Mkutano Mkuu
Kupata Kimbilio kutoka kwenye Dhoruba za Maisha
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Kupata Kimbilio kutoka kwenye Dhoruba za Maisha

Yesu Kristo na upatanisho wake ni kimbilio ambalo sisi sote tunalihitaji, bila kujali dhoruba ambazo zinagonga maisha yetu.

Nyuma katikati ya miaka ya tisini, wakati wa miaka yangu ya chuo, nilikuwa sehemu ya Kampuni ya Nne ya Idara ya Zimamoto ya Santiago huko Chile. Wakati nikitumikia huko, niliishi kwenye kituo cha zimamoto kama sehemu ya mlinzi wa usiku. Karibu na mwisho wa mwaka, niliambiwa kwamba napaswa kuwepo kwenye kituo cha zimamoto kipindi cha Mkesha wa Mwaka Mpya kwa sababu siku hiyo kunakuwa na dharura kila wakati. Kwa mshangao, nilijibu, “Kweli?”

Ndiyo, nakumbuka wakati nikingoja pamoja wa wafanyakazi wenzangu, saa sita za usiku, mafataki yalianza kurushwa katika mji wa Santiago. Tulianza kukumbatiana kila mmoja na kutakiana kheri ya mwaka mpya. Ghafla kengele kwenye kituo cha zimamoto zilianza kulia, kuashiria kuwa kulikuwa na dharura. Tulichukua vifaa vyetu na kuingia kwenye gari ya zima moto. Tukiwa njiani kuelekea kwenye dharura, tukiwa tunapita kwenye umati wa watu waliokuwa wakisherehekea mwaka mpya, niligundua kuwa walikuwa hawajali na hawakuchukua tahadhari. Walikuwa wamepumzika na kufurahia majira ya joto ya usiku. Lakini mahali pengine karibu, watu ambao tulikuwa tunaharakisha kuwasaidia walikuwa katika shida kubwa.

Uzoefu huu ulinisaidia mimi kutambua kwamba japokuwa maisha yetu nyakati zingine yanaweza kuwa yanakwenda vizuri, wakati utakuja kwa kila mmoja wetu kukutana na changamoto na dhoruba zisizotarajiwa ambazo zitasukuma kikomo cha uwezo wetu wa kuvumilia. Changamoto za kimwili, kiakili, kifamilia na za ajira; majanga ya asili; na mambo mengine ya maisha au kifo ni baadhi ya mifano ya dhoruba ambazo tutakutana nazo kwenye haya maisha.

Wakati tunakumbana na hizi dhoruba, mara nyingi tunapata hisia za kukata tamaa au hofu. Raisi Russel M. Nelson alisema,“Imani ndio kizio cha woga”—imani katika Bwana wetu Yesu Kristo (“Acha Imani Yako Ionekane,” Liahona, Mei 2014, 29). Kama ambavyo nimeona dhoruba ambazo zinaathiri maisha ya watu, nimehitimisha kuwa haijalishi ni aina gani ya dhoruba inayotugonga—bila ya kujali kuna suluhisho la hilo au ikiwa kuna mwisho wa kuonekana—kuna kimbilio moja tu, na ni sawa kwa kila aina ya dhoruba. Kimbilio hili moja lililotolewa na Baba wa Mbinguni ni Bwana wetu Yesu Kristo na Upatanisho Wake.

Hakuna yeyote kati yetu ambaye ameondolewa kwenye kukabiliana na hizi dhoruba. Helamani, nabii wa Kitabu cha Mormoni, alitufundisha kama ifuatavyo: “Kumbukeni, kumbukeni kwamba ni juu ya mwamba wa Mkombozi wetu, ambaye ni Kristo, Mwana wa Mungu, kwamba lazima mjenge msingi wenu; kwamba ibilisi atakapotuma mbele pepo zake kali, ndio, mishale yake kimbungani, wakati mvua yake ya mawe na dhoruba kali itapiga juu yenu, hautakuwa na uwezo juu yenu kuwavuta chini kwenye shimo la taabu na msiba usioisha, kwa sababu ya mwamba ambako kwake mmejengwa, ambao ni msingi imara, msingi ambako watu wote wakijenga hawataanguka” (Helamani 5:12).

