Ushuhuda Hai juu ya Kristo Aliye Hai
Ujumbe wa msingi wa Kitabu cha Mormoni ni kurejesha ufahamu sahihi wa kazi muhimu ya Yesu Kristo katika kuokoa na kuinuliwa kwa mwanadamu.
Siku ya jua ya majira ya kuchipua mnamo 2017, sherehe ya ufunguzi wa Hekalu la Paris ilikuwa ikiendelea vizuri wakati mwongozaji wageni mmoja aliposogelewa na mtu mmoja mwenye uso wenye huzuni. Alisema aliishi karibu na hekalu na alikiri kuwa alikuwa mpingaji mzuri wa ujenzi wake. Alisimulia kwamba siku moja alipokuwa akitazama kupitia dirisha la nyumba yake, aliona winchi ikishusha sanamu ya Yesu kutoka mawinguni na taratibu ikiiweka katika eneo la hekalu. Mtu yule alisema kwamba uzoefu huu ulibadilisha kabisa hisia zake juu ya Kanisa letu. Alitambua tulikuwa wafuasi wa Yesu Kristo na aliomba msamaha wetu kutokana na madhara ambayo alikuwa ameyasababisha kabla.
Sanamu ya Christus, ambayo hupendezesha eneo la Hekalu la Paris na majengo mengine ya Kanisa, hushuhudia upendo wetu kwa Mwokozi. Sanamu ya marumaru halisi ni kazi ya msanii wa kidenishi Bertel Thorvaldsen, ambaye aliichonga mnamo 1820—mwaka sawa na wa Ono la Kwanza. Sanamu inasimama katika utofauti wa kipekee na kazi za kisanii za wakati huo, ambayo kwa upana huelezea mateso ya Kristo msalabani. Kazi ya Thorvaldsen humuelezea Kristo aliye hai, ambaye alipata ushindi juu ya kifo, na kwa mikono iliyo wazi, huwaalika wote kuja Kwake. Makovu pekee ya misumari mikononi Mwake na miguuni na jeraha ubavuni Mwake hushuhudia mateso yasiyoelezeka Aliyoyavumilia ili kuwaokoa wanadamu wote.
Pengine sababu moja ya sisi kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kuipenda sanamu hii ni kwamba inatukumbusha maelezo yaliyotolewa katika Kitabu cha Mormoni ya Mwokozi kutembelea bara la Amerika:
“Na tazama, walimwona Mtu akiteremka kutoka mbinguni; na alikuwa amevaa joho refu leupe; na akaja chini na kusimama katikati yao; …
“Na ikawa kwamba alinyosha mkono wake mbele na kuzungumza kwa watu, akisema:
“Tazama, mimi ni Yesu Kristo, …
“… Na nimekunywa kutoka kwa kikombe kichungu ambacho Baba amenipatia, na nimemtukuza Baba kwa kujivika dhambi za ulimwengu.”1
Kisha aliwaalika kila mwanaume, mwanamke, na mtoto kuja mbele na kusukuma mikono yao ubavuni mwake, na kuhisi alama za misumari katika mikono Yake na katika miguu Yake; na hivyo walishuhudia wenyewe kwamba ni Yeye ambaye alikuwa Mesia aliyesubiriwa.2
Tukio hili kuu ni kilele cha Kitabu cha Mormoni. Habari “yote njema” ya injili inabebwa kwenye taswira hii ya Mwokozi kwa huruma akinyoosha “mikono Yake ya rehema”3 kumualika kila mtu kuja Kwake na kupokea baraka za Upatanisho Wake.
Ujumbe wa msingi wa Kitabu cha Mormoni ni kurejesha ufahamu sahihi wa kazi muhimu ya Yesu Kristo katika kuokoa na kuinuliwa kwa mwanadamu. Dhima hii inavumishwa kutoka ukurasa wa dibaji mpaka kwenye maneno ya mwisho kabisa ya mlango wa mwisho. Kwa karne nyingi za ukengeufu na mkanganyiko wa kiroho, maana kuu ya kile Mwokozi alichokifanya huko Gethsemane na Golgotha ilipotea na kuharibika. Ilikuwa ni furaha iliyoje ambayo Joseph Smith lazima aliihisi wakati, alipokuwa akitafsiri 1 Nefi, aligundua ahadi hii ya kustaajabisha: “Haya maandishi ya mwisho [Kitabu cha Mormoni] … yatathibitisha juu ya kweli kwa yale ya kwanza [Biblia] … na yatafahamisha vitu vilivyo wazi na vyenye thamani viliyotolewa kutoka kwao; na yatafahamisha makabila yote, lugha zote, na watu wote, kwamba Mwanakondoo wa Mungu ndiye Mwana wa Baba wa Milele, na Mwokozi wa ulimwengu; na kwamba lazima watu wote wamkubali yeye, kama sio hivyo, hawawezi kuokolewa.”4
Kweli za wazi na za thamani kuhusu Upatanisho wa Mwokozi zinarudiwa kote kwenye Kitabu cha Mormoni. Wakati nikiorodhesha baadhi ya kweli hizi, ninakualika kutafakari jinsi zilivyobadili au ambavyo zingebadili maisha yako.
