Kujua, Kupenda, na Kukua
Na sote tufikie kwenye kuelewa sehemu yetu katika kazi hii kuu ya kuhudumu ili kwamba tuweze kuwa zaidi kama Yeye.
Mnamo 2016 Kwaya ya Tarbenacle katika Temple Square ilikuja kutembelea Uholanzi na Ubelgiji. Na kwa kuwa nilikuwa nikijihusisha na tukio hilo la kufurahisha, nilikuwa na fursa ya kufurahia onyesho lao mara mbili.
Wakati wakiimba nilikuwa nikifikiria ilikuwa ni kazi nzuri kiasi gani kusafirisha kwaya ya ukubwa ule. Mawazo yangu yalivutwa kwenye ngoma ya upatu kubwa ambayo ilikuwa vigumu na pengine iligharimu fedha nyingi kuisafirisha ukilinganisha na zeze, tarumbeta, au vyombo vingine ambavyo kiurahisi ungeweza kuvibeba mkononi. Lakini kwa kuangalia uhusika kamili wa hii ngoma upatu, niligundua ilikuwa ikipigwa mara chache tu, wakati vyombo vingine vidogo vilikuwa vikitumika mara nyingi katika tamasha. Nilitafakari kwamba bila sauti ya ngoma ya upatu, tamasha lisingekuwa kama lilivyotakiwa kuwa na hivyo juhudi zilitakiwa kufanywa kuisafirisha hii ngoma ya upatu kubwa kuvuka bahari.
Wakati mwingine tunaweza kuhisi kuwa sisi ni kama ile upatu, tukifaa tu kupigwa katika sehemu ndogo ya tamasha. Lakini acha nikuambie kwamba sauti yako inaleta tofauti.
Tunahitaji vyombo vyote. Baadhi yetu tunajifunza kiurahisi na kufanya vizuri shuleni, wakati wengine wana vipaji vya usanii. Wengine hubuni na kutengeneza vitu au kuuguza, kulinda, au kufundisha wengine. Sote tunahitajika kuleta rangi na maana katika dunia.
Kwa wale ambao wanahisi kwamba hawana chochote cha kuchangia au kuamini kwamba hawana umuhimu au ushawishi kwa yeyote, kwa wengine wanaohisi kwamba wako juu ya dunia, na yoyote aliye katikati ya makundi hayo mawili, ningependa kutoa ujumbe huu.
Sehemu yoyote ulipo katika njia ya maisha, baadhi yenu mnaweza kuhisi kulemewa kiasi kwamba hamjichukulii kuwa mko katika njia ile. Ninataka kuwaalika mtoke gizani na kuja nuruni. Nuru ya injili itawapa joto na uponyaji na itawasaidia kuelewa ninyi ni nani hasa na lengo lenu ni lipi katika maisha.
Baadhi yetu tumekuwa tukitangatanga katika njia zilizokataliwa, ili kujaribu kupata furaha huko.
Tunaalikwa na Baba yetu waMbinguni mwenye upendo kutembea kwenye njia ya ufuasi na kurudi Kwake. Yeye anatupenda kwa upendo kamili.1
Je, njia ni ipi? Njia ni kumsaidia kila mmoja wetu kuelewa sisi ni akina nani kwa kuhudumiana.
Kwangu mimi, kuhudumu ni kuonesha upendo wa kiungu.2 Katika njia hiyo tunatengeneza mazingira ambapo wote mtoaji na mpokeaji wanapata hamu ya kutubu. Kwa maneno mengine, tunabadili mwelekeo na kuja karibu zaidi na kuwa zaidi kama Mwokozi wetu, Yesu Kristo.
Kwa mfano, hakuna haja ya kila mara kuwaambia wenzi wetu au watoto wetu muda wote wapi wanatakiwa kujiboresha; wanalijua hilo tayari. Ni katika kutengeneza mazingira ya namna hii ya upendo kwamba watakuwa na nguvu ya kufanya mabadiliko muhimu katika maisha yao na kuwa watu bora zaidi.
Katika njia hii toba inakuwa mchakato wa kila siku wa kujitakasa ambao unaweza kujumuisha kuomba radhi kwa tabia zisizofaa. Ninakumbuka na bado ninapitia hali ambapo nimekuwa mwepesi kuhukumu au mzito kusikiliza. Na hatimaye mwisho wa siku, katika sala yangu binafsi, nilihisi ushauri wa upendo kutoka mbinguni wa kutubu na kuwa bora zaidi. Mazingira ya upendo ambayo kwanza yalitengenezwa na wazazi wangu, kaka, na dada na baadaye mke wangu, watoto, na marafiki yamenisaidia kuwa mtu bora zaidi.
Sote tunajua wapi tunaweza kuwa bora zaidi. Hakuna haja ya kila mara kukumbushana, lakini kuna haja ya kupendana na kuhudumiana sisi kwa sisi na wengine na, katika kufanya hivyo, tunatoa mazingira ya utayari wa kubadilika.