Mzee Robert D. Hales, ambaye alikuwa na uzoefu wake mwenyewe kwenye kuvumilia dhoruba, alisema: “Mateso ni kwa wote; jinsi gani tunakabiliana na mateso ni mtu binafsi. Mateso yanaweza kutupeleka kwenye moja ya njia mbili. Yanaweza kuwa uzoefu wa kuimarisha na wa kutakasa yakichanganywa na imani, au yanaweza kuwa nguvu ya kuharibu katika maisha yetu ikiwa hatuna imani katika dhabihu ya upatanisho ya Bwana” (“Huzuni Yako Itageuzwa kuwa Shangwe,” Ensign, Nov. 1983, 66).

Ili kufurahia kimbilio ambalo Yesu Kristo na Upatanisho Wake vinatoa, lazima tuwe na imani Kwake—imani itakayoturuhusu kuinuka juu ya maumivu yote ya mtazamo wenye kikomo, wa kidunia. Ameahidi kwamba atafanya mizigo yetu iwe miepesi ikiwa tutakuja Kwake katika yote tunayofanya.

“Njooni kwangu, Alisema, “ninyi msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo: nanyi mtapata raha nafsini mwenu.

“Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi” (Mathayo11:28–30; ona pia Mosia 24:14–15).

Inasemekana kwamba “kwa mtu aliye na imani, maelezo si ya lazima. Kwa yule asiye na imani, hakuna maelezo yanayowezekana.” (Taarifa hii imehusishwa na Thomas Aquinas lakini ina uwezekano mkubwa wa kuwa ufafanuzi huru wa mambo ambayo alifundisha.) Walakini, tuna ufahamu mdogo wa mambo ambayo hufanyika hapa duniani, na mara nyingi hatuna majibu ya swali la kwa nini. Kwanini hili linatokea? Kwanini hili linatokea kwangu? Ni kipi napaswa kujifunza? Wakati majibu yanapotukwepa, hapo ndipo maneno yaliyosemwa na Mwokozi wetu kwa Nabii Joseph Smith huko jela ya Liberty yanahusika kikamilifu:

“Mwanangu, amani iwe katika nafsi yako; taabu yako na mateso yako yatakuwa kwa muda mfupi;

“Na halafu, kama utastahimili vyema, Mungu atakuinua juu” (Mafundisho na Maagano 121: 7–8).

Ingawa watu wengi wanaamini katika Yesu Kristo, swali la msingi ni ikiwa tunamwamini Yeye na ikiwa tunaamini mambo ambayo Yeye anatufundisha na kutuomba tufanye. Labda mtu anaweza kufikiria, “Yesu Kristo anajua nini juu ya kile kinachoendelea kwangu? Je, Anajuaje kile ninachohitaji ili niwe na furaha?” Kwa kweli, alikuwa Mkombozi na Mwombezi wetu ambaye nabii Isaya alikuwa akimzungumzia wakati aliposema:

“Alidharauliwa na kukataliwa na watu; mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko. …

“Kwa hakika amejichukulia unyonge wetu, na kubeba huzuni zetu. …

“Lakini alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu: adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake; na kwa kupigwa kwake sisi tumepona” (Isaya 53:3–5).

Mtume Petro pia alitufundisha kuhusu Mwokozi, akisema, “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki: na kwa kupigwa kwake mliponywa” (1 Petro 2:24).

Japokuwa mauaji ya Petro yalikuwa yanakaribia, maneno yake hayakuwa ya uwoga au kukata tamaa; bali, aliwafundisha watakatifu “kufurahi,” ingawa walikuwa “wamehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali.” Petro alitushauri kukumbuka kwamba “kujaribiwa kwa imani [yetu], … ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto,” ingepelekea kwenye “sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo” na kwenye wokovu wa roho [zetu]” (1 Petro 1:6–7, 9).

