Uwezo wa Kiroho
Kama mfuasi mwaminifu wa Yesu Kristo, unaweza kupokea uvuvio na ufunuo binafsi, unaokubaliana na amri Zake, ambao umetolewa kwa ajili yako.
Nilipokuwa nikitoka kwenye kambi ya Wasichana majira haya ya joto, msichana mzuri alinipatia ujumbe mfupi kwenye karatasi. Ndani yake, aliuliza, “Nawezaje kujua wakati Mungu anajaribu kuniambia kitu fulani?” Napenda swali lake. Nafsi zetu zinatamani uhusiano na nyumbani kwetu mbinguni. Tunataka kuhisi tunahitajika na wenye maana. Lakini wakati mwingine tunapata wakati mgumu kutofautisha kati ya mawazo yetu wenyewe na ushawishi mtulivu wa Roho. Manabii, wa zamani na wa sasa, wamefundisha kwamba kama kitu “kinaalika na kushawishi kufanya mema, kinatoka kwa Kristo.”1
Rais Russell M. Nelson ametoa mwaliko rahisi, wenye nguvu: “Wapendwa akina kaka na dada zangu, ninawasihi muongeze uwezo wenu wa kiroho wa kupokea ufunuo. … Chagua kufanya kazi ya kiroho inayohitajika ili kufurahia karama za Roho Mtakatifu na kuisikia sauti ya Roho mara kwa mara na kwa uwazi zaidi.”2
Hamu yangu asubuhi ya leo ni kuzungumza nanyi kutoka kwenye moyo wangu kuhusu njia nne za kuongeza uwezo wenu wa kiroho wa kupokea ufunuo.
1. Kuwa na Nia kuhusu Kutenga Muda na Mahali pa Kuisikia Sauti ya Mungu?
Unapotumia haki yako ya kujiamulia kutenga muda kila siku ili kuikaribia sauti ya Mungu, hasa katika Kitabu cha Mormoni, baada ya muda, Sauti Yake itakuwa dhahiri zaidi na yenye kujulikana vyema kwako.
Kinyume na hilo, vivuta mawazo na kelele ambazo zinajaza ulimwengu na nyumba zetu na maisha yetu vinaweza kufanya iwe vigumu kuisikia sauti Yake. Vivuta mawazo hivi vinaweza kutawala akili na mioyo yetu hadi tukakosa nafasi kwa ajili ya misukumo tulivu ya Roho Mtakatifu.
Nabii Joseph Smith alifundisha kwamba mara nyingi Mungu hujifunua Mwenyewe “kwa watu binafsi faraghani, katika vyumba vyao; nyikani au mashambani, na kwa kawaida bila kelele au msukosuko.”3
Shetani anataka kututenganisha na sauti ya Mungu kwa kutufanya tusiwe katika sehemu hizo tulivu. Kama Mungu huzungumza kwa sauti ndogo, tulivu, wewe na mimi tunahitaji kukaribia ili tuweze Kumsikia. Hebu fikiria kile ambacho kingetokea kama tungelikuwa na nia ya kuwa na muunganiko na mbingu jinsi ambavyo tunashinda tumeunganishwa kwenye Wi-Fi! Chagua muda na mahala, na uisikilize sauti ya Mungu kila siku. Na tunza miadi hii takatifu kwa utiifu mkamilifu, kwa maana mengi mno yanategemea hilo!
2. Tenda bila ya Kuchelewa
Unapopokea misukumo na kisha kutenda kwa nia, Bwana anaweza kukutumia. Kadiri unavyotenda, ndivyo sauti ya Roho inavyojulikana zaidi kwako. Utazidi kutambua mwongozo wa Mungu na kwamba Yu “tayari … kufunua fikra na mapenzi Yake.”4 Ukichelewa, unaweza kusahau msukumo au kukosa nafasi ya kumsaidia mtu fulani kwa niaba ya Mungu.
