Kumbukumbu za Kuelezeka Kiroho
Wakati changamoto binafsi au hali za kidunia zilizo nje ya uwezo wetu zinapotia giza njia yetu, kumbukumbu za kuelezeka kiroho kutoka katika kitabu chetu cha maisha ni kama mawe yatoayo mwanga ambayo husaidia kuangaza njia mbele yetu.
Miaka kumi na minane baada ya Ono la Kwanza, Nabii Joseph Smith aliandika kwa kina kuhusu uzoefu wake. Alikuwa amekabiliana na upinzani, mateso, dhihaka, vitisho, na mashambulizi ya kinyama.1 Lakini bado aliendelea kushuhudia kwa ujasiri juu ya Ono lake la Kwanza: “Hakika nilikuwa nimeuona mwanga, na katikati ya mwangaza huo niliwaona Watu wawili, nao kwa hakika waliongea nami; na ingawa nilichukiwa na kuteswa kwa kusema kwamba nimeona ono, lakini ilikuwa ni kweli. … Nami nilijua hivyo, nami nilijua kwamba Mungu alijua, na sikuweza kukataa.”
Katika nyakati zake ngumu, kumbukumbu ya Joseph ilirudi nyuma karibu miongo miwili kwenye uhakika wa upendo wa Mungu kwake na matukio ambayo yalikaribisha Urejesho ambao kwa muda mrefu ulitabiriwa. Akitafakari juu ya safari yake kiroho, Joseph alisema: “Simlaumu yoyote kwa kutoamini historia yangu. Kama nisingepitia kile ambacho nimepitia, mimi mwenyewe nisingekiamini.”3
Lakini uzoefu ulikuwa halisi, na kamwe hakuusahau wala kuukataa, kwa utulivu alithibitisha ushuhuda wake huku akielekea Carthage. “Ninakwenda kama mwana kondoo kwa mchinjaji,” alisema, “lakini nimetulia kama asubuhi ya majira ya joto; nina dhamira isiyo na kinyongo kwa Mungu, na kwa wanadamu wote.”4
Uzoefu Wako wa Kuelezeka Kiroho
Kuna somo kwetu katika mfano huu wa Nabii Joseph. Pamoja na mwongozo wa amani tunaoupata kutoka kwa Roho Mtakatifu, muda baada ya muda, Mungu anatuhakikishia kwa nguvu na kila mmoja kibinafsi kwamba Anatujua na kutupenda na kwamba Anatubariki kwa baraka mahususi na kwa uwazi. Kisha, katika nyakati zetu za magumu, Mwokozi huleta uzoefu huu tena katika akili zetu.
Fikiria juu ya maisha yako mwenyewe. Kwa miaka mingi, nimesikiliza maelfu ya uzoefu wa kiroho kutoka kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho kote ulimwenguni, ukinithibitishia bila shaka yoyote kwamba Mungu humjua na kumpenda kila mmoja wetu na kwamba Anatamani kwa dhati kujidhihirisha kwetu. Uzoefu huu unaweza kuja katika nyakati muhimu maishani mwetu au katika kile ambacho mwanzo kinaweza kuonekana kama matukio yasiyovutia, lakini mara zote husindikizwa na uthibitisho wa kiroho wa kipekee wa upendo wa Mungu.
Kukumbuka uzoefu huu wa kuelezeka wa kiroho hutupeleka kwenye kupiga magoti, na kusema kama alivyosema Nabii Joseph: “Kile nilichopokea kilitoka mbinguni. Ninajua, na ninajua kwamba Mungu anajua kwamba ninajua.”5
Mifano Minne
Tafakari kumbukumbu zako za kuelezeka kiroho wakati ninapoelezea mifano michache kutoka kwa wengine.
