“Ninayo Kazi kwa Ajili Yako”
Kila mmoja wetu analo jukumu muhimu la kutekeleza katika kuendeleza kazi ya Mungu.
Kwake Musa, Mungu alitangaza, “Na ninayo kazi kwa ajili yako”(Moses 1:6). Umewahi kujiuliza ikiwa Baba wa Mbinguni ana kazi kwa ajili yako? Je, kuna mambo muhimu ambayo amekuandalia—na hasa wewe—utimize? Ninashuhudia jibu ni “ndio!”
Zingatia Girish Ghimire, ambaye alizaliwa na kulelewa katika nchi ya Nepali. Kama kijana, alisomea kule China, ambapo mwanafunzi mwenzake alimjulisha kuhusu injili ya Yesu Kristo. Hatimaye, Girish alijiunga na Chuo cha Brigham Young kwa masomo ya baada ya kuhitimu na akakutana na mkewe wa baadaye. Walifanya makazi katika Bonde la Salt Lake na kupanga watoto wawili kutoka Nepali.
Miaka kadhaa baadaye, wakati zaidi ya wakimbizi 1,500 walitoka kambi zilizokuwa Nepali na kuhamia Utah,1 Girish alipata msukumo wa kutoa msaada. Akiwa na usahihi wa asili na uelewa wa lugha, Girish alihudumu kama mkalimani, mwalimu, na mnasihi. Baada ya kufanya makazi mapya katika jamii, baadhi ya wakimbizi wa kutoka Nepal walionyesha shauku ya kutaka kujua injilli. Tawi linalozungumza Kinepali liliundwa, na Girish baadaye alihudumu kama rais wa tawi. Pia alikuwa mhusika muhimu katika kutafsiri Kitabu cha Mormoni kwa Kinepali.
Unaweza kuona jinsi Baba wa Mbinguni alivyomtayarisha na kumtumia Girish?
Mungu Anayo Kazi kwa Kila Mmoja Wetu
Kina ndugu na kina dada, Mungu anayo kazi kwa kila mmoja wetu. Akizungumza na kina dada lakini akifundisha ukweli ambao unamfaa kila mtu, Rais Spencer W. Kimball alifundisha: “Kabla ya kuja [duniani, sisi] tulipewa kazi fulani. … Ingawa sasa hatukumbuki vipengee hasa, hii haibadilishi ukweli wa utukufu wa kile wakati mmoja tulichokubaliana nacho.”2 Ukweli wa kuadilisha kiasi gani! Baba yetu wa Mbinguni anayo mambo maalum na muhimu kwetu sisi ili tuyatimize (ona Waefeso 2:10).
Majukumu haya tukufu sio tu ya wachache wenye fadhila bali ni yetu wote—bila ya kujali jinsia, umri, mbari, utaifa, mapato, hali ya kijamii, au mwito wako Kanisani. Kila mmoja wetu analo jukumu muhimu la kutekeleza katika kuendeleza kazi ya Mungu (ona Musa 1:39).
Baadhi yetu tunauliza ikiwa Baba wa Mbinguni anaweza kututumia sisi kufanya michango muhimu. Lakini kumbuka, daima amewatumia watu wa kawaida kutekeleza mambo ya ajabu (ona 1 Wakorintho 1:27–28; M&M 35:13; 124:1). “[Sisi] ni mawakala” na “uwezo u ndani [yetu]”“kutekeleza haki nyingi”(M&M 58:27–28).3
Rasi Russell M. Nelson alielezea:
“Bwana ana mipango mingi juu yako kuliko ile uliyo nayo mwenyewe. Mmebakishwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya wakati na mahali hapa. …
Bwana anawahitaji muubadilishe ulimwengu. Mnapokubali na kufuata mapenzi Yake kwa ajili yenu, mtapajikuta mkitimiza yasiyowezekana”4
Kwa hivyo ni namna gani tunapata kuelewa na kutekeleza kazi ambayo Mungu ametukusudia? Acha nishiriki kanuni nne ambazo zitawasaidia.
