Washa Taa Yako
Manabii wanatuita sisi, dada zangu. Mtakuwa wema? Mtaielezea kwa ufasaha imani yenu? Mtawasha taa zenu?
Huenda msijue hili, lakini Rais Monson na Mimi ni mapacha. Siku ambayo nilizaliwa—saa ile ile—huko California Kaskazini, Thomas Monson akiwa na miaka 36 aliidhinishwa kama Mtume mpya. Nafurahia muunganiko wangu maalumu na binafsi na nabii wa Mungu, Rais Monson.
Manabii wanaongea kuhusu wanawake.1 Mtayasikia baadhi ya maneno yao katika mkutano huu. Kwa maneno yangu halisi ninarudi nyuma karibu miaka 40 ya unabii wa ajabu ulioandikwa na Rais Spencer W. Kimball. Septemba 1979 ilikuwa ni mara ya pili wanawake wa Kanisa ulimwenguniwaliweza kukutana katika mkutano mkuu wao wenyewe. Rais Kimball aliandaa hotuba yake, lakini siku ya mkutano ilipofika, alikuwa hospitalini. Hivyo badala yake, alimwomba mke wake, Camilla Eyring Kimball, kusoma hotuba kwa niaba yake.2
Dada Kimball alisoma maneno ya nabii, ambayo yalisisitiza ushawishi wa wanawake wa WSM kwa wanawake wazuri wa ulimwengu kabla ya Ujio wa Pili wa Mwokozi. Karibu na mwisho, kulikuwa na jambo la kushusha kwa wanawake wa Kanisa ambalo tumekuwa tukilizungumzia tangu kale.
Naomba ninukuu machache ambayo Rais Kimbal alisema:
“Mwisho, dada zangu wapendwa, naomba nipendekeze kwenu kitu ambacho hakijawahi kusemwa kabla au kwa njia hii. Wingi wa ukuaji mkubwa ambao unakuja kwenye Kanisa katika siku za mwisho utakuja kwa sababu wengi wa wanawake wema wa ulimwengu … watavutwa kuja Kanisani kwa idadi kubwa. Hii itatokea kwa kiasi kwamba wanawake wa Kanisa wataonyesha uadilifu na ufasaha katika maisha yao na kwa kiasi kwamba wanawake wa Kanisa wanaonekana wa kipekee na tofauti—katika njia za furaha—tofauti na wanawake wa ulimwengu.”
“Kati ya mashujaa halisi duniani ambao wataingia Kanisani ni wanawake ambao wanahusika zaidi na kuwa wenye haki kuliko kuwa wabinafsi. Mashujaa hawa wa kweli wana unyenyekevu wa kweli, ambao unakuwa na thamani kubwa kwenye uadilifu kuliko kuonekana. …
“… Itakuwa … mifano ya wanawake wa Kanisa [ambao] watakuwa nguvu kubwa katika ukuaji wa idadi na kiroho wa Kanisa katika siku za mwisho.”3
Ni maelezo mazuri sana ya kinabii. Kwa muhtasari:
-
Utakuwa ni uhusiano mzuri wa wanawake ambao utachangia ukuaji wa Kanisa katika miaka ijayo.
-
Urafiki ambao Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, wasichana, na wasichana wa Msingi hujenga, na wanawake na wasichana wa dhati, waaminifu, wa kiungu wa dini na imani zingine utakuwa nguvu kubwa jinsi Kanisa linavyokua katika siku za mwisho.
-
Rais Kimball aliwaita wanawake hawa toka upande mwingine “mashujaa” ambao watakuwa wanahusika zaidi kuwa wema kuliko wabinafsi, ambao watatuonyesha kwamba uadilifu una thamani zaidi kuliko kuonekana.
Nimekutana na wanawake wengi wazuri nikifanya kazi yangu duniani kote. Urafiki wao ni wa thamani kwangu. Mnawajua pia miongoni mwa marafiki na jirani zenu. Wanaweza kuwa au wasiwe waumini wa Kanisa kwa sasa, lakini tunaunganika kwa urafiki ambao ni muhimu. Basi, tunatendaje ya upande wetu? Tunapaswa kufanya nini? Rais Kimball alirejea kwenye vitu vitano:
Cha kwanza ni kuwa wenye haki. Kuwa mwenye haki haimaanishi kuwa mkamilifu au kutofanya makosa. Ina maana kuendeleza uhusiano na Mungu, kutubu dhambi zetu na makosa, na kwa uhuru kuwasaidia wengine.
