2010–2019
Basi Ninyi Mtakuwa Wakamilifu—Hatimaye
Oktoba 2017


2:3

Basi Ninyi Muwe Wakamilifu—Hatimaye

Ikiwa tutastahamili, kisha mahali fulani katika milele kustakaswa kwetu kutatimia na kukamilika.

Maandiko yaliandikwa kutubariki na kutuhimiza, na kwa kweli yanafanya hivyo. Tunatoa shukrani mbinguni kwa kila sura na aya ambayo tumepewa. Lakini umegundua ya kwamba mara kwa mara kifungu fulani kitaonekana ambacho hutukumbusha ya kwamba tunapungukiwa? Kwa mfano, Mahubiri juu ya Mlima yanaanza kwa hali za heri za kutuliza, lakini katika aya zinazofuata, tunaambiwa—miongoni mwa mengine—sio tu kwamba tusiue lakini hata tusikasirike. Tunaambiwa tusitende uzinzi lakini pia hata tusiwe na mawazo machafu. Kwa wale ambao wataitisha, tunapaswa kuwapa koti letu na kisha nguo yetu pia. Tunapaswa kuwapenda maadui wetu, kuwabariki wale wanaotulaani, na kuwatendea mema watuchukio.1

Ikiwa hayo ndiyo masomo yako ya asubuhi ya maandiko, na baada ya kusoma kufikia hapa tu una uhakika ya kwamba hautapata alama nzuri kwenye ripoti yako ya injili, amri ya mwisho katika mfululizo huo ni hakika utamaliza kazi: “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, Kama Baba yenu, … wa mbinguni alivyo mkamilifu.”2 Kwa sharti hili la mwisho, tunataka kurudi kitandani na tujifunike hata kwa kichwa. Malengo kama haya ya selestia yanaonekana kutushinda. Lakini hakika Bwana hawezi kutupatia amri Anayojua kwamba tutashindwa kuitii. Hebu tuone ni wapi utata huu utatufikisha.

Kanisani ninawasikia wengi ambao wanapambana na swala hili: “Mimi sio mstahiki vya kutosha.” “Nimepungukiwa mno.” “Kamwe sitaweza kutosha.” Mimi husikia haya kutoka kwa vijana. Mimi husikia haya kutoka kwa wamisionari. Mimi husikia haya kutoka kwa waumini wapya. Mimi husikia haya kutoka kwa waumini wa muda mrefu. Kama dada mmoja Mtakatifu wa Siku za Mwisho mwenye umaizi, Dada Darla Isackson, alisema, kwamba Shetani kwa namna fulani ameweza kufanya amri na maagizo kuonekana kama laana na lawama. Kwa wengine amegeuza maadili na misukumo ya injili kuwa kujichukia mwenyewe na kuleta dhiki.3

Kile ambacho nitasema sasa hakikani wala kupunguza amri yoyote Mungu amewahi kutupatia sisi.Ninaamini katika ukamilifu Wake, na ninajua sisi ni wana na mabinti Wake wa kiroho na tunao uwezekano wa kuwa kama Yeye alivyo. Pia ninajua ya kwamba, kama watoto wa Mungu, hatupaswi kujidhalilisha au kujikashifu, kama kwamba tunajiadhibu kwa njia fulani itatufanya tuwe yule mtu ambaye Mungu anataka tuwe. Hapana! Tukiwa na utayari wa kutubu na hamu ya kuzidisha haki katika mioyo yetu daima, natumaini kuwa tungeweza kutafuta kujiboresha katika njia ambayo haitusababishi kuathiriwa na vidonda vya tumboni au kukosa hamu ya chakula, kuwa na huzuni au kuharibu heshima yetu. Hiki sicho kile ambacho Bwana anawatakia watoto wa Msingi au mtu yeyote yule ambaye kwa uaminifu huimba, “Mimi ninajaribu kuwa kama Yesu.”4

Kuliweka swala hili kwenye muktadha, naweza kutukumbusha sisi sote kwamba tunaishi katika dunia iliyoanguka na kwa wakati huu sisi ni watu tulioanguka. Tuko katika ufalme wa telestia; inayoandikwa kwa herufi t, sio s. Kama Rais Russell M. Nelson alivyofundisha katika maisha ya sasa hivi ukamilifu ungali “haujakamilika.”5

Kwani ninaamini kwamba Yesu hakudhamiria mahubiri Yake juu ya mada hii kuwa nyundo ya maneno ya kutuponda sisi kuhusu mapungufu yetu. La, ninamini Yeye alidhamiria iwe kutukuza Mungu Baba wa Milele ni nani na nini na kile tunaweza kupokea pamoja Naye milele. Hata hivyo, nina shukrani kujua kwamba licha ya mapungufu yangu, angalau Mungu ni kamili—kwamba angalau Yeye, kwa mfano, anaweza kuwapenda maadui Zake, kwa sababu mara nyingi, kwa ajili ya “mwanadamu wa kawaida”6 na mwanamke aliye ndani yetu, mimi na wewe mara nyingine tunakuwa huyo adui. Ninayo shukrani kwamba angalau Mungu anaweza kuwabariki wale ambao humtumia Yeye vibaya kwa sababu, bila ya kutaka kufanya hivyo, sisi sote humtumia Yeye vibaya mara nyingine. Ninashukuru ya kwamba Mungu ni mwenye rehema na mpatanishi kwa sababu ninahitaji rehema na ulimwengu unahitaji amani. Bila shaka, yote tunayosema kuhusu wema wa Baba pia tunayasema kumhusu Mwanawe Pekee, ambaye aliishi na kufariki kwa ukamilifu huo huo.

