Tafakari Wema na Ukuu wa Mungu
Ninawaalika kukumbuka kila siku wema wa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo na kile Wao walichofanya kwa ajili yako.
Kwa nyakati zote, hata na hasa katika nyakati ngumu, manabii wametuhimiza kukumbuka ukuu wa Mungu na kutafakari kile Yeye alichotutendea sisi binafsi, kama familia na kama watu.1 Mwongozo huu unapatikana kote katika maandiko lakini ni dhahiri zaidi katika Kitabu cha Mormoni. Ukurasa wa jina unafafanua kwamba moja ya malengo ya Kitabu cha Mormoni ni “kuonyesha sazo la nyumba ya Israeli vitu vikubwa ambavyo Bwana aliwatendea baba zao.”2 Kitabu cha Mormoni kinahitimishwa kwa ombi la Moroni: “Tazama, ningewashauri kwamba mtakaposoma vitu hivi … kwamba mngekumbuka jinsi vile Bwana amekuwa na huruma kwa watoto wa watu … na kuitafakari katika mioyo yenu.”3
Mwendelezo wa maombi kutoka kwa manabii kwenye kutafakari juu ya ukuu wa Mungu ni wa kuvutia.4 Baba yetu wa Mbinguni anataka tukumbuke wema Wake na wa Mwana Wake Mpendwa, si kwa ajili ya kujisifu Kwao bali kwa ushawishi ambao kumbukumbu hiyo ya ukarimu Wao unao kwetu. Kwa kutafakari ukarimu Wao, mtazamo na uelewa wetu vinakuzwa. Kwa kutafakari huruma Yao, tunakuwa wanyenyekevu zaidi, wenye kuomba zaidi na imara zaidi.
Uzoefu mchungu wa aliyekuwa mgonjwa unaonesha jinsi shukrani kwa ukarimu na huruma vinavyoweza kutubadili. Mnamo mwaka 1987, nilipata kufahamiana na Thomas Nielson, mwanaume wa kusifika aliyehitaji upandikizaji wa moyo. Alikuwa na umri wa miaka 63 na aliishi Logan, Utah, Marekani. Kufuatia huduma ya jeshi wakati wa Vita ya II ya Dunia, alimuoa Donna Wilkes katika Hekalu la Logan Utah. Alikuja kuwa mwenye nguvu na mjenzi mwenye mafanikio. Katika miaka iliyofuata alifurahia hasa kufanya kazi pamoja na mjukuu wake mkubwa, Jonathan, kipindi cha likizo za shule. Wawili hao walijenga muunganiko wa kipekee, kwa sehemu kwa sababu Tom aliona sifa zake nyingi kwa Jonathan.
Tom aliona kusubiri kufadhiliwa moyo ilikuwa ya kuchosha. Hakuwa mtu mvumilivu sana. Amekuwa daima akiweza kuweka na kufikia malengo kupitia juhudi kubwa na dhamiri safi. Akipambana na matatizo ya moyo, maisha yake yakiwa hayasongi, Tom mara kwa mara aliniuliza nini nilikuwa nafanya kuharakisha mchakato. Kwa utani, alipendekeza njia ambazo ningeweza kutumia ambazo zingemfanya mfadhili wa moyo ajitokeze mapema.
Siku moja ya shangwe lakini pia ya kuogopesha, mfadhili bora wa moyo alipatikana kwa ajili ya Tom. Ukubwa na kundi la damu vilifanana, na mfadhili alikuwa kijana, miaka 16 tu. Moyo uliotolewa ufadhili ulikuwa wa Jonathan, mjukuu mpendwa wa Tom. Mapema siku hiyo, Jonathan alikuwa ameumia vibaya wakati gari alilokuwa akiendesha lilipogongwa na gari moshi iliyokuwa ikipita.
