2010–2019
Mashahidi, Akidi za Ukuhani wa Haruni, na Madarasa ya Wasichana
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


2:3

Mashahidi, Akidi za Ukuhani wa Haruni, na Madarasa ya Wasichana

Marekebisho ambayo tutatangaza sasa yamekusudiwa kuwasaidia wavulana na wasichana kukuza uwezo wao mtakatifu kibinafsi.

Wapendwa akina kaka na akina dada, ni furaha kubwa kuwa nanyi tena katika mkutano mkuu. Mapema wiki hii, matangazo yalifanywa kwa waumini wa Kanisa kuhusu mabadiliko katika sera kuhusu nani wanaweza kuwa mashahidi katika ibada za ubatizo na kuunganisha. Ningependa kusisitiza hoja hizo tatu.

  1. Ubatizo kwa niaba ya mtu aliyekufa unaweza kushuhudiwa na mtu yeyote aliye na kibali cha sasa cha hekaluni, ikijumuisha kibali chenye ukomo wa matumizi.

  2. Muumini yeyote aliyepokea endaumenti na aliye na kibali cha sasa cha hekaluni anaweza kutumika kama shahidi katika ibada za kuunganisha, za walio hai na kwa niaba ya wafu.

  3. Muumini yeyote wa Kanisa aliyebatizwa anaweza kutumika kama shahidi wa ubatizo wa mtu aliye hai. Mabadiliko haya yanahusu ubatizo wote nje ya hekalu.

Marekebisho haya ya sera ni ya kiutaratibu. Mafundisho na maagano ya msingi hayajabadilika. Yamewekwa sawa kuleta matokeo yanayohitajika katika ibada zote. Mabadiliko haya yanafaa kuongeza zaidi ushiriki wa familia katika ibada hizi.

Pia nilitaka kuzungumza nanyi kwa wakati huu kuwasilisha marekebisho ambayo yanahusu vijana wetu na viongozi wao.

Mtakumbuka kwamba nimewaalika vijana wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wajiandikishe katika jeshi la vijana la Bwana ili washiriki katika lengo kuu ulimwenguni leo—kuikusanya Israeli.1 Nilitoa mwaliko huu kwa vijana wetu kwa sababu wamebarikiwa kwa njia ya ajabu katika kuwafikia wengine na kushiriki kile wanachokiamini katika mtindo wa kusadikisha. Lengo la kukusanya ni sehemu muhimu ya kusaidia kuuandaa ulimwengu na watu wake kwa Ujio wa Pili wa Bwana.

Katika kila kata, jeshi la vijana la Bwana linaongozwa na askofu, mtumishi wa Mungu mwenye kujitolea. Wajibu wake wa kwanza kabisa ni kuwatunza wavulana na wasichana katika kata yake. Askofu na washauri wake wanaiongoza kazi ya akidi za Ukuhani wa Haruni na madarasa ya Wasichana katika kata.

Marekebisho ambayo tutatangaza sasa yamekusudiwa kuwasaidia wavulana na wasichana kukuza uwezo wao mtakatifu kibinafsi. Tunataka pia kuimarisha akidi za Ukuhani wa Haruni na madarasa ya Wasichana na kutoa msaada kwa maaskofu na viongozi wengine wakubwa wakati wanapokitumikia kizazi kinachochipukia.

Mzee Quentin L. Cook sasa ataelezea marekebisho yanayowahusu wavulana. Na jioni ya leo, katika kikao kikuu cha wanawake, Dada Bonnie H.Cordon, Rais Mkuu wa Wasichana, ataelezea marekebisho yanayohusu wasichana.

Urais wa Kwanza na wale Kumi na Wawili wameungana katika kuidhinisha juhudi hizi za kuwaimarisha vijana wetu. Oo, ni jinsi gani tunavyowapenda na kuwaombea! Wao ni “Tumaini la Israeli, jeshi la Sayuni, watoto wa siku iliyoahidiwa.”2 Tunaelezea ujasiri wetu mkamilifu katika vijana wetu na shukrani zetu kwa ajili yao. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli” (ibada ya vijana ulimwenguni kote , Juni 3, 2018), HopeofIsrael.ChurchofJesusChrist.org.

  2. “Hope of Israel,” Nyimbo za Kanisa, na. 259.