Njoo, Unifuate
Oktoba 7–13: “Tazama, Shangwe Yangu Imetimia.” 3 Nefi 17–19


Oktoba 7–13: ‘Tazama, Shangwe Yangu Imetimia.’ 3 Nefi 17–19,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2023)

“Oktoba 7–13. 3 Nefi 17–19,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2023)

Yesu akiwatokea Wanefi

Nuru ya Uso Wake Iling’ara juu Yao, na Gary L. Kapp

Oktoba 7–13: “Tazama, Shangwe Yangu Imetimia”

3 Nefi 17–19

Yesu Kristo alikuwa amehudumu kwa siku nzima katika nchi ya Neema, akifundisha injili Yake, akiwaacha watu waone na kugusa alama kwenye mwili Wake uliofufuka, na kushuhudia kwamba Yeye alikuwa Mwokozi aliyeahidiwa. Sasa ikafika muda wa kuondoka. “Tazama, muda wangu umewadia,” Yeye alisema (3 Nefi 17:1). Yeye alikuwa karibu kurudi kwa Baba Yake na Yeye alijua kwamba watu walihitaji muda kutafakari kile Yeye alichokuwa amewafundisha. Kwa hivyo, akiahidi kurudi tena siku iliyofuata, Aliuruhusu umati waende majumbani kwao. Lakini hakuna aliyeondoka. Hawakusema kile walichokuwa wakihisi, lakini Yesu aliweza kukihisi: walitumaini “angekaa nao kwa muda mrefu zaidi” (3 Nefi 17:5). Yeye alikuwa na mambo mengine muhimu ya kufanya, lakini kuonesha huruma kwa watoto wa Mungu daima ni kipaumbele cha juu Kwake. Kwa hiyo Yesu alikaa kwa muda mrefu zaidi. Kile kilichofuata pengine kilikuwa mfano wa huduma ya upendo zaidi iliyoandikwa katika maandiko. Wale waliokuwepo waliweza tu kusema kwamba ilikuwa haielezeki (ona 3 Nefi 17:16–17). Yesu Mwenyewe alitoa muhtasari wa mbubujiko huu wa kiroho wa papo kwa papo kwa maneno haya rahisi: “Sasa tazama, shangwe yangu imetimia” (3 Nefi 17:20).

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

3 Nefi 17; 18:24–25, 30–32

Mwokozi ni mfano wangu mkamilifu wa kuhudumu.

Karibia watu 2,500 walikuwepo wakati Mwokozi alipoonekana , licha ya wingi huo Yeye alipata njia ya kuwahudumia mmoja mmoja. Je, ni kipi umegudua kuhusu jinsi ambavyo Yeye alihudumu katika 3 Nefi 17; 18:24–25, 28–32? Je, ni mahitaji yapi ambayo Yeye aliyakidhi? Ni sifa zipi zilifanya kuhudumu Kwake kufanikiwe? Ungeweza pia kufikiria kuhusu jinsi Yeye anavyohudumu kwako. Wewe unawezaje kufuata mfano Wake? (Ona pia 3 Nefi 18:24–25 na 28–32.)

Ona pia “Jesus Christ Has Compassion and Heals the People” (video), Maktaba ya Injili.

3 Nefi 17:13–22; 18:15–25; 19:6–9, 15–36

Mwokozi alinifundisha jinsi ya kusali.

Fikiria vile ambavyo ingekuwa kumsikia Mwokozi akisali kwa ajili yako. Ni kwa jinsi gani uzoefu kama huo unaathiri jinsi unavyosali? Tafakari hili unapojifunza 3 Nefi 17:13–22; 18:15–25; 19:6–9, 15–36. Je, unajifunza nini kutokana na mfano na mafundisho ya Yesu Kristo kuhusu sala? Fikiria kutafuta umaizi kuhusu jinsi gani, wakati upi, wapi, kwa ajili ya nani, na kwa nini unasali. Je, ni umaizi upi mwingine unapata kutoka katika mistari hii?

Ona pia Mafundisho na Maagano 10:5.

3 Nefi 18:1–12

ikoni ya seminari
Ninaweza kujazwa na Roho wakati ninapopokea sakramenti.

Tunapofanya kitu kila mara, kinaweza kuwa desturi au kaida. Wakati mwingine tunaishia kukifanya bila hata kufikiria. Ni kwa jinsi gani unaweza kuzuia hilo lisitokee kwa ibada ya kila wiki ya sakramenti? Unaposoma 3 Nefi 18:1–12, tafakari jinsi unavyoweza “kujazwa” kiroho kila mara unapopokea sakramenti (ona pia 3 Nefi 20:1–9). Kulingana na mistari 5–7, 11, nini baadhi ya vitu unavyopaswa kuvifanya “daima”? Ungeweza pia kutafakari kwa nini Yesu alitupatia ibada ya sakramenti—na kama sakramenti inatimiza makusudi Yake katika maisha yako. Kwa nini sakramenti ni takatifu kwako?

Katika ujumbe wake “Mkumbuke Daima” (Liahona, Feb. 2018, 4–6), Rais Henry B. Eyring alitoa “mapendekezo matatu kuhusu kile ambacho unaweza kukumbuka kila wiki wakati unapopokea ishara takatifu za sakramenti. Ni kipi kinachokuvutia wewe sana kuhusu mapendekezo yake? Je, unaweza kufanya nini ili kuboresha kuabudu kwako wakati wa sakramenti na kote katika wiki?