Wazingatie Wengine
Kwanza, wazingatie wengine. Tunaweza kumfuata Kristo, “ambaye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema” (Matendo 10:38; ona pia 2 Nefi 26:24).
Baada ya kurejea kutoka misheni, nilikosa madhumuni niliyokuwa nimefurahia kila siku. Ni wazi, nilihitaji kuweka maagizo yangu, kupata elimu, kuanzisha familia, na kupata ajira. Lakini nilijiuliza ikiwa kulikuwa na zaidi ya hayo, au hata kitu maalum, ambacho Bwana alinitaka nifanye. Baada ya kutafakari kwa miezi kadhaa, nilipata aya hii: “Na, kama unataka, utakuwa chanzo cha kufanya mema mengi katika kizazi hiki” (M&M 11:8). Roho alinisaidia kuelewa kwamba lengo la msingi la majukumu matakatifu ni kubariki wengine na “kutenda mema zaidi.”
Tunaweza kufanya maamuzi katika maisha yetu—kama vile kitu cha kujifunza, kazi tutakayoifanya, au tutakapoishi—katika muktadha wa kuwasaidia wengine.
Familia moja ilihamia katika jiji jipya. Badala ya kutafuta nyumba katika ujirani wenye utajiri, walihisi msukumo wa kuhamia katika eneo lililoonekana kuwa na mahitaji mengi ya kijamii na kiuchumi. Kwa kipindi cha miaka mingi, Bwana amewatumia kutoa msaada kwa watu wengi na kuimarisha kata yao pamoja na kigingi.
Daktari mmoja aliendeleza kliniki ya kawaida lakini akahisi ameongozwa atenge siku moja kwa wiki kutoa huduma ya bure kwa watu ambao hawakuwa na bima ya afya. Kwa sababu ya bwana huyu na mkewe kuwa radhi kubariki wengine, Bwana aliwawezesha kutoa msaada kwa mamia ya wagonjwa waliohitaji msaada, huku wakilea familia kubwa.
Gundua na Ukuze Karama za Kiroho
Pili, Gundua na Ukuze Karama za Kiroho. Baba wa Mbinguni alitupatia karama hizi ili kutusaidia kutambua, kutenda, na kufurahia kazi aliyotupangia.
Baadhi yetu tunajiuliza, “Ninazo karama zozote?” Tena, jibu ni “ndio!” “Na kwa kila mwanaume [na mwanamke] kipawa kimetolewa na Roho wa Mungu … ili wote waweze kufaidika” (M&M 46:11–12; imetiliwa mkazo).5 Karama kadhaa zimeorodheshwa katika maandiko (ona 1 Wakorintho 12:1–11, 31; Moroni 10:8–18; M&M 46:8–26), lakini kuna nyingine zaidi.6 Baadhi inaweza kujumuisha kuwa mwenye huruma, kuonyesha matumaini, uhusiano mwema na wengine, kuwa mratibu mwenye ufanisi, kuzungumza au kuandika kwa ushawishi, kufundisha vizuri, na kufanya kazi kwa bidii.
Kwa hiyo tunaweza kujua vipi vipawa vyetu? Tunaweza kurejelea baraka yetu ya baba mkuu, tukawauliza wale ambao wanatufahamu vizuri, na kibinafsi kutambua kile ambacho kawaida tunakifanya vizuri na kukifurahia. Muhimu zaidi, tunaweza kumuomba Mungu (ona Yakobo 1:5; M&M 112:10). Anajua vipawa vyetu, kwa vile alitupatia (ona M&M 46:26).
Tunapogundua vipawa vyetu, tunao wajibu wa kuvikuza (ona Mathayo 25:14–30). Hata Yesu Kristo “Naye hakupokea utimilifu mwanzoni, bali [alikuza] kutoka neema hadi neema” (M&M 93:13).