Ninaharakisha kusema ya kwamba kuangazia mafanikio ya Baba na Mwana badala ya kufeli kwetu hakutatupa haki hata kidogo kwa maisha yenye kukosa nidhamu au kushusha viwango gezo vyetu. Hapana, kutoka mwanzoni injili imekuwa “kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, … Hata na sisi sote … tutakapoufikia … mtu kamili, hata cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.”7 Ninapendekeza tu angalau lengo moja la maandiko au amri inayoweza kutukumbusha ukuu wa kimo cha utimilifu wa Kristo8 ulivyo mtakatifu, kutia msukumo na upendo mkubwa zaidi na uvutiwaji Kwake na hamu kubwa zaidi kuwa kama Yeye.

“Ndio, mje kwa Kristo na Mkamilishwe Ndani Yake… ,” Moroni anasihi. “Na mpende Mungu na mioyo yenu, akili na nguvu zenu zote, basi … kwa neema yake mngekamilishwa katika Kristo.”9Tumaini letu la ukamilisho wa kweli ni kuupokea kama zawadi kutoka mbinguni—hatuwezi “kuipata kwa kazi.”Hivyo basi, neema ya Kristo hutupatia sio tu wokovu kutokana na huzuni na dhambi na mauti lakini pia wokovu kutokana na kuendelea kujikosoa.

Naomba nitumie mojawapo ya mafumbo ya Mwokozi kusema haya kwa njia tofauti kidogo. Mtumishi alidaiwa na mfalme wake idadi ya talanta 10,000. Akisikiliza mtumishi huyo akiombea subira na rehema, “bwana wa mtumwa yule akamhurumia, na … Akamsamehe … lile deni.” Lakini mtumishi yule yule alikataa kumsamehe mtumishi mwenzake ambaye aliyekuwa na deni lake la dinari 100. Aliposikia haya, mfalme alimlalamikia yule ambaye alikuwa amemsamehe, “Je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe?”10

Kunayo tofauti ya maoni miongoni mwa wasomi kuhusu thamani zilizotajwa hapa—sahamani kwa kutimia rejeo la hela za Kimarekani—lakini kurahisisha hesabu, ikiwa thamani ndogo, deni ambayo haikusamehewa dinari 100, tuseme, $100 kwa nyakati hizi, basi deni la talanta 10, 000 ambalo lilisamehewa bure laweza kuwa linakaribia $ bilioni 1—au zaidi.

Kama deni la kibinafsi, hiyo ni kiwango kubwa sana—kubwa kupita kuelewa kwetu. (Hakuna mtu awezaye kufanya manunuzi kiasi hicho!) Basi, kwa minajili ya fumbo hili,inapaswa kuwa zaidi ya uwezo wetu wa kuelewa; inapaswa kuwa zaidi ya uwezo wetu wa kufahamu, kuzungumzia chochote zaidi ya uwezo wetu wa kulipa.Hii ni kwa sababu hii sio simulizi kuhusu watumishi wawili wanaozozana katika Agano Jipya. Ni simulizi kutuhusu sisi, familia ya wanadamu iliyoanguka, wadaiwa katika maisha ya sasa, watenda hila, mahabusu wote. Kila mmoja wetu ni mdaiwa, hukumu ni kifungo kwa kila mmoja wetu. Na hapo ndipo sote tungebakia kama haingekuwa neema ya Mfalme ambaye anatuachilia huru kwa sababu anatupenda na “kusikia huruma kwa ajili yetu.”11

Yesu anatumia kipimo cha ajabu hapa kwa sababu Upatanisho Wake ni zawadi ya ajabu kupindukia iliyotolewa kwa gharama ambayo hatuwezi tukaelewa. Kwamba, inaonekana kwangu, angalau ni sehemu ya maana katika agizo la Yesu kuwa wakamilifu. Tunaweza kushindwa kuaonyesha ule ukamilifu wa talanta 10,000 Baba na Mwana wamefikia, lakini hio si kitu Kwao kuomba kwamba tuwe kidogo wa kiuungu katika vitu vidogo, kwamba tuseme na kutenda, kupenda, na kusamehe, kutubu, na kuboreka kwa angalau kiwango senti 100, ambacho ni wazi kiko katika uwezo wetu.

Kina ndugu na dada, isipokuwa Yesu, hakujakuwa na utendaji usio na makosa katika safari hii ya hapa duniani tunayofuata, kwa hivyo katika maisha ya duniani acha tutajitahidi kuboreka pasi kushikamana sana na kile ambacho wanasayansi wanaita “ukamilifu sumu.”12 Tunapaswa kuepukana na matarajio ya kuzidi kutuhusu sisi wenyewe, na wengine, na naweza kuongezea, wale wanaopewa miito ya kuhudumu Kanisani—ambayo kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho ina maana kila mtu, kwani wote tumeitwa kuhudumu mahali fulani.

