Mkutano Mkuu
Yeye Huenda Mbele Yetu
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Yeye Huenda Mbele Yetu

Bwana anaongoza Urejesho wa injili Yake na Kanisa Lake. Anaujua wakati ujayo kikamilifu. Anakualika wewe kwenye kazi.

Wapendwa akina kaka na dada zangu, nina shukrani kuwa pamoja nanyi katika mkutano huu mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Katika mwaliko wake wa kutafakari juu ya jinsi Urejesho wa Bwana wa Kanisa Lake katika kipindi hiki cha mwisho ulivyotubariki sisi na wapendwa wetu, Rais Russell M. Nelson aliahidi kwamba uzoefu wetu utakuwa sio tu wa kukumbukwa bali usiosahaulika.

Uzoefu wangu umekuwa wa kukumbukwa, kama nilivyo na uhakika kwamba wenu pia umekuwa hivyo. Kama utakuwa usio sahaulika hiyo ni juu ya kila mmoja wetu. Hiyo ina umuhimu kwangu kwa sababu uzoefu wa maandalizi ya mkutano huu umenibadili kwa njia ambayo ninataka uzoefu huo udumu. Acha nieleze.

Maandalizi yangu yalinirudisha kwenye kumbukumbu ya tukio katika Urejesho. Nimesoma kuhusu tukio hilo mara nyingi, lakini limekuwa siku zote kwangu kama taarifa ya mkutano muhimu ambao ulimhusu Joseph Smith, nabii wa Urejesho. Lakini wakati huu niliona katika maelezo jinsi Bwana anavyotuongoza, wafuasi Wake, katika Kanisa Lake. Niliona kile inachomaanisha kwa sisi binadamu kuongozwa na Mwokozi wa ulimwengu, Muumbaji—anayejua vitu vyote, vilivyopita, vilivyopo, na vijavyo. Anatufundisha hatua kwa hatua na kutuongoza, kamwe hatulazimishi.

Mkutano ninaouelezea ulikuwa wakati muhimu katika Urejesho. Ulikuwa mkutano wa siku ya Sabato uliofanyika mnamo Aprili 3, 1836, katika Hekalu la Kirtland Ohio, siku saba baada ya kuwekwa wakfu. Joseph Smith alielezea wakati huu mkuu katika historia ya ulimwengu kwa njia rahisi. Maelezo yake mengi yameandikwa katika Mafundisho na Maagano sehemu ya 110:

“Wakati wa alasiri, niliwasaidia Marais wengine katika kugawa Chakula cha Bwana kwa Kanisa, nikipokea kutoka kwa Mitume Kumi na Wawili, ambao zamu yao ilikuwa kuongoza kwenye meza takatifu kwa siku hii. Baada ya kufanya huduma hii kwa ndugu zangu, nilirejea kwenye mimbari, pazia likiwa limeshushwa, na nikapiga magoti, pamoja na Oliver Cowdery, kwa sala ya unyenyekevu na kimya kimya. Baada ya kuinuka kutoka kwenye sala, ono lifuatalo lilifunguliwa kwetu wote wawili.”1

“Pazia liliondolewa kutoka akilini mwetu, na macho yetu ya ufahamu yakafunguliwa.

“Tulimwona Bwana akiwa amesimama kwenye jukwaa la mimbari, mbele yetu; na chini ya miguu yake palikuwa na sakafu iliyofanywa kwa dhahabu safi, katika rangi kama ya kaharabu.

“Macho yake yalikuwa kama mwale wa moto; nywele za kichwa chake zilikuwa nyeupe kama theluji safi; uso wake uling’ara kupita mng’aro wa jua; na sauti yake ilikuwa kama sauti ya maji mengi yakimbiayo, hata sauti ya Yehova, akisema:

“Mimi ni kwanza na mwisho; Mimi ni yeye aliye hai, Mimi ni yule aliyeuawa; Mimi ni Mwombezi wenu kwa Baba.

“Tazama, dhambi zenu zimesamehewa; nanyi ni wasafi mbele zangu; kwa hiyo, inueni vichwa vyenu na kufurahi.