-
Upatanisho wa Yesu Kristo ni zawadi ya bure iliyotolewa kwa wote ambao wameishi, ambao sasa wanaishi, na ambao wataishi duniani.5
-
Kwa kuongezea kwenye kubeba mzigo wa dhambi zetu, Kristo alijichukulia mwenyewe huzuni zetu, unyonge, maumivu, magonjwa na magumu yote yaliyoko kwenye hali ya maisha ya kufa ya mwanadamu. Hakuna uchungu, maumivu, au huzuni ambao Yeye hakuupitia kwa ajili yetu.6
-
Dhabihu ya upatanisho ya Mwokozi huturuhusu kushinda matokeo hasi ya anguko la Adamu, ikijumuisha kifo cha kimwili. Kwa sababu ya Kristo, watoto wote wa Mungu wanaozaliwa duniani, bila kujali utakatifu wao, watapata kuunganishwa roho zao na miili kupitia nguvu ya Ufufuo7 na kurudi kwake Yeye “kuhukumiwa … kulingana na kazi [zao].”8
-
Kwa upande mwingine, kupokea baraka zote za Upatanisho wa Mwokozi ni kwa masharti katika bidii yetu9 katika kuishi “mafundisho ya Kristo.”10 Katika ono lake, Lehi aliona “njia nyembamba na iliyosonga”11 iendayo kwenye mti wa uzima. Tunda lake, ambalo huwakilisha upendo wa Mungu kama unavyoelezewa kupitia wingi wa baraka za Upatanisho wa Kristo, “ni lenye thamani na bora zaidi … [na] ni karama kuu zaidi ya karama zote za Mungu.”12 Ili kuweza kulipata tunda hili, lazima tutumie imani katika Yesu Kristo, tutubu, “tusikilize neno la Mungu,”13 tupokee ibada muhimu, na kushika maagano matakatifu mpaka mwisho wa maisha yetu.14
-
Kupitia Upatanisho Wake, Yesu Kristo si tu huosha dhambi zetu, lakini pia hutoa nguvu wezeshi ambayo kwayo wafuasi Wake wanaweza “[kuuvua] utu wa asili,”15 kuendelea “mstari juu ya mstari,”16 na kuongezeka katika utakatifu17 ili kwamba siku moja wangeweza kuwa viumbe wakamilifu katika mfano wa Kristo,18 wakiwa wastahiki kuishi tena na Mungu19 na kurithi baraka zote za ufalme wa mbinguni.20
Ukweli mwingine wa kufariji uliopo kwenye Kitabu cha Mormoni ni kwamba, japokuwa hauna mwisho na ni wa ulimwengu wote, Upatanisho wa Bwana ni zawadi binafsi ya kustaajabisha na ya upendo, ikimfaa kila mmoja wetu binafsi.21 Kama vile Yesu alivyowaalika kila mmoja wa wafuasi Wanefi kuhisi makovu Yake, Yeye alikufa kwa ajili ya kila mmoja wetu, binafsi, kana kwamba wewe au mimi tulikuwa ni mtu pekee duniani. Anatoa kwetu sisi mwaliko binafsi wa kuja Kwake na kupata baraka za kustaajabisha za Upatanisho Wake.22
Asili binafsi ya Upatanisho wa Kristo huwa zaidi halisi wakati tunapofikiria mifano ya wanaume na wanawake wa kustaajabisha katika Kitabu cha Mormoni. Baadhi yao ni Enoshi, Alma, Zeezromu, mfalme Lamoni na mke wake, na watu wa mfalme Benjamini. Hadithi zao za uongofu na shuhuda thabiti hutoa ushahidi hai wa jinsi mioyo na maisha yetu vinavyoweza kubadilishwa kupitia fadhila na rehema ya Bwana isiyo na mwisho.23
Nabii Alma aliwauliza watu wake swali hili la kupenya moyo. Alisema, “Ikiwa mmepata mabadiliko ya moyo, na ikiwa mmesikia kuimba wimbo wa upendo wa ukombozi, ningeuliza, mnaweza kuhisi hivyo sasa?”24 Swali hili ni muhimu hivi leo, kwa sababu kama wafuasi wa Bwana, nguvu yake ya ukombozi lazima iwe nasi, ituhamasishe, na kutubadili kila mmoja wetu na kila siku.
Swali la Alma lingeweza pia kurekebishwa kuuliza: Je, ni lini ilikuwa mara ya mwisho ulipohisi ushawishi mzuri wa Upatanisho wa Mwokozi maishani mwako? Hii hutokea wakati unapohisi shangwe “nzuri na tamu”25 inayokuja kwako ambayo hutoa ushuhuda kwenye nafsi yako kwamba dhambi zako zimesamehewa; au wakati majaribu makali ghafla yanapokuwa mepesi kubeba; au wakati moyo wako unapolainishwa na unaweza kutoa msamaha kwa mtu ambaye amekuumiza. Au inaweza kuwa kila mara unapoweza kujua uwezo wako wa kupenda na kutumikia wengine umeongezeka, au kwamba mchakato wa utakasaji unakufanya kuwa mtu tofauti, kukuweka katika mfano wa Kristo.26
Ninatoa ushahidi kwamba uzoefu huu wote ni halisi na ni ushahidi kwamba maisha yanaweza kubadilishwa kupitia imani katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Kitabu cha Mormoni kinaelezea kinagaubaga na kupanua uelewa wetu wa zawadi hii ya kiungu. Unaposoma kitabu hiki, utahisi sauti ya Kristo aliye hai akikualika kuja Kwake. Ninaahidhi kwamba ikiwa utakubali mwaliko huu na kuweka maisha yako kufuata mfano Wake, ushawishi Wake okozi utakuja maishani mwako. Kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu, Mwokozi atakubadilisha siku hadi siku “hata mchana mkamilifu”27 ambapo, kama Alivyosema “Utaona uso wangu na kujua kuwa Mimi ndiye.”28 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.