Miaka mingi iliyopita, patriaki wa kigingi aliyekuwa mzee akiwa na vali mbili za moyo zisizofanya kazi alimuomba kwa wakati huo-Daktari Russell M. Nelson kuingilia kati, ingawa kwa wakati ule hakukuwa na suluhisho la upasuaji kwa ajili ya vali ya pili isiyofanya kazi. Daktari Nelson hatimaye alikubali kufanya upasuaji. Haya ni maneno ya Rais Nelson:
“Baada ya kuweza kuondoa kikwazo kwenye vali ya kwanza, tulienda kwenye ya pili. Tuliikuta ikiwa ni nzima lakini ikiwa imetanuka sana kiasi kwamba haikuweza tena kufanya kazi kama ilivyotakiwa. Wakati tukiangalia vali hii, ujumbe ulikuja dhahiri mawazoni mwangu: Punguza mzingo wa sehemu ya duara. Nilifikisha ujumbe huo kwa msaidizi wangu. ‘Tishu za vali zitatosha ikiwa kwa usahihi tutapunguza sehemu ya duara kuelekea ukubwa wake wa kawaida.’
“Lakini kwa namna gani? … Taswira ilikuja kwa uwazi mawazoni mwangu, ikionesha jinsi ambavyo mishono ingeweza kufanyika—ili kufanya mkunjo hapa na mkunjo pale. … Bado ninakumbuka taswira ile—kiukamilifu pamoja na mistari ya nukta ambapo mishono ilitakiwa kuwekwa. Urekebishaji ulikamilika kama ulivyochorwa mawazoni mwangu. Tuliijaribu vali na kukuta uvujaji ulipungua kwa kiasi kikubwa. Msaidizi wangu alisema, ‘ni muujiza.’”6 Patriaki aliishi kwa miaka mingi.
Daktari Nelson alikuwa ameongozwa. Na alijua kuwa Mungu alijua kwamba yeye alikuwa ameongozwa.
Mimi pamoja na Kathy tulikutana na Beatrice Magré huko Ufaransa miaka 30 iliyopita. Beatrice hivi karibuni aliniambia juu ya tukio ambalo liliathiri maisha yake ya kiroho muda mfupi baada ya yeye kubatizwa akiwa kijana. Haya ni maneno yake:
“Vijana wa tawi letu walisafiri pamoja na viongozi wao kwenda ufuko wa Lacanau, mwendo wa saa moja na nusu kutoka Bordeaux.
“Kabla ya kurudi nyumbani, mmoja wa viongozi aliamua kuogelea kwa mara ya mwisho na akazamia kwenye mawimbi na miwani yake. Alipoibuka, miwani yake ilikuwa imetoweka. … Ilikuwa imepotelea baharini.
“Kupotea kwa miwani yake kungemzuia kuendesha gari lake. Tungekwama mbali na nyumbani.
“Dada aliyejawa na imani alipendekeza kwamba tusali.
“Nilinung’unika kwamba kusali kusingetusaidia chochote, na kwa kusuasua nilijiunga na kundi kusali kwenye eneo la wazi wakati tukisimama kwenye maji ya kahawia ya kina cha kiunoni.
“Baada ya sala kumalizika, nilinyosha mikono yangu ili kumrushia maji kila mtu. Wakati nikisafisha sehemu ya juu ya bahari ili nichote maji, miwani yake ikaegema mikononi mwangu. Hisia kali ilipenya nafsi yangu kwamba Mungu kweli husikia na kujibu sala zetu.”7
Miaka arobaini na mitano baadae, alikumbuka kama vile ilikuwa imetendeka jana. Beatrice alikuwa amebarikiwa, na alijua kwamba Mungu alijua kuwa yeye alijua kwamba alikuwa amebarikiwa.
Uzoefu wa Rais Nelson na Dada Magré ulikuwa wa tofauti kabisa, hata hivyo, kwa wote wawili, uzoefu wa kuelezeka kiroho usiosahaulika wa upendo wa Mungu ulitiwa ndani ya mioyo yao.
Matukio haya ya kuelezeka mara nyingi huja katika kujifunza kuhusu injili ya urejesho au katika kushiriki injili na wengine.
Picha hii ilipigwa São Paulo, Brazili, mnamo 2004. Floripes Luzia Damasio wa kigingi cha Ipatinga Brazli alikuwa na miaka 114. Akiongelea kuhusu uongofu wake, Dada Damasio aliniambia kwamba wamisionari katika kijiji chake walikuwa wametoa baraka za ukuhani kwa mtoto aliyekuwa akiumwa sana ambaye kimiujiza alipona. Yeye alitaka kujua zaidi. Wakati aliposali kuhusu ujumbe wao, ushuhuda usiopingika wa Roho ulithibitisha kwake kwamba Joseph Smith alikiwa ni nabii wa Mungu. Akiwa na miaka 103, alibatizwa, na akiwa na miaka 104, alipata endaumenti. Kila mwaka baada ya hapo, alitumia masaa 14 kwa safari ya basi ili kuwa hekaluni kwa wiki moja. Dada Damasio alikuwa amepokea uthibitisho wa kimbingu, na alijua kwamba Mungu alijua kuwa yeye alijua kwamba uthibitisho ulikuwa wa kweli.
