Kupatwa Kiroho
Usiruhusu mikanganyiko ya maisha izuie nuru ya mbinguni.
Mnamo Agosti 21 mwaka huu, matukio mawili adimu yalifanyika na kuvuta nadhari ya watu kote duniani. La kwanza ikiwa ni maadhimisho ya 90 ya siku ya kuzaliwa kwa nabii wetu mpendwa, Rais Thomas S. Monson. Wakati huo, nilikuwa na jukumu kule Eneo la Pasifiki na nilikuwa na msisimuko kwa kuwa watakatifu wa Australia, Vanuatu, New Zealand, na French Polynesia hawakuwa tu wanajua kuhusu hatua hii muhimu ya kibinafsi, bali pia walifurahia kuisherehekea. Nilijihisi mwenye bahati kushiriki katika kuonyesha hisia zao njema za imani na upendo kwa bwana huyu mzuri. Ni mvuto wa ajabu kuona mwunganisho Watakatifu wa Siku za Mwisho walio nao na nabii wao.
Bila shaka, Rais Monson, akiwajali wale ambao wanataka kumtakia siku njema ya kuzaliwa kwake, alielezea kuwa zawadi bora ya siku ya kuzaliwa: “Mtafute mtu ambaye anapitia matatizo au anayeugua au aliye mpweke na umtendee jambo fulani. Ni hayo pekee ningeuliza.”1 Tunakupenda na kukuidhinisha, Rais Monson.
Kupatwa kwa jua
Tukio lingine adimu na la mbinguni lililofanyika siku hiyo pia na kuwavutia mamilioni ulimwenguni, ilikuwa kupatwa kamili kwa jua. Hili ilikuwa mara ya kwanza kupatwa kwa jua kama huku kulikuwa kumepita kote Marekani miaka 99 iliyopita.2 Je, umeshawahi kuona kupatwa kwa jua? Pengine naweza kuelezea kwa utondoti zaidi.
Kupatwa kwa jua kamili kunatokea wakati ambapo mwezi husonga kati ya dunia na jua, na karibu kuzuia kabisa mwangaza wowote kutoka kwenye uso wa jua.3 Ukweli kwamba hili linaweza kufanyika ni ajabu kwangu. Ukidhania jua kama ukubwa wa tairi ya baiskeli ya kawaida, mwezi kwa kulinganisha karibu kamwe ni ukubwa wa changarawe.
Inawezekanaje kwamba chanzo halisi cha joto, mwanga, na uhai kinaweza kuzuiwa kabisa na kitu kwa kulinganisha ni kidogo mno?
Ingawaje jua ni kubwa mara 400 zaidi kuliko mwezi, pia liko mbali mara 400 zaidi na dunia.4 Kutokana na taswira hii ya dunia, jiometri hii inafanya jua na mwezi kuonekana kuwa na ukubwa sawa. Wakati inapolingana tu kwa njia sahihi, mwezi unaonekana kukinga jua zima. Marafiki na familia yangu ambao walikuwa katika maeneo ya kupatwa kwa jua walielezea jinsi mwangaza uligueka kuwa giza, nyota zikatokea, na ndege wakaacha kuimba. Hewa ikawa baridi, wakati halijoto katika kupatwa yaweza kupungua kwa zaidi ya nyuzi 20 Farenhaiti (nyuzi 11 Selsiasi).5
Walielezea hali ya kustahika, mshangao, na hata wasiwasi, wakijua kupatwa huleta mahafa fulani. Hata hivyo, wote walichukua tahadhari ili kuzuia athari za kudumu kwa macho au “upofu wa kupatwa” wakati wa tukio la kupatwa. Usalama unaweza kupatikana kwa sababu walivaa miwani yenye chujio maalum kwenye lenzi ambayo ilikinga macho yao kutokana na athari zinazoweza kutokea.
Analojia
Katika hali kama hiyo ambapo mwezi mdogo mno unaweza kuzuia jua tukufu, na kuzima mwanga na joto lake, kupatwa kwa kiroho yaweza kutendeka wakati tunaporuhusu vizuizi vidogo vyenye kuleta matatizo—yale tunayokabiliana nayo katika maisha ya kila siku—kusogea karibu kiasi cha kwamba yanazuia ubora, mwangaza, na joto la nuru ya Yesu Kristo na injili Yake.
Mzee Neal A. Maxwell aliendeleza analojia hii zaidi aliposema: “Hata kitu kidogo kama kidole gumba cha mwanadamu, kinapowekwa karibu sana na jicho, kinaweza kumzuia kuona jua lililo kubwa mno. Na bado jua likiwa lingali lipo. Upofu unamjia mwanadamu kupitia matendo yake mwenyewe. Wakati tunapoleta vitu vingine karibu sana, na kuvifanya kipaumbele tunazuia uwezo wetu wa kuona mbinguni.”6
Ni wazi, hakuna mmoja wetu anayetaka kwa makusudi kuzuia uwezo wetu wa kuona mbinguni au kuruhusu kupatwa kiroho kutokea katika maisha yetu. Hebu nishiriki mawazo fulani ambayo yanaweza kutusaidia kuzuia kupatwa kiroho kusababisha athari za kudumu za kiroho.
Miwani ya Injili: Inadumisha Taswira ya Injili
Unakumbuka maelezo yangu ya miwani maalum inayotumika kuwakinga wale ambao wanatazama kupatwa kwa jua kutokana na madhara ya macho au hata upofu wa kupatwa? Kutazama kupatwa kiroho kupitia lenzi za Roho zenye kulinda na kulainisha huleta mtazamo wa kiroho, hivyo basi kutulinda kutokana na upofu wa kiroho.
Hebu tuzingatie mifano kadhaa. Tukiwa na maneno ya manabii katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu kama mshauri wetu, tunaweza kutazama mwangaza wa mbinguni uliozuiliwa kiasi kupitia “miwani ya injili,”kuepukana na madhara ya kupatwa Kiroho.
Sasa tunawezaje kuvaa miwani ya injili? Hapa kuna baadhi ya mifano: Miwani yetu ya injili inatujulisha kwamba Bwana anataka kwamba sisi tupokee sakramenti kila wiki na kwamba Yeye anataka sisi tujifunze maandiko na kusali kila siku. Pia yanatujulisha kwamba Shetani atatutia majaribuni tusifanye hivyo. Tunajua kwamba ajenda yake ni kutupokonya haki yetu ya kujiamulia kupitia mkanganyiko na majaribu ya kilimwengu. Hata katika siku za Ayubu, labda kulikuwa na wengine waliopatwa kiroho, ikielezwa kuwa “Wao hupatwa na giza wakati wa mchana, hupapasa mchana vilevile kama usiku.”7
Kina kaka na kina dada, ninapoongea juu ya kuona kupitia miwani ya kiroho, tafadhali jua kwamba sipendekezi ya kwamba tukatae kutambua au kujadili changamoto tunazokumbana nazo au kwamba tutembee kwa furaha bila kujua mitego na maovu adui ameweka mbele yetu. Mimi siongei juu ya kuvalia pazia—bali kinyume kabisa. Mimi, ninapendekeza ya kwamba tutazame changamoto kupitia lenzi za injili. Mzee Dallin H.Oaks alisema kwamba “taswira ni uwezo wa kuona habari zote husika katika mahusiano ya maana.”8 Taswira ya injili hupanua uoni wetu hata mandhari ya milele.
Wakati unapovalia “miwani ya injili,” utapata mtazamo na uoni ulioboreshwa, katika njia unavyofikiria kuhusu vipaumbele vyako, shida zako, majaribu yako, na hata makosa yako. Utaona mwangaza angavu ambao hungeweza kuuona bila.
Kinyume, sio tu mabaya ambayo yanaweza kusababisha kupatwa kiroho maishani mwetu. Mara nyingi, jitihada nzuri na chanya ambazo kwazo tunajitolea zaweza kufuatana kwa karibu sana kiasi cha kuzuia mwanga wa injili na kuleta giza. Hizi hatari au mikanganyiko inaweza kujumuisha elimu na mafanikio, uwezo, ushawishi, hamu ya kufaulu, hata talanta na vipawa.
Rais Dieter F. Uchtdorf amefundisha kuwa, “kila adili ikizidishwa kupita kiasi huwa uovu.… Wakati hufika ambapo matukio muhimu huwa mizigo mizito na matarajio,usumbufu wa kuchukiza.”9
Naomba nishiriki kwa maelezo zaidi mifano ambayo inaweza kuwa kichocheo cha kuepuka kupatwa kiroho kwetu.
Mitandao ya Kijamii
Miezi kadhaa iliyopita, nilizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Wanawake kule BYU.10 Nilielezea jinsi teknolojia ikijumuisha mitandao ya kijamii huwezesha kueneza “ufahamu wa Mwokozi … kila taifa, kabila, lugha, na watu.”11 Teknolojia hizi hujumuisha tovuti za Kanisa kama vile LDS.org na Mormon.org; programu-tumizikama vile Gospel Library, Mormon Channel, LDS Tools, na Family Tree; na mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na Facebook, Twitter, na Pinterest. Mbinu hizi zimezalisha mamia ya mamilioni ya likes, shares, views, retweets, na pins na zimekuwa za kufaa sana na zenye ufanisi katika kushiriki injili na familia, marafiki, na washirika.
Licha ya maadili yote na utumizi unaofaa wa teknolojia hizi, kuna hatari zinazohusika nazo kwamba, wakati inapoletwa karibu sana, tunaweza kupatwa kiroho na kuweza kuzuia mwangaza na joto la injili.
Utumizi wa mitandao ya kijamii, programu tumizi, na michezo unaweza kuwa na matumizi mabaya ya muda na unaweza kupunguza uhusiano wa moja kwa moja. Kupoteza mazungumzo ya kibinafsi kunaweza kuathiri ndoa, kuchukua nafasi ya desturi za thamani za kiroho na kusonga ukuzaji wa ujuzi wa kijamii, hasa miongoni mwa vijana.
Hatari mbili zaidi zinahusiana na mitandao ya kijamiii ni uhalisi unaothaminiwa na ulinganishaji unaodhoofisha.
Nyingi (ikiwa kama si zote) kati ya picha zinazowekwa katika mitandao ya kijamii huonekana kuonyesha maisha katika hali bora zaidi—mara nyingi jinsi isivyo. Sote tumeona picha nzuri za mapambo ya nyumbani, maeneo ya ajabu ya likizo, picha zenye tabasamu, maandalizi ya chakula yaliyofanywa kwa uangalifu, na picha za mili isiyowezekana kupatikana.
Hapa, kwa mfano, ni picha ambayo unaweza kuona kwenye akaunti ya mtandao wa kijamii ya mtu fulani. Hata hivyo, haionyeshi taswira kamiliya kile kinachotendeka kwa kweli katika maisha halisi.
Kulinganisha maisha yetu ya kawaida na yale ya wengine ambayo yamehaririwa vizuri, maisha yaliyoundwa kikamilifu kama inavyoonekana katika mitandao ya kijamii, inaweza kutuacha na hisia za kukata tamaa, wivu, na hata kushindwa.
Mtu mmoja ambaye alikuwa amechangia posti zake nyingi alisema, pengine kwa utani, “Nini haja ya kuwa na furaha ikiwa hutaisambaza?”12
Kama vile Dada Bonnie L. Oscarson alivyotukumbusha asubuhi ya leo, mafanikio maishani hayategemei likes ngapi tunazopata au “marafiki” wangapi au watu wanaotufuata tulio nao. Hata hivyo, inahusiana na kushirikiana kwa njia za maana pamoja na wengine na kuongeza mwangaza katika maisha yao.
Kwa matumaini, tunaweza kujifunza kuwa halisi zaidi, kupata ucheshi zaidi, na kuhisi kukata tamaa mara chache wakati tunapokumbana na picha zinazoweza kuoyesha ulimbwende na ambao mara nyingi husababisha ulinganishi unaodhoofisha.
Ullinganishi unaonekana sio tu ishara ya nyakati zetu bali pia ulikuwa katika nyakati zilizopita. Mtume Paulo alionya watu katika siku zake kwamba “wao wenyewe wakijipima nafsi zao na nafsi zao, na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili.”13
Kukiwa na matumizi mengi ya teknolojia yanayofaa na yenye mwongozo, acha tuitumie kufundisha, kuhamasisha, na kujiinua sisi wenyewe na kuwahimiza wengine kuwa bora—badala ya kuonyesha ulimbwende wetu? Acha pia tufundishe na kuonyesha matumizi ya haki ya teknolojia kwa kizazi kinachochipuka na kuonya dhidi ya hatari zinazohusika na matumizi yake mabaya. Kuitazama mitandao ya kijamii kupitia lenzi za injili, tunaweza kuizuia kuwa kupatwa kiroho katika maisha yetu.
Kiburi
Hebu sasa tushughulikie kizuizi kikuu cha kiburi. Kiburi ni kinyume cha unyenyekevu ambao ni “utayari wa kutii mapenzi ya Bwana.”14 Wakati tuna kiburi, sisi huonekana kujisifu badala ya kuwasifu wengine, ikiwa ni pamoja na Bwana. Kiburi mara nyingi huwa shindani; ni tabia ya kutafuta kuwa na zaidi na kudhania sisi ni bora kuliko wengine. Kiburi mara nyingi husababisha hisia za hasira na chuki; kinasababisha mtu kuwa na kinyongo au kukataa kutoa msamaha. Kiburi, hata hivyo, chaweza kumezwa na sifa kama ya Kristo ya unyenyekevu.
