Wanawake wa Maagano kwenye Ubia na Mungu
Kuwa mwanamke wa agano kwenye ubia na Mungu ni jinsi mabinti wakuu na wema wa Mungu daima wamelea, wameongoza, na kuhudumu.
Nina shukrani kwa ajili ya baraka ya kuwahutubia, mabinti wa agano wa Mungu. Usiku huu, dhumuni langu ni kuwatia moyo katika huduma kuu ambayo kwayo mmeitwa. Ndio, kila binti wa Mungu anayesikiliza sauti yangu amepokea wito kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.
Wito wako ulianza wakati ulipowekwa kwenye maisha ya kufa, katika sehemu na muda uliochaguliwa kwa ajili yako na Mungu anayekujua kikamilifu na kukupenda kama binti Yake. Katika ulimwengu wa roho, alikujua na alikufundisha na kukuweka ambapo ungekuwa na fursa, isiyo ya kawaida katika historia ya ulimwengu, kualikwa kwenye kisima cha maji ya ubatizo. Pale, ungesikia maneno haya yakitamkwa na mtumishi aliyeitwa wa Yesu Kristo: “Kwa mamlaka niliyopewa na Yesu Kristo, ninakubatiza katika jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Amina.”1
Wakati ulipotoka majini, ulikuwa umekubali wito mwingine wa kutumikia. Kama binti mpya wa agano wa Mungu, uliweka ahadi na ulipokea jukumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ambalo kwalo ulithibitishwa kama muumini. Uliagana na Mungu kujichukulia juu yako jina la Yesu Kristo, kutii amri Zake, na kumtumikia Yeye.
Kwa kila mtu anayefanya maagano haya, huduma ambayo Bwana anamwita kufanya itakuwa imestahili kikamilifu kwa mtu yule. Mabinti na wana wa agano wa Mungu, hata hivyo, wote wanashiriki wito mmoja muhimu na wenye furaha. Ni kuwatumikia wengine kwa ajili Yake.
Akizungumza na akina dada, Rais Russell M. Nelson alitoa muhtasari wa kupendeza wa wito wa Bwana kwenu kujiunga Naye katika kazi Yake. Rais Nelson aliuelezea wito wenu kwa njia hii: “Bwana alisema, ‘Kazi yangu na utukufu wangu [ni] kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.’ (Musa 1:39.) Kwa hivyo bintiye-mfuasi mwaminifu anaweza kwa dhati kusema, ‘Kazi yangu na utukufu wangu ni kuwasaidia wapendwa wangu kufikia lengo hilo la mbinguni.’
“Kumsaidia mwanadamu mwingine kufikia uwezekano wake wa selestia ni sehemu ya misheni takatifu ya mwanamke. Kama mama, mwalimu, au mtakatifu mlezi, anafinyanga udongo wenye uhai kwa umbo la matumaini yake. Kwa ubia na Mungu, lengo lake takatifu ni kuzisaidia roho kuishi na nafsi kuinuliwa. Hiki ndicho kipimo cha uumbaji wake. Ni chenye kuadilisha, kuelimisha, na kuinua.”2
Huwezi kujua ni lini, au kwa urefu gani wa muda, misheni yako binafsi itakuwa imefokasi kwenye huduma katika miito kama vile mama, kiongozi, au dada mhudumiaji. Bwana, kutokana na upendo, hatuachii uchaguzi wa muda, au utaratibu wa mpangilio wa majukumu yetu. Bado mnajua kutokana na maandiko na manabii walio hai kwamba majukumu haya yote yatakuja, ama katika maisha haya au yajayo, kwa kila binti wa Mungu. Na yote hayo ni matayarisho kwa ajili ya uzima wa milele katika familia zenye upendo—“zawadi kubwa kuliko zote za Mungu.”3
Utakuwa mwenye busara kufanya juhudi zote kujiandaa sasa ukiwa na mwisho akilini mwako. Jukumu hilo limefanywa rahisi zaidi kwa sababu kila mojawapo ya majukumu haya yanahitaji maandalizi yanayofanana.
Acha tuanze na jukumu la kuwa dada mhudumiaji. Iwe una jukumu hilo kama binti wa- miaka-10 katika familia ambayo baba amefariki, au kama rais wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama ambaye mji wake hivi karibuni uliathirika kwa moto, au wakati upo hospitalini ukipata nafuu kutokana na upasuaji—una nafasi ya kutimiza wito wako kutoka kwa Bwana kuwa binti Yake mhudumiaji.
Hayo yanaonekana kuwa majukumu tofauti kabisa ya uhudumiaji. Hata hivyo yote yanahitaji maandalizi yenye nguvu, moyo wa upendo, imani isiyo ya woga kwamba Bwana hatoi amri isipokuwa atayarishe njia, na hamu ya kwenda na kutenda kwa ajili Yake.4
Kwa sababu alikuwa amejiandaa, binti wa miaka-10 aliweka mikono yake kumzunguka mama yake mjane na kusali kujua jinsi ya kuisaidia familia yake. Na anabakia katika hilo.