Je, ni kipi kingine unaweza kufanya ili kuabudu kwa njia yenye maana zaidi? Ungeweza kujiuliza maswali kama haya: “Ni kwa jinsi gani dhabihu ya Mwokozi inayashawishi maisha yangu ya kila siku?” “Ni kipi ninachofanya vyema kama mfuasi Wake, na ni kipi ninaweza kuboresha?”

Ona pia Mathayo 26:26–28; Jeffrey R. Holland, “Tazama Mwanakondoo wa Mungu,” Liahona, Mei 2019, 44–46; “Twapokea Sakramenti,” Nyimbo za Dini, na. 90; “Jesus Christ Introduces the Sacrament” (video), Maktaba ya Injili; Mada za Injili, “Sakramenti,” Maktaba ya Injili.

Ruhusu muda wa kutafakari. Wakati mwingine, kujifunza maandiko huwa mseto wa kusoma, kusali, na kutafakari. Unaporuhusu muda wa utulivu wa kutafakari na kuzungumza na Mungu kuhusu kitu ambacho unajifunza, unaweza kuongeza nguvu za neno Lake katika maisha yako.

3 Nefi 18:22–25

Ninaweza “kuinua juu” nuru ya Yesu Kristo.

Tuseme ungekuwa na rafiki ambaye hajui lolote kuhusu Yesu Kristo isipokuwa kwamba wewe ni mmoja wa wafuasi Wake. Ni kipi rafiki yako angehitimisha kumhusu Yeye, kulingana na matendo yako? Inamaanisha nini kwako “Kwa hivyo, inueni juu nuru yenu ili iangaze juu ya dunia? (3 Nefi 18:24). Ni mialiko ipi mingine Mwokozi aliitoa katika 3 Nefi 18:22–25 ambayo inakusaidia uinue nuru hiyo?

Ona pia Bonnie H. Cordon, “Ili Wapate Kuona,” Liahona, Mei 2020, 78–80.

3 Nefi 18:36–37; 19:6–22

Wafuasi wa Yesu Kristo hutafuta kipawa cha Roho Mtakatifu.

Fikiria kuhusu sala zako za hivi karibuni. Je, sala zako zinakufundisha nini kuhusu matamanio yako ya kina? Baada ya kushinda siku nzima katika uwepo wa Mwokozi, makutano “waliomba wapate kile ambacho walikitamani zaidi”—kipawa cha Roho Mtakatifu (3 Nefi 19:9). Kwa nini kipawa cha Roho Mtakatifu ni cha kutamanika sana? Unaposoma vifungu hivi, tafakari matamanio yako mwenyewe kwa ajili ya wenzi wa Roho Mtakatifu. Je, ni kwa jinsi gani unaweza kwa dhati zaidi kutafuta wenzi huu?

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la Liahona na magazeti ya Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana.

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

3 Nefi 17:7, 20–25

Mwokozi anampenda kila mmoja wa watoto wa Baba wa Mbinguni.

  • Ungeweza kutumia picha kama zile zilizo katika muhtasari huu au video “Jesus Christ Prays and Angels Minister to the Children” (Maktaba ya Injili) ili kuwasaidia watoto wako wapate twasira ya tukio hilo katika 3 Nefi 17. Fikiria kusoma virai au mistari kutoka 3 Nefi 17 ambavyo vinasisitiza upendo wa Mwokozi kwa watu (kama vile mstari wa 7 na 20–25). Watoto wako wangeweza kuchora picha zao wenyewe wakiwa na Yesu. Wanapofanya hivyo, wasaidie wafikirie njia ambazo Yesu ameonesha upendo Wake kwao.

Yesu akiwabariki watoto

Tazama Wadogo Wenu, na Gary L. Kapp

3 Nefi 18:1–12

Ninaweza kumfikiria Yesu wakati ninapopokea sakramenti.

  • Pengine ungeweza kuwaalika watoto wako wakuambie nini kinatendeka wakati wa sakramenti. Kisha ungeweza kusoma 3 Nefi 18:1–12 na waombe watoto wanyanyue mkono wakati wanaposikia jambo ambalo linafanana na kile tunachofanya leo. Ni kipi Yesu Kristo anatutaka sisi tukumbuke au tufikirie wakati wa sakramenti? (ona 3 Nefi 18:7, 11).

3 Nefi 18:15–24; 19:6–9, 15–36

Yesu alinifundisha jinsi ya kusali.

  • Kuimba pamoja wimbo kuhusu sala, kama vile “A Child’s Prayer” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 12–13), ni njia nzuri ya kuwasaidia watoto wako wafikirie kuhusu kwa nini tunasali. Wewe na watoto wako kisha mngeweza kusoma 3 Nefi 18:18–21 na kuzungumza kuhusu kitu ambacho Yesu alifundisha kuhusu sala. Kuwaalika watoto wako wakuambie jinsi wanavyohisi wakati wanaposali kungeweza kuwasaidia washiriki shuhuda zao juu ya sala.

  • Inaweza kuwa burudani kwa watoto kuenda kuwinda baadhi ya baraka za thamani za sala. Ungeweza kuandika marejeleo ya maandiko yafuatayo kwenye vipande vya karatasi na uvifiche: 3 Nefi 18:15; 3 Nefi 18:20; 3 Nefi 18:21; 3 Nefi 19: 9; na 3 Nefi 19:23. Watoto wako kisha wangeweza kutafuta karatasi na kusoma mistari, wakitafuta mambo ambayo Yesu Kristo au wanafunzi Wake waliyafundisha kuhusu sala.

Kwa ajili ya mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

malaika wakiwa wamemzingira Yesu na watoto wa Wanefi

Malaika Waliwahudumia, na Walter Rane