Kutimizwa kwa Unabii
Unabii ambao umekwisha kutimia kwa Urejesho wa utimilifu wa injili ya Yesu Kristo ni mwingi.
Wapendwa kaka zangu na dada zangu, nimeheshimiwa kuongea nanyi katika mkutano mkuu huu wa kihistoria tunapoadhimisha siku ya kukumbuka Ono la Kwanza la Joseph Smith la kumwona Mungu Baba na Mwanaye Yesu Kristo, mahali ambapo, pasi na swali, ni Kijisitu Kitakatifu. Ono lile lilikuwa ni mwanzo mtukufu wa Urejesho wa injli na vingine vyote vilivyofunuliwa, kuanzia Kitabu cha Mormoni hadi kurudishwa kwa mamlaka na funguo za ukuhani, kuanzishwa kwa Kanisa la kweli la Bwana, mahekalu ya Mungu, na manabii na mitume ambao huongoza kazi katika siku hizi za mwisho.
Kwa kusudi takatifu, manabii wa kale wa Mungu, wakiwa wameongozwa na Roho Mtakatifu, walitoa unabii wa Urejesho na kile ambacho kingekuja katika siku yetu, kipindi cha mwisho cha maongozi ya Mungu na utimilifu wa nyakati. Kazi hii hasa “iliipa msukumo mioyo” ya waonaji wa mwanzo.1 Kwa vizazi vya nyakati zote, walitabiri, waliota ndoto, waliona maono, na kutoa unabii juu ya siku zijazo za ufalme wa Mungu duniani, ambao Isaya aliuita “kazi ya ajabu na muujiza.”2
Unabii ambao umekwisha kutimizwa kwa Urejesho wa utimilifu wa injili ya Yesu Kristo, ikijumuisha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ni mwingi. Leo, hata hivyo, nitagusia mchache niupendao. Unabii huu nilifundishwa na mwalimu wangu wa darasa la Msingi na magotini mwa malaika mama yangu.
Danieli, yule aliyewashindisha njaa simba kwa imani yake katika Bwana Yesu Kristo na sala ya kuomba malaika wa Mungu wa kumtumikia, ni mmoja wa watu walioiona siku yetu katika ono. Akitafsiri ndoto kwa ajili ya Mfalme Nebkadreza wa Babilonia, Danieli alitoa unabii kuwa Kanisa la Bwana litaibuka katika siku za mwisho kama jiwe dogo “lilichongwa mlimani bila kazi ya mikono.”3 “Bila kazi ya mikono,” ikimaanisha kwa mbingu kuingilia, Kanisa la Bwana lingeongezeka katika ukubwa hadi limeijaza dunia yote “kamwe [lisiangamizwe] … [bali] lisimame milele.”4
Ni ushahidi wa maana sana kwamba maneno ya Danieli yanatimizwa pale waumini wa Kanisa, kutoka ulimwenguni kote, wanapotazama na kusikiliza mkutano huu leo.
Petro Mtume mwaminifu alielezea “zamani za kufanywa upya vitu vyote … tokea mwanzo wa ulimwengu.”5 Mtume Paulo aliandika kwamba katika utimilifu wa nyakati, Mungu “atavijumlisha … vitu vyote katika Kristo,”6 “Yesu Kristo mwenyewe akiwa jiwe kuu la pembeni.”7 Niliuhisi unabii huo kwa nguvu sana wakati niliposhiriki katika uwekaji wakfu wa Hekalu la Roma Italia. Manabii na mitume wote walikuwa pale wakitoa ushuhuda juu ya Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu, kama walivyofanya Petro na Paulo. Kanisa ni mfano ulio hai wa kufanywa upya, akina kaka na akina dada, na waumini wetu ni mashahidi wa unabii huo mtukufu wa kale.
Yusufu wa Misri alitoa unabii kwamba katika siku za mwisho: “Bwana Mungu wangu atamwinua mwonaji, ambaye atakuwa mwonaji bora kwa uzao wa viuno vyangu.”8 “Kwani atafanya kazi ya [Bwana].”9 Joseph Smith, nabii wa Urejesho, alikuwa ndiye huyo mwonaji.
Yohana Mfunuzi alitoa unabii juu ya malaika wa Mwenyezi Mungu akileta pamoja vipengele muhimu kwa ajili ya Urejesho kwa maneno haya: “Kisha nikaona malaika mwingine akiruka katikati ya mbingu, mwenye injili ya milele awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa, na kabila na lugha, na jamaa.”10 Moroni alikuwa ndiye huyo malaika. Yeye aliiona siku yetu kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Mormoni. Katika kujitokeza kulikojirudia, yeye alimwandaa Joseph Smith kwa ajili ya huduma yake, ikijumuisha kutafsiri Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo.