Wanawake waliotubu hubadilisha mwenendo wa historia. Nina rafiki aliyekuwa kwenye ajali ya gari alipokuwa mdogo na kutokana na hilo, akapatwa na ulevi wa madawa ya maumivu. Baadaye, wazazi wake walitengana. Akapata ujauzito toka kwenye mahusiano mafupi, na uraibu ukaendelea. Lakini usiku mmoja, aliangalia machafuko na uchafu wa maisha yake na akasema, “Imetosha.” Na akamlilia Mwokozi Yesu Kristo ili amsaidie. Alisema amejifunza kwamba Yesu Kristo alikuwa na nguvu sana kuliko hali yake mbaya na kwamba angetegemea nguvu Zake na akitembea kwenye barabara ya toba.
Kwa kumrudia Bwana na mapito Yake, alibadilisha mwelekeo wa historia yake na mvulana wake mdogo na mume wake mpya. Ni mwema, na ana moyo mzuri kwa wengine ambao wamefanya makosa na wanataka kubadilika. Na kama sisi wote, si mkamilifu, lakini anajua jinsi ya kutubu na kuendelea kujaribu.
Kitu cha pili ni kujieleza kwa ufasaha. Kujieleza kwa ufasaha ni kueleza vizuri jinsi unavyojisikia kuhusu kitu fulani na kwa nini. Mwanzoni mwa mwaka huu, kulikuwa na taarifa kwenye ukurasa wangu wa facebook ambazo zilishusha hadhi ya Ukristo. Nikazisoma na nikakasirika lakini nikazipuuza. Hata hivyo, mtu ninayemjua ambaye siyo muumini wa imani yetu alichangia kwa maneno yake mwenyewe. Aliandika: “[Hii ni] tofauti kabisa na kile Yesu alichoshikilia—alikuwa … kiini [katika] nyakati zake kwa sababu … aliuweka sawa ulimwengu. … Yeye [aliongea na] wazinzi, [alikula] na mtoza ushuru … , alikuwa rafiki wa wanawake na watoto wasiokuwa na nguvu … , [na] alisimulia hadhithi ya Msamaria Mwema. … Inafuata kwamba … Wakristo wa kweli watajitahidi kuwa wapenda watu ZAIDI ulimwenguni.” Niliposoma hayo, nilijiuliza mwenyewe, “Kwa nini sikuandika vile?”
Kila mmoja wetu anahitaji kuwa mzuri katika kuelezea sababu za imani yetu. Je, unahisije kuhusu Yesu Kristo? Kwa nini unabaki Kanisani? Kwa nini unaamini Kitabu cha Mormoni ni maandiko? Je, unapata wapi amani yako? Inajalisha nini kwamba nabii ana kitu cha kuongea mwaka 2017? Unajuaje kuwa ni nabii wa kweli? Tumia sauti yako na uwezo wako kuelezea kile unachojua na kuhisi—kwenye mitandao ya kijamii, katika maongezi ya kimya kimya na rafiki zako, kwenye maongezi na wajukuu zako. Waambie kwa nini unaamini, unajisikiaje, kama uliwahi kuwa na shaka, ulivukaje, na Yesu Kristo ana maana gani kwako. Kama Mtume Petro alivyosema, “Msiogope … ; bali mtakaseni Bwana katika mioyo yenu: na kuweni tayari wakati wote kutoa majibu kwa kila mtu atakaye waulizeni sababu ya tumaini ambalo lipo ndani yako.”4
Kitu cha tatu ni kuwa tofauti. Acha niwaambieni hadithi ambayo ilitokea Julai hii huko Panama City Beach Florida.5 Wakati wa jioni, Roberta Ursrey aliwaona wanawe wawili wakilia kuomba msaada mita 90 baharini. Walikuwa wamesombwa na mkondo mkali na walikuwa wanazolewa kupelekwa kilindini. Wenza waliokuwa karibu walijaribu kuwaokoa wale wavulana, nao pia wakasombwa na mkondo. Wanafamilia wa Ursrey walipiga mbizi kwenda kuwaokoa waogeleaji waliokuwa wakitaabika, na ghafla watu tisa walisombwa na mkondo mkali.
