Mkutano Mkuu
Ili wapate kuona
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Ili wapate kuona

Angalia na uombe kwa ajili ya fursa za kufanya nuru yako iangaze ili wengine waweze kuona njia ya kwenda kwa Yesu Kristo.

Akina kaka na akina dada, mioyo yetu imebarikiwa na kufanywa upya na Roho ambaye tumemhisi kwenye mkutano huu.

Picha
Nguzo ya mwamga

Miaka mia mbili iliyopita, nguzo ya mwanga ilitua juu ya kijana mdogo kwenye msitu wa miti. Katika mwanga huo, Joseph Smith alimuona Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo. Nuru yao ilirudisha nyuma giza la kiroho lililofunika dunia na kuelekeza njia mbele kwa ajili ya Joseph Smith—na kwetu sisi sote. kwa sababu ya nuru iliyofunuliwa siku hiyo, tunaweza kupokea utimilifu wa baraka zinazopatikana kupitia Upatanisho wa Mwokozi wetu, Yesu Kristo.

Kwa sababu ya Urejesho wa injili Yake, tunaweza kujazwa na nuru ya Mwokozi wetu. Walakini, hiyo nuru haikukusudiwa kwako na mimi pekee. Yesu Kristo ametuagiza “acha nuru yenu iangae mbele ya hawa watu, ili wapate kuyaona matendo yenu, na kumtukuza Baba yenu aliye mbinguni.”1 Nimekuja kupenda maneno “ili wapate kuona.” Ni mwaliko wa dhati kutoka kwa Bwana kuwa na nia zaidi ya kusaidia wengine kuona njia na hivyo kuja kwa Kristo.

Picha
Mzee L. Tom Perry

Wakati nilipokuwa na umri wa miaka 10, familia yetu ilikuwa na heshima ya kumkaribisha Mzee L. Tom Perry wa Akidi ya Mitume Kumi na wawili wakati alipokuwa kwenye jukumu katika mji wangu.

Mwisho wa siku, familia yetu na ya Perry tulikaa sebuleni kwetu kufurahia mkate wa mama yangu wa kupendeza wakati Mzee Perry akisimulia hadithi kuhusu Watakatifu ulimwenguni. Nilivutiwa sana.

Giza lilianza kuingia wakati mama yangu aliponiita jikoni na kuuliza swali rahisi: “Bonnie, je! Ulilisha kuku?”

Moyo wangu ulishuka; Sikuwa nimewalisha. Kwa kutotaka kuondoka kwenye uwepo wa Mtume wa Bwana, nilipendekeza kwamba kuku wangeweza kufunga hadi asubuhi.

Mama yangu alijibu kwa kukataa “hapana.” Wakati huohuo, Mzee Perry aliingia jikoni na kwa sauti yake ya kupendeza na yenye shauku aliuliza, “Je! Nilisikia kuna mtu anahitaji kulisha kuku? Je! Mimi na mwanangu tunaweza kuungana nawe?”

Lo, ilikuwa shangwe iliyoje sasa kuwalisha kuku! Nilikimbia kuleta tochi yetu kubwa ya manjano. Kwa furaha, niliongoza mbele, nikiruka juu ya njia iliyoharibika hadi kwenye kizimba cha kuku. Nikiwa na tochi ikibembea mikononi mwangu, tulivuka shamba dogo la mahindi na kupita katikati ya shamba la ngano.

Tulipofikia mtaro mdogo wa umwagiliaji ambao ulipita katikati ya njia , niliruka bila kufikiri kama nilivyokuwa nimefanya mara nyingi hapo awali. Sikujali juhudi za Mzee Perry kuwepo kwenye njia ya giza, isiyojulikana. Mwanga wangu wa kucheza cheza haukumsaidia kuona mtaro. Bila taa iliyotulia ya kuonea, aliingia moja kwa moja ndani ya maji na kutoa sauti kubwa ya maumivu. Nikiwa nimeshikwa na hofu, niligeuka kuona rafiki yangu mpya akiondoa mguu wake uliolowa maji kutoka mtaroni na kukung’uta maji kutoka kwenye kiatu kikubwa cha ngozi.

