Waangalifu Siku Zote kwenye Sala (Alma 34:39; Moroni 6:4; Luka 21:36)
Uangalifu endelevu unahitajika ili kukabiliana na hali ya kuridhika na kuwa wa kawaida.
Kwa dhati ninaomba msaada wa Roho Mtakatifu kwa ajili yenu na kwa ajili yangu tunapofurahia na kuabudu pamoja.
Mnamo Aprili 1976, Mzee Boyd K. Packer alizungumza mahususi na vijana wa Kanisa katika mkutano mkuu. Katika ujumbe wake maarufu wenye kichwa cha habari “Mamba wa Kiroho,” aliezea jinsi wakati wa jukumu lake huko Afrika aliwaona mamba wenye kujificha walivyonyemelea mawindo wasio na habari. Kisha akafananisha mamba na Shetani, ambaye huwavizia vijana wasio waangalifu kwa kuficha asili ya kufisha ya dhambi.
Nilikuwa na umri wa miaka 23 wakati Mzee Packer alipotoa hotuba hiyo, na mimi na Susan tulikuwa tukitarajia kuzaliwa kwa mtoto wetu wa kwanza katika siku chache tu. Tulivutiwa na yaliyokuwemo katika ujumbe wake kuhusu kujiepusha na dhambi na jinsi kwa ufanisi alivyotumia tabia ya kawaida ya wanyama kufundisha somo muhimu la kiroho.
Mimi na Susan pia tumesafiri kwenda Afrika kwenye majukumu mengi. Na tumepata fursa za kuwaona wanyama wazuri ambao wanaishi kwenye bara hilo. Kwa kukumbuka athari ya mazungumzo ya Mzee Packer katika maisha yetu, tumejaribu kuchunguza na kujifunza masomo kutoka kwenye tabia za wanyama pori wa Afrika.
Ninataka kuelezea tabia na mbinu za duma wawili ambao mimi na Susan tuliwaangalia katika uwindaji wao na kuhusisha baadhi ya mambo kadhaa ambayo tuligundua kwenye maisha ya kila siku ya injili ya Yesu Kristo.
Duma na Paa
Duma ni wanyama walio na kasi zaidi duniani na hufikia kasi kubwa ya kukimbia kama maili 75 kwa saa (120 km/saa). Wanyama hawa wazuri wanaweza kuharakisha kutoka hali ya kusimama hadi kasi ya kukimbia haraka kama maili 68 kwa saa (109 km/saa) chini ya sekunde tatu. Duma ni wanyama walao wanyama wengine ambao huvizia mawindo yao na hutimka kutokea umbali mfupi kufukuza na kushambulia.
Mimi na Susan tulitumia takribani masaa mawili kuwaangalia duma wawili wakinyatia kundi kubwa la topi, paa wanaojulikana sana na walioenea sana Afrika. Nyasi ndefu, na kavu za savanna ya Kiafrika zilikuwa kahawia na ziliwaficha kabisa wanyama walao wanyama wengine walipokuwa wakifuata kundi la paa. Duma walijitenga kutoka kwa kila mmoja kwa karibu yadi 100 (mita 91) lakini walifanya kazi kwa pamoja.
Wakati duma mmoja alipokaa wima kwenye nyasi na hakusogea, duma mwingine alichuchumaa chini na polepole kutambaa kusogelea paa ambao hawakuhisi chochote. Kisha duma aliyekuwa amekaa wima alitoweka kwenye nyasi wakati ule ule ambapo duma mwingine alikaa wima. Mtindo huu wa kubadilishana wa duma mmoja akichuchumaa chini na kutambaa mbele wakati duma mwingine akikaa wima kwenye nyasi uliendelea kwa muda mrefu. Ujanja wa mkakati ulikusudiwa kuwavuruga na kuwahadaa paa na hivyo kugeuza umakini wao mbali na hatari iliyowakaribia. Kwa uvumilivu na uimara, duma hao wawili walifanya kazi kama timu kupata chakula chao kijacho.