Mvulana mmoja alichora mchoro wa kutangaza viwango vya kidini. Niliyoipenda zaidi ilikuwa picha ya Mwokozi, ambayo nakala yake imetundikwa nyumbani kwetu. Ndugu huyu alikuza na kutumia vipawa vyake vya usanii. Kupitia kwake, Baba wa Mbinguni amewatia msukumo wengine kuboresha ufuasi wao.
Mara nyingine sisi tunahisi kuwa hatuna vipawa vyovyote muhimu. Siku moja msichana aliyevunjika moyo alisihi, “Bwana, huduma yangu binafsi ni ipi? Alijibu, “Watambue wengine.” Kilikuwa kipawa cha kiroho! Tangu wakati huo, yeye amepata furaha kwa kuwatambua wale ambao mara nyingi husahaulika, na Mungu ametenda kupitia kwake ili kuwabariki wengi. Baadhi ya vipawa vyetu vya kiroho vinaweza kukosa kutufanya maarufu kulingana na viwango gezi vya dunia, lakini ni muhimu kwa Mungu na kazi Yake.7
Tumia Dhiki
Tatu, tumia dhiki. Majaribu yetu hutusaidia kugundua na kujitayarisha kwa ajili ya kazi Baba wa Mbinguni aliyonayo kwetu. Alma alieleza, “Baada ya shida nyingi, Bwana … amenifanya kuwa chombo mikononi mwake” (Mosia 23:10).8 Kama Mwokozi, ambaye dhabihu yake ya upatanisho inamuwezesha kutusaidia (ona Alma 7:11–12), tunaweza kutumia ufahamu ambao umepatikana kutokana na matukio magumu kuinua, kuimarisha, na kubariki wengine.
Baada ya afisa mtendaji wa kuajiri na mwenye mafanikio kufutwa kazi, alisoma baraka zake za baba mkuu na kuhisi ametiwa msukumo kuanzisha kampuni ya kuwasaidia wataalamu wengine kupata kazi. (Alinisaidia hata mimi kupata kazi wakati familia yetu ilirejea kutoka misheni.) Bwana alitumia jaribio lake kama njia ya kuwabariki wengine, huku akimpa kazi yenye maana zaidi.
Vijana wanandoa walipata mtoto aliyezaliwa mfu. Kwa mioyo iliyovunjika, waliamua kutoa heshima kwa ajili ya binti yao kwa kutoa ushauri wa kisaikolojia na usaidizi wa muhimu kwa wazazi waliokuwa katika hali kama yao. Bwana amefanya kazi kupitia kwao kwa sababu ya huruma yao maalum, iliyotokana na dhiki.
Mtegemee Mungu
Ya nne mtegemee Mungu. Wakati tunapomuomba kwa imani na dhamira ya kweli, atatufunulia wito wetu mtakatifu.9 Mara tukishagundua, atatusaidia kutimiza kazi hizo. “Vitu vyote vipo mbele ya macho [Yake]” (M&M 38:2), na katika nyakati zinazofaa, atafungua milango (ona Ufunuo 3:8; Ibrahimu 2:8) iliyo muhimu kwetu. Alimtuma hata Mwanawe, Yesu Kristo, ili tuweze kumtegemea Yeye kwa ajili ya nguvu zinazozidi uwezo wetu wa kawaida (ona Wafilipi 4:13; Alma 26:12).
Ndugu mmoja, anayehusika na uamuzi wa serikali ya mitaa, alihisi msukumo wa kugombea wadhifa katika ofisi ya umma. Licha ya changamoto nyingi katika kampeni, alikuwa na imani na alipata fedha za kugombea. Hatimaye, hakushinda lakini alihisi Bwana alikuwa amemuongoza na kumpa nguvu ya kuangazia maswala muhimu katika jumuia.
Mama mzazi pekee, anayewatunza watoto walio na ulemavu, alikuwa na shaka kama angeweza kukidhi vilivyo mahitaji ya familia yake. Ingawaje ilikuwa vigumu, anahisi kuimarishwa na Bwana kutekeleza wajibu wake muhimu zaidi hadi kufanikiwa.