3. Pata Utumishi Wako kutoka kwa Bwana
Sala ambayo Baba wa Mbinguni anaonekana kuijibu kwa haraka ni ombi letu kuongozwa kwa mtu anayehitaji msaada wetu. Rais Eyring ametufundisha kutafuta ufunuo kwa kumuuliza Mungu mtu ambaye tunaweza kumsaidia kwa niaba Yake. “Ikiwa utauliza maswali kama hayo, Roho Mtakatifu atakuja na utahisi misukumo kuhusu vitu ambavyo unaweza kufanya kwa ajili ya watu wengine. Utakapoenda na kufanya vitu hivyo, uko katika utumishi wa Bwana, na wakati upo katika utumishi wa Bwana, unakuwa mstahiki wa kipawa cha Roho Mtakatifu.”5
Unaweza kusali na kumwomba Mungu utumishi. Unapofanya hivyo, Yeye anaweza kutumia ujuzi wako wa kawaida kufanikisha kazi Yake ya ajabu.
Babu yangu, Fritz Hjalmar Lundgren, alihama kutoka Sweden akiwa na umri wa miaka 19. Aliwasili Marekani, peke yake, akiwa na sanduku na miaka rasmi sita tu ya kisomo. Akiwa hawezi kuzungumza Kingereza, alisafiri kwenda Oregon na kufanya kazi huko kama mpasua mbao na kisha baadaye, pamoja na bibi yangu na mama yangu, walijiunga na Kanisa. Hakuwahi kusimamia kata, lakini kama mwalimu wa nyumbani mwaminifu, alizirejesha familia tofauti zaidi ya 50 katika uhudhuriaji kamili Kanisani. Ni kwa jinsi gani aliweza kufanya hivyo?
Baada ya kifo cha babu, nilikuwa nikipitia sanduku la karatasi zake na kupata barua iliyoandikwa na mwanaume ambaye alikuwa amerudi kanisani kwa sababu ya upendo wa Babu. Barua hiyo ilisema, “Siri ya kaka Fritz, ninaamini, ni kwamba siku zote yuko katika utumishi wa Baba wa Mbinguni.”
Barua hiyo ikuwa imetoka kwa Kaka Wayne Simonis. Babu alimtembelea na kuweza kumjua kila mwanafamilia. Baada ya muda, Babu aliwaambia kwamba walihitajika na akawaalika wahudhurie kanisani. Lakini Jumapili hiyo, Kaka Simonis aliamka na mawazo mawili—hakuwa amemaliza kuweka paa upya juu ya nyumba yake na mvua ilitarajiwa wiki hiyo. Aliamua kwamba angeenda kanisani, amsalimu Babu kwa mkono, na kisha angeondoka na kurudi nyumbani amalizie kuweka paa. Familia yake ingeweza kuhudhuria mkutano wa sakramenti bila yeye.
Mpango wake ulikuwa unaendelea vizuri hadi, akiwa juu ya paa, alimsikia mtu akipanda ngazi. Kwa maneno yake: “Wakati nilipotazama juu, … akiwa amesimama juu ya ngazi alikuwa Kaka Fritz. Alinipatia tu lile tabasamu kubwa. Mwanzoni, niliona aibu na kuhisi kama mtoto mdogo aliyekamatwa kwa kukwepa shule. Kisha … nikahisi hasira. [Lakini Kaka Fritz] alivua tu koti lake la suti na kulitundika kwenye ngazi. Alipokuwa akikunja mikono ya shati lake jeupe, alinigeukia na kusema, ‘Kaka Simonis, una nyundo nyingine? Kazi hii lazima itakuwa muhimu sana la sivyo usingeiacha familia yako, na kama ni muhimu kiasi hicho, ningependa kukusaidia.’ Nilipotazama machoni mwake, niliona tu ukarimu na upendo kama wa Kristo. Hasira yangu iliondoka. … Niliviweka vifaa vyangu chini Jumapili ile na kumfuata rafiki yangu mwema kushuka ngazi na kurejea kanisani.”
Babu alipokea utumishi wake kutoka kwa Bwana, na alijua alihitajika kuwatafuta kondoo waliopotea. Kama vile wale wanaume wanne waliombeba rafiki yao aliyepooza juu ya paa na kumshusha chini ili apate kuponywa na Yesu Kristo,6 hivyo ndivyo pia utumishi wa Babu unamfikisha juu ya paa. Bwana hutuma ufunuo kwa wale wanaotafuta kuwasaidia wengine.
