Mkutano Mkuu
Mpango Mkuu
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


2:3

Mpango Mkuu

Sisi ambao tunaujua mpango wa Mungu na ambao tumefanya agano kuushiriki tuna jukumu la wazi la kufundisha kweli hizi.

Hata katikati ya majaribu na changamoto za kipekee, hakika tumebarikiwa! Mkutano huu mkuu umetupatia mmiminiko wa utajiri na furaha ya Urejesho wa injili ya Yesu Kristo. Tumefurahia katika ono la Baba na Mwana ambalo lilianzisha Urejesho. Tumekumbushwa juu ya ujio wa kimuujiza wa Kitabu cha Mormoni, ambacho lengo lake kuu ni kushuhudia juu ya Yesu Kristo na mafundisho Yake. Tumefanywa upya kwa uhalisia wenye furaha wa ufunuo—kwa manabii na kwetu binafsi. Tumesikia shuhuda za thamani za Upatanisho usio na mwisho wa Yesu Kristo na za uhalisia wa ufufuko Wake. Na tumefunzwa kweli zingine za utimilifu wa injili Yake iliyofunuliwa kwa Joseph Smith baada ya Mungu Baba kutangaza kwa nabii huyo mpya aliyeitwa: “Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!” (Joseph Smith—Historia ya 1:17).

Tumethibitishiwa katika ufahamu wetu wa urejesho wa ukuhani na funguo zake. Tumefanywa upya katika ari yetu ya kufanya Kanisa la Bwana lililorejeshwa kujulikana kwa jina lake sahihi, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Na tumealikwa kuungana katika kufunga na kuomba ili kupunguza madhara ya sasa na ya baadaye ya maradhi ya kutisha ulimwenguni kote. Asubuhi ya leo tulipata msukumo kutoka kwa nabii wa Bwana aliye hai akiwasilisha tangazo la kihistoria la Urejesho. Tunathibitisha utangazwaji wake kwamba “wale wote ambao kwa sala wanajifunza ujumbe wa Urejesho na kutenda kwa imani watabarikiwa kupata ushahidi wao wenyewe wa utakatifu wake na wa lengo lake la kuuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili ulioahidiwa wa Bwana wetu na Mwokozi, Yesu Kristo.”1

Mpango

Yote haya ni sehemu ya mpango mtakatifu ambao lengo lake ni kuwawezesha watoto wa Mungu kuinuliwa na kuwa kama Yeye. Ukirejelewa katika maandiko kama “mpango mkuu wa furaha,” “mpango wa ukombozi,” na “mpango wa wokovu” (Alma 42:8, 11, 5), mpango huo—uliofunuliwa katika Urejesho—ulianza na Baraza Mbinguni. Kama roho, tulitamani kupata maisha ya milele yaliyofurahiwa na wazazi wetu wa mbinguni. Wakati huo tulikuwa tumeendelea kadiri tulivyoweza bila uzoefu wa maisha ya duniani katika mwili wa nyama. Ili kutupa uzoefu huo, Mungu Baba alipanga kuumba dunia hii. Katika maisha ya duniani yaliyopangwa, tungechafuliwa na dhambi pale tunapokabiliana na upinzani muhimu kwa ajili ya ukuaji wetu kiroho. Pia tungekuwa chini ya kifo cha kimwili. Ili kutuokoa kutokana na kifo na dhambi, mpango wa Baba yetu wa Mbinguni ungemtoa Mwokozi. Ufufuko Wake ungewakomboa wote kutokana na kifo, na dhabihu Yake ya upatanisho ingelipa gharama inayohitajika kwa wote kusafishwa kutokana na dhambi kwa masharti yaliyoamriwa ili kuchochea ukuaji wetu. Upatanisho huu wa Yesu Kristo ni kiini cha mpango wa Baba.

