Nyumba za Kupendeza
Mwokozi ni mhandisi mkamilifu, mjenzi na msanifu wa ndani. Mradi Wake ni ukamilifu na shangwe ya milele ya nafsi zetu.
Hivi karibuni bango katika Jiji la Salt Lake lilivutia macho yangu. Lilitangaza kampuni ya samani na usanifu wa ndani. Kwa urahisi lilisomeka, “Kuhudumia Nyumba za Kupendeza katika Jiji la Salt Lake.”
Ujumbe ulikuwa wa kushawishi—“nyumba ya kupendeza” ni nini? Nilijikuta nikitafakari kuhusu swali hilo, hasa kwa kuzingatia watoto ambao mimi pamoja na mke wangu, Kathy, tuliwalea na watoto ambao wao wanawalea leo. Sawa na wazazi kila mahali, tulikuwa na hofu na kuomba juu ya familia yetu. Bado tunafanya hivyo. Kwa dhati tunataka kile kilicho bora zaidi kwao. Ni kwa jinsi gani wao na watoto wao wanaweza kuishi katika nyumba za kupendeza? Nimetafakari juu ya nyumba za waumini wa Kanisa ambazo mimi na Kathy tumebahatika kuzitembelea. Tumekuwa tukialikwa kwenye nyumba huko Korea na Kenya, Ufilipino na Peru, Laos na Latvia. Acha nishiriki mawazo manne kuhusu nyumba za kupendeza.
Kwanza, kutoka katika mtazamo wa Bwana, kujenga nyumba za kupendeza kunahusisha kila kitu kuhusu sifa binafsi za watu wanaoishi humo. Nyumba hizi hazifanywi za kupendeza katika njia yoyote muhimu na ya kudumu kwa samani zake au kwa thamani halisi au nafasi ya kijamii ya watu wanaozimiliki. Sifa ya kupendeza ya nyumba yoyote ni taswira ya Kristo iliyoakisiwa kwa wakazi wa nyumba hiyo. Kile chenye umuhimu zaidi ni usanifu wa ndani wa mioyo ya wakazi, si jengo lenyewe.
Sifa za Kristo zinapatikana “baada ya muda”1 kwa maendeleo ya makusudi kwenye njia ya agano. Sifa kama za Kristo hupamba maisha ya wale wanaojitahidi kuishi kwa wema. Wanajaza nyumba kwa nuru ya injili, iwe sakafu ni udongo au marumaru. Hata kama uko peke yako katika nyumba yako ambaye unafuata amri ya “tafuta mambo haya,”2 unaweza kuchangia kwenye usanifu wa kiroho wa nyumba ya familia yako.
Tunafuata ushauri wa Bwana wa “kujiandaa [wenyewe]; kutayarisha kila kitu kinachohitajika; na kuijenga nyumba” kwa kuandaa, kutayarisha na kujenga maisha yetu ya kiroho, siyo makazi halisi. Wakati kwa uvumilivu tunapofuata njia ya Mwokozi ya agano, nyumba yetu inakuwa “nyumba ya utukufu, nyumba ya utaratibu [na] nyumba ya Mungu.”3
Pili, wakazi katika nyumba za kupendeza hutenga muda wa kujifunza maandiko na maneno ya manabii walio hai kila siku. Rais Russell M. Nelson ametualika “kuzibadilisha” na “kuzifanya upya” nyumba zetu kwa kujifunza injili.4 Mwaliko wake unatambua kwamba nyumba za kupendeza huruhusu kazi muhimu ororo, ya ukuaji binafsi na hubadili udhaifu wetu. Toba ya kila siku ni nyenzo ya badiliko ambayo inatusaidia kuwa wakarimu zaidi, wenye kupenda zaidi na wenye kuelewa zaidi. Kujifunza maandiko kunatusogeza karibu na Mwokozi, ambaye upendo wake mkarimu na rehema vinatusaidia kwenye ukuaji wetu.
Biblia, Kitabu cha Mormoni, na Lulu ya Thamani Kuu vinasimulia hadithi za familia, hivyo, haishangazi kwamba juzuu hizo takatifu ni vitabu visivyoweza kulinganishwa kwa ajili ya kujenga nyumba za kupendeza. Vinaandika nyakati za hofu za wazazi, hatari za majaribu, ushindi wa uadilifu, majaribu ya ukame na ya neema, na vitisho vya vita na tuzo za amani. Tena na tena maandiko yanatuonesha jinsi familia zilivyofanikiwa kupitia kuishi kwa uadilifu na jinsi wanavyoshindwa kwa kutafuta njia zingine.
