Kuungana katika Kufanya Kazi ya Mungu
Njia bora zaidi ya kutimiza uwezekano wetu wa kiungu ni kufanya kazi pamoja, tukibarikiwa na nguvu na mamlaka ya ukuhani.
Dada zangu na kaka zangu wa kupendeza, ni furaha kuwa nanyi. Popote mnaposikiliza, ninatoa kumbatio kwa dada zangu na salamu ya mikono ya upendo kwa kaka zangu. Tumeungana katika kazi ya Bwana.
Tunapofikiria juu ya Adamu na Eva, mara nyingi wazo letu la kwanza ni la maisha yao ya kupendeza katika Bustani ya Edeni. Nadhani kwamba hali ya hewa ilikuwa safi kila wakati—si joto sana na si baridi sana—na kwamba matunda na mboga nyingi, tamu zilikua karibu ya ufiko wao ili waweze kula wakati wotote walipotaka. Kwa kuwa huu ulikuwa ulimwengu mpya kwao, kulikuwa na mengi ya kugundua, kwa hivyo kila siku ilikuwa ya kupendeza pale walipoingiliana na maisha ya wanyama na kutafiti mazingira yao mazuri. Pia walipewa amri za kutii na walikuwa na njia tofauti za mtazamo wa maagizo hayo, ambayo yalisababisha wasiwasi na mkanganyiko kiasi mwanzoni. 1 Lakini walipofanya maamuzi ambayo yalibadilisha maisha yao milele, walijifunza kufanya kazi pamoja na kuungana katika kufanikisha madhumuni ambayo Mungu alikuwa nayo kwao—na kwa watoto Wake wote.
Sasa watazame wanandoa hawa katika maisha ya duniani. Walilazimika kufanya kazi kwa ajili ya chakula chao, wanyama wengine waliwaona wao kama chakula, na kulikuwa na changamoto ngumu ambazo wangeweza kuzishinda kama tu wangeshauriana na kusali pamoja. Ninadhani kulikuwa na angalau baadhi ya nyakati walikuwa na maoni tofauti juu ya jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo. Walakini, kupitia Anguko, walikuwa wamejifunza kwamba ilikuwa muhimu kutenda kwa umoja na upendo. Katika mafunzo waliyopokea kutoka kwa vyanzo vya kiungu, walifundishwa mpango wa wokovu na kanuni za injili ya Yesu Kristo ambazo hufanya mpango huo uweze kufanya kazi. Kwa sababu walielewa kuwa kusudi lao la kidunia na lengo la milele vilikuwa sawa, walipata kuridhika na mafanikio katika kujifunza kufanya kazi kwa upendo na haki pamoja.
Watoto walipozaliwa kwao, Adamu na Eva walifundisha familia yao kile walichojifunza kutoka kwa wajumbe wa mbinguni. Walikuwa wamejikita katika kuwasaidia watoto wao pia kuelewa na kukumbatia kanuni hizo ambazo zingewafanya kuwa na furaha katika maisha haya, na pia kuwa tayari kurudi kwa wazazi wao wa mbinguni baada ya kuongeza uwezo wao na kudhihirisha utii wao kwa Mungu. Kwenye mchakato huo, Adamu na Eva walijifunza kuthamini nguvu zao tofauti na kusaidiana katika kazi yao muhimu ya milele. 2
Wakati karne na baadaye milenia zilipokuja na kupita, ufafanuzi wa michango yenye msukumo wa kiungu ya wanaume na wanawake na ya kutegemeana ilifunikwa kwa habari potofu na kutoelewana. Kipindi cha muda kati ya mwanzo huo wa kupendeza katika Bustani ya Edeni na sasa, adui amefanikiwa sana katika lengo lake la kuwagawa wanaume na wanawake katika jaribio lake la kuteka mioyo yetu. Lusiferi anajua kwamba ikiwa ataweza kuharibu umoja ambao wanaume na wanawake wanahisi, kama ataweza kututatiza juu ya thamani yetu ya kiungu na majukumu ya agano, atafanikiwa kuharibu familia, ambazo ni vitengo muhimu vya umilele.
Shetani huchochea ulinganifu kama zana ya kuunda hisia za kuwa mkubwa au duni, akificha ukweli wa milele kwamba tofauti za kiasili za wanaume na wanawake zimetolewa na Mungu na zina thamani sawasawa. Amejaribu kubeza michango ya wanawake kwenye familia na kwa asasi za kiraia, na hivyo kupunguza ushawishi wao kwa ajili ya wema. Kusudi lake limekuwa la kuchochea kupigania madaraka badala ya kusherehekea michango ya kipekee ya wanaume na wanawake ambayo inamkamilisha kila mmoja na kuchangia umoja.
