Marekebisho ya Kuimarisha Vijana
Vijana zaidi wa kiume na wa kike watainuka kuzipita changamoto na kubaki kwenye njia ya agano kwa sababu ya fokasi hii ya juu kwa vijana wetu.
Asante, Rais mpendwa Nelson, kwa mwongozo huo wa kiufunuo wa kufurahisha kuhusiana na kuwa mashahidi wakati wa ubatizo na mwongozo ambao umetuomba kushiriki ili kusaidia kuimarisha vijana na kukuza uwezekano wao mtakatifu.
Kabla sijashiriki marekebisho hayo, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa njia ya kipekee ambayo waumini wameitikia marekebisho katika Urejesho endelevu wa injili. Kama Rais Nelson alivyopendekeza mwaka jana, mmepata vitamini zenu!1
Kwa shangwe mnajifunza Njoo, Unifuate nyumbani.2 Pia mmeitikia marekebisho kanisani. Washiriki wa akidi ya wazee na akina dada wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama kwa umoja hufanya kazi ya wokovu.3
Shukrani zetu hazina kipimo.4 Tunashukuru hasa kwamba vijana wetu wanaendelea kubakia imara na waaminifu.
Vijana wetu wanaishi katika wakati wa kufurahisha lakini pia wenye changamoto. Chaguzi zipatikanazo ni nyingi zaidi mno. Mfano mmoja: simu janja ya kisasa hutoa ufikiaji wa taarifa muhimu sana na zenye kuinua, ikiwa ni pamoja na historia ya familia na maandiko matakatifu. Kwa upande mwingine, ina upumbavu, mmomonyoko wa maadili, na uovu ambao haukupata kuwepo hapo zamani.
Ili kuwasaidia vijana wetu kuchunguza mkanganyiko huu wa chaguzi, Kanisa limeandaa mipango mitatu mikubwa na ya kufaa. Kwanza, mtaala umeimarishwa na kupanuliwa hadi nyumbani. Pili, programu ya watoto na vijana ambayo inajumuisha shughuli za kufurahisha na maendeleo binafsi uliwasilishwa Jumapili iliyopita na Rais Russell M. Nelson, Rais M. Russell Ballard, na Maofisa Wakuu. Mpango wa tatu ni mabadiliko ya kimuundo ili kuwafanya vijana kuwa fokasi muhimu ya maaskofu wetu na viongozi wengine. Fokasi hii lazima iwe na nguvu ya kiroho na iwasaidie vijana wetu kuwa jeshi la vijana ambalo Rais Nelson amewaomba kuwa.
Mifumo Inayofungamana
Juhudi hizi, pamoja na zile zilizotangazwa miaka michache iliyopita, siyo mabadiliko yaliyojitenga. Kila moja ya marekebisho ni sehemu muhimu ya mfumo unaofungamana ili kubariki Watakatifu na kuwaandaa kukutana na Mungu.
Sehemu moja ya mfumo inahusiana na kizazi chipukizi. Vijana wetu wanaombwa kuchukua majukumu zaidi binafsi katika umri mdogo—bila wazazi na viongozi kufanya kile ambacho vijana wanaweza kufanya wao wenyewe.5
Tangazo
Leo tunatangaza mabadiliko ya kimuundo kwa ajili ya vijana katika ngazi za kata na vigingi. Kama Rais Nelson alivyofafanua, Dada Bonnie H. Cordon atajadili mabadiliko kwa ajili ya Wasichana jioni hii. Kusudi moja la mabadiliko nitakayojadili sasa ni kuimarisha wenye Ukuhani wa Haruni, akidi, na urais wa akidi. Mabadiliko haya yanashabihiana na utamaduni wetu katika Mafundisho na Maagano 107:15, ambayo inasema, “Uaskofu ni urais wa ukuhani huu [wa Haruni], na unashikilia funguo au mamlaka hayo.”
Mojawapo ya majukumu ya kiroho ya askofu ni kuwasimamia makuhani na kuketi katika baraza pamoja nao, akiwafundisha majukumu ya ofisi yao.6 Kwa kuongezea, mshauri wa kwanza katika uaskofu atakuwa na jukumu maalum kwa walimu na mshauri wa pili kwa mashemasi.
Vivyo hivyo, ili kufungamana na ufunuo huu katika Mafundisho na Maagano, Urais wa Wavulana katika ngazi ya kata utaondolewa. Ndugu hawa waaminifu wamefanya mengi mema, na tunatoa shukrani kwao.
