2010–2019
Je, Wakati wa Miujiza Umekoma?
Oktoba 2017


2:3

Je, Wakati wa Miujiza Umekoma?

Lengo letu kuu linapaswa kuwa ni kuhusu miujiza ya kiroho ambayo inapatikana kwa watoto wote wa Mungu.

Mwaka mmoja uliopita, nilipokuwa na jukumu katika jimbo la California, niliandamana na rais wa kigingi kuwatembelea Clark na Holly Fales na familia yao nyumbani kwao. Nilielezwa kuwa walikuwa hivi karibuni wameshuhudia muujiza. Tulipowasili, Clark alijitahidi kusimama na kutusalimia kwa vile alikuwa amevalia gango mgongoni, gango shingoni, na magango mikononi.

Zaidi tu ya miezi miwili iliyotangulia, Clark, mwanawe Ty, na karibu wavulana wengine 30 na viongozi walifunga safari ya kukwea kilele cha Mlima Shasta wenye urefu wa futi 14, 180 (mita 4, 322), mojawapo ya vilele vya urefu mkubwa zaidi kule California. Siku ya pili ya safari hiyo ngumu, wengi kati ya wakwezi hao walifika kileleni—mafanikio ya kusisimua ambayo yaliwezekana kwa sababu ya matayarisho ya miezi mingi.

Mtu mmoja kati ya watu wa kwanza kufika kileleni siku hiyo alikuwa Clark. Baada ya mapumziko kidogo karibu na pembeni mwa kilele, alisimama na kuanza kutembea. Alipokuwa akifanya hivyo, alijikwa na kuanguka nyuma pembeni mwa jabali, na kuanguka kwa kina cha futi 40 (12 m) na kisha kubingirika chini ya mteremko wenye barafu kwa futi zingine 300 (91 m). Ajabu ni kwamba, Clark alinusurika lakini yeye aliumia vibaya sana na kushindwa kusonga.

Miujiza ambayo Clark alishuhudia wakati wa tukio hili la maumivu mengi ilikuwa tu inaanza. Miongoni mwa watu wa kwanza kumfikia “ilitokea kuwa” kundi la wakwezi ilijumuisha viongozi waokoaji wa mlimani na wataalamu wa matibabu ya dharura. Mara moja walimtibu Clark mshtuko na kumpa vifaa vya kuuweka mwili wake uwe na joto. Kundi hili pia “ilitokea kuwa” walikuwa wakifanya majaribio ya kifaa kipya cha mawasiliano na wakatuma ombi la dharura la msaada kutoka eneo ambalo simu za mkono haziwezi kupata mawimbi. Helikopta ndogo ilitumwa mara moja kwenda Mlima Shasta kutoka umbali wa saa moja. Baada ya majaribio mawili hatari ya kutua na ambayo hayakufaulu kwenye mwinuko ambao ulikuwa umesukuma mbali na mipaka ya utenda kazi wa ndege hiyo, na ikipambana na upepo mkali sana, rubani alianza jaribio la tatu na la mwisho. Helikopta ilipokaribia kutoka kwa upande tofauti, “ilitokea kuwa” upepo ulibadilika na ndege hiyo iliweza kutua kwa muda wa kutosha tu kwa kundi hilo kumpenyeza Clark kwa uchungu kwenye chumba kidogo kichoko nyuma ya kiti cha rubani.

Wakati Clark alipotathminiwa katika kituo cha maumivu, uchunguzi ulidhihirisha kwamba alikuwa amevunjika kwenye sehemu kwenye shingo, mgongo, mbavu, na vifundo vya mikono; pafu lililotoboka; na mikwaruzo na michubuko ya ngozi. “Ilitokea kuwa” mpasuaji mashuhuri wa maumivu ya nyurolojia alikuwa kwenye zamu siku hiyo; yeye huwa katika hospitali hii mara chache tu katika mwaka. Baadaye daktari alisema ya kwamba hajawahi kuona mtu yeyote amepata majeraha makubwa kwenye uti wa mgongo na mishipa ya karotini na kusalia hai. Clark hakutarajiwa tu kuwa hai bali pia kurudi katika hali ya kawaida ya afya. Akijielezea kama agnostiki, mpasuaji alisema hali ya Clark iikuwa kinyume na mafunzo yake ya kisayansi kuhusu majeraha ya nyurolojia na inaweza tu kuelezewa kama muujiza.

Clark na Holly walipokuwa wakimalizia kusimulia tukio hili lenye mhemko, ilikuwa vigumu kwangu kuzungumza. Haikuwa tu kwa sababu ya miujiza iliyokuwa wazi, bali kwa sababu ya mkubwa zaidi. Nilikuwa na msukumo mkubwa sana—ushuhuda wa kiroho—kwamba Holly na kila mmoja ya watoto hao watano ambao waliketi sebuleni wakiwa wamewazingira wazazi wao wana imani kubwa kiasi cha kwamba wangekubali matokeo yoyote ambayo yangetokea siku ile na bado wangefanikiwa kiroho. Clark na Holly pamoja na watoto wao wakubwa wawili, Ty na Porter, wako nasi leo hii katika Kituo cha Mikutano.

Katika kutafakari tukio la familia ya Fales, nimefikiria sana kuhusu hali ya familia zingine nyingi mno. Iweje kuhusu Watakatifu wa Siku za Mwisho walio wengi mno walio na imani tele, wanaopokea baraka za ukuhani, wanaoombewa siku zote, wanaoweka maagizo, waliojawa na matumaini ambao miujiza yao kamwe haiji? Angalau katika njia ambayo wanaelewa muujiza. Angalau katika njia ambayo wengine wanaonekana kupokea miujiza.

Iweje kuhusu wale wanaoteseka kutokana na taabu kubwa—kimwili, kiakili, kimhemko—kwa miaka mingi au miongo mingi au kwa maisha yao yote? Iweje kuhusu wale wanaofariki wakiwa wadogo mno?

Miezi miwili tu iliyopita, wanandoa wawili walio na sifu za hekalu, walio na watoto watatu wanaohudumu misheni na watoto wengine watano baina yao, waliondoka kwenye ndege ndogo kwa safari fupi. Ninaamini ya kwamba walisali kwa ajili ya usalama wao kabla ya safari na wakasali kwa bidii wakati ndege yao ilipopata hitilafu mbaya za kimitambo kabla ya kuanguka. Hakuna aliyenusurika. Iweje juu yao?

Je, watu wazuri na wapendwa wao wana sababu ya kuuliza swali lililoulizwa na Mormoni: “Je, Wakatiwa Miujiza Umekoma?”1

Ufahamu wangu mdogo hauwezi kuelezea kwa nini mara nyingine kuna usaidizi wa kiungu na mara nyingine hakuna. Lakini pengine tunakosa kuelewa muujiza ni nini.

Mara nyingi sisi huelezea muujiza kama uponyaji bila maelezo kamili ya sayansi ya kimatibabu au kuepuka hatari ya kuangamiza kwa kutii msukumo dhahiri. Hata hivyo, unaweza kufafanua muujiza kama “tukio la manufaa lililoletwa kupitia uwezo mtukufu ambao wanadamu hawawezi kuelewa”2 inatoa mtazamo mpana zaidi kuhusu maswala ya milele kiasili. Ufafanuzi huu pia unaturuhusu kutafakari kazi muhimu ya imani katika kupokea muujiza.

Moroni alifundisha, “Na wala kwa muda wowote hakujawa na yeyote ambaye amefanya miujiza mpaka awe na imani.”3 Amoni alitangaza, “Kwa hivyo Mungu ametoa njia ili mwanadamu, kwa imani, aweze kutenda miujiza mikuu.”4 Bwana alifunua kwa Joseph Smith, “Kwani Mimi ni Mungu, … na nitaonyesha miujiza … kwa wale wote waaminio katika jina langu.”5

Mfalme Nebukadreza aliamuru kwamba Shadraka, Meshaki, na Abednego wasujudie sanamu ya dhahabu aliyoiweka kama mungu, akitisha kuwa, “msipoisujudia, mtatupwa… katika tanuru iwakayo moto.” Kisha akawasuta “Ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu?”6

Hawa wafuasi watatu waaminifu walisema: “Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto. … Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako.”7

Walikuwa na imani kamili kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kuwaokoa, “kama si hivyo,” walikuwa na imani kamili kwa mpango Wake.

Sawa na hiyo, Mzee David A. Bednar wakati mmoja alimuuliza mvulana ambaye alikuwa ameomba baraka ya ukuhani, “Ikiwa ni mapenzi ya Baba yetu wa Mbinguni kwamba uhamishwe kupitia mauti hadi katika ujana wako hadi ulimwengu wa roho kuendelea na huduma yako, una imani ya kutosha kukubali mapenzi yake ya kutokupona?”8 Sisi tuna imani “kutokupona” kutokana na mateso ya dunia ili tuweze kuponywa milele?

Swali muhimu kutafakari ni “Ni wapi tunaweka imani yetu?” Je, imani yetu inalenga tu kuondolewa uchungu na mateso, au iko imara kwake Mungu Baba na mpango Wake mtakatifu na kwa Yesu Kristo na Upatanisho wake? Imani katika Baba na Mwana inatuwezesha kuelewa na kukubali mapenzi Yao tunapojitayarisha kwa maisha ya milele.

Leo natoa ushuhuda kuhusu miujiza. Kuwa mtoto wa Mungu ni muujiza.9 Kupokea mwili kwa mfano wake na sura yake ni muujiza.10 Baraka ya Mwokozi ni muujiza.11 Upatanisho wa Yesu Kristo ni muujiza.12 Uwezekano wa uzima wa milele ni muujiza.13

Huku ikiwa ni vyema kusali na kushughulikia usalama wa kimwili na uponyaji wakati wa maisha yetu ya sasa, lengo letu kuu linapaswa kuhusu miujiza ya kiroho ambayo inapatikana kwa watoto wote wa Mungu. Haijalishi kabila letu, haijalishi utaifa wetu, haijalishi kile ambacho tumetenda ikiwa tumetubu, haijalishi yale ambayo tumetendewa—kila mmoja wetu ana fursa sawa ya kupokea miujiza hii. Tunaishi muujiza, na miujiza zaidi iko mbele yetu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.