“Na acha mioyo ya ndugu zenu na ifurahi, na acha mioyo ya watu wangu wote ifurahi, ambao, kwa nguvu zao, wameijenga nyumba hii kwa ajili ya jina langu.

“Kwani tazama, nimeikubali nyumba hii, na jina langu litakuwa humu; nami nitajionyesha kwa watu wangu kwa rehema katika nyumba hii.

“Ndiyo, nitajitokeza kwa watumishi wangu, na kusema nao kwa sauti yangu mwenyewe, kama watu wangu watashika amri zangu, na hawataichafua nyumba hii takatifu.

“Ndiyo mioyo ya maelfu na makumi ya elfu itafurahia kwa furaha kuu kwa matokeo ya baraka zitakazomwagwa, na kwa endaomenti ambayo watumishi wangu wamepewa katika nyumba hii.

“Na umaarufu wa nyumba hii utaenea hadi nchi za kigeni; na huu ni mwanzo wa baraka ambazo zitamwagwa juu ya vichwa vya watu wangu. Hivyo ndivyo. Amina.

“Baada ya ono hili kufungwa, mbingu zilitufungukia tena; na Musa akatokea mbele yetu, na kutukabidhi funguo za kukusanyika kwa Israeli kutoka pande nne za dunia, na kuongozwa kwa makabila kumi kutoka nchi ya kaskazini.

“Baada ya hili, Elia alitokea, na kutukabidhi kipindi cha injili ya Ibrahimu, akisema kwamba kupitia sisi na uzao wetu vizazi vyote baada yetu sisi vitabarikiwa.

“Baada ya ono hili kufungwa, ono jingine kubwa na tukufu likatukia juu yetu; kwani Eliya nabii, aliyechukuliwa mbinguni bila ya kuonja mauti, alisimama mbele yetu, na kusema:

“Tazama, wakati umetimia kikamilifu, ambao ulinenwa kwa kinywa cha Malaki—ukishuhudia kwamba yeye [Eliya] lazima atatumwa, kabla ya kuja kwa siku ile iliyo kuu na ya Bwana—

“Kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na ya watoto iwaelekee baba, dunia yote isije ikapigwa kwa laana—

“Kwa hiyo, funguo za kipindi hiki zimekabidhiwa mikononi mwenu; na kwa hili ninyi mpate kujua kwamba siku ile iliyo kuu na ya kutisha ya Bwana i karibu, hata milangoni.”2

Sasa, Nimesoma maelezo hayo mara nyingi. Roho Mtakatifu alikuwa amethibitisha kwangu kwamba maelezo yalikuwa ya kweli. Lakini nilipojifunza na kusali kujiandaa kwa mkutano huu, Niliona kwa uwazi zaidi nguvu za Bwana kuongoza kwa ukamilifu wafuasi Wake katika kazi Yake.

Miaka Saba kabla ya Musa kukabidhi kwa Joseph funguo za kukusanyika kwa Isreal katika Hekalu la Kirtland, “Joseph alijifunza kutoka ukurasa wa jina wa Kitabu cha Mormoni kwamba kusudi lake lilikuwa ‘kuonesha sazo la nyumba ya Israeli … kwamba waweze kujua maagano ya Bwana, kwamba hawakutupiliwa mbali milele.’ Katika mwaka wa 1831, Bwana alimwambia Joseph kwamba kukusanyika kwa Israeli kungeanzia Kirtland, ‘Na kutoka hapo [Kirtland], yeyote nimtakaye atakwenda mbele miongoni mwa mataifa yote … kwani Israeli itaokolewa, na nitawaongoza.’”3

Ingawa kazi ya umisionari ilihitajika ili kukusanya Israeli, Bwana aliwapa msukumo wa kiungu viongozi Wake kuwafundisha wale Kumi na Wawili, ambao walikuja kuwa baadhi ya wamisionari wetu wa mwanzo, “Kumbuka, hamtakiwi kwenda kwa mataifa mengine, mpaka mtakapopokea endaomenti yenu.”4