4. Amini na kuwa na Tumaini
Hivi karibuni, nilisoma katika maandiko kuhusu mmisionari mwingine mkuu ambaye alipokea utumishi wake kutoka kwa Bwana. Haruni alikuwa akimfundisha mfalme wa Walamani, ambaye alijiuliza kwa nini kaka wa Haruni hakuja kumfundisha. “Na Haruni akamwambia mfalme: Tazama, Roho wa Bwana amemtuma mahali pengine.”7
Roho aliuzungumzia moyo wangu: kila mmoja wetu ana misheni tofauti ya kutimiza, na wakati mwingine Roho anaweza kututuma “mahali pengine.” Kuna njia nyingi za kujenga ufalme wa Mungu kama wafuasi wa Yesu Kristo wanaofanya maagano, wanaotunza maagano. Kama mfuasi wake mwaminifu, unaweza kupokea uvuvio na ufunuo binafsi, unaokubaliana na amri Zake, ambao umetolewa kwa ajili yako. Mnazo misheni za kipekee na majukumu ya kipekee ya kutekeleza maishani na mtapewa mwongozo wa kipekee kuyatimiza.
Nefi, kaka ya Yaredi, na hata Musa wote walitakiwa kuvuka sehemu kubwa iliyokuwa na maji—na kila mmoja ilifanya hivyo kwa njia tofauti. Nefi “aliunda mbao kwa ufundi maalumu.”8 Kaka ya Yaredi alijenga mashua ambazo zilikuwa “zimekazwa kama bakuli.”9 Na Musa “alienda katika nchi kavu katikati mwa bahari.”10
Kila mmoja wao alipokea mwongozo binafsi, uliowafaa wao, na kila mmoja alionesha uaminifu na kutenda. Mungu anawakumbuka wale wanaotii na, kwa maneno ya Nefi, “atatayarisha njia kwa ajili yetu [sisi ili] kutimiza kitu ambacho ameamuru.”11 Gundua kwamba Nefi anasema, “njia ”—si “ile njia.”
Je, sisi tunakosa au kupuuza utumishi binafsi kutoka kwa Bwana kwa sababu ametayarisha “njia” tofauti na ile tunayoitarajia?
Babu yangu alielekezwa mahali pasipo pa kawaida—akiwa amevalia suti, juu ya paa, Jumapili. Mtumaini Mungu akuongoze, hata kama njia hiyo inaonekana tofauti na ile uliyotarajia au ni tofauti na zingine.
Watakatifu wa Siku za Mwisho huja katika maumbo na ukubwa tofauti, lakini “wote ni sawa kwa Mungu”—“weusi kwa weupe, wafungwa na walio huru, wake kwa waume,” waseja na wana ndoa, tajiri na maskini, vijana na wazee, muumini wa maisha yote na muongofu mpya.12 Haijalishi wewe ni nani au kile unachofanya, umealikwa kwenye meza ya Bwana.13
Wakati kutafuta na kufanya mapenzi ya Baba ni kiini cha maisha yako ya kila siku, utaweza, bila shaka, kuongozwa kubadilika na kutubu.
Programu mpya ya Kanisa kwa ajili ya watoto na vijana imejengwa juu ya msingi wa kujifunza jinsi ya kutafuta ufunuo, kugundua kile ambacho Bwana angetutaka tufanye, na kisha kutenda kulingana na mwongozo huo. Kila mmoja wetu, bila kujali umri au hali, tunaweza kujitahidi kutafuta, kupokea, na kutenda. Unapofuata mpangilio huu wa milele uliotawazwa kwa ajili ya siku zetu, utamkaribia Yesu Kristo—Upendo Wake, Nuru Yake, Mwongozo Wake, Amani Yake, na nguvu Zake za kuponya na kuwezesha. Na utaongeza uwezo wako wa kiroho wa kuwa chombo cha kila siku cha mikono Yake katika kufanikisha kazi Yake kuu. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.