Wakisimama kati ya kundi kubwa la paa na duma waliokaribia walipokuwa paa kadhaa wakubwa na wenye nguvu waliosimama wima kama walinzi kwenye vilima vya mchwa. Mtazamo ulioimarishwa wa ardhi zenye nyasi kutoka kwenye vilima vidogo uliwawezesha paa hawa walinzi kutazama dalili za hatari.
Kisha ghafla, wakati duma wakionekana kuwa karibu vya kutosha kushambulia, kundi lote la paa liligeuka na kukimbia. Sijui kama au kwa namna gani walinzi wa paa waliwasiliana na kundi kubwa, lakini kwa njia fulani onyo lilitolewa, na paa wote walienda mahali penye usalama.
Na duma walifanya nini baadaye? Bila kuchelewa, duma hao wawili walianza tena mtindo wao wa kubadilishana wa duma mmoja kuchuchumaa chini na kutambaa mbele wakati duma mwingine akikaa wima kwenye nyasi. Mpangilio huu wa kuwinda uliendelea. Hawakuacha. Hawakuacha wala kuchukua muda wa mapumziko. Hawakusita katika kufuata mkakati wao wa kuvuruga na kugeuza. Mimi na Susan tulitazama duma wakitoweka kwa mbali, kila wakati wakisogea karibu zaidi na kundi la paa.
Usiku ule mimi na Susan tulikuwa na mazungumzo ya kukumbukwa kuhusu yale tuliyoona na kujifunza. Tulijadili pia uzoefu huu na watoto na wajukuu zetu na kugundua masomo mengi ya muhimu. Sasa nitaelezea matatu kati ya masomo hayo.
Somo #1—Jihadharini na Uovu wa Ulaghai Uliofichika
Kwangu, duma ni wanyama wenye manyoya laini, wenye nguvu, na viumbe wa kuvutia. Ngozi ya manjano na nyeupe-kijivu na madoa meusi ya duma huwa kama ufiche mzuri ambao huwafanya wanyama hawa wasionekane wanapokuwa wakiwinda mawindo yao kwenye nyasi za Kiafrika.
Katika njia sawa na hiyo, mawazo na vitendo vyenye hatari kiroho mara nyingi vinaweza kuonekana kuwa vya kupendeza, vya kutamanika, au vya kufurahisha. Kwa hivyo, katika ulimwengu wetu wa kisasa, kila mmoja wetu anahitaji kujihadhari na ulaghai mbaya ambao hujifanya kuwa mzuri. Kama vile Isaya alivyoonya, “Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu!”1
Katika kipindi cha kukanganya wakati ukiukwaji wa utakatifu wa maisha ya mwanadamu unadhihirishwa kama haki na machafuko yanaelezewa kama uhuru, ni jinsi gani tumebarikiwa kuishi katika kipindi hiki cha siku za mwisho wakati nuru ya injili iliyorejeshwa inaweza kuangaza kwa mng’aro katika maisha yetu na kutusaidia kutambua udanganyifu wa giza na vivuta mawazo vya adui.
“Kwani wale walio na hekima na kupokea ukweli, na kumchukua Roho Mtakatifu kuwa kiongozi wao, na hawajadanganyika—amini ninawaambia, hawatakatiliwa chini na kutupwa katika moto, bali watastahimili siku ile.”2
Somo # 2—Kaa Macho na Chukua Tahadhari
Kwa paa, muda mfupi wa kutokujali au kutokuwa wasikivu kunaweza kukaribisha shambulio la haraka kutoka kwa duma. Vivyo hivyo, hali ya kuridhika na kuwa wa kawaida kiroho hutufanya tuwe hatarini kwenye kurubuniwa na adui. Kutofikiria kiroho kunaleta hatari kubwa katika maisha yetu.