Inaonekana kwamba Hekalu la Kirtland lilikuwa muhimu katika mpango wa hatua kwa hatua wa Bwana kwa angalau sababu mbili: Kwanza, Musa alingojea mpaka hekalu lilipomalizika kujengwa ili kurejesha funguo za kukusanyika kwa Israeli. Na pili, Rais Joseph Fielding Smith alifundisha kwamba “Bwana aliwaamrisha Watakatifu kujenga hekalu [Hekalu la Kirtland] ambamo angeweza kufunua funguo za mamlaka na ambamo mitume wangeweza kupata endaomenti na kutayarishwa kupogoa shamba lake la mizabibu kwa mara ya mwisho.”5 Ingawa endaomenti ya hekaluni kama tunavyoijua leo haikutolewa katika Hekalu la Kirtland, katika kutimiza utabiri, matayarisho ya ibada za hekaluni yalianza kutambulishwa huko, sambamba na mbubujiko wa mafunuo ya kiroho ambayo yaliwaimarisha wale walioitwa kwenda kwenye umisionari kwa endaomenti zilizoahidiwa za “nguvu kutoka juu”6 ambazo ziliongoza kwenye mkusanyiko mkubwa mno kupitia huduma ya umisionari.

Baada ya funguo za kukusanyika kwa Israeli kukabidhiwa kwa Joseph, Bwana alimpa mwongozo wa kiungu Nabii kuwatawanya washiriki wa wale Kumi na Wawili kwenye misheni. Nilipokuwa najifunza, ikawa wazi kwangu kwamba Bwana alikuwa ameandaa kwa kina njia kwa ajili ya wale kumi na wawili kwenda misheni ughaibuni ambako watu walikuwa wametayarishwa kuamini na kuwakubali. Baada ya muda, maelfu, kupitia kwao, wangeletwa katika Kanisa la Bwana lililorejeshwa.

Kulingana na kumbukumbu zetu, inakisiwa kwamba watu kati ya 7,500 na 8,000 walibatizwa wakati wa misheni mbili za wale Kumi na Wawili kwenye visiwa vya Uingereza. Hii ilijenga msingi kwa ajili ya kazi ya umisionari huko Ulaya. Mnamo mwishoni mwa karne ya 19, kiasi cha watu 90,000 walikuwa wamekusanyika Marekani, wengi katika hawa wakija kutoka Visiwa vya Uingereza na Scandinavia.7 Bwana alikuwa amempa mwongozo wa kiungu Joseph na wamisionari wale waaminifu waliokwenda kufanya kazi kutimiza mavuno ambayo lazima yalionekana, wakati huo, makubwa zaidi yao. Lakini Bwana, kwa mtazamo Wake mkamilifu na maandalizi, alifanya iwezekane.

Unakumbuka inavyoonekana kuwa lugha rahisi na takribani ya kishairi kutoka sehemu ya 110 ya Mafundisho na Maagano:

“Tazama, wakati umetimia kikamilifu, ambao ulinenwa kwa kinywa cha Malaki—ukishuhudia kwamba yeye [Eliya] lazima atatumwa, kabla ya kuja kwa siku ile iliyo kuu na ya Bwana—

“Kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na ya watoto iwaelekee baba zao, dunia yote isije ikapigwa kwa laana—

Kwa hiyo, funguo za kipindi hiki zimekabidhiwa mikononi mwenu; na kwa hili ninyi mpate kujua kwamba siku ile iliyo kuu na ya kutisha ya Bwana i karibu, hata milangoni.”8

Ninashuhudia kwamba Bwana aliona mbali zaidi kwenye siku zijazo na jinsi ambavyo Angetuongoza kumsaidia kukamilisha makusudi Yake katika siku za mwisho.

Wakati nilipokuwa nahudumia katika Uaskofu Simamizi miaka mingi iliyopita, nilipewa jukumu la kusimamia muundo na maendeleo ya kundi ambalo liliunda kile tulichokiita FamilySearch. Kwa umakini ninasema kwamba mimi “nilisimamia” kuundwa kwake, badala ya kusema mimi “niliongoza”. Watu wengi wenye akili sana waliacha kazi zingine na walikuja kujenga kile Bwana alichotaka.

