Ujumbe wa Utangulizi
Tunapaswa kutafuta, kwa kila njia tunayoweza, kumsikiliza Yesu Kristo, ambaye anasema nasi kupitia nguvu na huduma ya Roho Mtakatifu.
Wapendwa akina kaka na dada zangu, tunapowakaribisha kwenye mkutano huu mkuu wa kihistoria wa Aprili 2020 wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, kwa sababu mnazozijua, ninasimama mbele yenu kwenye ukumbi usio na watu!
Sikujua, wakati nilipowaahidi kwenye mkutano mkuu wa Oktoba 2019 kwamba mkutano huu wa Aprili utakuwa “wa kukumbukwa” na “usiosahaulika,” kwamba kuzungumza na umma uliopo wa watu wasiozidi 10 kungeufanya mkutano huu uwe wa kukumbukwa na usiosahaulika kwangu! Lakini bado ufahamu kwamba mnashiriki matangazo kwa njia ya kielektroniki, na uimbaji mzuri wa kwaya wa wimbo “It Is Well with My Soul,” unaleta faraja kuu nafsini mwangu.
Kama mjuavyo, mahudhurio katika mkutano huu mkuu yamekuwa madogo kama sehemu yetu ya kuwa raia wema ulimwengu na kufanya yote tunayoweza kuzuia kuenea kwa COVID-19. Virusi hivi vimekuwa na madhara makubwa kote ulimwenguni. Pia vimebadilisha kwa muda mikutano yetu ya Kanisa, huduma ya umisionari, na kazi ya hekalu.
Ingawa vizuizi vya leo vinahusiana na virusi hatari, majaribu binafsi ya maisha ni makubwa zaidi ya janga hili. Majaribu ya siku za usoni yanaweza kutokana na ajali, janga la asili, au maumivu binafsi yasiyotarajiwa.
Je, tunawezaje kuvumilia majaribu ya aina hiyo? Bwana amekwishatuambia kwamba “kama mmejitayarisha hamtaogopa.”1 Bila shaka, tunaweza kuhifadhi akiba zetu wenyewe za chakula, maji, na pesa. Lakini muhimu pia ni hitaji letu la kujaza ghala zetu za kiroho kwa imani, ukweli, na ushuhuda.
Tamanio letu la juu katika maisha ni kujitayarisha kukutana na Muumba wetu. Tunafanya hivi kwa kujaribu kila siku kuwa zaidi kama Mwokozi wetu, Yesu Kristo.2 Na tunafanya hivyo pale tunapotubu kila siku na kupokea utakaso Wake, uponyaji, na nguvu za kuimarisha. Ndipo tunapoweza kuhisi amani na furaha ya kudumu, hata kwenye nyakati za misukosuko. Hii ndiyo sababu kwa nini Bwana ametuomba sisi kusimama katika mahali patakatifu na “wala tusiondoshwe.”3
Mwaka huu, tunaadhimisha kumbukumbu ya miaka 200 ya moja ya matukio muhimu sana katika historia ya ulimwengu—yaani, kuonekana kwa Mungu Baba na Mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo, kwa Joseph Smith. Katika ono lile, Baba wa Mbinguni alimtambulisha Yesu Kristo na akasema: “Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!”4
Ushauri huo aliopewa Joseph ni kwa kila mmoja wetu. Tunapaswa kutafuta, kwa kila njia tunayoweza, kumsikiliza Yesu Kristo, ambaye anasema nasi kupitia nguvu na huduma ya Roho Mtakatifu.
Lengo la mkutano huu na kila mkutano mkuu ni kutusaidia kumsikiliza Yeye. Tumeomba, na tunakualika uombe, kwamba Roho wa Bwana awe pamoja nasi kwa wingi sana kwamba uweze kusikiliza jumbe ambazo Mwokozi anazo mahususi kwa ajili yako—jumbe ambazo zitaleta amani katika nafsi yako. Jumbe ambazo zitaponya moyo wako uliovunjika. Jumbe ambazo zitaangazia akili yako. Jumbe ambazo zitakusaidia kujua nini cha kufanya wakati ukisonga mbele kupita nyakati za misukosuko na majaribu.
Tunaomba kwamba mkutano huu uwe wa kukumbukwa na usiosahaulika kwa sababu ya jumbe utakazozisikia, matangazo ya kipekee ambayo yatatolewa, na uzoefu ambao utakaribishwa kushiriki.
Kwa mfano, katika kuhitimisha kikao cha Jumapili asubuhi, tutakusanya mkutano mtakatifu ulimwenguni kote wakati nitakapowaongoza katika Kupaza sauti takatifu za Hosanna. Tunaomba kwamba huu utakuwa ukumbusho wa kiroho kwenu wakati tukielezea kwa pamoja shukrani yetu kubwa kwa Mungu Baba na Mwanaye Mpendwa kwa Kuwasifu kwa njia hii ya kipekee.
Kwa tendo hili takatifu, tunatumia vitambaa vya mkononi visafi vyeupe. Lakini kama huna, unaweza kupunga tu mkono wako. Baada ya kupaza sauti za Hosanna, umati utaungana na kwaya katika kuimba “The Spirt of God.”5
Kaka zangu na dada zangu wapendwa, mkutano huu utakuwa wa kupendeza sana. Mwaka huu utakuwa wa kipekee wakati tunapofokasi kwa dhati kwa Mwokozi na injili Yake iliyorejeshwa. Matokeo muhimu zaidi ya kudumu ya mkutano huu wa kihistoria ni pale mioyo yetu itakapobadilika na sisi kuanza safari ya maisha yote ya kumsikiliza Yeye.
Karibuni kwenye mkutano mkuu wa Aprili 2020! Ninajua kwamba Mungu, Baba yetu wa Mbinguni, na Mwanaye, Yesu Kristo, wanatujali. Watakuwa pamoja nasi wakati wote wa siku hizi mbili tukufu wakati tunapojaribu kutafuta kusonga karibu Nao na Kuwaheshimu. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.