Nefi alieleza jinsi katika siku za mwisho Shetani atakavyojaribu kuwalaghai watoto wa Mungu kwenye hisia za uongo za “usalama wa kimwili, kwamba watasema: Yote yako salama Sayuni; ndio, Sayuni inafanikiwa, yote ni mema—na hivyo ibilisi anadanganya roho zao, na kuwapeleka kwa makini hadi jahanamu.”3
Uangalifu endelevu unahitajika ili kukabiliana na hali ya kuridhika na kuwa wa kawaida. Kuwa macho ni hali au tendo la kutazama kwa uangalifu hatari au magumu yanazowezekana. Na kutazama kunamaanisha kitendo cha kuwa macho ili kuchunga na kulinda. Katika muktadha wa kiroho, tunahitaji kuwa macho na kuwa makini kwa misukumo ya Roho Mtakatifu na ishara ambazo zinakuja kutoka kwa walinzi wa Bwana juu ya minara.4
“Ndio, na pia nawasihi … kwamba muwe waangalifu ndani ya sala bila kikomo, ili msipotezwe na majaribio ya ibilisi, … kwani tazama, hakupatii zawadi ya kitu kizuri.”5
Kufokasi maisha yetu ndani ya Mwokozi na kwa Mwokozi na injili Yake kunatuwezesha kushinda mazoea ya mwanadamu wa tabia ya asili ya kusinzia na kuwa mzembe kiroho. Wakati tumebarikiwa kwa macho ya kuona na masikio ya kusikia,6 Roho Mtakatifu anaweza kuongeza uwezo wetu wa kutazama na kusikiliza wakati tunapoweza kuwa tunadhani hatuhitaji kutazama au kusikiliza au wakati hatudhani chochote kinaweza kuonekana au kusikika.
“Kesheni basi, ili muweze kuwa tayari.”7
Somo # 3—Elewa nia ya Adui
Duma ni mla wanyama ambaye kwa asili anawinda wanyama wengine. Siku nzima, kila siku, duma ni mla wanyama.
Shetani ni “adui wa haki na wale wanaotafuta kutii mapenzi ya Mungu.”8 Siku nzima, kila siku, kusudi na dhumuni lake pekee ni kuwafanya wana na binti za Mungu wenye huzuni kama yeye alivyo.9
Mpango wa furaha wa Baba umeundwa kutoa mwelekeo kwa watoto Wake, kuwasaidia kupata uzoefu wa furaha ya kudumu, na kuwaleta nyumbani salama wakiwa na miili iliyofufuliwa, iliyoinuliwa. Shetani anafanya kazi kuwafanya wana na binti za Mungu kukanganyikiwa na kutokuwa na furaha na kuzuia maendeleo yao ya milele. Adui hufanya kazi bila kuchoka kushambulia vipengele vya mpango wa Baba ambao anauchukia mno.
Shetani hana mwili, na maendeleo yake ya milele yamezuiliwa. Kama vile maji yanayotiririka kwenye mto yanavyozuiliwa na bwawa, vivyo hivyo maendeleo ya milele ya adui yanazuiwa kwa sababu yeye hana mwili. Kwa sababu ya uasi wake, Lusiferi amejizuilia mwenyewe baraka zote za kibinadamu na uzoefu uliowezeshwa kupitia mwili wa nyama na mifupa. Mojawapo ya maana zenye nguvu za kimaandiko za neno aliyelaaniwa inaoneshwa katika kutokuwa kwake na uwezo wa kuendelea kukua na kuwa kama Baba yetu wa Mbinguni.