Kwa hivyo, kwa miaka mingi na kote ulimwenguni, uelewa kamili wa kiungu wa kutegemeana na michango na majukumu tofauti ya wanawake na wanaume kwa kiasi kikubwa vimepotea. Wanawake katika jamii nyingi walipata kuwa duni kwa wanaume badala ya wenzi sawa, shughuli zao zikiwa na ukomo kwenye wigo mwembamba. Maendeleo ya kiroho yalipungua kuwa mchuruziko wakati wa nyakati hizo za giza; kwa kweli, nuru ndogo ya kiroho ingeweza kupenya akili na mioyo iliyolowekwa katika mila za kutawaliwa.
Na kisha nuru ya injili iliyorejeshwa iliangaza “juu ya mwangaza wa jua” 3 wakati Mungu Baba na Mwanaye, Yesu Kristo, walipomtokea kijana Joseph Smith mapema katika majira ya kuchipua ya mwaka 1820 katika eneo takatifu la miti huko New York. Tukio hilo lilianzisha mmiminiko wa ufunuo wa siku za leo kutoka mbinguni. Mojawapo ya mambo ya kwanza ya Kanisa la asili la Kristo kurejeshwa ilikuwa mamlaka ya ukuhani wa Mungu. Wakati Urejesho ulipoendelea kujifunua, wanaume na wanawake walianza kutambua upya umuhimu na uwezekano wa kufanya kazi kama washirika, walioidhinishwa na kuelekezwa na Yeye katika kazi hii takatifu.
Mnamo 1842, wakati wanawake wa Kanisa lililokuwa changa walipotaka kuunda kikundi rasmi kusaidia katika kazi, Rais Joseph Smith alihisi mwongozo wa kiungu kuwaandaa “chini ya ukuhani kufuatia mfano wa ukuhani.” 4 Alisema, “Sasa ninageuza ufunguo kwenu katika jina la Mungu …— Huu ni mwanzo wa siku nzuri. ” 5 Na tangu ufunguo ule ulipogeuzwa, fursa za kielimu, kisiasa, na kiuchumi kwa wanawake zimeanza kupanuka pole pole ulimwenguni kote. 6
Muungano huu mpya wa Kanisa kwa wanawake, ulioitwa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, haukuwa sawa na miungano mingine ya wanawake wakati huo kwa sababu ulianzishwa na nabii ambaye alitumia mamlaka ya ukuhani kuwapa wanawake mamlaka, majukumu matakatifu, na nafasi rasmi ndani ya muundo wa Kanisa, si mbali na muundo huo. 7
Kuanzia siku ya Nabii Joseph Smith hadi yetu, urejesho unaoendelea wa mambo yote umeleta mwangaza juu ya umuhimu wa mamlaka na nguvu za ukuhani katika kuwasaidia wanaume na wanawake kufanikisha majukumu yao matakatifu yaliyowekwa. Hivi karibuni tumefundishwa kuwa wanawake ambao wameteuliwa chini ya maelekezo ya funguo za ukuhani hufanya kazi kwa mamlaka ya ukuhani katika miito yao. 8
Mnamo Oktoba 2019, Rais Russell M. Nelson alifundisha kwamba wanawake ambao wamepata endaumenti kwenye hekalu wana nguvu ya ukuhani maishani mwao na majumbani mwao pale wanaposhika maagano hayo matakatifu ambayo wamefanya na Mungu. 9 Alifundisha kuwa “mbingu ziko wazi kwa wanawake ambao wamepokea endaumenti ya nguvu ya Mungu ikitiririka kutoka kwenye maagano yao ya ukuhani kama ilivyo kwa wanaume ambao wana ukuhani.” Na alimhimiza kila dada, “kuleta kwa ukarimu nguvu ya Mwokozi kusaidia familia yako na wengine unaowapenda.” 10
Kwa hivyo hiyo inamaanisha nini kwako wewe na mimi? Kuelewa mamlaka ya ukuhani na nguvu hubadilisha vipi maisha yetu? Mojawapo ya funguo ni kuelewa kwamba wakati wanawake na wanaume wanapofanya kazi pamoja, tunafanikisha kazi kubwa kuliko tunavyofanikisha tukifanya kwa kutengana. 11 Majukumu yetu ni usaidizi badala ya ushindani. Japokuwa wanawake hawateuliwi kwenye ofisi ya ukuhani, kama ilivyooneshwa hapo awali, wanawake wanabarikiwa na nguvu ya ukuhani pale wanapotunza maagano yao, na hufanya kazi kwa mamlaka ya ukuhani wakati wanapoteuliwa kwenye wito.
Katika siku nzuri ya Agosti, nilikuwa na bahati ya kukaa chini na Rais Russell M. Nelson katika nyumba iliyojengwa upya ya Joseph na Emma Smith huko Harmony, Pennsylvania, karibu na pale Ukuhani wa Haruni uliporejeshwa katika siku hizi za mwisho. Katika mazungumzo yetu, Rais Nelson alizungumzia juu ya jukumu muhimu ambalo wanawake wametimiza katika Urerejesho.
Rais Nelson: “Mojawapo ya mambo muhimu ambayo ninakumbushwa wakati ninapokuja kwenye eneo hili la Urejesho wa Ukuhani ni jukumu muhimu ambalo wanawake wametimiza katika Urejesho.
“Wakati Joseph mwanzo alipoanza kutafsiri Kitabu cha Mormoni, je, nani aliandika? Kweli, alifanya kidogo, lakini sio sana. Emma aliingilia.
“Na kisha namfikiria Joseph akienda kwenye vichaka kuomba karibu na nyumba yao katika Palmyra, New York. Je, alikwenda wapi? Alikwenda kwenye Kijisitu Kitakatifu. Je, kwa nini alikwenda huko? Kwa sababu huko ndiko mama alipokwenda alipohitaji kusali.
“Hao ni wanawake wawili tu ambao walikuwa na majukumu muhimu katika Urejesho wa Ukuhani na katika Urejesho wa Kanisa. Bila shaka, tunaweza kusema wake zetu wana umuhimu leo kama walivyokuwa wakati huo. Kwa kweli, wao ni muhimu.”
Kama Emma na Lucy na Joseph, tunafanikiwa zaidi wakati tuko tayari kujifunza kutoka kwa kila mmoja na tumeungana katika lengo letu la kuwa wafuasi wa Yesu Kristo na kusaidia wengine kwenye njia hiyo.
Tumefundishwa kuwa “ukuhani hubariki maisha ya watoto wa Mungu kwa njia nyingi. … Katika miito ya [Kanisa], ibada za hekalu, mahuhusiano ya kifamilia, huduma tulivu ya binafsi, wanawake na wanaume Watakatifu wa Siku za Mwisho husonga mbele kwa nguvu na mamlaka ya ukuhani . Kutegemeana huku kwa wanawake na wanaume katika kufanikisha kazi ya Mungu kupitia nguvu Zake ni kiini cha injili ya Yesu Kristo iliyorejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith.” 12
Umoja ni muhimu kwa kazi ya kiungu ambayo tumefadhiliwa na kuitwa kuifanya, lakini haitokei tu. Inahitaji bidii na muda wa kushauriana kwa dhati—kusikilizana, kuelewa maoni ya wengine, na kushiriki uzoefu—lakini mchakato unaleta maamuzi yenye mwongozo zaidi. Iwe nyumbani au katika majukumu yetu ya Kanisa, njia bora zaidi ya kutimiza uwezekano wetu wa kiungu ni kufanya kazi pamoja, tukibarikiwa na nguvu na mamlaka ya ukuhani katika majukumu yetu tofauti lakini yenye kuleta heshima.
Ushirikiano huo unaonekanaje katika maisha ya wanawake wa agano leo? Acha nishiriki mfano mmoja.
Alison na John walikuwa na ushirikiano ambao ulikuwa wa kipekee. Walipanda baisikeli ndefu ya watu wawili kwa mbio fupi na ndefu. Ili kushindana kwa mafanikio kwenye baiskeli hiyo, madereva wawili lazima wawe katika maelewano. Lazima wawe wameegemea upande mmoja kwa wakati unaofaa. Mmoja hawezi kumtawala mwingine, lakini lazima wawasiliane kwa uwazi na kila mmoja kufanya sehemu yake. Nahodha, mbele, ana udhibiti wa wakati gani wa kushika breki na wakati gani wa kusimama. Anayesaidia, akiwa nyuma, anahitaji kuwa makini kwa kile kinachoendelea na kuwa tayari kutoa nguvu ya ziada ikiwa watasalia nyuma kidogo au ikiwa wanasogea karibu sana na waendesha baiskeli wengine. Lazima waasaidiane ili kupata maendeleo na kufikia malengo yao.