Rais wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama alikuwa amejiandaa kuhudumu kabla ya moto usiotegemewa katika eneo lake. Alikuwa amekuja kuwajua na kuwapenda watu wale. Imani yake katika Yesu Kristo ilikuwa imekua kwa miaka mingi kutokana na kupata majibu ya sala zake kwa ajili ya Bwana kumsaidia katika huduma ndogo ndogo kwa ajili Yake. Kwa sababu ya maandalizi yake ya muda mrefu, alikuwa tayari na mwenye shauku kuwapanga dada zake kuwahudumia watu na familia zenye shida.
Dada aliyekuwa akipata ahueni hospitalini kutokana na upasuaji alikuwa amejiandaa kuwahudumia wagonjwa wenzake. Alikua ameishi maisha yake yote akimhudumia Bwana kwa kila mgeni kama vile alikuwa jirani na rafiki. Wakati alipohisi katika moyo wake wito wa kuhudumu hospitalini, aliwahudumia wengine kwa ujasiri mwingi na upendo mkubwa kiasi kwamba wagonjwa wengine walianza kutamani asipone haraka.
Katika njia kama hiyo ambayo unajiandaa kuhudumu, unaweza na lazima ujiandae kwa ajili ya wito wako kuwa kiongozi kwa ajili ya Bwana wito utakapokuja. Itahitaji imani katika Yesu Kristo, iliyo na mizizi katika upendo wako wa kina wa maandiko, ili kuongoza watu na kufundisha neno Lake bila woga. Ndipo utakuwa umejiandaa kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenza wako daima. Utakuwa na shauku ya kusema, “Nitafanya” wakati mshauri wako katika urais wa Wasichana anaposema, kwa hofu kubwa katika sauti yake, “Dada Alvarez ni mgonjwa leo. Nani atafundisha darasa lake?”
Inachukuwa maandalizi sawa na hayo kwa ajili ya siku ya kupendeza wakati Bwana anapokuita kwenye jukumu kama mama. Lakini itahitaji pia moyo wenye upendo zaidi kuliko uliouhitaji awali. Itahitaji imani katika Yesu Kristo zaidi ya ile ilichowahi kutokea kabla katika moyo wako. Na itahitaji uwezo kusali kwa ajili ya ushawishi, mwongozo, na faraja ya Roho Mtakatifu zaidi ya vile ulivyowahi kuhisi inawezekana.
Unaweza kwa kufikiria kuuliza jinsi mwanaume wa umri wowote anavyoweza kujua nini akina mama wanahitaji. Ni swali halali. Wanaume hawawezi kujua kila kitu, lakini tunaweza kujifunza baadhi ya masomo kwa ufunuo kutoka kwa Mungu. Na tunaweza pia kujifunza mengi kwa kuchunguza, wakati tunapochukua fursa kumtafuta Roho atusaidie kuelewa kile tunachoona.
Nimekuwa nikimchuguza Kathleen Johnson Eyring kwa miaka 57 tuliyooana. Yeye ni mama wa wavulana wanne na wasichana wawili. Hivi leo, amekubali wito wa kuwa ushawishi wa umama kwa wana familia wa karibu zaidi ya mia na mamia wengine ambao amewaasili katika moyo wake wa umama.
Mnakumbuka maelezo kamili ya Rais Nelson ya kazi maalumu takatifu ya mwanamke—ikiwa ni pamoja na kazi maalumu ya umama: “Kama mama , mwalimu, au mtakatifu mlezi, anafinyanga udongo uliyo hai kwenye umbo la matumaini yake. Kwa ubia na Mungu, lengo lake takatifu ni kuzisaidia roho kuishi na nafsi kuinuliwa. Hiki ndicho kipimo cha uumbaji wake.”5
Kwa kadiri ninavyoweza kufahamu, mke wangu, Kathleen, amefuata wajibu huo, uliotolewa kwa mabinti wa Baba yetu. Cha msingi kinaonekana kwangu kuwa maneno “anafinyanga udongo uliyo hai kwenye umbo la matumaini yake … katika ubia na Mungu.” Hakulazimisha. Alifinyanga. Na alikuwa na kigezo kwa ajili ya matumaini yake, na kwa hicho alijaribu kufinyanga wale aliowapenda na kuwazaa. Kigezo chake kilikuwa injili ya Yesu Kristo—kama nilivyoona kupitia uchunguzi wa sala kwa miaka mingi.
Kuwa mwanamke wa agano kwenye ubia na Mungu ni jinsi mabinti wakuu na wema wa Mungu daima wamezaa, wameongoza, na kuhudumu, wakitumikia katika njia na sehemu yoyote Yeye aliyoandaa kwa ajili yao. Ninaahidi kwamba utapata furaha katika safari yako ya nyumbani mbinguni pale unaporudi Kwake kama binti wa Mungu atunzaye maagano.
Ninashuhudia kwamba Mungu Baba yu haina anapenda. Yeye atasikia na kujibu sala zako. Mwanawee Mpendwa analiongoza, katika kila kitu, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Rais Russell M. Nelson ni nabii Wake aliye hai. Na Joseph Smith alimwona na alizungumza na Mungu Baba na Yesu Kristo katika kijisitu cha miti huko Palmyra, New York. Ninajua kwamba hilo ni kweli. Ninashuhudia pia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wako; Yeye anakupenda. Na kupitia Upatanisho Wake, unaweza kutakaswa na kuinuliwa kwenye miito ya juu na mitakatifu ambayo itakuja kwako. Nashuhudia hivyo, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.