Hapa kuna kumbukumbu ya kiroho kutoka misheni yangu ya kwanza huko Ufaransa miaka 48 iliyopita.
Wakati tukitafuta watu, mimi pamoja na mwenzangu tuliacha Kitabu cha Mormoni kwa mwanamke mzee. Tuliporudi nyumbani kwa mwanamke huyo takribani wiki moja baadae, alifungua mlango. Kabla ya neno lolote kuzungumzwa, nilihisi nguvu ya kushikika ya kiroho. Hisia kali ziliendelea wakati Dada Alice Audubert alipotukaribisha ndani na kutuambia alikuwa amesoma Kitabu cha Mormoni na alijua kilikuwa cha kweli. Wakati tukiondoka nyumbani kwake siku hiyo, nilisali, “Baba wa Mbinguni, tafadhali nisaidie kamwe nisisahau kile ambacho nimekihisi.” Sijawahi kusahau.
Katika nyakati zinazoonekana kama za kawaida, kwenye mlango unaofanana na mamia ya milango mingine, nilihisi nguvu ya mbinguni. Na nilijua kwamba Mungu alijua kuwa nilijua kwamba dirisha la mbinguni lilikuwa limefunguliwa.
Maalum kwa mtu binafsi na Isiyoweza kukataliwa
Kumbukumbu hizi za kuelezeka kiroho huja kwa nyakati tofauti na katika njia tofauti, zikiwa maalum kwa kila mmoja wetu.
Fikiria kuhusu mifano yako unayopenda katika maandiko. Wale waliokuwa wakimsikiliza Mtume Petro “walichomwa mioyoni mwao.”8 mwanamke wa Kilamani Abishi aliamini lile “ono kuu aliloona baba yake.”9 Na sauti ilikuja katika akili ya Enoshi.10
Rafiki yangu Clayton Christensen alielezea uzoefu mmoja wakati wa usomaji wa Kitabu cha Mormoni kwa sala za dhati katika njia hii: “Roho nzuri, tulivu, ya kupendeza … ilinizunguka na kuijaza nafsi yangu, ikinifunika katika hisia za upendo ambao sikuwahi kuufikiria ningeuhisi [na hisia hizi ziliendelea usiku baada ya usiku].”11
Kuna nyakati ambapo hisia za kiroho huzama kwa kina mioyoni mwetu kama moto, zikiangaza nafsi zetu. Joseph Smith alielezea kwamba wakati mwingine sisi tunapokea “mpapaso wa ghafla wa mawazo” na mara chache “utiririkaji halisi wa maarifa.”12
Rais Dallin H. Oaks, katika kumjibu mwanaume ambaye alidai kamwe hakuwahi kuwa na uzoefu kama huo, alishauri, “pengine sala zako zimekuwa zikijibiwa tena na tena, lakini umekuwa na matarajio yako yaliyojikita kwenye ishara kubwa au sauti kubwa sana kwamba unadhani hujapata jibu.”13 Mwokozi Mwenyewe aliongea juu ya watu wenye imani kubwa ambao “Walikuwa [wamebarikiwa] kwa moto na Roho Mtakatifu, [lakini wao] hawakujua.”14
Ni kwa jinsi gani Wewe Unamsikiliza Yeye?
Tumemsikia hivi karibuni Rais Russell M. Nelson akisema: “Ninakualikeni kufikiria kwa kina na mara nyingi kuhusu swali hili la msingi: Ni kwa jinsi gani wewe unamsikiliza Yeye? Mimi pia ninakualikeni kuchukua hatua za kumsikiliza Yeye vizuri zaidi na mara nyingi zaidi.”15 Amerudia mwaliko huo asubuhi ya leo.
