Usinidanganye
Tunapotii amri za Mungu, daima tutaongozwa katika njia sahihi na hatutadanganywa.
Leo, ninatoa maneno ya ushauri kwa kila mmoja, lakini hasa kwenu kizazi kinachochipukia—Watoto wa Msingi, wavulana, na wasichana. Mnapendwa kwa dhati na nabii wa Bwana katika siku yetu, Rais Russell M. Nelson—zaidi kiasi kwamba alizungumza na wengi wenu mwaka uliopita katika matangazo ya ibada maalumu ya vijana ulimwenguni kote yenye kichwa cha habari “Tumaini la Israeli.”1 Mara nyingi huwa tunamsikia Rais Nelson akiwaita hivyo kwa ufasaha kabisa—“tumaini la Israeli,” kizazi kinachochipukia na nguvu ya siku zijazo ya Kanisa lililorejeshwa la Yesu Kristo.
Rafiki zangu wadogo, ningependa kuanza kwa kushiriki hadithi mbili za familia.
Dalmatia 102
Miaka mingi iliyopita, nilifika nyumbani baada ya kazi na nilishtuka kuona rangi nyeupe ikiwa imetapakaa kila mahali—kwenye sakafu, kwenye mlango wa gereji, na kwenye nyumba yetu ya matofali mekundu. Nilikagua sehemu ya tukio kwa ukaribu na nikagundua rangi ilikuwa haijakauka. Mkondo wa rangi uliongoza kuelekea upande wa nyuma wa ua na kwa hivyo niliufuata. Huko, nilimkuta mwanangu wa miaka mitano akiwa na brashi ya kupakia rangi mkononi mwake, akimkimbiza mbwa wetu. Labrado wetu mzuri mweusi alikuwa amepakazwa rangi nusu ya mwili wake!
“Unafanya nini?” Niliuliza kwa sauti yenye shauku.
Mwanangu alisita, akanitazama, akamtazama mbwa, akaitazama brashi ya kupakia rangi iliyokuwa ikidondosha rangi, na kusema, “Nataka tu mbwa aonekane kama wale mbwa wenye madoadoa meusi kwenye sinema—unamfahamu, yule aliye na Dalmatia 101.”
Nilimpenda mbwa wetu. Nilidhani alikuwa mkamilifu, lakini siku hiyo mwanangu alikuwa na wazo tofauti.
Paka Mdogo Mwenye Milia
Hadithi yangu ya pili inajikita kumzunguka Mjomba Mkuu Grover aliyeishi katika nyumba iliyojitenga, mbali na mji. Mjomba Gover alikuwa anaendelea kuzee sana. Tulifikiria wana wetu walipaswa kukutana naye kabla hajaaga dunia. Kwa hivyo, alasiri moja, tulifanya safari ndefu kwenda nyumbani kwake. Tuliketi pamoja kuzungumza naye na kumtambulisha kwa wana wetu. Si muda mrefu katika mazungumzo, wavulana wetu wawili wadogo, labda miaka mitano na sita, walitaka kwenda nje kucheza.
Mjomba Grover, aliposikia ombi lao, aliinama na uso wake ukaangaliana na nyuso zao. Uso wake ulikuwa umezeeka sana na mgeni kiasi kwamba wavulana walimuogopa kidogo. Aliwaambia, kwa sauti yake ya kizee, “Muwe waangalifu—kuna vicheche wengi huko nje.” Tuliposikia hili, mimi na Lesa tulishtuka sana; tulikuwa na wasiwasi kuwa wangedhuriwa na kicheche! Wavulana punde walienda nje kucheza wakati sisi tukiendelea na mazungumzo.
Baadaye, wakati tulipoingia ndani ya gari kwenda nyumbani, niliwauliza wavulana, “Mliona kicheche?” Mmoja wao alijibu, “Hapana, hatukumwona kicheche yoyote, lakini tulimuona paka mdogo mweusi aliyekuwa na mstari mweupe mgongoni mwake!”
Mdanganyifu Mkuu
Hadithi hizi kuhusu watoto wasio na hatia wakigundua kitu fulani kuhusu maisha na uhalisia zinaweza kumfanya kila mmoja wetu atabasamu, lakini pia zinaelezea dhana yenye maana zaidi.
Katika hadithi ya kwanza, mwana wetu mdogo alikuwa na mbwa mzuri kama mnyama kipenzi; licha ya hilo, alichukua kopo la rangi na, akiwa na brashi ya kupakia rangi mkononi, alikusudia kubuni uhalisia wake mwenyewe wa kufikirika.
Katika simulizi ya pili, wavulana walikuwa na furaha wasijue hatari fidhuli iliyowakabili kutokana na kicheche. Kwa kutoweza kutambua vizuri kile hasa walichokuwa wamekabiliana nacho, walikuwa kwenye hatari ya kuteseka baadhi ya matokeo ya bahati mbaya. Hizi ni hadithi za utambulisho wa kimakosa—kudhania kitu halisi kuwa kitu tofauti. Katika kila tukio, matokeo yalikuwa madogo.
Hata hivyo, wengi leo wanapambana na maswala kama haya kwa kiwango kikubwa. Ama wanashindwa kuona vitu namna vilivyo kihalisia au hawatosheki na ukweli. Zaidi ya hayo, kuna nguvu zinazohusika leo zilizokusudiwa kutuongoza kwa makusudi mbali na ukweli halisi. Udanganyifu na uongo huu unaenda zaidi ya utambulisho wa kimakosa usio na hatia na mara nyingi huwa na matokeo mabaya, si madogo.
Shetani, baba wa uongo na mdanganyifu mkuu, atatutaka tushuku vitu kama vilivyo kiuhalisia na ama tupuuzie kweli za milele au kuzibadili kwa kitu ambacho kinaonekana cha kufurahisha zaidi. “Yeye hufanya vita na watakatifu wa Mungu”2 na ametumia milenia nyingi akifikiria na kufanyia mazoezi uwezo wa kuwashawishi watoto wa Mungu ili waamini kwamba wema ni uovu na uovu ni wema.
Amejiwekea sifa yake mwenyewe ya kuwasadikisha wanadamu kwamba vicheche ni watoto wa paka tu au kwamba, kwa kupaka rangi, unaweza kumbadili Labrado kuwa Dalmatia!
Hebu sasa tutazame mfano wa kanuni hii hasa inayopatikana katika maandiko, wakati Musa nabii wa Bwana alipokutana uso-kwa-uso na hali sawa na hii. “Musa alikuwa amenyakuliwa juu katika mlima mrefu[;] … naye akamwona Mungu uso kwa uso, na akaongea naye.”3 Mungu alimfundisha Musa kuhusu utambulisho wake wa milele. Ingawa Musa alikuwa mwanadamu na si mkamilifu, Mungu alifundisha kwamba Musa alikuwa “mfano wa Mwanangu wa Pekee; na Mwanangu wa Pekee … atakuwa Mwokozi.”4
Kwa ufupi, katika ono hili la ajabu, Musa alimuona Mungu, na pia alijifunza kitu muhimu juu yake mwenyewe:, alikuwa hakika mwana wa Mungu.
Sikiliza kwa makini kile kilichotokea wakati ono hili la ajabu lilipofunga. “Na ikawa kwamba … Shetani akaja kumjaribu,” akisema, “Musa, mwana wa mtu, niabudu mimi!”5 Musa kwa ujasiri akamjibu: “Wewe ni nani? Kwa maana tazama, mimi ni mwana wa Mungu, katika mfano wa Mwanawe wa Pekee; na u wapi utukufu wako, hata nipate kukuabudu?”6
Kwa maneno mengine, Musa alisema: “Huwezi kunidanganya mimi, kwa maana najua mimi ni nani. Niliumbwa kwa mfano wa Mungu. Huna nuru na utukufu Wake. Kwa hivyo kwa nini nikuabudu wewe au ninaswe na udanganyifu wako?”
Sasa sikiliza kwa makini jinsi Musa anavyoendelea kujibu. Anasema, “Nenda zako, Shetani; usinidanganye.”7
Kuna mengi tunayoweza kujifunza kutokana na jibu la Musa lenye nguvu kwa majaribu kutoka kwa adui. Ninawaalika mjibu kwa njia sawa na hiyo wakati mnapohisi kushawishiwa na majaribu. Muamuru adui wa nafsi yako kwa kusema, “Ondoka! Wewe huna utukufu. Usinijaribu au kunidanganya! Kwa maana najua mimi ni mwana wa Mungu. Na daima nitamlilia Mungu wangu kwa ajili ya msaada Wake.”