Manabii wengine walitabiri juu ya siku yetu. Malaki aliongelea juu ya Eliya kuigeuza “mioyo ya baba iwaelekee watoto, na ya watoto iwaelekee baba zao.”11 Eliya amekuja, na kama matokeo yake, leo tunayo mahekalu 168 yanayofanya kazi yaliyotapakaa duniani. Kila hekalu limejaa waumini wenye kustahili wakifanya maagano matakatifu na kupokea baraka takatifu za ibada kwa ajili yao wenyewe na mababu zao waliofariki dunia. Kazi hii takatifu iliyoelezwa na Malaki ni “kitovu cha mpango wa Muumbaji kwa ajili ya hatima ya milele ya watoto Wake.”12
Sisi tunaisha katika kipindi hicho kilichotolewa unabii; sisi ni watu tuliopewa jukumu la kuashiria kuingia kwa Ujio wa Pili wa Yesu Kristo; sisi tutawakusanya watoto wa Mungu, wale ambao watasikia na kukumbatia kweli, maagano, na ahadi za injili isiyo na mwisho. Rais Nelson anaiita changamoto “kubwa, kusudi kubwa, na kazi kubwa zaidi duniani leo.”13 Juu ya muujiza huu ninatoa ushahidi wangu.
Kwa uteuzi wa Rais Russell M. Nelson, mnamo Februari mwaka huu, nililiweka wakfu Hekalu la Durban Afrika Kusini. Ilikuwa ni siku ambayo nitaikumbuka maisha yangu yote. Nilikuwa na waumini ambao wamekuja kwenye injili kama Yeremia alivyotoa unabii hapo zamani—“mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja.”14 Mafundisho ya Yesu Kristo yanatuunganisha sisi sote—ulimwenguni kote—kama wana na mabinti wa Mungu, kama akina kaka na akina dada katika injili. Bila kujali tunaonekanaje au tunavaaje, sisi ni watu wamoja na Baba yetu yu Mbinguni ambaye mpango wake kutoka mwanzo ulikuwa na uko kwa ajili ya familia Yake kuunganishwa tena kwa kufanya na kushika maagano matakatifu ya hekaluni.
Kwa lile kusanyiko dogo la watu wenye ukuhani katika darasa pale Kirtland, Ohio, mwaka 1834, Nabii Joseph alitoa unabii, “Ni kikundi kidogo tu cha Ukuhani mnakiona hapa usiku huu, lakini Kanisa hili litaijaza Amerika Kaskazini na Kusini—litaujaza ulimwengu.”15
Miaka ya hivi karibuni nimetembea ulimwenguni kote ili kukutana na waumini wa Kanisa. Ndugu zangu wa Akidi ya Kumi na Wawili wamekuwa na majukumu yanayofanana na haya. Bado, ni nani anayeweza kufikia ratiba ya mpendwa wetu nabii, Rais Nelson, ambaye safari zake katika miaka miwili ya mwanzo kama Rais wa Kanisa zimempeleka kukutana na Watakatifu katika nchi 32 na majimbo ya Marekani16 ili kumshuhudia Kristo aliye hai.
Ninakumbuka wakati nilipopokea wito wangu wa umisionari kama kijana. Nilitaka kutumikia Ujerumani, kama baba yangu, kaka, na shemeji yangu. Bila kusubiri watu warejee nyumbani, nilikimbia kwenye sanduku la barua na nikafungua wito ule. Nilisoma kwamba nilikuwa nimeitwa kwenda katika Misheni ya Eastern States, iliyokuwa na makao makuu yake kule New York City. Nilivunjika moyo, hivyo nilikwenda ndani na kufungua maandiko yangu ili kupata faraja. Nilianza kwa kusoma katika Mafundisho na Maagano: “Tazama, na lo, ninao watu wengi katika eneo hili, katika maeneo ya jirani; na mlango wenye kuleta matokeo yanayotakiwa wakufaa utafunguliwa katika maeneo ya jirani katika nchi za mashariki.”17 Unabii huo, uliotolewa kwa Nabii Joseph Smith mwaka 1833, ulikuwa ni ufunuo kwangu mimi. Nilijua wakati huo nilikuwa nimeitwa kwenye misheni sahihi Bwana anayotaka mimi nikatumikie. Nilifundisha Urejesho na mwanzo wake wa kuvutia wakati Baba yetu wa Mbinguni aliposema na Joseph Smith na kumwambia, “Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!”18
Wa kipekee kwa Kanisa zima ni unabii wa Isaya, uliotolewa zaidi ya miaka 700 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo: “Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, … na mataifa yote watauendea.”19
Akilini mwangu leo, napiga taswira ya mamilioni ya waumini na marafiki zetu waliounganishwa katika jambo hili kielekroniki kwa njia ya televisheni, intaneti, au njia nyinginezo. Tumekaa chini kana kwamba tuko pamoja “juu ya vilima.”20 Ilikuwa ni Brigham Young aliyesema maneno ya kinabii “Hapa ni mahali sahihi.”21 Watakatifu hawa, baadhi yao ni mababu zangu waanzilishi, walifanya kazi kuijenga Sayuni katika Rocky Mountains “kupitia mapenzi na matakwa yake yeye mwenye kuamuru mataifa ya dunia.”22
Nimesimama leo juu ya ardhi takatifu ambayo imewavutia mamilioni ya wageni. Mwaka 2002, Jiji la Salt Lake lilikuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi. Kwaya ya Tabenako iliimba wakati wa sherehe za ufunguzi, na Kanisa lilitoa maonesho ya muziki na programu kwa ajili ya wageni na washiriki kutoka mataifa mengi, mengi sana. Daima nitakumbuka kuliona hekalu katika mahali pa nyuma nyakati za matangazo ya usiku ya televisheni ya ulimwenguni kote.