Kuhusiana na hayo, Leo Tolstoy aliandika wakati mmoja kuhusu padri ambaye alikashifiwa na mmoja wa waumini wake kwa kukosa kuishi kwa uhakika jinsi alivyostahili, mkosoaji akiamua ya kwamba kanuni ambazo mhubiri mwenye makosa alifundisha lazima zilikuwa za kupotosha.

Katika kujibu ukosoaji huo, padri huyo anasema: “Tazama maisha yangu sasa na ulinganishe na yale ya awali. Utaona ya kwamba ninajaribu kuishi ukweli ninaohubiri.” Akiwa ameshindwa kuishi kulingana na maadili ya juu aliyofundisha, padri anakubali amefeli. Lakini analia:

“Nishambulie, [ukipenda] nimejiletea haya mwenyewe,” …“lakini [usishambulie] njia ninayoifuata. Ikiwa ninaifahamu njia ya kuelekea nyumbani [lakini] ninaifuata nikiwa mlevi, je, njia siyo sawa kwa sababu tu ninayumbayumba kutoka upande mmoja hadi mwingine? …

“… Usiseme kwa sauti kubwa na raha, ‘Hebu muangalie! … Muone anatambaa kwa kinamisi!’ La, usinichekelee, lakini toa … usaidizi wako [kwa yeyote anayejaribu kufuata njia inayoelekea tena kwa Mungu.]”13

Kina ndugu na kina dada, kila mmoja wetu anatamania kuishi zaidi maisha kama Kristo kuliko tunavyofanikiwa kuishi kila mara. Ikiwa tutakubali hayo kwa uaminifu na kujaribu kujiboresha, sisi sio wanafiki; sisi ni wanadamu. Na tuweze kukataa kuruhusu upuuzi wetu wa maisha ya sasa, na mapungufu yetu yasiyoepukika hata ya wale wanaume na wanawake bora walio karibu nasi, kutufanya wabeuzi kuhusu kweli za injili au tumaini la siku zijazo au uwezekano wa uungu wa kweli. Kama tukistamili, kisha mahali fulani katika milele utakaso wetu utatimizwa na kukamilishwa—ambayo ndio maana ya ukamilisho katika Agano Jipya.14

Ninashuhudia kwamba kudra kuu, inayopatikana kwetu kwa ajili ya Upatanisho wa Bwana Yesu Kristo, ambaye Yeye Mwenyewe aliendelea “kutoka neema hadi neema”15 mpaka akapokea katika kutokufa Kwake16 ukamilifu wa utimilifu wa utukufu wa selestia.17 Ninashuhudia ya kwamba wakati huu na kwa wakati wowote ule, Yeye akiwa na mikono yenye makovu ya misumari, anatuenezea neema ile ile, akitushikilia na kututia moyo, pasikutuachilia mpaka tufike salama nyumbani pamoja Naye katika kumbatio la Wazazi wa Mbinguni. Kwa siku kamili kama hiyo, nitaendelea kujitahidi, hata kwa unyonge. Kwa zawadi kama hiyo, nitaendelea kutoa shukrani, hata kama hazitoshi. Ninafanya hivyo katika lile jina la Ukalimifu lenyewe, la Yule ambaye hajawahi kuwa mzito au myonge lakini yule atupendae sisi wote tulivyo, hata Bwana Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Mathayo 5:1-47.

  2. Mathayo 5:48.

  3. Ona Darla Isackson, “Satan’s Counterfeit Gospel of Perfectionism,” Meridian Magazine, Juni1, 2016, ldsmag.com.

  4. “I’m Trying to Be Like Jesus,” Kitabu cha Watoto cha Wimbo, 78–79.

  5. Ona Russell M. Nelson, “Perfection Pending,” Ensign, Nov. 1995, 86–88.

  6. Mosia 3:19

  7. Waefeso 4:12–13.

  8. Waefeso 4:13.

  9. Moroni 10:32; imetiliwa mkazo.

  10. Ona Mathayo 18:24–33.

  11. Mafundisho na Maagano 121:4.

  12. Ona Joanna Benson na Lara Jackson, “Nobody’s Perfect: A Look at Toxic Perfectionism and Depression,” Millennial Star, Mar. 21, 2013, millennialstar.org.

  13. “The New Way,” Leo Tolstoy: Spiritual Writings (2006), 81–82.

  14. Kwa uchunguzi wa kuelimisha wa maana ya neno la Kituruki linalotumika katika Agano Jipya kumaanisha kamilifu (“teleios”), ona hotuba ya mkutano mkuu ya Rais Russell M. Nelson Oktoba 1995 “Perfection Pending” (Ensign, Nov. 1995, 86-87).

  15. Mafundisho na Maagano 93:13.

  16. Ona Luka 13:32.

  17. Ona Mafundisho na Maagano 93:13.