Uhusiano, hata na wanafamilia wa karibu na wapendwa, hasa pamoja na wanafamilia wa karibu na wapendwa—hata baina ya waume na wake—unakuzwa kwa unyenyekevu na unazuiwa na kiburi.
Miaka mingi iliyopita, mtendaji wa kampuni ya uuzaji alinipigia simu kuzungumza kuhusu kampuni yao ambayo ilikuwa inanunuliwa na washindani wao. Yeye pamoja na wafanyikazi wenzake katika makao makuu walikuwa na hofu kubwa kwamba wangepoteza kazi zao. Akijua ya kwamba niliwafahamu vizuri mameneja wakuu wa kampuni nunuzi, aliniuliza ikiwa nilikuwa radhi kumtambulisha na kutoa udhamini mzuri kwa niaba yake, na hata kupanga mkutano kwa niaba yake. Alimalizia kwa kutoa kauli ifuatayo: “Unajua wanavyosema? Wapole wataangamia!’”
Nilielewa maoni yake yalidhamiriwa kama ucheshi. Nilielewa utani wake. Lakini kulikuwa na kanuni muhimu ambayo niliona hatimaye itakuwa ya manufaa kwake. Nilijibu, “Kusema kweli, hivyo sivyo wasemavyo. Hakika, ni kinyume. ‘Walio wapole … kwani watarithi dunia’15 ndivyo wanavyosema.”
Kupitia uzoefu wangu Kanisani na pia katika kazi yangu, baadhi ya watu wakuu, wenye ufanisi mkubwa ambao nimepata kuwajua wamekuwa wapole na wanyenyekevu zaidi.
Unyenyekevu na upole ni kama chanda na pete. Tupate kuelewa ya kwamba “hakuna yeyote anayekubaliwa mbele ya Mungu, isipokuwa yule aliye mnyenyekevu na mpole katika moyo.”16
Ninaomba ya kwamba tutajitahidi kuepuka kupatwa kiroho na kiburi kwa kukumbatia maadili ya unyenyekevu.
Hitimisho
Kuhitimisha, kupatwa kwa jua hakika ni tukio la ajabu la asili wakati ambapo uzuri, joto, na mwangaza wa jua unaweza kufunikwa kabisa kwa kulinganisha na kitu kidogo mno, na kusababisha giza na baridi.
Tukio sawa na hili laweza kuigwa katika hali ya kiroho, wakati kwa vinginevyo maswala madogo mno yanavutwa karibu sana na kuzuia uzuri, joto, na mwangaza wa mbinguni wa Injili ya Yesu Kristo, na kuibadili na giza lenye baridi.
Miwani ambayo imeundwa kulinda uwezo wa kuona wa wale walio katika eneo la kupatwa na jua kamili yaweza kuzuia madhara ya kudumu na hata upofu.17 “Miwani ya injili” inayojumuisha ufahamu na ushuhuda wa kanuni za injili na maagizo hutoa taswira ya injili ambayo pia vile vile inaleta ulinzi mkuu wa kiroho na kuweka wazi kwa mtu aliyehatarishwa na madhara ya kupatwa kiroho.
Kama ukigundua chochote ambacho kinaonekana kuzuia nuru na furaha ya injili katika maisha yako, nakualika ukiweke katika mtazamo wa injili. Tazama kupitia lenzi za injili na uwe na tahadhari kutoruhusu mambo duni na yasiyofaa katika maisha kuzuia twasira yako ya milele ya mpango mkuu wa furaha. Kwa kifupi, usiruhusu mikanganyiko ya maisha izuie nuru ya mbinguni.
Ushuhuda
Ninashuhudia ya kwamba haijalishi kizuizi ambacho kinaweza kuzuia uwezo wako wa kuona mwanga wa injili, mwanga huo bado upo. Chanzo cha joto, ukweli, na mwangaza ni injili ya Yesu Kristo. Ninashuhudia juu ya Baba wa Mbinguni mwenye upendo; Mwanawe, Yesu Kristo, na jukumu Lake kama Mwokozi wetu na Mkombozi wetu. Katika jina la Yesu Kristo, amina