Hapakuwa na kamba. Hapakuwa na waokozi. Polisi walituma boti ya waokoaji, lakini watu baharini walihangaika kwa dakika 20 na walikuwa wamechoka na wanazama ndani ya maji. Miongoni mwa waliokuwa wakiangalia pale baharini alikuwa Jessica Mae Simmons. Yeye na mumewe walipata wazo la kutengeneza mnyororo wa watu. Walisema kwa sauti kubwa kwamba watu walio ufukweni wawasaidie, na watu wengi waliunganisha mikono na kutembea kuingia baharini. Jessica aliliambia gazeti: “Kuwaona watu kutoka jamii na jinsia tofauti wakiungana kuwasaidia wageni KABISA [ilikuwa] ni jambo zuri kuliona!!”6 Mnyonyoro wa watu 80 ulijinyosha kuelekea kwa waogeleaji. Angalia picha hii ya tukio hilo la kushangaza.
Kila mmoja pale ufukweni angeweza kufikiri majibu ya kawaida na waliduwazwa. Lakini wanandoa wawili, katika sekunde chache, walifikiria suluu tofauti. Uvumbuzi na uumbaji ni zawadi za kiroho. Tunaposhika maagano yetu, inaweza kutufanya sisi tuwe tofauti na wengine katika tamaduni na jamii zetu, lakini inatupa sisi nafasi ya kiroho ili tuweze kufikiri suluu tofauti, mbinu tofauti, matumizi tofauti. Hatuwezi kuwa pamoja na ulimwengu mara zote, lakini kuwa tofauti kwenye njia chanya kunaweza kuwa njia nzuri kwa wengine ambao wanataabika.
Kitu cha nne ni kuwa dhahiri. Dhahiri ina maana kuweza kutambulika wazi zaidi. Acha nirudi kwenye hadithi ya Jessica Mae Simmons ufukweni. Baada ya ule mnyororo wa watu kunyooshwa kuelekea kwa waogeleaji, alijua angeweza kusaidia. Jessica Mae alisema, “Naweza kuvuta pumzi yangu … na kwenda kwenye bwawa la olimpiki kiurahisi! [Nilijua jinsi ya kutoka kwenye mkondo mkali.] Nilijua ningeweza kumleta [kila mwogeleaji] kwenye mnyororo wa watu.”7 Yeye na mumewe walichukua boya na kuogelea kwenye mnyororo hadi wao na mwokoaji mwingine walipowafikia waogeleaji na kisha kuwasafirisha kwenye mnyororo na kuwapeleka sehemu salama ya ufukweni. Jessica alikuwa na kipaji cha ajabu; alijua kuogelea kwenye mkondo mkali.
Injili ya urejesho inajulikana na kutambulika wazi zaidi. Lakini lazima tuwe dhahiri kuhusu jinsi tunavyoifuata.Kama vile Jessica alivyofanya mazoezi ya kuogelea, tunahitaji kufanya mazoezi ya kuishi injili kabla ya dharura ili, bila kuogopa, tutakuwa na nguvu ya kuweza kusaidia wakati wengine wanaposukumwa na mkondo.
Na mwisho, kitu cha tano ni kufanya cha kwanza hadi cha nne kwa furaha. Kuwa na furaha hakunamaanishi kuweka tabasamu la plastiki kwenye uso wako bila kujali nini kinaendelea. Lakini inamaanisha kutii sheria za Mungu na kuwajenga na kuwainua wengine.8 Tunapojenga, tunapoinua mizigo ya wengine, hubariki maisha yetu kwa namna ambayo majaribu yetu hayawezi kuondoa. Nina nukuu ya Rais Gordon B. Hinckley ambayo imewekwa sehemu ninayoiona kila siku: Alisema: “Huwezi … kujenga kwa kukosa rajua au ubeuzi. Unatazamia kwa matumaini, unafanya kazi kwa imani, na mambo yanafanyika”9.