Tatu, nyumba za kupendeza zinafuata ramani iliyobuniwa na Bwana kwa ajili ya nyumba Yake ya kupendeza, hekalu. Kujenga hekalu kunaanza na hatua za msingi—kusafisha kichaka na kuweka sawa ardhi. Juhudi hizo za mwanzo za kutayarisha ardhi zinaweza kufananishwa na kutii amri za msingi. Amri ni msingi ambao juu yake ufuasi unajengwa. Ufuasi imara hutuongoza kwenye kuwa thabiti, wasio tingishika na wasio hamishika,5 sawa na mhimili wa chuma wa hekalu. Mhimili huu imara humruhusu Bwana kumtuma Roho Wake kuibadili mioyo yetu.6 Kupata badiliko kuu la moyo ni kama kuongeza mapambo ya kupendeza kwenye sehemu ya ndani ya hekalu.
Tunapoendelea katika imani, Bwana taratibu anatubadilisha. Tunapokea sura Yake katika nyuso zetu na kuanza kutafakari upendo na uzuri wa sifa Yake.7 Tunapokuwa kama Yeye, tutajisikia tuko nyumbani katika nyumba Yake, na Yeye atajisikia yuko nyumbani katika nyumba zetu.
Tunaweza kudumisha muunganiko wa karibu wa nyumba zetu na nyumba Yake kwa kustahili kwa ajili ya, na kutumia kibali cha hekaluni mara nyingi kadiri hali zinavyoruhusu. Tunapofanya hivyo, utakatifu wa nyumba ya Bwana unakaa katika nyumba yetu pia.
Hekalu la kupendeza la Salt Lake linasimama karibu. Likijengwa na waanzilishi kwa nyenzo duni, vifaa vya kawaida, na juhudi zisizokoma, hekalu lilijengwa kuanzia 1853 hadi 1893. Kizuri zaidi waumini wa mwanzo wa Kanisa walichoweza kutoa katika uhandisi, usanifu na mapambo ya ndani vilijenga kazi bora ambayo inatambuliwa na mamilioni.
Takribani miaka 130 imepita tangu hekalu lilipowekwa wakfu. Kama alivyosema jana Mzee Gary E. Stevenson, kanuni za uhandisi zilizotumika kusanifu hekalu zimebadilishwa kwa viwango vipya, salama zaidi. Kushindwa kuongeza uhandisi wa hekalu na kurekebisha udhaifu wa jengo kungesaliti kujiamini kwa waanzilishi, ambao walifanya yote waliyoweza na kisha kuacha uangalizi wa hekalu kwa vizazi vinavyoendelea.
Kanisa limeanzisha mradi wa miaka minne wa urejesho ili kuboresha jengo la hekalu na nguvu ya kuhimili tetemeko la ardhi.8 Msingi, sakafu na kuta vitaimarishwa. Maarifa bora zaidi ya uhandisi yanayopatikana leo yatalileta hekalu kwenye viwango vya kisasa. Hatutaweza kuona mabadiliko kwenye jengo, lakini matokeo yake yatakuwa halisi na muhimu. Katika kazi hii yote, sifa za kupendeza za usanifu wa ndani ya hekalu zitatunzwa.
Tunapaswa kufuata mfano uliotolewa kwetu kwa ukarabati wa Hekalu la Salt Lake na kuchukua muda kutathmini uhandisi wetu binafsi wa kiroho ili kuhakikisha kuwa ni wa kisasa. Tathmini binafsi ya mara kwa mara, ikiambatana na kumuuliza Bwana, “Nimepungukiwa na nini tena?”9 inaweza kumsaidia kila mmoja wetu kuchangia kwenye kujenga nyumba ya kupendeza.
Nne, nyumba za kupendeza ni kimbilio kutoka kwenye dhoruba za maisha. Bwana ameahidi kwamba wale wanaotii amri za Mungu “wanafanikiwa katika nchi.”10 Mafanikio ya Mungu ni nguvu ya kusonga mbele licha ya matatizo ya maisha.