Ni matumaini yetu kwamba uaskofu utatoa msisitizo na fokasi kubwa kwenye majukumu ya ukuhani ya wavulana na kuwasaidia katika majukumu yao ya akidi. Watu wazima washauri wa Wavulana wenye uwezo wataitwa ili kusaidia urais wa akidi ya Ukuhani wa Haruni na uaskofu katika majukumu yao.7 Tuna hakika kuwa wavulana na wasichana watainuka kuzipita changamoto na kubaki kwenye njia ya agano kwa sababu ya fokasi hii ya juu kwa vijana wetu.
Katika mfumo uliotolewa na Bwana, askofu ana jukumu juu ya kila mtu katika kata. Anawabariki wazazi wa vijana pamoja na vijana. Askofu mmoja aligundua kwamba wakati alipokuwa akimshauri mvulana ambaye alitatizwa na ponografia, angeweza kumsaidia mvulana katika toba yake wakati tu allipowasaidia wazazi kuitikia kwa upendo na uelewa. Uponyaji wa mvulana huyo ulikuwa uponyaji kwa familia yake na uliwezekana kupitia askofu akifanya kazi kwa niaba ya familia nzima. Kijana huyo sasa amekuwa mstahiki wa Ukuhani wa Melkizedeki na mmisionari wa muda wote.
Kama tukio hili linavyopendekeza, marekebisho haya:
-
Yatawasaidia maaskofu na washauri wao kufokasi kwenye majukumu yao ya msingi kwa vijana na watoto wa Msingi.
-
Yataweka nguvu na majukumu ya Ukuhani wa Haruni kwenye kitovu cha maisha na malengo binafsi ya kila mvulana.
Marekebisho haya pia:
-
Yanasisitiza majukumu ya urais wa akidi za Ukuhani wa Haruni na mfumo wao wa moja kwa moja wa kutoa taarifa kwa uaskofu.
-
Yanahimiza viongozi watu wazima kusaidia na kushauri urais wa Ukuhani wa Haruni katika kukuza nguvu na mamlaka ya ofisi yao.
Kama ilivyobainishwa, marekebisho haya hayapunguzi jukumu la uaskofu kwa wasichana. Kama vile Rais Nelson alivyotoka kufundisha, “Jukumu la kwanza kabisa la [askofu] ni kuwatunza wavulana na wasichana wa kata yake.”8
Je, maaskofu wetu wapendwa wafanyao kazi kwa bidii wanawezaje kutimiza jukumu hili? Kama mnavyokumbuka, mnamo mwaka 2018 akidi za Ukuhani wa Melkizedeki zilibadilishwa ili kufanya kazi kwa karibu zaidi na Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama ili kwamba akidi za wazee na Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama waweze, chini ya maelekezo ya askofu, kusaidia kufanya majukumu muhimu ambayo hapo awali yalichukua muda mwingi wa askofu. Majukumu haya ni pamoja na kazi ya umisionari na historia ya familia na hekalu kwenye kata9—pamoja na kuwahudumia kwa kiasi kikubwa washiriki wa kata.
Askofu hawezi kunaibisha baadhi ya majukumu, kama vile kuwaimarisha vijana, kuwa muamuzi mkuu, kuwajali wale wenye uhitaji, na kusimamia fedha na maswala ya kimwili. Haya, hata hivyo, ni machache ya yale ambayo tuliyaelewa hapo zamani. Kama Mzee Jeffrey R. Holland alivyoelezea mwaka jana wakati marekebisho ya akidi za Ukuhani wa Melkizedeki yalipotangazwa: “Askofu anaendelea kubaki, ndiyo, kuhani mkuu msimamizi wa kata. Mfungamano huu mpya [wa akidi za wazee na Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama] unapaswa kumfanya asimamie kazi ya Ukuhani wa Melkizedeki na Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama bila kumhitaji kufanya kazi yoyote ya makundi haya.”10
Kwa mfano, Rais wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama na rais wa Akidi ya wazee, kama walivyopangiwa, wanaweza kuchukua jukumu kubwa katika kushauriana na watu wazima—kama vile rais wa Wasichana anavyoweza kushauriana na Wasichana. Wakati askofu pekee ndiye anayeweza kuhudumu kama muamuzi mkuu, viongozi hawa wengine pia wana haki ya kupokea ufunuo kutoka mbinguni ili kusaidia katika changamoto ambazo hazihitaji muamuzi mkuu au zinazohusisha unyanyasaji wa aina yoyote.11
Hiyo haimaanishi kuwa msichana hawezi au hatakiwi kuzungumza na askofu au wazazi wake. Fokasi yao ni vijana! Lakini inamaanisha kwamba kiongozi wa Wasichana anaweza kutimiza kikamilifu mahitaji binafsi ya msichana. Uaskofu unajali wasichana kama ilivyo kwa wavulana, lakini tunatambua nguvu ambayo huja kutokana na kuwa na viongozi wa wasichana ambao ni imara, wanaojihusisha, na wenye fokasi ambao hupenda na kushauri, pasikuchukua majukumu ya urais wa darasa bali kwa kuwasaidia vijana kufanikiwa katika majukumu hayo.