Petro aliendelea:

“Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho:

“Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake, mfurahi kwa shangwe” (1 Petro 4:12–13).

Raisi Russell M. Nelson alifundisha kwamba “Watakatifu wanaweza kuwa na furaha katika kila hali. … Wakati fokasi ya maisha yetu ipo katika mpango wa Mungu wa wokovu … na Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kuhisi furaha bila kujali nini kinatokea—au hakitokei—katika maisha yetu. Furaha inakuja kutoka Kwake na kwa sababu Yake. Yeye ni chanzo cha furaha yote” (“Furaha na Kuendelea Kusalia Kiroho,” Liahona, Nov. 2016, 82).

Kwa kweli, ni rahisi kusema haya yote wakati hatupo katikati ya dhoruba kuliko kuishi na kuyatumia wakati wa dhoruba. Lakini kama kaka yako, natumai unajisikia kuwa ninatamani sana kushiriki nawe jinsi ilivyo muhimu kujua kuwa Yesu Kristo na Upatanisho Wake ni kimbilio ambalo sisi sote tunalihitaji, bila kujali dhoruba ambazo zinagonga maisha yetu.

Ninajua kwamba sisi wote ni watoto wa Mungu, kwamba Anatupenda, na kwamba hatupo peke yetu. Ninakualika uje na uone kuwa Yeye anaweza kufanya mizigo yako kuwa miepesi na kuwa kimbilio unalotafuta. Njoo na uwasaidie wengine kupata kimbilio wanalotamani. Njoo na ukae nasi kwenye kimbilio hili, ambalo litakusaidia kuhimili dhoruba za maisha. Hakuna shaka moyoni mwangu kwamba ikiwa utakuja, utaona, utasaidia, na utakaa.

Nabii Alma alishuhudia yafuatayo kwa mwana wake Helamani: “Kwani najua kwamba wote watakaoweka imani yao katika Mungu watasaidiwa kwa majaribio yao, na taabu zao, na mateso yao, na watainuliwa juu katika siku ya mwisho” (Alma 36:3).

Mwokozi Mwenyewe alisema:

Kwa hiyo, mioyo yenu na ifarijike juu ya Sayuni; kwa kuwa wenye mwili wote wako mikononi mwangu; tulieni na jueni kuwa Mimi ni Mungu. …

“Kwa hiyo, msiogope hata kwa mauti; kwani katika ulimwengu huu shangwe yenu siyo kamilifu, bali ndani yangu shangwe yenu ni kamilifu” (Mafundisho na Maagano 101:16, 36).

Wimbo “Be Still, My Soul,” ambao umegusa moyo wangu mara nyingi, una ujumbe wa faraja kwa mioyo yetu. Maneno ya wimbo yanasomeka kama ifuatavyo:

Tulia, Roho Yangu: muda unakwenda

Wakati tutakapokuwa na Bwana milele,

Wakati kukata tamaa, huzuni, na woga vimeondoka,

Huzuni imesahaulika, upendo safi kabisa umerejeshwa.

Tulia, Roho yangu: wakati mabadiliko na machozi yamekwisha,

Sote tukiwa salama na waliobarikiwa tutakutana hatimaye. (Nyimbo za Kanisa, na. 124).

Tunapokabiliwa na dhoruba za maisha, ninajua kwamba ikiwa tutafanya kwa juhudi zetu zote na kumtegemea Yesu Kristo na upatanisho Wake kama kimbilio letu, tutabarikiwa kwa utulivu, faraja, nguvu, uvumilivu, na utulivu ambao tunautafuta, kwa uhakika mioyoni mwetu kwamba mwisho wa wakati wetu hapa duniani, tutasikia maneno ya Bwana: “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu: … ingia katika furaha ya bwana wako” (Mathayo 25:21). Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha