Mkutano Mkuu
Ukuhani wa Melkizedeki na Funguo
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Ukuhani wa Melkizedeki na Funguo

Katika Kanisa mamlaka ya ukuhani yanatumika chini ya maelekezo ya kiongozi wa ukuhani ambaye anashikilia funguo za ukuhani huo.

Nimechagua kuongelea zaidi kuhusu ukuhani wa Mungu, swala lililokwisha ongelewa na wanenaji watatu waliotangulia ambao wametufunza jinsi ukuhani unavyobariki maisha ya wanawake, wavulana na wasichana.

Ukuhani ni nguvu na mamlaka ya kiungu yanayomilikiwa kwa uaminifu kutumika kwa ajili ya kazi ya Mungu kwa manufaa ya watoto Wake wote. Ukuhani siyo wale waliotawazwa kwenye ofisi ya kuhani au wale wanaotumia mamlaka yake. Wanaume wanaoshikilia ukuhani siyo ukuhani. Wakati hatupaswi kuwarejelea wanaume waliotawazwa kama ukuhani, ni vyema kuwarejelea kama wenye ukuhani.

Nguvu za ukuhani zinapatikana kote katika kanisa na katika mpangilio wa familia. Lakini nguvu ya ukuhani na mamlaka ya ukuhani hutenda kazi tofauti ndani ya kanisa kuliko zinavyofanya katika familia. Hii yote ni kulingana na kanuni zilizowekwa na Bwana. Lengo la mpango wa Mungu ni kuwaongoza watoto wake katika uzima wa milele. Familia za duniani ni za muhimu katika mpango huo. Kanisa lipo kutoa mafundisho, mamlaka, na ibada zilizo muhimu kuendeleza uhusiano wa kifamilia katika umilele. Hivyo, mpangilio wa familia na Kanisa la Yesu Kristo vina uhusiano wa pamoja wenye kuimarishana. Baraka za ukuhani—kama vile utimilifu wa injili na ibada kama ubatizo, uthibitisho na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, endaumenti ya hekaluni, na ndoa ya milele—vinapatikana sawasawa kwa wanaume na wanawake.1

Ukuhani tunaouongelea hapa ni Ukuhani wa Melkizedeki, uliorejeshwa mwanzoni mwa Urejesho wa injili. Joseph Smith na Oliver Cowdery walitawazwa na Petro, Yakobo na Yohana, ambao walijitangaza “kuwa wanashikilia funguo za ufalme, na za kipindi cha utimilifu wa nyakati” (Mafundisho na Maagano 128:20). Mitume hawa waandamizi walipokea mamlaka hayo kutoka kwa Mwokozi Mwenyewe. Mamlaka mengine yote au ofisi katika ukuhani ni viambatanisho kwenye Ukuhani wa Melkizedeki (Ona Mafundisho na Maagano 107:5), kwani “unashikilia haki za urais, na unao uwezo na mamlaka juu ya ofisi zote katika kanisa katika vipindi vyote vya ulimwengu” (Mafundisho na Maagano 107:8).

Katika Kanisa, mamlaka ya ukuhani wa juu, Ukuhani wa Melkizedeki, na mdogo au Ukuhani wa Haruni yanatumika chini ya maelekezo ya kiongozi wa ukuhani, kama askofu au rais, ambaye anashikilia funguo za ukuhani huo. Kuelewa matumizi ya mamlaka ya ukuhani katika kanisa, lazima tuelewe kanuni za funguo za ukuhani.

Funguo za Ukuhani wa Melkizedeki za ufalme zilitolewa na Petro, Yakobo, na Yohana, lakini hiyo haikukamilisha urejesho wa funguo za ukuhani. Baadhi ya funguo za ukuhani zilikuja baadaye. Kufuatia uwekaji wakfu wa hekalu la kwanza la kipindi hiki cha maongozi ya Mungu huko Kirtland, Ohio, manabii watatu—Musa, Elia, na Eliya—walirejesha “funguo za kipindi hiki,” zikiwemo funguo zihusianazo na kukusanya Israeli na kazi ya mahekalu ya Bwana (ona Mafundisho na Maagano 110), kama ambavyo Rais Eyring ametoka kuelezea kwa ushawishi.

Mfano unaofahamika zaidi wa kazi za funguo uko katika utendaji wa ibada za ukuhani. Ibada ni tendo la dhati linalomaanisha ufanyaji wa maagano na ahadi ya baraka. Katika kanisa, ibada zote hufanywa chini ya mamlaka ya kiongozi wa ukuhani anayeshikilia funguo za ibada hiyo.