Nilipowatembelea Tom na Donna hospitalini, walikuwa wamefadhaishwa. Ni ngumu kufikiria kile walichokuwa wakipitia, kwa kujua kwamba maisha ya Tom yangeweza kurefushwa kwa kutumia moyo wa mjukuu wao. Mwanzo, walikataa kufikiria moyo uliotolewa kutoka kwa wazazi wenye huzuni wa Jonathan, binti yao na mkwe wao. Tom na Donna walifahamu, hata hivyo, kwamba ubongo wa Jonathan ulikuwa umekufa, na walikuja kuelewa kwamba maombi yao ya mfadhili wa moyo kwa ajili ya Tom hayakusababisha ajali ya Jonathan. Hapana, moyo wa Jonathan ulikuwa zawadi ambayo ingeweza kumbariki Tom katika wakati wake wa uhitaji. Walitambua kwamba jambo fulani zuri lingetokana na ajali hii na waliamua kuendelea.
Utaratibu wa upandikizaji ulienda vizuri. Baada ya hilo, Tom alikuwa mtu tofauti. Badiliko lilikuwa zaidi ya afya iliyoboreka au hata shukrani. Aliniambia kwamba alitafakari kila asubuhi juu ya Jonathan, juu ya binti yake na mkwe wake, juu ya zawadi aliyopokea na juu ya kile zawadi hiyo ilichohitaji. Japokuwa ucheshi wake halisi wa kupendeza na ujasiri viliendelea kuwa dhahiri, niligundua kwamba Tom alikuwa mtu wa ibada zaidi, mwenye kujali zaidi na mwenye moyo wa ukarimu zaidi.
Tom aliishi miaka 13 zaidi baada ya upandikizaji, miaka ambayo vinginevyo asingeishi. Wasifu wake ulisema kuwa miaka hii ilimruhusu kugusa maisha ya familia yake pamoja na wengine kwa ukarimu na upendo. Alikuwa mfadhili wa faragha na mfano wa tumaini na ushupavu.
Kama vile Tom, kila mmoja wetu amepokea zawadi ambazo hatuwezi kujipa sisi wenyewe, zawadi kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye Mpendwa, ikiwa ni pamoja na ukombozi kupitia dhabihu ya upatanisho wa Yesu Kristo.5 Tumepokea uzima katika ulimwengu huu; tutapokea maisha ya mwili baada ya haya, na wokovu wa milele na kuinuliwa—kama tutachagua—yote kwa sababu ya Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.
Kila mara tunapotumia, kunufaika, au hata kufikiria zawadi hizi, tunapaswa kuzingatia dhabihu, ukarimu na huruma ya watoaji. Unyenyekevu kwa watoaji hufanya zaidi ya kutufanya tu wenye shukrani. Kufikiria juu ya baraka Zao kunaweza na kunapaswa kutubadili.
Badiliko moja la kusifika lilikuwa lile la Alma Mdogo. Wakati Alma alipokuwa “akizunguka kumuasi Mungu,”6 malaika alimtokea. Kwa “sauti kama ya radi,”7 malaika alimkemea Alma kwa kulitesa Kanisa na “kuiba mioyo ya watu.”8 Malaika aliongeza onyo hili: “Nenda, na ukumbuke utumwa wa babu zako …; na ukumbuke vile vitu vikuu ambavyo [Mungu] amewatendea.”9 Kati ya maonyo yote yanayowezekana, hilo ndilo malaika alilosisitiza.
Alma alitubu na kukumbuka. Baadaye alishiriki maonyo ya malaika kwa mwana wake Helamani. Alma alishauri, “Ningetaka kwamba ufanye vile nilivyofanya, kwa kukumbuka utumwa wa babu zetu; kwani walikuwa katika utumwa, na hapakuwa na yeyote ambaye angewaokoa isipokuwa awe Mungu wa Ibrahimu, … Isaka, na … Yakobo; na kwa kweli aliwakomboa katika mateso yao.”10 Alma alisema kwa urahisi, “ninaweka tumaini langu ndani yake.”11 Alma alielewa kwamba kwa kukumbuka ukombozi kutoka utumwani na msaada wakati wa “majaribio na taabu za kila aina,” tunakuja kumjua Mungu na uhakika wa ahadi Zake.12
Wachache kati yetu wana uzoefu wa kuvutia kama wa Alma, na bado badiliko letu linaweza kuwa kubwa. Mwokozi alisihi zama za kale:
“Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu: nami nitatoa moyo wa jiwe … , nami nitawapa moyo wa nyama.
