Mkutano Mkuu
Mng’aro Mkamilifu wa Tumaini
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Mng’aro Mkamilifu wa Tumaini

Kwa sababu Urejesho ulithibitisha tena ukweli wa msingi kwamba Mungu hufanya kazi katika ulimwengu huu, tunaweza kutumaini, tunapaswa kutumaini, hata wakati tunapokumbana na matatizo makubwa zaidi.

Oktoba iliyopita, Rais Russell M. Nelson alitualika kutazamia mbele mkutano huu wa Aprili 2020 kwa kila mmoja wetu katika njia zetu wenyewe kutazama nyuma ili kuona mkono mtukufu wa Mungu katika kurejesha injili ya Yesu Kristo. Mimi na Dada Holland tulichukua mwaliko huo wa kinabii kwa dhati. Tulijichukulia kama tulioishi mwanzoni mwa miaka ya 1800, tukitazama imani za dini za wakati huo. Katika mazingira hayo ya dhahania, tulijiuliza, “Nini kinakosekana hapa? Ni nini tungetamani kuwa nacho? Ni nini tunategemea Mungu atatoa katika kuitikia matamanio yetu ya kiroho?”

Vema, kwa jambo moja, tulitambua kwamba karne mbili zilizopita tungekuwa tukitumainia sana urejesho wa dhana sahihi ya Mungu kuliko wengi wao wa kipindi hicho walivyokuwa, Akijificha kama ambavyo Yeye daima amekuwa akionekana kuwa nyuma ya karne za makosa na kutoelewana. Kwa kuazima kirai kutoka kwa William Ellery Channing, mtu maarufu wa dini wa siku hizo, tungetazamia “sifa ya Mungu kama mzazi,” ambayo Channing aliifikiria kama “Fundisho la kwanza kuu la Kikristo.”1 Fundisho kama hilo lingemtambua Mungu kama Baba mwenye kujali wa Mbinguni, na si kama hakimu mkali atoaye maamuzi makali au kama mwenye nyumba mtoro ambaye hapo mwanzo alijishugulisha na masuala ya kidunia lakini sasa alikuwa ametingwa mahali fulani pengine katika ulimwengu.

Ndiyo, matumaini yetu mnamo 1820 yangekuwa ni kumsikia Mungu akizungumza kwa uwazi wakati huu kama Yeye alivyofanya wakati uliopita, Baba wa kweli, katika dhana ya upendo wa juu wa neno hilo. Bila shaka Yeye asingekuwa asiyejali, mtawala dhalimu ambaye aliwachagua kabla watu wachache kwa ajili ya wokovu na kisha kuwapeleka waliosalia wa familia ya mwanadamu kwenye hukumu. Hapana, Angekuwa yule ambaye kila tendo lake, kwa tamko takatifu, lingekuwa “kwa ajili ya manufaa ya ulimwengu; kwani anaupenda ulimwengu”2 na kila kilicho hai ndani yake. Upendo huo ungekuwa ni sababu Yake kuu ya kumtuma Yesu Kristo, Mwanaye wa Pekee, duniani.3

Tukimzungumzia Yesu, kama tungeliishi katika miaka hiyo ya mwanzo ya karne ya 19, tungetambua kwa mshangao mkuu kwamba mashaka kuhusu uhalisia wa maisha na Ufufuko wa Mwokozi vilikuwa vikianza kuchukua nafasi muhimu kwenye Ukristo. Kwa hivyo, tungelitumainia kuja kwa ushahidi kwa dunia nzima ambao ungethibitisha ushuhuda wa kibiblia kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana halisi wa Mungu, Alfa na Omega, na Mwokozi pekee ambaye ulimwengu huu utawahi kumfahamu. Ingekuwa miongoni mwa matumaini yetu ya dhati kwamba ushahidi mwingine wa kimaandiko ungeletwa, kitu ambacho kingejumuisha ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo, ukipanua na kuongeza uelewa wetu wa kuzaliwa Kwake kimiujiza, huduma ya kushangaza, dhabihu ya upatanisho, na Ufufuko wa kitukufu. Kwa kweli nakala hiyo ingekuwa “utakatifu … [ulioshushwa] chini kutoka mbinguni; na ukweli … [uliotoka] duniani.”4

Kwa kuchunguza ulimwengu wa Kikristo katika siku hizo, tungetumaini kumpata mtu aliyeidhinishwa na Mungu kwa mamlaka ya kweli ya ukuhani ambaye angetubatiza, kutupa kipawa cha Roho Mtakatifu, na kusimamia ibada zote za injili zilizo muhimu kwa ajili ya kuinuliwa. Mnamo 1820, tungetumainia kuona kutimizwa kwa unabii wa Isaya, Mika, na manabii wengine wa kale kuhusu kurejea kwa nyumba tukufu ya Bwana.5 Tungefurahia kuona utukufu wa mahekalu matakatifu yakianzishwa tena, pamoja na Roho, ibada, nguvu, na mamlaka ya kufundisha kweli za milele, kuponya majeraha binafsi, na kuunganisha familia pamoja milele. Ningetafuta sehemu yoyote na kila mahali ili kumpata mtu aliyepewa idhini ya kuniambia mimi na kipenzi changu Patricia kwamba ndoa yetu katika mpangilio huo ilikuwa imefungwa kwa muda na milele yote, kamwe kutosikia au kuwekwa juu yetu laana ya kuumiza ya “mpaka kifo kiwatenganishe.” Najua kwamba “katika nyumba ya Baba [yetu] kuna makao mengi,”6 lakini, nikiongea binafsi, kama ningekuwa mwenye bahati sana kiasi cha kurithi moja ya hayo, isingekuwa ya kufaa kwangu kama vile kibanda kilichozeeka ikiwa Pat na watoto wetu wasingekuwa nami kushiriki urithi huo. Na kwa mababu zetu, baadhi yao ambao waliishi na kufa zamani bila hata ya kusikia jina la Yesu Kristo, tungetumainia ile dhana kuu ya haki na rehema ya kibiblia irejeshwe—desturi ya walio hai ya kufanya ibada okozi kwa ajili ya ndugu zao waliokufa.7 Hakuna kazi ambayo ningeweza kuifikiria ingeelezea kwa utukufu zaidi tamanio la upendo la Mungu kwa kila mmoja wa watoto Wake duniani bila kujali lini waliishi au wapi walifariki.

Naam, orodha yetu ya matumaini ya mwaka 1820 ingeweza kuendelea, lakini pengine ujumbe muhimu zaidi wa Urejesho ni kwamba matumaini hayo yasingekuwa bure. Kwa kuanzia katika Kijisitu Kitakatifu na kuendelea mpaka leo hii, matamanio haya yalianza kuvikwa uhalisia na kuwa, kama Mtume Paulo na wengine walivyofundisha, nanga ya roho, yenye salama, yenye nguvu.8 Kile ambacho awali kilikuwa kikitumainiwa tu kimekuwa sasa historia.

Na hivyo ndivyo kukumbuka kwetu miaka 200 ya fadhila za Mungu kwa ulimwengu. Lakini nini tunakitazamia mbele? Bado tunayo matumaini ambayo bado hayajatimizwa. Hata tunapozungumza, tunapigana vita “ya watu wote” na COVID-19, ukumbusho wa dhati kwamba virusi ambavyo ni vidogo mara9 1,000 ya ukubwa wa mchanga10 vinaweza kuangamiza idadi yote ya watu na uchumi wa ulimwengu. Tunaomba kwa ajili ya wale waliopoteza wapendwa kwenye janga hili la sasa, vilevile kwa ajili ya wale ambao kwa sasa wameathirika au wako katika hatari. Hakika tunaomba kwa ajili ya wale wanaotoa huduma nzuri kabisa ya afya. Wakati tutakapoishinda—na tutaishinda—na tuweze kuwa sawa kwenye msimamo wa kuukomboa ulimwengu kutokana na virusi vya njaa na kukomboa ujirani na mataifa kutokana na virusi vya umasikini. Na tutumainie shule ambapo wanafunzi wanafunzwa—si kutishwa kwamba watapigwa risasi—na kwa ajili ya karama ya heshima binafsi kwa kila mtoto wa Mungu, kutodhuriwa kwa chuki yoyote ya rangi, ukabila, au ya dini. Kinachoimarisha yote haya ni tumaini letu lisilopungua kwa ajili ya kujitoa zaidi kwenye amri kuu mbili: kumpenda Mungu kwa kufuata ushauri Wake na kuwapenda jirani zetu kwa kuonesha ukarimu na huruma, uvumilivu na msamaha.11 Maelekezo haya mawili matakatifu, bado—na milele yatakuwa—tumaini halisi pekee ambalo tunalo kwa ajili ya kuwapa watoto wetu ulimwengu bora zaidi ya huu wanaoujua sasa.12

Katika kuongezea kwenye kuwa na matamanio haya ya kiulimwengu, wengi katika wasikilizaji hawa leo wana matumaini binafsi ya dhati: tumaini la ndoa kuimarika, au nyakati zingine tumaini la kuwa tu na ndoa; tumaini la kushinda uraibu; tumaini la mtoto aliyeasi kurejea; tumaini la kukoma kwa maumivu ya aina nyingi ya kimwili na kihisia. Kwa sababu Urejesho ulithibitisha tena ukweli wa msingi kwamba Mungu hufanya kazi katika ulimwengu huu, tunaweza kutumainia, tunapaswa kutumainia, hata wakati tunapokumbana na matatizo makubwa zaidi. Hiki ndicho maandiko yalichomaanisha wakati Ibrahimu alipoweza kuwa na tumaini wakati ambapo hapakuwa na tumaini13—hilo ni, aliweza kuamini bila kujali kila sababu ya kutoamini —kwamba yeye pamoja na Sara wangeweza kupata mtoto ambapo hilo lilionekana haliwezekani kabisa. Hivyo, nauliza, “ikiwa mengi ya matumaini yetu ya mwaka 1820 yangeanza kutimizwa kwa mwako wa nuru tukufu kwa mvulana mdogo akipiga magoti kwenye kijisitu huko kaskazini ya New York, kwa nini sisi tusitumaini kwamba hamu na matamanio ya haki kama ya Kristo bado inaweza kwa kushangaza, kimiujiza kujibiwa na Mungu wa matumaini yote?” Sote tunahitaji kuamini kwamba kile tunachotamani katika haki kinaweza siku moja, kwa njia tofauti, kwa jinsi tofauti kuwa chetu.

Akina kaka na akina dada, tunajua baadhi ya mapungufu ya kidini mwanzoni mwa karne ya 19 yalikuwa yapi. Zaidi, tunajua kitu fulani kuhusu mapungufu ya kidini leo hii ambacho bado kinaacha njaa na matumaini ya baadhi pasipo kutimia. Tunajua baadhi ya kutoridhika huko kunawaongoza baadhi ya watu mbali kutoka kwenye taasisi za juu za kidini za mahali husika. Tunajua pia, kama mwandishi mmoja mwenye hasira alivyoandika, kwamba “viongozi wengi wa kidini [wa leo] wanaonekana hawaelewi” katika kushughulikia mmomonyoko huu, wakitoa kama mjibizo “chakula cha fikra hasi juu ya uungu, ishara nyepesi ya ushawishi, uzushi uliotayarishwa kwa umakini, [au wakati mwingine] vitu visivyo na maana”14—na vyote wakati ambapoi ulimwengu ukihitaji mengi zaidi, wakati kizazi chipukizi kikistahili mengi zaidi, na wakati ambapo katika wakati wa Yesu Alitoa mengi zaidi. Kama wafuasi wa Kristo, tunaweza katika siku yetu kuinuka zaidi ya Waisraeli wa kale ambao walilia, “Mifupa yetu imekauka, na tumaini letu limepotea.”15 Bila shaka, kama hatimaye tunapoteza tumaini, tunapoteza urithi wetu endelevu wa milele. Ilikuwa ni karibu kabisa na lango la jehanamu kwamba Dante aliandika onyo kwa wote waliosafiri kupitia Divina Commedia: yake “Acha matumaini yote,” alisema “wale mnaoingia humu.”16 Hakika wakati tumaini linapoondoka, kile tunachobakia nacho ni mwali wa moto mkubwa ukiwaka kila sehemu.

Hivyo, wakati migongo yetu ikiwa ukutani na, kama wimbo wa kanisa unavyosema, “Wasaidizi wengine hushindwa na faraja hutoweka,”17 kati ya mema yetu ya muhimu sana itakuwa ni hii zawadi ya tumaini iliyounganishwa thabiti kwenye imani yetu katika Mungu na hisani kwa wengine.