Adui, hata hivyo, haachi kwa urahisi nia zake za kuangamiza katika kutudanganya na kutufanya kuwa duni. Bila shaka hakufanya hivyo kwa Musa, badala yake alitaka kumsababisha Musa kusahau yeye alikuwa nani milele.
Utadhani alikuwa na ghadhabu ya kitoto, “Shetani alilia kwa sauti kubwa, na kujitapa juu ya nchi, na kuamuru, akisema: Mimi ndiye Mwana wa Pekee, niabudu mimi.”8
Acha tufanye mapitio. Je, umesikia kile alichosema? “Mimi ndiye Mwana wa Pekee. Niabudu mimi!”
Muongo mkuu alisema, kwa kweli, “usiogope; sitakudhuru—mimi siyo kicheche; mimi ni mtoto tu wa paka mwenye rangi nyeusi na nyeupe nisiye na hatia.”
Musa kisha akamlingana Mungu na kupokea nguvu Zake takatifu. Ingawa adui alitetemeka na nchi kutingishika, Musa hakukubali kushindwa. Sauti yake ilikuwa imara na dhahiri. “Ondoka kwangu, Shetani,” alisema “kwa maana ni Mungu huyu mmoja tu nitakayemwabudu, ambaye ndiye Mungu wa utukufu.”9
Hatimaye, “akaondoka … kutoka katika uwepo wa Musa.”10
Baada ya Bwana kujidhihirisha na kumbariki Musa kwa ajili ya utiifu wake, Bwana alisema:
“Heri wewe, Musa, kwa maana … nawe utafanywa kuwa mwenye nguvu kushinda maji mengi. …
“Na lo, Mimi nipo pamoja nawe, hata mwisho wa siku zako.”11
Ushindi wa Musa dhidi ya adui ni mfano dhahiri na wa kuelimisha kwa kila mmoja wetu, bila kujali hatua yetu katika maisha. Ni ujumbe wenye nguvu kwa ajili yako binafsi—ili uweze kujua cha kufanya wakati anapojaribu kukudanganya. Kwani wewe, kama Musa, umebarikiwa na karama ya usaidizi wa mbinguni.
Amri na Baraka
Ni jinsi gani unaweza kupata usaidizi huu wa mbinguni, na usidanganywe au kukubali kushindwa na majaribu? Njia dhahiri kwa ajili ya msaada mtakatifu ilisisitizwa tena katika kipindi hiki na Bwana mwenyewe wakati aliposema: “Hivyo basi, mimi Bwana, nikijua majanga yajayo juu ya wakazi wa dunia, nimemwita mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, na kusema naye kutoka mbinguni, na nikampa yeye amri.”12 Tukitumia maneno rahisi, tunaweza kusema kwamba, Bwana, anayejua “mwisho kutoka mwanzo,”13 anajua changamoto za kipekee katika siku yetu. Kwa hivyo, Yeye ametayarisha njia kwa ajili yetu ili kushinda changamoto na majaribu, mengi ambayo huja kama matokeo ya moja kwa moja ya ushawishi wa udanganyifu wa adui na mashambulizi yake.
Njia hiyo ni rahisi. Kupitia watumishi Wake, Mungu huzungumza nasi, watoto Wake, na kutupatia amri. Tunaweza kutamka upya mstari huo niliounukuu na kusema, “Mimi, Bwana … nimemwita mtumishi wangu [Rais Russell M. Nelson], na kusema naye kutoka mbinguni, na nikampa yeye amri.” Je, huo si ukweli mtukufu?
Ninashuhudia kwa dhati kwamba Bwana kwa uhalisia wote alizungumza na Joseph Smith kutoka mbinguni, akianza na Ono kuu la Kwanza. Yeye pia anazungumza na Rais Nelson katika wakati wetu. Ninashuhudia kwamba Mungu alizungumza na manabii katika enzi zilizopita na kuwapa amri zilizokusudiwa kuwaongoza watoto Wake kwenye furaha katika maisha haya na utukufu katika maisha yajayo.