Katika mazingira sawa na hayo tunajifunza sisi ni kina nani hasa na kazi yetu itakuwa ipi katika sura hii ya mwisho ya historia ya ulimwengu kabla ya Ujio wa Pili wa Mwokozi.
Ikiwa unajiuliza kuhusu sehemu yako, ningependa kukualika kutafuta sehemu ambapo unaweza kuwa peke yako na kumuomba Baba wa Mbinguni kufanya ijulikane kwako sehemu ipi unatakiwa kuchukua. Jibu labda litakuja taratibu na kisha dhahiri zaidi wakati tumeweka miguu yetu thabiti zaidi katika njia ya agano na njia ya kuhudumu.
Tunapitia baadhi ya changamoto sawa na zile Joseph Smith alizokumbana nazo wakati alipokuwa “katikati ya vita vya maneno na makelele ya maoni.” Tunaposoma maneno yake mwenyewe, mara nyingi alijisemea nafsini mwake: “Je, nini kifanyike? Nani kati yao hawa wote aliye sahihi; au, je, wote si sahihi? Kama yeyote kati yao yu sahihi, ni yupi, na nitajuaje?”3
Kwa ufahamu alioupata katika waraka wa Yakobo, ambao ulisema “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa,”4 Joseph hatimaye aliamua “kumuuliza Mungu.”5
Tunasoma zaidi kwamba “ilikuwa ni mara ya kwanza katika maisha [yake] kufanya jaribio la jinsi hii, kwani licha ya wasi wasi [wake] wote kamwe [hakuwahi] kufanya jaribio la kuomba kwa sauti.”6
Na inaweza kuwa hivyo kwetu kwa mara ya kwanza kabisa kumwendea Muumba wetu katika njia ambayo hatujawahi kufanya kabla.
Kwa sababu ya jaribio la Joseph, Baba wa Mbinguni na Mwana Wake, Yesu Kristo, walimtokea, wakimuita kwa jina, na kama matokeo tuna uelewa dhahiri kabisa wa sisi ni kina nani na kwamba tuna thamani.
Tunasoma zaidi kwamba katika miaka yake ya ujana, Joseph “alishutumiwa na wale ambao walitakiwa kuwa rafiki [zake] na wale [waliotakiwa] kumchukulia kwa ukarimu.”7 Vivyo hivyo sisi tunaweza kutegemea kiasi cha upinzani wakati tunapoishi maisha ya ufuasi.
Kama kwa sasa unahisi huwezi kuwa sehemu ya okestra na njia ya toba inaonekana ngumu kwako, tafadhali jua kwamba kama tutajitahidikatika njia hiyo, mzigo utaondolewa mabegani mwetu na kutakuwa na nuru tena. Baba wa Mbinguni kamwe hatatuacha wakati tunapomwendea. Tunaweza kuanguka na kusimama tena, na Yeye atatusaidia kufuta mavumbi kutoka magotini mwetu.
Baadhi yetu tumejeruhiwa, lakini huduma ya kwanza ya Bwana imetufunga majeraha vya kutosha kuziba vidonda vyetu vyote.
Na hivyo ni upendo huo, upendo kamilif ambao pia tunauita hisani au “upendo msafi wa Kristo,”8 ambao unahitajika katika nyumba zetu ambapo wazazi huwahudumia watoto wao na watoto wazazi wao. Kupitia upendo huo, mioyo itabadilishwa na nia kuzaliwa ili kutenda mapenzi Yake.
Ni upendo huo ambao unahitajika katika kutendeana kwetu sisi kwa sisi kama watoto wa Baba wa Mbinguni na kama waumini wa Kanisa Lake na ambao utatuwezesha kuvijumuisha vyombo vyote vya muziki katika okestra zetu ili kwamba tuweze kuimba kiutukufu pamoja na kwaya za malaika wa mbingu wakati mwokozi atakapokuja tena.
Ni upendo huo, nuru hiyo inayohitajika kuangaza na kumulika mazingira yetu wakati tukiendelea na maisha ya kila siku. Watu watagundua nuru na watavutwa kwenye nuru hiyo. Hiyo ndiyo aina ya kazi ya umisionari ambayo itawavuta wengine “kuja na kutazama, kuja na kusaidia, na kuja na kukaa.”9 Tafadhali, wakati umepokea ushuhuda wako kuhusu kazi hii kuu na sehemu yetu katika kazi hiyo, acha tufurahie pamoja na nabii wetu mpendwa Joseph smith, ambaye alitangaza “Kwani nimeona ono; nami najua hivyo, nami nilijua kwamba Mungu alijua, na sikuweza kukataa.”10
Ninashuhudia kwenu kwamba ninajua mimi ni nani, na ninajua ninyi ni kina nani. Sisi sote ni watoto wa Baba wa Mbinguni anayetupenda. Na Yeye hakutuleta hapa ili tushindwe bali turudi Kwake kwa utukufu. Kwamba tuweze sote kuelewa sehemu yetu katika kazi hii kuu ya kuhudumu ili kwamba tuweze kuwa zaidi kama Yeye wakati Mwokozi atakapokuja tena ni sala yangu katika jina la Yesu Kristo, amina.