Katika mwaka huu wa maadhimisho ya miaka mia mbili, tunapoangalia nyuma kuona yote ambayo tumepewa na kufurahi katika utambuzi wa matumaini mengi kutimizwa, ninapaza tamko la mmisionari aliyerudi wa kike ambaye alisema kwetu huko Johannesburg miezi michache iliyopita, “[Sisi] hatukupiga hatua hii kubwa katika urejesho ili tukomee hapa katika kuendelea na kupokea ufunuo.”18

Nikifupisha moja ya maneno ya mwisho yaliyowahi kuandikwa kwenye maandiko, ninasema pamoja na nabii Nefi na dada yule kijana:

“Ndugu zangu [na dada zangu] wapendwa, baada ya [kupokea matunda haya ya kwanza ya Urejesho], ningeuliza je, yote yamekamilishwa? Tazama, nawaambia, Hapana. …

“… Lazima msonge mbele mkiwa na imani imara katika Kristo, mkiwa na mng’aro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na wanadamu wote. … Kama mtafanya hivyo[,] … asema Baba: Mtapokea uzima wa milele.”19

Ninatoa shukrani, kaka zangu na dada zangu, kwa yote ambayo tumepewa katika kipindi hiki kikuu na cha mwisho cha vipindi vyote vya maongozi ya Mungu, kipindi cha maongozi ya Mungu cha urejesho wa injili ya Yesu Kristo. Vipawa na baraka ambazo hutiririka kutokana na injili hiyo humaanisha kila kitu kwangu—kila kitu—kwa hivyo katika juhudi za kutoa shukrani kwa Baba yangu wa Mbinguni kwa ajili ya hizo, nina “ahadi za kutimiza, na mwendo wa kutembea kabla sijalala, na mwendo wa kutembea kabla sijalala.”20 Na tusonge mbele tukiwa na upendo mioyoni mwetu, tukitembe katika “mng’aro wa tumaini”21 uangazao njia ya matarajio matakatifu ambayo tumekuwa nayo kwa miaka 200 sasa. Ninashuhudia kwamba wakati ujao utakuwa wenye miujiza-tele na baraka tele kama wakati uliopita ulivyokuwa. Tuna kila sababu ya kutumainia baraka hata kuu kuliko zile ambazo tayari tumekwisha zipokea kwa sababu hii ni kazi ya Mungu Mwenyezi, hili ni Kanisa la ufunuo unaoendelea, hii ni injili ya Kristo yenye rehema na ukarimu usio na mwisho. Ninatoa ushuhuda wa kweli hizi zote na zingine zaidi katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. “The Essence of the Christian Religion,” katika The Works of William E. Channing (1888), 1004.

  2. 2 Nefi 26:24.

  3. Ona Yohana 3:16–17.

  4. Musa 7:62.

  5. Ona Isaya 2:1–3; Ezekieli 37:26; Mika 4:1–3; Malaki 3:1.

  6. Yohana 14:2.

  7. Ona 1 Wakorintho 15:29; Mafundisho na Maagano 128:15–17.

  8. Ona Waebrania 6:19; Etheri 12:4.

  9. Ona Na Zhu pamoja na wengine, “A Novel Coronavirus from Patients with Pneumonia in China, 2019,” New England Journal of Medicine, Feb. 20, 2020, 727–33.

  10. Ona “Examination and Description of Soil Profiles,” katika Soil Survey Manual, ed. C. Ditzler, K. Scheffe, and H. C. Monger (2017), nrcs.usda.gov.

  11. Ona Mathayo 22:36–40; Marko 12:29–33; ona pia Mambo ya Walawi 19:18; Kumbukumbu la Torati 6:1–6.

  12. Ona Etheri 12:4.

  13. Ona Warumi 4:18.

  14. R. J. Snell, “Quiet Hope: A New Year’s Resolution,” Public Discourse: The Journal of the Witherspoon Institute, Dec. 31, 2019, thepublicdiscourse.com.

  15. Ezekieli 37:11.

  16. Hiki ni kifungu cha maneno kama kilivyotafsiriwa mara nyingi. Hata hivyo, tafsiri halisi zaidi ni “All hope abandon, ye who enter here” (Dante Alighieri, “The Vision of Hell,“ in Divine Comedy, trans. Henry Francis Cary [1892], canto III, line 9).

  17. “Abide with Me!” Nyimbo za Kanisa, na. 166.

  18. Judith Mahlangu (multistake conference near Johannesburg, South Africa, Nov. 10, 2019), in Sydney Walker, “Elder Holland Visits Southeast Africa during ‘Remarkable Time of Growth,’” Church News, Nov. 27, 2019, thechurchnews.com.

  19. 2 Nefi 31:19–20; msisitizo umeongezwa.

  20. “Stopping by Woods on a Snowy Evening,” lines 14–16, in The Poetry of Robert Frost: The Collected Poems, ed. Edward Connery Lathem (1969), 225.

  21. 2 Nefi 31:20.

Chapisha