Mungu anaendelea kutoa amri kwa nabii wetu aliye hai leo hii. Mifano ni mingi—usawa katika maelekezo ya injili yanayolenga nyumbani, yanayosaidiwa na Kanisa; kubadilishwa kwa ualimu wa nyumbani na wa kutembelea kuwa kuhudumu; marekebisho kwenye kanuni na ibada za hekaluni; na programu mpya ya Watoto na Vijana. Ninashangazwa na wema na huruma ya Baba mpendwa wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, ambao walirejesha Kanisa la Mwokozi duniani kwa mara nyingine na kumwita nabii katika siku yetu. Urejesho wa injili ya Yesu Kristo unasawazisha nyakati za hatari kwa utimilifu wa nyakati.
Uovu Kamwe Haujapata Kuwa Furaha
Utiifu kwa amri zilizotolewa kwa nabii wetu ni muhimu si tu katika kuepuka ushawishi wa mdanganyifu lakini pia katika kupata shangwe na furaha ya kudumu. Fomyula hii takatifu ni rahisi sana: haki, au utiifu kwa amri, huleta baraka, na baraka huleta furaha, au shangwe, katika maisha yetu.
Hata hivyo, kwa njia sawa na ile ambayo adui alijaribu kumdanganya Musa, anatafuta kukudanganya wewe. Siku zote amejifanya kuwa kitu ambacho sicho. Siku zote anajaribu kuficha uhalisia wake. Anadai kwamba utiifu utafanya maisha yako yawe yenye huzuni na kwamba utakunyima furaha.
Je, unaweza kufikiria kuhusu baadhi ya mbinu zake za kudanganya? Kwa mfano, yeye hutoa maelezo pungufu ya madhara haribifu ya madawa ya kulevya au unywaji pombe na badala yake hupendekeza kwamba itakuletea raha. Anatuzamisha ndani ya vitu hasi ambavyo vinaweza kupatikana katika mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na milinganisho ya kudhoofisha na uhalisia usio wa kweli. Kwa kuongezea, anaficha maudhui ya kudhuru yanayopatikana mtandaoni, kama vile pornografia, mashambulizi dhahiri dhidi ya wengine kupitia udhalimu wa mtandaoni, na kusambaza habari zisizo za kweli ili kusababisha wasiwasi na hofu katika mioyo na akili zetu. Kwa ujanja ananong’ona, “Nifuate tu, na hakika utakuwa na furaha.”
Maneno yaliyoandikwa karne nyingi zilizopita na nabii wa Kitabu cha Mormoni yanafaa hasa kwa siku yetu: “Uovu kamwe haujapata kuwa furaha.”14 Na tuweze kutambua udanganyifu wa Shetani vile jinsi ulivyo. Na tuweze kustahimili na kuutambua uongo na ushawishi wa yule anayetafuta kuangamiza nafsi zetu na kuiba furaha yetu ya wakati huu na utukufu wetu wa siku za baadaye.
Wapendwa akina kaka na dada zangu, ni lazima tuendelee kuwa waaminifu na waangalifu, kwa maana hiyo ndiyo njia pekee ya kutambua ukweli na kusikia sauti ya Bwana kupitia watumishi Wake. “Kwani Roho huzungumza ukweli wala sio uwongo. … Vitu hivi vimedhihirishiwa wazi wazi kwetu, kwa wokovu wa nafsi zetu. … Kwani Mungu alivizungumza pia kwa manabii wa kale.”15 Sisi ni Watakatifu wa Mwenyezi Mungu, tumaini la Israeli! Je, Tutasita? Je, “Tutaona haya au kukimbia vita? La! … Kwa amri ya Mungu, nafsi, moyo, na mkono, waaminifu na wakweli daima tutakuwa.”16
Ninatoa ushahidi wangu juu ya Mtakatifu wa Israeli—hata jina la Yesu Kristo. Ninashuhudia juu ya upendo Wake wa kudumu, ukweli, na shangwe ambayo inawezeshwa na dhabihu Yake ambayo haina mwisho na ni ya miele. Tunapotii amri Zake, daima tutaongozwa katika njia sahihi na hatutadanganywa. Katika jina takatifu la Mwokozi wetu, Yesu Kristo, amina.