“Nami nitatia roho yangu ndani yenu. …
“… Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.”13
Mwokozi aliyefufuka aliwaambia Wanefi jinsi badiliko hili linavyoanza. Aliainisha sifa muhimu katika mpango wa Baba wa Mbinguni wakati Aliposema:
“Na Baba yangu alinituma ili nipate kuinuliwa juu kwenye msalaba; na baada ya kuinulia juu kwenye msalaba, kwamba ningeleta watu wote kwangu. …
“Na kwa sababu hii nimeinuliwa juu; kwa hivyo, kulingana na uwezo wa Baba nitawaleta watu wote kwangu.”14
Nini kinahitajika kwa wewe kuweza kuletwa kwa Mwokozi? Tafakari kujishusha kwa Yesu Kristo kwenye mapenzi ya Baba Yake, ushindi Wake dhidi ya kifo, kujichukulia juu Yake dhambi na makosa yako, upokeaji Wake wa nguvu ya Baba kufanya maombezi kwa ajili yako, ukombozi Wake mkuu kwako.15 Je, mambo haya hayatoshi kukuleta Kwake? Yanatosha kwangu mimi. Yesu Kristo “anasimama kwa mikono iliyo wazi, akitumaini na kuwa tayari kutuponya, kutusamehe, kutusafisha, kutuimarisha na kututakasa [wewe na mimi].”16
Kweli hizi zinapaswa kutupa moyo mpya na kutupa msukumo wa kuchagua kumfuata Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Lakini bado hata mioyo mipya inaweza “kuwa katika hatari ya kutangatanga, … hatari ya kumwacha Mungu ambaye [sisi] tunampenda.”17 Ili kushinda tabia hii, tunahitaji kutafakari kila siku kwenye zawadi ambazo tumepokea na kile ambacho zinahitaji. Mfalme Benjamini alishauri, “nataka mkumbuke, na kila wakati mshikilie ukumbusho, wa ukuu wa Mungu … na wema wake na subira yake kwenu nyinyi.”18 Ikiwa tutafanya hivyo, tunastahili kwa ajili ya baraka za kupendeza za kimbingu.
Kutafakari wema na rehema ya Mungu kunatusaidia kuwa wepesi zaidi kupokea kiroho. Kama matokeo, ongezeko la wepesi kuhisi kiroho linaturuhusu kupata uelewa wa ukweli wa mambo yote kwa uweza wa Roho Mtakatifu.19 Hii inajumuisha ushuhuda wa ukweli wa Kitabu cha Mormoni, kujua kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwokozi wetu binafsi na Mkombozi na kukubali kwamba injili Yake imerejeshwa katika siku hizi za mwisho.20
Tunapokumbuka ukuu wa Baba yetu wa Mbinguni na Yesu Kristo na kile Walichofanya kwa ajili yetu, hatutawachukulia Wao kwa kupuuza, kama vile ambavyo Tom hakupuuzia moyo wa Jonathan. Katika njia ya furaha na unyenyekevu, Tom alikumbuka kila siku tukio baya lililomletea ongezeko la maisha. Katika shangwe ya kujua kwamba tunaweza kuokolewa na kuinuliwa, tunahitaji kukumbuka kwamba wokovu na kuinuliwa vinakuja kwa gharama kubwa.21 Tunaweza kwa unyenyekevu kuwa na shangwe pale tunapotambua kwamba bila Yesu Kristo, tunaangamizwa, lakini tukiwa Naye, tunaweza kupokea zawadi kuu ambayo Baba wa Mbinguni anaweza kutoa.22 Hakika, unyenyekevu huu unaturuhusu kufurahia ahadi “ya uzima wa milele katika ulimwengu huu” na hatimaye kupokea “uzima wa milele … hata utukufu katika mwili usiokufa” katika ulimwengu ujao.23
Tunapotafakari wema wa Baba yetu wa Mbinguni na Yesu Kristo, uaminifu wetu Kwao unaongezeka. Sala zetu zinabadilika kwa sababu tunajua Mungu ni Baba yetu na sisi tu watoto Wake. Tunatafuta si kubadili mapenzi yake bali kufunganisha mapenzi yetu na Yake na kujihakikishia sisi wenyewe baraka ambazo Yeye anataka kutoa, kwa masharti ya sisi kuziomba.24 Tunatafuta kuwa wapole zaidi, wasafi zaidi, imara zaidi, zaidi kama Kristo.25 Mabadiliko haya yanatustahilisha kwa baraka zaidi za kimbingu.