Urais wa Kwanza walikuwa wameweka lengo la kupunguza urudufu wa ibada. Wasiwasi wao mkubwa ulikuwa kutoweza kujua kama ibada za mtu zilikuwa tayari zimefanywa. Kwa miaka mingi—au kilichoonekana kama miaka mingi—Urais wa Kwanza uliniuliza, “Lini utakuwa umekamilisha?”

Kwa sala, bidii, na dhabihu binafsi ya watu wenye uwezo mkubwa, kazi ilikamilishwa. Ilifanyika hatua kwa hatua. Jukumu la kwanza lilikuwa kufanya FamilySearch iwe ya kirafiki kwa wale ambao hawakuwa na uwezo wa kompyuta. Mabadiliko mengi yalikuja, na ninajua yataendelea kuja, kwani wakati wowote tunapoanza kutatua tatizo moja lililopata msukumo wa kiungu, tunafungua mlango kwa ajili ya ufunuo zaidi kwa ajili ya maendeleo angalau yenye umuhimu sawa ila tu hayajaonekana bado. Hata leo, FamilySearch inakuwa kile Bwana anachohitaji kwa ajili ya sehemu ya Urejesho Wake—na si tu kwa ajili ya kuepuka urudufu wa ibada.

Bwana anatuacha tufanye maboresho ili kusaidia watu kupata hisia za uzoefu na hata upendo kwa ajili ya mababu zao na kukamilisha ibada zao za hekaluni. Sasa, jinsi Bwana alivyojua ingetokea, vijana wanakuwa washauri wa kompyuta kwa wazazi wao na waumini wa kata. Wote wamepata shangwe kuu katika huduma hii.

Roho ya Eliya inabadili mioyo ya vijana na wazee, watoto na wazazi, wajukuu na mababu. Mahekalu hivi karibuni kwa furaha yatapanga fursa za ubatizo na ibada nyingine takatifu. Hamu ya kuwatumikia mababu zetu na uunganishaji wa wazazi na watoto inakua.

Bwana aliona yote yakija. Alipanga kwa ajili hiyo, hatua kwa hatua, kama alivyofanya kwa mabadiliko mengine katika Kanisa Lake. Amewalea na kuwaandaa watu waaminifu wanaochagua kufanya mambo magumu vizuri. Siku zote amekuwa kwa upendo mwenye subira katika kutusaidia kujifunza “mstari juu ya mstari, kanuni juu ya kanuni, hapa kidogo na pale kidogo.”9 Yeye ni thabiti katika mpangilio wa matakwa yake, na bado anahakikisha kwamba dhabihu mara zote huleta baraka endelevu ambazo hatukuziona kabla.

Ninahitimisha kwa kuelezea shukrani zangu kwa Bwana—Yeye ambaye alimpa mwongozo wa kiungu Rais Nelson kunialika mimi kufanya dhabihu ili kujiandaa kwa ajili ya mkutano huu. Kila saa na kila sala wakati wa kujiandaa kwangu ilileta baraka.

Ninawaalika wote wanaosikia ujumbe huu au kusoma maneno haya kuwa na imani kwamba Bwana anaongoza Urejesho wa injili Yake na Kanisa Lake. Anakwenda mbele yetu. Anaujua wakati ujayo kikamilifu. Anakualika wewe kwenye kazi. Anakujumuisha wewe katika hilo. Anao tayari mpango kwa ajili ya huduma yako. Na hata unapotoa dhabihu, utajisikia furaha pale unapowasaidia wengine kuinuka na kuwa tayari kwa ajili ya ujio Wake.

Ninashuhudia kwenu kwamba Mungu Baba yu hai. Yesu ndiye Kristo. Hili ni kanisa Lake. Yeye anakujua na anakupenda. Yeye anakuongoza. Yeye ametayarisha njia kwa ajili yako. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Chapisha