Miaka yote, maraisi wa Marekani, wafalme, majaji, mawaziri wakuu, mabalozi, na maafisa kutoka nchi nyingi wamefika Jijini Salt Lake na kukutana na viongozi wetu. Rais Nelson alikuwa mwenyeji wa viongozi wa Association for the Advancement of Clored People, jumuiya ya Kimarekani inayokusudia kudai haki sawa pasipo ubaguzi wa rangi. Ninakumbuka kusimama bega kwa bega na marafiki na viongozi hawa wakati Rais Nelson alipoungana nao katika kudai ustaarabu na maelewano baina ya jamii ulimwenguni.23
Wengi zaidi wamekuja Temple Square na kukutana katika baraza na viongozi wa Kanisa. Kwa mfano, mwaka uliopita, kwa kuwataja wachache tu, tulikaribisha Mkutano wa 68 wa Jumuiya za Kiraia za Umoja wa Mataifa (United Nations 68th Civil Society), mkutano wa dunia nzima, na kwa mara ya kwanza wa aina yake kufanyika nje ya Jiji la New York. Tumekutana na Kamati ya Masuala ya Kidini ya Vietnam na mabalozi kutoka Cuba, Ufilipino, Argentina, Romania, Sudani, Qatar, na Saudi Arabia. Tulimkaribisha pia katibu mkuu wa Jumuiya za Kiislamu Ulimwenguni (Muslim World League).
Kile ninachokielezea hapa ni kutimia kwa unabii wa Isaya kwamba katika siku za mwisho, mataifa yatauendea “mlima wa nyumba ya Bwana.”24 Hekalu kuu la Salt Lake linasimama katikati ya unabii huo mkuu na mtukufu.
Siyo sura ya nchi ambayo huwavutia watu, ingawa pia mpangilio wetu ni mzuri; ni kiini cha dini safi kinachooneshwa katika roho, ukuaji, wema, na ukarimu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na watu wake; upendo wetu kama Mungu anavyopenda na msimamo wetu kwa ajili ya kusudi kubwa zaidi, kile Joseph Smith alichokiita, “kusudi la Kristo.”25
Hatujui lini Kristo atarudi, lakini hili tunalijua. Lazima tujiandae moyoni na akilini, tuwe wenye kustahili kumpokea Yeye, na kuheshimiwa kuwa sehemu ya vyote ambavyo vilitolewa unabii zamani.
Ninashuhudia kuwa Rais Russell M. Nelson ni nabii wa Bwana duniani, na pembeni yake ni Mitume waliotwa na Mungu, kukubaliwa kama manabii, waonaji, na wafunuzi. Na, wapendwa kaka zangu na dada zangu, Urejesho unaendelea.
Ninafunga kwa unabii wa Joseph Smith, maneno ambayo nayashuhudia kuwa kweli: “Hakuna mkono mchafu unaweza kuisimamisha kazi isiendelee; adha inaweza kuongezeka, makundi yaweza kujikusanya, majeshi yaweza kusimama, uzushi unaweza kukashifu, lakini ukweli wa Mungu utasonga mbele kwa ujasiri, kiungwana, na kwa uhuru, hadi umepenya kila bara, kutembelea kila tabia, umefagia kila nchi, na kusikika katika kila sikio, hadi pale malengo ya Mungu yatakapokamilika, na Yehova Mkuu atakaposema kazi imekwisha.”26 Ninashuhudia kwamba unabii huu wa Joseph Smith unatimia.
Ninaahidi unapofuata ushauri wenye mwongozo wa kiungu wa mpendwa nabii wetu, Rais Russell M. Nelson, washauri wake, Mitume, na viongozi wengine wa Kanisa, na unapowasikiliza manabii wa kale ambao walitabiri juu ya siku yetu, utajazwa, kwa kina moyoni na rohoni mwako, kwa roho na kazi ya Urejesho. Ninaahidi utauona mkono wa Mungu katika maisha yako, utasikia ushawishi Wake, na kuhisi upendo Wake. Katika jina la Yesu Kristo, pamoja na shukrani kwa ajili ya Urejesho wa injili Yake na Kanisa Lake, kama ushahidi wa upendo Wake usio na mfano, amina.