Ibada mara nyingi hufanywa na watu waliotawazwa kwenye ofisi katika ukuhani wakitenda chini ya maelekezo ya mwenye kushikilia funguo za ukuhani. Mfano, wenye kushikilia ofisi mbalimbali katika Ukuhani wa Haruni huudumu katika ibada ya sakramenti chini ya funguo na maelekezo ya askofu, ambaye hushikilia funguo za Ukuhani wa Haruni. Kanuni kama hiyo hutumika kwenye ibada za ukuhani ambapo wanawake huudumu ndani ya hekalu. Japo wanawake hawashikilii ofisi katika ukuhani, wanafanya ibada takatifu za hekaluni chini ya mamlaka ya rais wa hekalu, ambaye hushikilia funguo za ibada za hekaluni.

Mfano mwingine wa mamlaka ya ukuhani chini ya maelekezo ya yule anayeshikilia funguo ni mafundisho ya wanaume na wanawake walioitwa kufundisha injili, iwe katika madarasa ya kata zao za nyumbani au eneo la misheni. Mifano mingine ni wale wanaoshikilia nafasi za uongozi katika kata na kutumia mamlaka ya ukuhani katika uongozi wao kwa sababu ya miito yao na kwa kutengwa na kwa maelekezo ya kiongozi wa ukuhani anayeshikilia funguo katika kata au kigingi. Hivi ndivyo mamlaka na nguvu za ukuhani zinavyotumika na kufurahiwa katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.2

Mamlaka ya ukuhani pia hutumiwa na baraka zake kutambuliwa katika familia za Watakatifu wa Siku za Mwisho. Kwa familia namaanisha mwanaume mwenye ukuhani na mwanamke ambao wameoana pamoja na watoto wao. Pia ninahusisha tofauti kutoka katika mahusiano bora kama yale yaliyosababishwa na kifo au talaka.

Kanuni ya kwamba mamlaka ya ukuhani yanaweza tu kutumika chini ya maelekezo ya yule ambaye ana funguo kwa ajili ya kazi hiyo ni muhimu katika Kanisa, lakini hii haitumiki katika familia. Mfano, baba anasimamia na kutumia ukuhani katika familia yake kwa mamlaka ya ukuhani aliyonayo. Hana haja ya kupata maelekezo au ruhusa ya anayeshikilia funguo za ukuhani ili kufanya kazi mbalimbali za familia yake. Hizi zikihusisha kushauri wanafamilia yake, kufanya vikao vya familia, kutoa baraka za ukuhani kwa mkewe na wanawe, au kutoa baraka za uponyaji kwa wanafamilia au watu wengine.3 Mamlaka za kanisa huwafunza wanafamilia lakini haziwaelekezi katika kutumia mamlaka ya ukuhani katika familia.

Kanuni kama hiyo hutumika pale baba akiwa hayupo na mama ni kiongozi wa familia. Mama anasimamia katika nyumba yake na ni chombo katika kuleta nguvu na baraka za ukuhani ndani ya familia yake kupitia endaumenti na kuunganishwa kwake hekaluni. Japo haruhusiwi kutoa baraka za ukuhani ambazo hutolewa tu na mtu anayeshikilia ofisi fulani katika ukuhani, anaweza kufanya kazi zingine zote za uongozi wa familia. Kwa kufanya hivyo, anatumia nguvu za ukuhani kwa manufaa ya watoto anaowasimamia katika nafasi yake ya uongozi katika familia.4

Kama akina baba wangekuza ukuhani wao katika familia zao wenyewe, ingesogeza mbele kazi ya Kanisa zaidi ya kingine chochote ambacho wangeweza kufanya. Akina baba wanaoshikilia Ukuhani wa Melkizedeki watumie mamlaka yao “kwa njia ya ushawishi, kwa uvumilivu, kwa upole na unyenyekevu, na kwa upendo usio unafiki” (Mafundisho na Maagano 121: 41). Kiwango hicho cha juu kwa ajili ya utumiaji wa mamlaka yote ya ukuhani ni muhimu zaidi katika familia. Wanaoshikilia ukuhani pia wanapaswa kutii amri ili waweze kuwa na nguvu za ukuhani kutoa baraka kwa wanafamilia wao. Wanapaswa kukuza mahusiano yenye upendo ya familia ili kwamba wanafamilia wawaombe baraka. Na wazazi lazima wahimize upatikanaji zaidi wa baraka za ukuhani katika familia.5

Katika vikao hivi vya mkutano, tunapotafuta kimbilio la muda mfupi kutokana na wasiwasi wetu wa maisha haya pamoja na maradhi ya kutisha , tumefundishwa kanuni kuu za umilele. Ninawahimiza kila mmoja wetu kuweka jicho lake “safi” kupokea kweli hizi za milele ili kwamba miili yetu “iwe yenye nuru kamilifu” (3 Nefi 13:22).