Mnamo 2002 nilijifunza somo muhimu kuhusu matatizo. Nikiwa Asunción, Paraguay, nilikutana na marais wa vigingi vya jiji. Wakati huo, Paraguay ilikabiliwa na janga baya la kifedha, na waumini wengi wa Kanisa walikuwa wakiteseka na kutoweza kukidhi mahitaji yao. Sikuwahi kurudi Amerika ya Kusini tangu nilipomaliza misheni yangu na sikuwahi kufika Paraguay. Nilikuwa nikihudumu tu katika Urais wa Eneo lile kwa wiki chache. Nikiwa na hofu kuhusu kutoweza kwangu kutoa mwongozo kwa wale marais wa vigingi, niliwaomba waniambie tu nini kilikuwa kikienda vizuri katika vigingi vyao. Rais wa kigingi wa kwanza aliniambia kuhusu mambo yaliyokuwa yakienda vizuri. Aliyefuata alitaja mambo ambayo yalienda vizuri na matatizo machache. Wakati tulipofika kwa rais wa kigingi wa mwisho, yeye alitaja tu mfululizo wa changamoto za kuleta hofu. Wakati marais wa vigingi walipoelezea ukubwa wa tatizo, nilipata ongezeko la mashaka, karibu kukata tamaa, kuhusu nini cha kusema.
Mara tu rais wa kigingi wa mwisho alikuwa akikamilisha kutoa mawazo yake, wazo lilinijia akilini: “Mzee Clayton, waulize swali hili: ‘Marais, juu ya waumini katika vigingi vyenu wanaolipa zaka kamili, wanaolipa matoleo ya mfungo kwa ukarimu, wanaokuza miito yao Kanisani, kwa hakika wanatembelea familia zao kama walimu wa nyumbani au walimu watembeleaji11 kila mwezi, wanafanya jioni ya familia nyumbani, wanajifunza maandiko na kusali kama familia kila siku, ni wangapi kati yao wana matatizo wasiyoweza kuyashughulikia wao wenyewe bila Kanisa kuingilia na kutatua matatizo kwa ajili yao?’”
Kwa kuitikia msukumo niliopokea, niliwauliza marais wa vigingi swali hilo.
Walinitazama kwa mshangao wenye ukimya na kisha kusema, “Pues, ninguno,” ikimaanisha “Vema, hakuna.” Kisha wao wakaniambia kwamba hakuna muumini aliyefanya mambo yote hayo aliyekuwa na matatizo ambayo hawakuweza kuyatatua wao wenyewe. Kwa nini? Kwa sababu waliishi katika nyumba za kupendeza. Maisha yao ya uaminifu yaliwapa nguvu, ono, na msaada wa kimbingu waliohitaji kwenye ghasia ya kiuchumi ambayo iliwazunguka.
Hii haina maana kwamba wenye haki hawatapata magonjwa, kuteseka kwa ajali, kukabiliwa na kurudi nyuma kibiashara, au kukabili magumu mengine mengi katika maisha. Maisha ya duniani daima yanaleta changamoto, lakini muda baada ya muda nimeona kwamba wale wanaojitahidi kutii wanabarikiwa kusonga mbele kwa amani na tumaini. Baraka hizo zinapatikana kwa kila mmoja.12
Daudi alitamka, “Bwana asipoijenga nyumba, waijengao wafanya kazi bure.”13 Popote unapoishi, bila kujali nyumba yako inaonekanaje, na bila kujali muundo wa familia yako, unaweza kujenga nyumba ya kupendeza kwa ajili ya familia yako. Injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo inatoa ramani kwa ajili ya nyumba hiyo. Mwokozi ni mhandisi mkamilifu, mjenzi na msanifu wa ndani. Mradi Wake ni ukamilifu na shangwe ya milele ya nafsi zetu. Kwa usaidizi Wake wa upendo, nafsi yako inaweza kuwa yote Yeye anayotaka iwe na unaweza kuwa toleo bora zaidi la wewe mwenyewe, lililotayarishwa kuanzisha na kuishi katika nyumba bora zaidi
Kwa shukrani ninashuhudia kwamba Mungu na Baba yetu sote yu hai. Mwanaye, Bwana Yesu Kristo, ni Mwokozi na Mkombozi wa wanadamu wote. Wanatupenda kwa ukamilifu. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni ufalme wa Mungu duniani. Manabii na mitume walio hai wanaliongoza leo. Kitabu cha Mormoni ni cha kweli. Injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo ni ramani kamilifu kwa ajili ya kujenga nyumba za kupendeza. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.