Kwa sababu mwili ni muhimu sana katika mpango wa furaha wa Baba na maendeleo yetu ya kiroho, Lusiferi anatafuta kuharibu maendeleo yetu kwa kutujaribu tutumie miili yetu vibaya. Rais Russell M. Nelson amefundisha kwamba usalama wa kiroho hatimaye upo katika “‘kutochukua kamwe hatua ya kwanza ya ushawishi wa kwenda mahali ambapo haupaswi kwenda na kufanya kile ambacho haupaswi kufanya.’ … Kama binadamu sisi sote tuna matamanio ya [kimwili] ambayo ni ya lazima kwa maisha yetu. ‘Matamanio haya ni muhimu kabisa kwenye mwendelezo wa maisha. Kwa hivyo, Adui anafanya nini? … Anatushambulia kupitia matamanio yetu. Anatujaribu kula vitu ambavyo hatupaswi kula, kunywa vitu ambavyo hatupaswi kunywa, na kupenda kama ambavyo hatupaswi kupenda!’”10
Mojawapo ya kejeli kuu za umilele ni kwamba adui, ambaye ana huzuni kwa sababu hana mwili, anatualika na kutushawishi tushiriki katika huzuni yake kupitia utumiaji mbaya wa miili yetu. Nyenzo hasa ambayo yeye hana na hawezi kuitumia ndiyo shabaha ya msingi ya majaribio yake ya kututega kwenye maangamizo kimwili na kiroho.
Kuelewa nia ya adui ni muhimu kwa matayarisho mazuri kwa ajili ya mashambulio yanayowezekana.11 Hasa kwa sababu Kapteni Moroni alijua nia ya Walamani, alikuwa amejiandaa kukutana nao wakati wa ujio wao na alikuwa mshindi.12 Na kanuni hiyo hiyo na ahadi hiyo inatumika kwa kila mmoja wetu.
“Kama mmejitayarisha hamtaogopa.”
“Na hivyo muweze kuiepuka nguvu ya adui.”13
Mwaliko, Ahadi na Ushuhuda
Kama vile masomo muhimu yanavyoweza kupatikana kwa kuchunguza tabia ya duma na paa, vivyo hivyo kila mmoja wetu anapaswa kutafuta masomo na maonyo yanayopatikana katika matukio rahisi ya maisha ya kila siku. Tunapotafuta akili na moyo ulio wazi kwa ajili ya kupokea mwongozo wa mbinguni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, ndipo baadhi ya maagizo makubwa zaidi ambayo tunaweza kupokea na maonyo mengi yenye nguvu ambayo yanaweza kutulinda yatatokana na uzoefu wetu wa kawaida. Mifano yenye nguvu ipo ndani ya maandiko na katika maisha yetu ya kila siku.
Nimeangazia masomo matatu tu kati ya mengi ambayo yanaweza kutambuliwa katika tukio ambalo mimi na Susan tulipata huko Afrika. Ninawaalika na kuwahimiza mtafakari juu ya kisa hiki cha duma na paa na mtambue masomo ya ziada kwa ajili yenu na familia zenu. Tafadhali kumbukeni daima kwamba nyumbani kwenu ndiyo kituo cha kweli cha kujifunza na kuishi injili.
Mnapoitikia kwa imani mwaliko huu, mawazo yenye uvuvio yatakuja kwenye akili yenu, hisia za kiroho zitavimba katika moyo wenu, na mtatambua matendo ambayo hayana budi kufanywa au kuendelezwa ili kwamba muweze “kujitwalia deraya zote [za Mungu], mpate kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, muweze kusimama.”14
Ninaahidi kwamba baraka za matayarisho mazuri na kinga ya kiroho vitatiririka maishani mwenu mnapokuwa waangalifu kwenye sala kwa umakini na bila kukoma.
Ninashuhudia kwamba kusonga mbele kwenye njia ya agano kunatoa usalama wa kiroho na kunaalika furaha ya kudumu kwenye maisha yetu. Na ninatoa ushahidi kwamba Mwokozi aliyefufuka na aliye hai atatuidhinisha na kutuimarisha katika nyakati nzuri na mbaya. Juu ya kweli hizi ninashuhudia katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.