Katika Baraza Mbinguni, watoto wote wa kiroho wa Mungu walitambulishwa kwenye mpango wa Baba, ikiwa ni pamoja na matokeo yake na majaribu ya duniani, usaidizi wake wa kimbingu, na takdiri yake tukufu. Tuliona mwisho kutokea mwanzo. Idadi yote ya viumbe waliowahi kuzaliwa hapa duniani walichagua mpango wa Baba na kuupigania katika pambano la kimbingu lililofuatia. Wengi pia walifanya maagano na Baba Kuhusu kile ambacho wangefanya hapa duniani. Katika njia ambazo bado hazijafunuliwa, matendo yetu katika ulimwengu wa roho yameshawishi hali zetu katika maisha ya duniani.

Maisha ya duniani na Ulimwengu wa Roho

Sasa nitafupisha baadhi ya vipengele vya msingi vya mpango wa Baba jinsi vinavyotuathiri wakati wa safari zetu za maisha ya duniani na katika ulimwengu wa roho unaofuatia.

Lengo la maisha ya duniani na ukuaji wa baada ya maisha hayo ambao unaweza kufuatia ni kwa ajili ya watoto wa Mungu kuwa kama Yeye alivyo. Hili ni tamanio la Baba wa Mbinguni kwa watoto Wake wote. Ili kufikia takdiri hii ya furaha, sheria za milele zinahitaji kwamba tuwe viumbe waliotakaswa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo ili tuweze kuishi katika uwepo wa Baba na Mwana na kufurahia baraka za kuinuliwa. Kama Kitabu cha Mormoni kinavyofundisha, Anawakaribisha “wote kuja kwake na kupokea wema wake; na hamkatazi yeyote anayemjia, weusi kwa weupe, wafungwa na walio huru, wake kwa waume; na anawakumbuka kafiri; na wote ni sawa kwa Mungu” (2 Nefi 26:33; ona pia Alma 5:49).

Mpango mtakatifu kwa ajili yetu kuwa kile tulichokusudiwa kuwa unatuhitaji sisi kufanya chaguzi za kukataa upinzani mwovu ambao unawashawishi binadamu kutenda kinyume na amri za Mungu na mpango Wake. Unahitaji pia kwamba tuwe chini ya upinzani wa binadamu wengine, kama vile kutokana na dhambi za wengine au kutokana na kasoro za kuzaliwa. Wakati mwingine ukuaji wetu unaohitajika unafikiwa vizuri zaidi kwa mateso na majaribu kuliko kwa faraja na utulivu. Na hakuna upinzani huu wowote wa duniani ungeweza kufikia lengo lake la milele ikiwa uingiliaji kati mtakatifu ungetupa faraja kutokana na matokeo yote mabaya ya maisha ya duniani.

Mpango unafunua takdiri yetu katika umilele, lengo na hali za safari yetu katika maisha ya duniani, na usaidizi wa kimbingu tutakaopokea. Amri za Mungu zinatuonya dhidi ya kutangatanga kwenye hali za hatari. Mafundisho ya viongozi wenye mwongozo wa kiungu huongoza njia yetu na kutoa hakikisho ambalo linasaidia safari yetu ya milele.

Mpango wa Mungu hutupatia mahakikisho makuu manne ili kusaidia safari yetu kupita maisha ya duniani. Yote yametolewa kwetu kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo, ambao ni kiini cha mpango. La kwanza unatuhakikishia kwamba kupitia mateso Yake kwa ajili ya dhambi ambazo tunatubu, tunaweza kusafishwa kuondokana na dhambi hizo. Kisha hakimu wa mwisho mwenye rehema “hatazikumbuka tena” (Mafundisho na Maagano 58:42).

Pili, kama sehemu ya Upatanisho wa Mwokozi wetu, Yeye alijichukulia juu Yake unyonge wa wanadamu wengine wote. Hii inatusaidia kupokea usaidizi mtakatifu na nguvu za kustahimili mizigo isiyoepukika ya maisha, ya binafsi na ya jumla, kama vile vita na tauni. Kitabu cha Mormoni kinatoa maelezo yetu yaliyo wazi ya kimaandiko juu ya nguvu hii muhimu ya Upatanisho. Mwokozi alijichukulia “maumivu na magonjwa [na unyonge] wa watu wake. … Atajichukulia unyonge wao, ili moyo wake ujae rehema, kulingana na mwili, ili ajue kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao” (Alma 7:11–12).

Tatu, Mwokozi, kupitia Upatanisho Wake usio na mwisho, anatangua ukomo wa kifo na kutupatia hakikisho lenye furaha kwamba sisi sote tutafufuka. Kitabu cha Mormoni kinafundisha, “Huu urejesho utakuwa kwa wote, wote wazee na vijana, wote wafungwa na huru, waume na wake, wote waovu na wenye haki; na hakuna hata unywele wa vichwa vyao utakaopotea; lakini kila kitu kitarejeshwa mahali pake kamili” (Alma 11:44).

Tunasherehekea uhalisia wa Ufufuko mnamo msimu huu wa Pasaka. Hii inatupa mtazamo na nguvu za kuvumilia changamoto za maisha zinazompata kila mmoja wetu na wale tunaowapenda, mambo kama vile kasoro za kimwili, kiakili au kihisia tunazopata wakati wa kuzaliwa au tunazopitia wakati wa maisha yetu ya duniani. Kwa sababu ya Ufufuko, tunajua kwamba kasoro hizi za maisha haya ni za muda tu!

Injili ya urejesho inatuhakikishia kwamba Ufufuko unaweza kujumuisha fursa ya kuwa na wanafamilia wetu—mume, mke, watoto na wazazi. Hii ni motisha yenye nguvu kwa ajili yetu kutimiza majukumu ya familia yetu katika maisha ya duniani. Inatusaidia kuishi pamoja katika upendo kwenye maisha haya kwa matarajio ya muunganiko na mahusiano ya furaha kwenye maisha ya baadaye.

Nne na mwisho, ufunuo wa siku za leo unatufundisha kwamba maendeleo yetu hayahitaji kuwa na mwisho kwenye maisha ya duniani. Machache tu yamefunuliwa kuhusu hakikisho hili muhimu. Tunaambiwa kwamba maisha haya ndiyo wakati wa kujitayarisha kukutana na Mungu na kwamba tusiahirishe toba yetu (ona Alma 34:32–33). Bado, tunafundishwa kwamba katika ulimwengu wa roho injili inahubiriwa hata kwa “waovu na wasiokuwa watiifu ambao waliukataa ukweli” (Mafundisho na Maagano 138:29) na kwamba wale waliofundishwa huko wana uwezekano wa kutubu kabla ya Hukumu ya Mwisho (ona mistari 31–34, 57–59).

Hapa ni baadhi ya misingi mingine ya mpango wa Baba yetu wa Mbinguni.

Injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo inatupa mtazamo wa kipekee juu ya mada za ubikira, ndoa na kuzaa watoto. Inafundisha kwamba ndoa kulingana na mpango wa Mungu ni muhimu kwa ajili ya kukamilisha lengo la mpango wa Mungu, kutoa mpangilio mtakatifu uliochaguliwa kwa ajili ya kuzaliwa mwanadamu, na kuwaandaa wanafamilia kwa uzima wa milele. “Ndoa imeamriwa na Mungu kwa mwanadamu,” Bwana alisema, “… kwamba dunia iweze kutimiza hatma ya uumbwaji wake” (Mafundisho na Maagano 49:15–16). Katika hili, mpango Wake, ndiyo, huenda kinyume na baadhi ya nguvu imara za kidunia katika sheria na mila.

Uwezo wa kuumba maisha ni uwezo wa kutukuka ambao Mungu amewapa watoto Wake. Matumizi yake yaliagizwa katika amri ya kwanza kwa Adamu na Eva, lakini amri nyingine muhimu ilitolewa ili kukataza matumizi yake mabaya. Nje ya mahusiano ya ndoa, matumizi yoyote ya uwezo wa kuzaa katika hatua moja au nyingine ni dhambi ya kushusha hadhi na upotovu wa sifa kuu ya kiungu ya wanaume na wanawake. Mkazo ambao injili ya urejesho inaweka kwenye sheria ya ubikira ni kwa sababu ya lengo la uwezo wetu wa kuzaa katika kukamilisha mpango wa Mungu.

Nini Kinafuata?

Wakati wa kumbukumbu hii ya miaka 200 ya Ono la Kwanza, ambalo lilianzisha Urejesho, tunaujua mpango wa Mungu na tunatiwa moyo na karne mbili za baraka zake kupitia Kanisa Lake lililorejeshwa. Katika mwaka huu wa 2020, tuna kile wataalamu wa afya wanachokiita ono la 20/20 kwa ajili ya matukio yaliyopita.

Tunapotazama wakati ujao, hata hivyo, ono letu lina uhakika kidogo tu. Tunajua kwamba karne mbili baada ya Urejesho, ulimwengu wa roho sasa una wingi wa wafanyakazi wenye uzoefu wa kukamilisha kuhubiri ambako kunafanyika huko. Pia tunajua kwamba sasa tunayo mahekalu mengi ya kufanyia ibada za milele kwa wale wanaotubu na kuikumbatia injili ya Bwana upande wowote wa pazia la kifo. Yote haya yanaendeleza mpango wa Baba yetu wa Mbinguni. Upendo wa Mungu ni mkuu kiasi kwamba, isipokuwa kwa wachache ambao kwa makusudi wanakuwa wana wa upotevu, Ametayarisha takdiri ya utukufu kwa ajili ya watoto Wake wote (ona Mafundisho na Maagano 76:43).

Tunajua kwamba Mwokozi atarudi na kwamba kutakuwa na milenia ya utawala wa amani ili kukamilisha sehemu ya maisha ya duniani ya mpango wa Mungu. Pia tunajua kwamba kutakuwa na ufufuko tofauti, wa wenye haki na wasio haki, kwa hukumu ya mwisho ya kila mtu daima ikifuatia ufufuko wake.

Tutahukumiwa kulingana na matendo yetu, matamanio ya mioyo yetu, na aina ya mtu tuliyekuwa. Hukumu hii itasababisha watoto wote wa Mungu kuendelea kwenye ufalme wa utukufu ambao kwa ufalme huo utiifu wao umewastahilisha na ambapo watajisikia vizuri. Hakimu wa yote haya ni Mwokozi wetu, Yesu Kristo (ona Yohana 5:22; 2 Nefi 9:41). Uelewa wake mkuu unampatia Yeye ufahamu mkamilifu wa matendo na matamanio yetu yote, yale ambayo hayakufanyiwa toba au hayakubadilishwa na yale yaliyofanyiwa toba au ya haki. Kwa hiyo, baada ya hukumu Yake sote tutakiri “kwamba hukumu zake ni za haki” (Mosia 16:1).

Katika kuhitimisha, ninashiriki msimamo ambao nimeupata katika barua nyingi na kwa kurejea maombi mengi ya kurudi Kanisani baada ya jina kuondolewa au ukengeufu. Wengi wa waumini wetu hawaelewi mpango huu wa wokovu, ambao unajibu maswali mengi kuhusu injili na sera zenye mwongozo wa kiungu za Kanisa lililorejeshwa. Sisi ambao tunaujua mpango wa Mungu na ambao tumefanya agano kuushiriki, tuna jukumu la wazi la kufundisha kweli hizi na kufanya yote tuwezayo kuzifikisha kwa wengine na katika hali zetu wenyewe katika maisha ya duniani. Ninashuhudia juu ya Yesu Kristo, Mwokozi na Mkombozi wetu, ambaye anafanya yote yawezekane, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. “Urejesho wa Utimilifu wa Injili ya Yesu Kristo: Tangazo la Miaka Mia Mbili kwa Ulimwengu,” katika Russell M. Nelson, “Msikilize Yeye,” Liahona, Mei 2020, 91.