Alison alielezea: “Kwa muda kidogo wa mwanzo, mtu aliye katika nafasi ya nahodha angesema ‘Simama’ wakati tunahitaji kusimama na ‘kushika breki’ wakati tunahitaji kuacha kunyonga pedeli. Baada ya muda, mtu ambaye alikuwa nyuma alijifunza kujua wakati nahodha alipokuwa karibu kusimama au kushika breki, na hakuna maneno yaliyohitajika kusemwa. Tulijifunza kuwa kwenye tuni na jinsi kila mmoja alivyokuwa akifanya na tuliweza kujua wakati mmoja alipokuwa akihangaika na [kisha] mwingine alijaribu kuchukua usukani. Kwa kweli yote ni kuhusu kuamini na kufanya kazi pamoja.” 13
John na Alison walikuwa wameungana si tu wakati walipooendesha baiskeli yao, lakini walikuwa na umoja katika ndoa yao vile vile. Kila mmoja alitaka furaha ya mwingine zaidi kuliko yake mwenyewe; kila mmoja alitafuta uzuri kwa mwenzake na alijitahidi kushinda yale yasiyo mazuri ndani yake. Walifanya zamu kuongoza na walifanya zamu kutoa zaidi wakati mwenzi mmoja alipokuwa anasumbuka. Kila mmoja alithamini michango ya mwingine na walipata majibu mazuri kwa changamoto zao pale walipoweka pamoja talanta na nyenzo zao. Kwa kweli wamefungwa pamoja kupitia upendo kama wa Kristo.
Kuwa zaidi kwenye tuni na mfumo wa kiungu wa kufanya kazi pamoja kwa umoja ni muhimu katika siku hizi za ujumbe wa “ mimi kwanza” ambao unatuzunguka. Wanawake wanavyo vipawa vya kipekee, vya kiungu 14 na wanapewa majukumu ya kipekee, lakini hayana umuhimu wa juu—au wa chini—kuliko vipawa na majukumu ya wanaume. Yote yameundwa na yanahitajika ili kutimiza mpango mtakatifu wa Baba wa Mbinguni wa kumpa kila mmoja wa watoto Wake nafasi nzuri ya kutimiza uwezekano wake wa Kiungu.
Leo, “tunahitaji wanawake ambao wana ujasiri na maono ya mama yetu Eva” 15 ili kuungana na kaka zao katika kuleta nafsi kwa Kristo. 16 Wanaume wanahitaji kuwa wenza wa kweli kuliko kudhani wana jukumu la pekee au kutenda kama wenza wa “kujifanya” wakati wanawake wakifanya kazi nyingi. Wanawake wanahitaji kuwa tayari “kujitokeza mbele [na] kuchukua nafasi [zao] sahihi na zinazohitajika” 17 kama washirika kuliko kufikiria wanahitaji kufanya yote peke yao au kungojea kuambiwa nini cha kufanya. 18
Kuwaona wanawake kama washiriki muhimu haihusu kuunda usawa bali inahusu kuelewa ukweli wa mafundisho. Badala ya kuanzisha mpango wa kufanikisha hilo, tunaweza kufanya kazi kwa bidii kuwathamini wanawake kama Mungu anavyofanya: kama washirika muhimu katika kazi ya wokovu na kuinuliwa.
Je tuko tayari? Je, tutajitahidi kushinda upendeleo wa kitamaduni na badala yake tukumbatie mpangilio na mazoea ya kiungu yaliyojikita juu ya msingi wa mafundisho? Rais Russell M. Nelson anatualika “kutembea bega kwa bega katika kazi hii takatifu … [ili] kusaidia kuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili wa Bwana.” 19 Tunapofanya hivyo, tutajifunza kuthamini michango ya kila mtu na kuongeza ufanisi ambao kupitia huo tunatimiza majukumu yetu ya kiungu. Tutahisi furaha kubwa kuliko tulivyowahi kuona.
Hebu kila mmoja wetu achague kuungana katika njia ya Bwana yenye msukumo wa kiungu ili kusaidia kazi Yake kwenda mbele. Katika jina la Mwokozi wetu Mpendwa, Yesu Kristo, amina.