Neno la Tahadhari
Wakati ambapo Mungu hutusaidia kutimiza kazi takatifu, adui hufanya juhudi za kuvuruga na kutukatisha tamaa ili tuache maisha yenye maana.
Dhambi pengine ni kikwazo kikuu zaidi, chenye kutia utusitusi hisia zetu kwa Roho Mtakatifu na kuzuia uwezo wetu wa kupata nguvu za kiroho. Ili tutekeleze kazi ambayo Baba wa Mbinguni ametupatia, tunapaswa kujitahidi kuwa wasafi (ona 3 Nefi 8:1). Je, tunaishi kwa namna ambayo Mungu anaweza kutenda kupitia kwetu?
Shetani pia anatafuta kutuvuruga kwa mambo yasiyo ya muhimu. Bwana alimuonya kiongozi wa zamani wa Kanisa, “Akili yako imekuwa juu ya mambo ya dunia zaidi kuliko mambo yangu, Muumba wako, na huduma ambayo wewe umeitiwa” (D&C 30:2). Je, tunajishughulisha na mambo ya dunia kiasi cha kwamba tunachepuka kutoka kwenye kazi zetu tukufu?
Kwa kuongezea, Shetani anatukatisha tamaa kupitia hisia za kuwa na upungufu. Anafanya kazi yetu ionekane ngumu zaidi au ya kutisha. Hata hivyo, tunaweza kumuamini Mungu! Anatupenda. Anataka sisi tufanikiwe. Yeye “atakayetutangulia [sisi]; atakuwa pamoja na [sisi], hatakupungukia [sisi]” (Kumbukumbu 31:8; ona pia Zaburi 32:8; Mithali 3:5–6; Mathayo 19:26; M&M78:18).
Shetani anaweza kutusukuma tuone kazi yetu kama kitu bure kuliko kazi zilizopangiwa wengine. Kila kazi kutoka kwa Mungu ni muhimu, na tutapata furaha “tunapotukuza kile Bwana ametuamuru [sisi]”
Mungu anapotenda kupitia kwetu, adui anaweza akatujaribu tupokee sifa za mafanikio yoyote. Hata hivyo, tunaweza kuiga unyenyekevu wa Mwokozi kwa kufuta sifa za kibinafsi na kumsifu Baba (ona Mathayo 5:16; Musa 4:2). Wakati ambapo mwanahabari alijaribu kumtambua Mama Tereza kwa wito wa maisha yake wa kuwasaidia maskini, alijibu himahima: “Ni kazi [ya Mungu]. Mimi ni kama … penseli mkononi mwake. … Anafanya kufikiria. Anafanya kuandika. Penseli haihusiki na chochote. Penseli inaruhusiwa tu kutumika.”10
Hitimisho
Ndugu zangu na dada wapendwa, ninaalika kila mmojawetu “tujitoeni [wenyewe] kwa Mungu … kama silaha za haki” (Warumi 6:13). Kujitoa kunahusisha kumjulisha kuwa tunataka kutumika, kutafuta mwongozo wake, na kupata nguvu zake.
Kama kawaida, tunaweza kumuiga Yesu Kristo, mfano wetu kamili. Katika maisha kabla ya dunia, Baba wa Mbinguni aliuliza, “Nimtume nani?”
Na Yesu akajibu, “Niko hapa, nitume mimi” (Ibrahimu 3:27; ona pia Isaya 6:8).
Yesu Kristo alikubali, akajitayarisha, na kutekeleza wajibu Wake uliopangwa tangu zamani kama Mwokozi na Mkombozi wetu. Alitenda mapenzi ya Baba (ona Yohana 5:30; 6:38; 3 Nefi 27:13) na kukamilisha kazi Yake takatifu.
Tunapofuata mfano wa Kristo na kujitolea kwa ujasiri kwake Mungu, ninashuhudia ya kwamba atatutumia kuendeleza kazi Yake na kubariki wengine. Katika jina la Yesu Kristo, amina