Mfano wa roho ya furaha na matumaini, ni msichana wa miaka 13 ninaemjua aitwaye Elsa ambaye familia yake inahamia Baton Rouge, Lousiana, maili 1,800 (2,900 km) mbali na rafiki zake. Si kitu rahisi unapokuwa na miaka 13 kuhamia sehemu mpya. Elsa alikuwa hana uhakika kuhusu kuhama hivyo baba yake akampa baraka. Punde alipopewa baraka, simu ya mama yake ikapokea ujumbe mfupi. Wasichana wanaoishi huko Lousiana walituma picha hii ikiwa na maneno “Tafadhali hamia kwenye kata yetu!”10
Wasichana hawa walikuwa na uhakika wangempenda Elsa hata kabla hawajaonana naye. Shauku yao iliunda matumaini kwa Elsa kuhusu kuhama na ikajibu sala yake kuhusu kama kila kitu kitakuwa sawa.
Kuna nguvu ambayo inatokana na furaha na matumaini ambayo hayatubariki sisi tu—humjenga kila mtu. Kitu chochote kidogo ufanyacho kuangaza furaha ya kweli kwa wengine inaonyesha kwamba tayari unabeba tochi ambayo Rais Kimball aliwasha.
Nilikuwa na miaka 15 wakati hotuba ya Rais Kimball ilipotolewa. Sisi tulio zaidi ya miaka 40 tumekuwa tukibeba jukumu hili toka kwa Rais Kimball tangu siku hiyo. Sasa, ninamwangalia mwenye miaka 8, miaka 15, na miaka 20, na miaka 35, na nakuachieni tochi hii ninyi. Ninyi ni viongozi wa baadaye wa Kanisa hili, na itakuwa juu yenu kuibeba nuru hii isonge mbele na kutimiza unabii huu. Sisi tulio wakubwa zaidi ya miaka 40 tunaunganisha mikono yetu na yenu na kuhisi uwezo na nguvu zenu. Tunawahitaji ninyi.
Sikilizeni andiko hili lipatikanalo katika Mafundisho na Maagano 49:26–28. Linaweza kuwa limeandikwa kwa hali tofauti, lakini jioni hii kwa Roho Mtakatifu, natumaini mtalichukua kama wito binafsi katika kazi hii takatifu.
“Tazama, ninawaambia, enendeni kama nilivyowaamuru; tubuni dhambi zenu zote; ombeni nanyi mtapokea; bisheni nanyi mtafunguliwa.
“Tazama, nitakwenda mbele yenu na nitawafuata nyuma; na nitakuwa katikati yenu, na wala hamtaaibika.
“Tazama, Mimi ni Yesu Kristo, na naja haraka.”11
Mimi ninamwomba kila mmoja wenu kujiweka katika sehemu ambayo mnaweza kuhisi upendo karimu ambao Mungu anao kwa ajili yenu. Hamwezi kujiweka mbali na upendo huo. Unapohisi upendo Wake, unapompenda Yeye, utatubu na kutii amri Zake. Mnapotii amri Zake, Atawatumia katika kazi Yake. Kazi na utukufu Wake ni kuhuishwa na uzima wa milele wa wanawake na wanaume.
Manabii wanatuita sisi, dada zangu. Mtakuwa wema? Mtaielezea kwa ufasaha imani yenu? Mnaweza kustahimili kuwa dhahiri na tofauti? Je, furaha yenu licha ya majaribu yenu itawaleta wengine walio wazuri na wa kipekee na wale wanaohitaji urafiki wenu? Mtawasha taa zenu? Ninashuhudia Bwana Yesu Kristo atakwenda mbele yetu na kuwa katikati yetu.
Ninamalizia kwa maneno ya nabii wetu mpendwa,Thomas S. Monson: “Dada zangu wapendwa, hii ni siku yenu, huu ni wakati wenu.”12 Katika jina la Yesu Kristo, amina