Kwa kiatu kilicholowa na kurusha maji, Mzee Perry alinisaidia kulisha kuku. Tulipomaliza, aliagiza kwa upendo, “Bonie, ninahitaji kuona njia. Nahitaji nuru iangaze ninakoenda.”

Nilikuwa nikiangaza taa yangu lakini si kwa njia ambayo ingemsaidia Mzee Perry. Sasa, nikijua kuwa alihitaji taa yangu ili kuongoza njia kwa usalama, nililenga tochi mbele kabisa ya hatua zake na tuliweza kurudi nyumbani kwa ujasiri.

Wapendwa akina kaka na dada zangu, kwa miaka nimeitafakari kanuni niliyojifunza kutoka kwa Mzee Perry. Mwaliko wa Bwana wa kuacha nuru yetu iangaze si tu kuhusu kupunga bila utaratibu mwali wa mwanga na kufanya ulimwengu kwa ujumla angavu. Ni kuhusu kufokasi nuru yetu ili wengine waweze kuona njia ya kwenda kwa Kristo. Ni kukusanya Israeli upande huu wa pazia—kuwasaidia wengine kuona hatua inayofuata kwenda mbele katika kufanya na kutunza maagano na Mungu.2

Mwokozi alishuhudia, “Tazama mimi ndimi nuru; nimewapatia mfano.”3 Wacha tuangalie moja ya mifano Yake.

Mwanamke pale kisimani alikuwa Msamaria ambaye hakumjua Yesu Kristo na alitazamwa na watu wengi kama mtu aliyetengwa katika jamii yake. Yesu alikutana naye na akaanzisha mazungumzo. Alizungumza naye juu ya maji. Kisha alimwongoza kupata nuru zaidi wakati alipojitangaza kuwa “maji yaliyo hai.”4

Kristo kwa huruma alimfahamu na alifahamu mahitaji yake. Alikutana na mwanamke mahali alipokuwa na kuanza kwa kuzungumzia jambo lililojulikana na la kawaida. Kama Angeliachia hapo, ungekuwa mkutano mzuri. Lakini isingelisababisha mwanamke aende mjini kutangaza, “Njoni, mtazame … : Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?”5 Polepole, kupitia mazungumzo, alimgundua Yesu Kristo, na licha ya mambo yake ya nyuma, akawa chombo cha nuru, akiangaza njia kwa ajili ya wengine kuona.6

Sasa wacha tuangalie watu wawili ambao walifuata mfano wa Mwokozi wa kuangaza nuru. Hivi karibuni rafiki yangu Kevin alikuwa ameketi karibu na afisa biashara wakati wa chakula cha jioni. Alihofu kuhusu nini cha kuzungumza kwa masaa mawili. Kufuatia msukumo, Kevin aliuliza, “Niambie kuhusu familia yako. Wanatokea wapi?”

Bwana huyo alijua kidogo juu ya urithi wake, kwa hivyo Kevin akatoa simu yake, akisema, “Nina programu ambayo inaunganisha watu kwa familia zao. Wacha tuone kile tunachoweza kupata.”

Baada ya majadiliano marefu, rafiki mpya wa Kevin aliuliza, “Kwa nini familia ni muhimu sana katika kanisa lenu?”

Kevin alijibu kwa urahisi, “Tunaamini kwamba tunaendelea kuishi baada ya kifo. Ikiwa tutawatambua mababu zetu na kupeleka majina yao sehemu takatifu inayoitwa hekalu, tunaweza kufanya ibada za ndoa ambazo zitaweka familia zetu pamoja hata baada ya kifo.”7

Kevin alianza na kitu ambacho yeye na rafiki yake mpya walikuwa nacho. Kisha akapata njia ya kushuhudia juu ya nuru na upendo wa Mwokozi.

