Mkutano Mkuu
Jinsi Ukuhani Unavyobariki Vijana
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Jinsi Ukuhani Unavyobariki Vijana

Kupitia ukuhani, tunaweza kuinuliwa. Ukuhani huleta nuru kwenye ulimwengu wetu.

Ninashukuru kuwepo mahala hapa. Wakati mwanzo nilipojua kwamba ningepata nafasi ya kunena nanyi hivi leo, nilihisi kufurahi sana lakini wakati huo huo kunyenyekezwa sana. Nimetumia wakati mwingi nikifikiria kile ambacho ningeweza kushiriki, na ninatumaini Roho atazungumza nanyi moja kwa moja kupitia ujumbe wangu.

Kwenye Kitabu cha Mormoni, Lehi anatoa baraka kwa kila mmoja wa wanawe kabla ya kufa ambayo inawasaidia kuona nguvu zao na uwezekano wao wa milele. Mimi ndiye wa mwisho kwa watoto wanane, na mwaka huu uliopita nimekuwa mtoto pekee nyumbani kwa mara ya kwanza. Kutokuwa na ndugu na marafiki wa karibu na kutokuwa na mtu wa kuongea naye imekuwa ngumu kwangu. Kumekuwa na usiku wakati nimehisi upweke sana. Ninashukuru kwa wazazi wangu, ambao wamejaribu wawezavyo kunisaidia. Mfano wa hili ni wakati baba yangu alipojitolea kunipa baraka za ukuhani za faraja wakati hasa wa changamoto. Baada ya baraka yake, mambo hayakubadilika mara moja, lakini niliweza kuhisi amani na upendo kutoka kwa Baba yangu wa Mbinguni na kutoka kwa baba yangu. Ninahisi kubarikiwa kuwa na baba mwenye kustahili ambaye anaweza kutoa baraka za ukuhani wakati wowote ninapozihitaji na ambaye hunisaidia kuona nguvu zangu na uwezekano wangu wa milele, kama vile Lehi alivyofanya wakati alipowabariki wana wake.

Bila kujali hali yako, unaweza kila wakati kupata baraka za ukuhani. Kupitia wanafamilia, marafiki, akina kaka wanaowahudumu, viongozi wa ukuhani, na Baba wa Mbinguni ambaye hatakuacha, unaweza kupokea baraka za ukuhani. Mzee Neil L. Andersen alisema: “Baraka za ukuhani ni kubwa kuliko mtu yule anayeombwa kuhudumia kipawa hicho. … Tukiwa wenye kustahili, ibada za ukuhani zinaimarisha maisha yetu.”1

Usisite kuomba baraka upohitaji mwongozo zaidi. Ni katika nyakati zetu ngumu ndipo tunamhitaji zaidi Roho atusaidie. Hakuna aliye mkamilifu, na sote tunapata shida. Wengine wetu tunaweza kuteseka dhiki, msongo wa mawazo, uraibu, au hisia kwamba hatutoshi. Baraka za ukuhani zinaweza kutusaidia kushinda changamoto hizi na kupokea amani kadiri tunavyoendelea mbele katika siku zijazo. Natumaini kuwa tunajitahidi kuishi kwa kustahili kupokea baraka hizi.

Njia nyingine ukuhani unavyotubariki ni kupitia baraka za patriaki. Nimejifunza kugeukia baraka yangu ya patriaki kila ninapohisi huzuni au upweke. Baraka yangu hunisaidia kuona uwezekano wangu na mpango halisi ambao Mungu anao kunihusu. Inanifariji mimi na kunisaidia kuona zaidi ya mtazamo wangu wa kidunia. Inanikumbusha mimi vipawa na baraka nitakazopata ikiwa nitaishi kwa kustahili. Pia hunisaidia mimi kukumbuka na kujihisi amani kuwa Mungu atatoa majibu na kufungua milango kwa wakati unaofaa wakati ninapohitaji sana.

Baraka za patiriaka husaidia kutuandaa kurudi kuishi na Baba yetu wa Mbinguni. Ninajua baraka za patiriaka zinatoka kwa Mungu na zinaweza kutusaidia kugeuza udhaifu wetu kuwa nguvu. hizi si jumbe kutoka kwa mtabiri-bahati; baraka hizi zinatuambia kile tunachohitaji kusikia. Ni kama Liahona kwa kila mmoja wetu. Tunapomweka Mungu kwanza na kuwa na imani katika Yeye, atatuongoza kupita nyika yetu wenyewe.

Kama vile Mungu alivyombariki Joseph Smith kwa ukuhani ili baraka za injili ziweze kurejeshwa, tunaweza kupokea baraka za injili maishani mwetu kupitia ukuhani. Kila wiki tunapewa nafasi na fursa ya kupokea sakramenti. Kupitia ibada hii ya ukuhani, tunaweza kuwa na Roho kuwa nasi kila wakati, ambaye anaweza kutusafisha na kututakasa. Ikiwa unahisi hitaji la kuondoa kitu kutoka kwenye maisha yako, mfikie kiongozi anayeaminika ambaye anaweza kukusaidia kuingia kwenye njia sahihi. Viongozi wenu wanaweza kuwasaidia kupata nguvu kamili za Upatanisho wa Yesu Kristo.

Shukrani kwa ajili ya ukuhani, tunaweza pia kupokea baraka za ibada za hekalu. Tangu niweze kuingia hekaluni, nimeifanya iwe lengo na kipaumbele kuhudhuria mara kwa mara. Kwa kutenga muda na kutoa dhabihu inayohitajika ili kuwa karibu na Baba yangu wa Mbinguni katika nyumba Yake takatifu, nimebarikiwa kupokea ufunuo na misukumo ambayo imenisaidia sana katika maisha yangu yote.

Kupitia ukuhani, tunaweza kuinuliwa. Ukuhani huleta nuru kwenye ulimwengu wetu. Mzee Robert D. Hales alisema: “Bila nguvu ya ukuhani, ‘dunia yote ingeharibiwa kabisa’ (Ona M&M 2:1–3). Hapangekuwa na nuru, hakuna matumaini—giza tu.”2

Mungu anashangilia kwa ajili yetu. Anataka sisi turejee kwake. Yeye anatujua sisi binafsi. Anakujua. Anatupenda. Anatujua kila wakati na anatubariki hata wakati tunahisi hatustahili. Anajua kile tunachohitaji na wakati tunapokihitaji.

“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa:

“Kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.” (Mathayo 7:7–8).

Ikiwa bado huna ushuhuda juu ya ukuhani, ninakutia moyo usali na kuomba kujua mwenyewe juu ya nguvu yake, kisha soma maandiko ili usikie maneno ya Mungu. Ninajua kuwa ikiwa tutafanya bidii kupata nguvu ya ukuhani wa Mungu katika maisha yetu, tutabarikiwa. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Neil L. Anderson, “Power in the Priesthood,” Liahona, Nov. 2013, 92.

  2. Robert D. Hales, “Blessings of the Priesthood,” Ensign, Nov. 1995, 32.

Chapisha