Kwa kutambua kwamba kila kitu kizuri kinatoka kwa Yesu Kristo, tutaonesha imani yetu kwa ufasaha zaidi kwa wengine.26 Tutakuwa na ujasiri wakati tunapokabiliwa na kile kinachoonekana kuwa jukumu na hali zisizowezekana.27 Tutaimarisha ari yetu ya kutunza maagano tuliyofanya ya kumfuata Mwokozi.28 Tutajazwa na upendo wa Mungu, tutataka kuwasaidia wenye mahitaji bila kuhukumu, kuwapenda watoto wetu na kuwalea katika uadilifu, kuhifadhi msamaha wa dhambi zetu na daima kufurahia.29 Haya ni matunda ya ajabu ya kukumbuka wema na rehema ya Mungu.
Kinyume chake, Mwokozi alionya, “Na katika lolote mwanadamu hamkosei Mungu, au ghadhabu ya Mungu haiwaki kwa yeyote, isipokuwa wale tu wasiokiri mkono Wake katika mambo yote.”30 Sidhani kwamba Mungu anafedheheshwa wakati tunapomsahau Yeye. Bali, ninadhani Yeye anakatishwa tamaa kwa kiasi kikubwa. Anajua kwamba tumejizuilia wenyewe fursa ya kusogea karibu Naye kwa kumkumbuka Yeye na wema Wake. Kisha tunakosa nafasi ya Yeye kusogea karibu nasi na baraka maalumu Yeye alizoahidi.31
Ninawaalika kukumbuka kila siku wema wa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo na kile Wao walichofanya kwa ajili yako. Ruhusu kutafakari kwako juu ya wema Wao kufunge imara zaidi Kwao moyo wako unaotangatanga.32 Tafakari huruma Yao, na utabarikiwa kwa ongezeko la uharaka wa kuhisi kiroho na kuwa zaidi kama Kristo. Kutafakari huruma Yao kutakusaidia “kuvumilia kwa uaminifu hadi mwisho,” hadi “upokelewe mbinguni” ili “uishi na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho.”33
Baba yetu wa Mbinguni, akimtaja Mwanaye Mpendwa, alisema, “Msikilize Yeye!”34 Unapofanyia kazi maneno hayo na kumsikiliza Yeye, kumbuka, kwa furaha na kwa unyenyekevu, kwamba Mwokozi anapenda kurejesha kile usichoweza kurejesha; Anapenda kuponya majeraha usiyoweza kuponya; Anapenda kurekebisha kile ambacho hakiwezi kurekebishika;35 Yeye anafidia yasiyo sawa yote yaliyoshurutishwa kwako;36 na Anapenda kuponya kabisa hata mioyo iliyovunjika.37
Wakati nilipofikiria juu ya zawadi kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni na kutoka kwa Yesu Kristo, nimepata kujua upendo Wao usio na mwisho na huruma Yao isiyoelezeka kwa watoto wote wa Baba wa Mbinguni.38 Ufahamu huu umenibadilisha, na utakubadilisha pia. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.