Katika mafundisho yake kwa umati yaliyorekodiwa katika Biblia na katika Kitabu cha Mormoni, mwokozi alifundisha kwamba miili ya duniani huweza kuwa na nuru kamilifu au giza kuu. Sisi, hata hivyo, tunataka tujazwe nuru, na Mwokozi wetu alitufundisha jinsi ya kufanya hili. Tunapaswa kusikiliza jumbe kuhusu kweli za milele. Alitumia mfano wa jicho letu, ambalo kupitia kwalo tunaingiza nuru katika miili yetu. Kama jicho letu “liko moja”—kwa maneno mengine kama tumejikita katika kupokea nuru na uelewa—Alieleza, “mwili wako wote utajaa nuru” (Mathayo 6:22; 3 Nefi 13:22). Lakini kama “jicho letu ni ovu”—ikimaanisha kwamba, kama tukitafuta uovu na kuuchukua huo ndani ya miili yetu—Ameonya, “mwili wako wote utajaa giza” (mstari wa 23). Kwa maneno mengine, nuru au giza katika miili yetu hutegemea na jinsi tunavyoona—au kupokea— kweli za milele tunazofundishwa.

Tunapaswa kufuata mwaliko wa Mwokozi wa kutafuta na kuomba ili kuelewa kweli za milele. Ameahidi kwamba Baba yetu wa Mbinguni yuko radhi kumfunza kila mmoja kweli wanazozitafuta (ona 3 Nefi 14:8). Kama tutatamani hili na kuweka jicho letu safi kupokea, Mwokozi anaahidi kwamba kweli za milele “zitafunguliwa” kwetu (ona 3 Nefi 14:7–8).

Kinyume chake, Shetani ana hamu ya kuvuruga kufikiri kwetu au kutupotosha kwenye mambo ya muhimu kama utendaji kazi wa ukuhani wa Mungu. Mwokozi alionya kuhusu hao “manabii wa uwongo, ambao huwajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali” (3 Nefi 14:15). Alitupatia jaribio hili kutusaidia kuchagua ukweli kutoka katika mafundisho tofauti ambayo huweza kutukanganya: “Mtawatambua kwa Matunda yao,” Alifundisha (3 Nefi 14:16). “Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri” (mstari wa 18). Kwa hivyo, tutafute matokeo—“matunda”—ya kanuni zinazofundishwa na watu wanaozifundisha. Hilo ndilo jibu zuri sana kwa vipingamizi vingi tunavyovisikia dhidi ya Kanisa na mafundisho yake na sera na uongozi. Fuata jaribio Mwokozi alilofundisha. Tafuta matunda—matokeo.

Tunapofikiria matunda ya injili na Kanisa lililorejeshwa la Yesu Kristo, tunashangilia kwa jinsi Kanisa, katika maisha ya waumini wake walio hai, limepanuka kutoka mikusanyiko ya eneo katika milima ya Magharibi kufikia umati wa waumini miloni 16 wakaao katika mataifa tofauti na Marekani. Kwa ukuaji huo, tumehisi kuongezeka kwa uwezo wa Kanisa kusaidia washiriki wake. Tunasaidia katika kutii amri, katika kutimiza majukumu ya kuhubiri injili iliyorejeshwa, katika kukusanya Israeli, na katika kujenga mahekalu ulimwenguni kote.

Tunaongozwa na nabii, Rais Russell M. Nelson, ambaye uongozi wake umetumiwa na Bwana kufikia maendeleo tuliyoyahisi katika miaka yote miwili ya uongozi wake. Sasa tutabarikiwa kusikia kutoka kwa Rais Nelson, ambaye atatufundisha jinsi ya kuzidisha maendeleo yetu katika Kanisa hili la Yesu Kristo lililolejeshwa katika nyakati hizi za changamoto.

Ninashuhudia ukweli wa vitu hivi na kuungana nanyi katika kumuombea nabii wetu, ambaye baadaye tutasikia kutoka kwake, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha