiri mkubwa kwa ajili ya injili ya Yesu Kristo.”20 Kwa hiyo, wapendwa akina kaka na akina dada, wale ambao wamejichukulia juu yao jina la Mwokozi, wakiamini katika ahadi Zake na kuvumilia hadi mwisho, wataokolewa21 na wataishi na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho.22

Sote tunapata hali zisizofaa katika maisha yetu ambazo hutufanya tuhisi huzuni, bila msaada, bila tumaini, na wakati mwingine kudhoofishwa. Baadhi ya hisia hizi zinaweza kutuongoza kumuuliza Bwana: “Kwa nini ninapitia hali hizi?” au “Kwa nini matarajio yangu hayafikiwi? Hata hivyo, ninafanya kila kitu kwa uwezo wangu kubeba msalaba wangu na kumfuata Mwokozi!”

Rafiki zangu wapendwa, lazima tukumbuke kwamba kujichukulia juu yetu msalaba wetu hujumuisha kuwa mnyenyekevu na kumwamini Mungu na katika hekima Yake isiyo na mwisho. Lazima tutambue kwamba Yeye anamjua kila mmoja wetu na mahitaji yetu. Ni muhimu pia kukubali ukweli kwamba wakati wa Bwana ni tofauti na wetu. Wakati mwingine tunatafuta baraka na kuweka kikomo cha muda kwa Bwana kuitimiza. Hatuwezi kuwekea masharti uaminifu wetu Kwake kwa kumuwekea kikomo cha muda kwa majibu ya matamanio yetu. Tunapofanya hivi, tunafanana na Wanefi wenye kushuku kutoka nyakati za kale, ambao waliwafanyia mzaha ndugu zao kwa kusema kwamba muda ulikuwa umepita kwa utimizwaji wa maneno yaliyozungumzwa na Samweli Mlamani, wakileta mkanganyiko kati ya wale walioamini.23 Tunahitaji kumwamini Bwana vya kutosha kutulia na kujua kwamba Yeye ni Mungu, kwamba Anajua vitu vyote, na kwamba Anamjua kila mmoja wetu.24

Mzee Soares akimhudumia Dada Calamassi

Nilipata nafasi hivi karibuni kumhudumia dada mjane aliyeitwa Franca Calamassi, ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa kudhoofisha. Dada Calamassi alikuwa mtu wa kwanza wa familia yake kujiunga na Kanisa la urejesho la Yesu Kristo. Japokuwa mumewe hakuwahi kamwe kubatizwa, alikubali kukutana na wamisionari na mara kadhaa kuhudhuria mikutano ya Kanisa. Licha ya hali hizi, Dada Calamassi alibaki mwaminifu na kuwalea watoto wake wanne katika injili ya Yesu Kristo. Mwaka mmoja kufuatia kifo cha mumewe, Dada Calamassi aliwapeleka watoto wake hekaluni, na walishiriki kwenye ibada takatifu na waliunganishwa pamoja kama familia. Ahadi zilizounganika na ibada hizi zilimletea tumaini kubwa, shangwe na furaha kuu ambayo ilimsaidia kuendelea na maisha.

Familia ya Calamassi hekaluni

Wakati dalili za mwanzo za ugonjwa zilipoanza kuonekana, askofu wake alimpa baraka. Wakati ule alimwambia askofu wake kwamba alikuwa tayari kukubali mapenzi ya Bwana, akionesha imani yake ya kuponywa vilevile imani yake ya kuvumilia ugonjwa wake hadi mwisho.

Wakati wa matembezi yangu, nikiwa nimeshikilia mkono wa dada Calamassi na kutazama machoni mwake, niliona mng’aro wa kimalaika ukitokea kwenye uso wake—ukiashiria ujasiri wake katika mpango wa Mungu na mng’aro wake wa tumaini katika upendo na mpango wa Baba kwa ajili yake.25 Nilihisi ushupavu wake imara wa kuvumilia katika imani yake hadi mwisho kwa kujitwika msalaba wake, licha ya changamoto alizokuwa akipitia. Maisha ya dada huyu ni ushuhuda wa Kristo, maelezo ya imani yake na uaminifu Kwake.

Akina kaka na akina dada, ninashuhudia kwenu kwamba kujitwika msalaba wetu na kumfuata Mwokozi kunatuhitaji tufuate mfano Wake na kujitahidi kuwa kama Yeye,26 kwa subira tukikabiliana na hali za maisha, tukikana na kuchukia tamaa za mwanadamu wa tabia ya asili, na kusubiri kwa Bwana. Mwandishi wa Zaburi aliandika:

“Umngoje Bwana: uwe jasiri, upige moyo konde: naam, umngoje Bwana.”27

“Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.”28

Ninashuhudia kwenu kwamba kwa kufuata nyayo za Bwana wetu na kumngoja Yeye ambaye ni mponyaji mkuu wa maisha yetu kutatupatia pumziko la nafsi zetu na kufanya mizigo yetu rahisi na miepesi.29 Kwa mambo haya ninashuhudia katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.