Tunamsikiliza Yeye kwenye sala zetu, nyumbani mwetu, katika maandiko, katika nyimbo za kanisa, kwa ustahiki tunapokula sakramenti, wakati tukitangaza imani yetu, wakati tukiwahudumia wengine, na wakati tukihudhuria hekaluni pamoja na waumini wenzetu. Nyakati za kuelezeka kiroho huja wakati kwa sala tukisikiliza mkutano mkuu na tunapotii vyema zaidi amri. Na watoto, uzoefu huu ni kwa ajili yenu pia. Kumbuka, Yesu “alifundisha na kuwahudumia watoto … na [watoto] walizungumza … vitu vikubwa na vya ajabu.”16 Bwana alisema:
“[Maarifa haya] yametolewa kwenu kupitia Roho, … na isingekuwa kwa uwezo wangu msingeweza [kuyapata];
“Kwa hiyo basi, ninyi mnaweza kushuhudia kwamba mmesikia sauti yangu, na mnayajua maneno yangu.”17
Tunaweza “kumsikiliza Yeye” kwa sababu ya baraka ya Upatanisho wa Mwokozi usio na mfano.
Wakati hatuwezi kuchagua muda wa kupokea uzoefu huu wa kuelezeka, Rais Henry B. Eyring alitoa ushauri huu katika maandalizi yetu: “Usiku wa leo, na kesho usiku, unaweza kusali na kutafakari, ukiuliza maswali: Je, Mungu alituma ujumbe ambao ulikuwa mahususi kwa ajili yangu? Je, niliona mkono Wake katika maisha yangu au maisha ya [familia] yangu?”18 Imani, utii, unyenyekevu, na nia ya dhati hufungua madirisha ya mbinguni.19
Kielelezo
Ungeweza kufikiria juu ya kumbukumbu zako za kiroho katika njia hii. Kwa sala endelevu, uamuzi wa dhati kushika maagano yetu, na kipawa cha Roho Mtakatifu, tunasonga katika njia yetu kwenye maisha. Wakati changamoto binafsi, mashaka, au kuvunjika moyo vinapotia giza njia yetu, au wakati hali za kidunia zilizo nje ya uwezo wetu hutupeleka katika kujiuliza kuhusu siku zijazo, kumbukumbu za kuelezeka kiroho kutoka katika kitabu chetu cha maisha ni kama mawe yatoayo mwanga ambayo husaidia kuangaza njia mbele yetu, kutuhakikishia kwamba Mungu anatujua, anatupenda, na amemtuma Mwanaye, Yesu Kristo, ili kutusaidia kurudi nyumbani. Na wakati mtu anapoweka pembeni kumbukumbu zake za kuelezeka na anapotea au kukanganyikiwa, tunawaelekeza kwa Mwokozi wakati tunaposhiriki pamoja nao imani yetu na kumbukumbu zetu, tukiwasaidia kugundua tena nyakati hizo za kiroho za thamani ambazo awali walizithamini.
Baadhi ya uzoefu ni mtakatifu sana kiasi kwamba tunaulinda katika kumbukumbu zetu za kiroho na hatuushiriki.20
“Malaika wanazungumza kwa uwezo wa Roho Mtakatifu; kwa hivyo, wanazungumza maneno ya Kristo.”21
“malaika [hawajakoma] kuwahudumia watoto wa watu.
“Kwani tazama, wako chini ya [Kristo], kuhudumu kulingana na … neno la amri yake, wakijidhihirisha kwa wale walio na imani ya nguvu na akili imara katika kila kitu cha uchamungu.”22
Lakini huyo “Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, … atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”23
Kumbatia kumbukumbu zako takatifu. Ziamini. Ziandike. Zishiriki kwa familia yako. Amini kwamba zinakuja kwako kutoka kwa Baba wa Mbinguni na Mwanaye Mpendwa.24 Acha zilete uvumilivu kwenye mashaka yako na uelewa katika magumu yako.25 Ninaahidi kwamba wakati kwa hiari ukizikubali na kwa umakini kuthamini matukio ya kuelezeka kiroho katika maisha yako, zaidi na zaidi yatakuja kwako. Baba wa Mbinguni anakujua na anakupenda!
Yesu ndiye Kristo, injili Yake imerejeshwa, na tunapobakia waaminifu , ninashuhudia tutakuwa Wake milele, katika jina la Yesu Kristo, amina.