Dada Cordon atashiriki mabadiliko mengine ya kufurahisha kwa wasichana jioni ya leo. Mimi, hata hivyo, natangaza kwamba marais wa kata wa Wasichana sasa watatoa ripoti kwa na kushauriana moja kwa moja na askofu wa kata. Hapo awali, jukumu hili lingeweza kutolewa kwa mshauri, lakini kuendelea mbele, wasichana watakuwa ni jukumu la moja kwa moja la mtu ambaye anashikilia funguo za kusimamia katika kata. Rais wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama ataendelea kutoa ripoti moja kwa moja kwa askofu.12
Katika ngazi kuu na katika vigingi, tutaendelea kuwa na urais wa Wavulana. Katika ngazi ya Kigingi, mshauri wa baraza atakuwa rais wa Wavulana13 na, pamoja na washauri wa baraza waliopewa jukumu juu ya Wasichana na Msingi, watakuwa sehemu ya kamati ya kigingi ya Ukuhani wa Haruni–Wasichana. Ndugu hawa watafanya kazi na urais wa kigingi wa Wasichana kwenye kamati hii. Mshauri wa rais wa kigingi akiwa kama mwenyekiti, kamati hii itakuwa na umuhimu zaidi kwa sababu programu nyingi na shughuli katika mpango mpya kwa Watoto na Vijana zitakuwa katika ngazi ya kigingi.
Washauri hawa wa baraza, chini ya maelekezo ya urais wa kigingi, wanaweza kutumika kama nyenzo kwa askofu na akidi za Ukuhani wa Haruni katika njia sawa na ile ya huduma itolewayo na washauri wa baraza kwa akidi za wazee kwenye kata.
Kama jambo linalohusiana na hilo, mshauri mwingine wa baraza atatumikia kama rais wa Shule ya Jumapili wa kigingi na, ikihitajika, anaweza kutumikia kwenye kamati ya Ukuhani wa Haruni–Wasichana.14
Mabadiliko ya ziada ya kimuundo yatafafanuliwa zaidi katika taarifa iliyotumwa kwa viongozi. Mabadiliko haya ni pamoja na:
-
Baraza la vijana la kata litachukua nafasi ya mkutano wa uaskofu wa kamati ya vijana.
-
Neno “Mutual” litapumzishwa na kuwa “shughuli za Wasichana,” “shughuli za akidi za Ukuhani wa Haruni,” au “shughuli za vijana” ambazo zitafanyika kila wiki pale inapowezekana.
-
Bajeti ya kata kwa ajili ya shughuli za vijana itagawanywa sawa kwa ajili ya wavulana na wasichana kulingana na idadi ya vijana katika kila taasisi. Kiasi cha kutosheleza kitatolewa kwa ajili ya shughuli za Msingi.
-
Katika ngazi zote—kata, kigingi, na zote—tutatumia neno “taasisi” badala ya neno “kikundi saidizi.” Wale wanaoongoza katika ngazi kuu kwenye Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, Wasichana, Wavulana, Msingi na Shule ya Jumapili watajulikana kama “Maafisa Wakuu.” Wale wanaoongoza taasisi katika ngazi za kata na vigingi watajulikana kama “maafisa wa kata” na “maafisa wa Kigingi.”15
Marekebisho yaliyotangazwa leo yanaweza kuanza mara tu matawi, kata, wilaya, na vigingi vikiwa tayari, lakini mpaka Januari 1, 2020 yanapaswa kuanza kutumika. Marekebisho haya, yanapojumuishwa na kuunganishwa na marekebisho ya zamani, yanawakilisha juhudi ya kiroho na ya kitaasisi inayoendana na mafundisho ili kubariki na kumuimarisha kila mwanamume, mwanamke, kijana na mtoto, yakimsaidia kila mmoja kufuata mfano wa Mwokozi wetu, Yesu Kristo, tunapoendelea kwenye njia ya agano.
Wapendwa akina kaka na akina dada, ninaahidi na ninashuhudia kwamba marekebisho haya ya kina, chini ya maelekezo ya rais na nabii aliyevuviwa, Russell M. Nelson, yatamuwezesha na kumuimarisha kila muumini wa Kanisa. Vijana wetu watajenga imani kubwa kwa Mwokozi, watalindwa kutokana na majaribu ya adui, na watasimama tayari kukabiliana na changamoto za maisha. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.