Hadithi ya pili ni juu ya Ella, mwanachuo mwenza mchezaji wa mpira wa kikapu. Mfano wake ulianza wakati alipokea wito wa misheni akiwa mbali shuleni. Alichagua kufungua wito wake mbele ya timu yake. Hawakujua chochote kuhusu Kanisa la Yesu Kristo na hawakuelewa hamu ya Ella ya kutumikia. Aliomba tena na tena ili kujua jinsi ya kuelezea wito wake wa misheni kwa njia ambayo wanatimu wenzake wangemhisi Roho. Jibu lake?

“Nilifanya PowerPoint,” Ella alisema, “kwa sababu mimi ni mzuri kwa njia hiyo.” Aliwaambia juu ya uwezekano wa kuhudumu katika moja ya misheni 400-na zaidi na uwezekano wa kujifunza lugha. Alionesha maelfu ya wamisionari ambao tayari wanahudumu. Ella alihitimisha kwa picha ya Mwokozi na ushuhuda huu mfupi: “Mpira wa kikapu ni moja ya mambo muhimu sana maishani mwangu. Nilitembea nchi mzima na kuiacha familia yangu ili kucheza na kocha huyu na timu hii. Vitu viwili tu ambavyo ni muhimu sana kwangu kuliko mpira wa kikapu ni imani yangu na familia yangu.”8

Sasa, ikiwa unafikiria, “Hii ni mifano mikubwa ya wati 1,000, lakini mimi ni bulb ya wati 20,” kumbuka kwamba Mwokozi alishuhudia, “Mimi ni mwangaza ambao mtainua.”9 Anatukumbusha kwamba Yeye ataleta nuru ikiwa tu tutawaelekeza wengine Kwake.

Wewe na mimi tuna nuru ya kutosha kushiriki sasa hivi. Tunaweza kuangazia hatua inayofuata ili kumsaidia mtu kumkaribia Yesu Kristo, na kisha hatua inayofuata, na inayofuata.

Jiulize, “Nani anayehitaji nuru uliyonayo ili kupata njia wanayohitaji lakini hawaoni?”

Rafiki zangu wapendwa, kwa nini kuangaza nuru yetu ni muhimu sana? Bwana ametuambia kwamba “Kwani bado wako wengi duniani … ambao huzuiliwa kuupata ukweli kwa sababu tu hawajui mahali pa kuupata.”10 Tunaweza kusaidia. Tunaweza kuangaza nuru yetu kwa makusudi ili wengine waone. Tunaweza kutoa mwaliko.11 Tunaweza kutembea safarini pamoja na wale ambao wanachukua hatua kumwelekea Mwokozi, haijalishi jinsi gani tunasitasita. Tunaweza kuikusanya Israeli.

Ninashuhudia kwamba Bwana atakuza kila juhudi ndogo. Roho Mtakatifu atatupa msukumo kujua nini cha kusema na kufanya. Majaribio kama hayo yanaweza kututaka kutoka katika eneo letu la faraja, lakini tunaweza kuwa na uhakika kwamba Bwana atasaidia nuru yetu kuangaza.

Jinsi gani nina furaha kwa ajili ya nuru ya Mwokozi, ambayo inaendelea kuongoza Kanisa hili kupitia ufunuo.

Picha
Mwokozi akiwa ameshikilia taa

Ninawaalika sisi sote kufuata mfano wa Yesu Kristo na kuwa wenye huruma na kuwatambua wale wanaotuzunguka. Angalia na uombe kwa ajili ya fursa za kufanya nuru yako iangaze ili wengine waweze kuona njia ya kwenda kwa Yesu Kristo. Ahadi yake ni kubwa: “Yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”12 Ninashuhudia kwamba Mwokozi wetu, Yesu Kristo, ndiye njia, ukweli, uzima, nuru, na upendo wa ulimwengu. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha