Mkutano Mkuu
“Acheni Nyumba Hii Na Ijengwe Kwa Jina Langu”
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


2:3

“Acheni Nyumba Hii Na Ijengwe Kwa Jina Langu”

(Mafundisho na Maagano 124:40)

Maagano yanayopokelewa na ibada zinazofanywa katika mahekalu ni muhimu katika kutakasa mioyo yetu na hatima ya kuinuliwa kwa wana na mabinti za Mungu.

Katika kijisitu kitakatifu miaka 200 iliyopita, kijana Joseph Smith alimuona na kuzungumza na Mungu, Baba wa Milele, na Mwanaye, Yesu Kristo. Kutoka Kwao, Joseph alijifunza juu ya ukweli wa uhalisia wa Uungu na juu ya ufunuo endelevu wakati ono hili kutoka juu lilipoanzisha katika siku za mwisho “kipindi cha utimilifu wa nyakati.”1

Takribani miaka mitatu baadaye, katika kujibu sala ya dhati usiku wa Septemba 21, 1823, chumba cha kulala cha Joseph kilijawa na mwangaza hadi kikawa na “mwanga mkali zaidi kuliko jua la saa sita.”2 Kiumbe akamtokea kando ya kitanda chake, akamwita kijana mvulana kwa jina, na kutamka “alikuwa ni mjumbe aliyetumwa kutoka katika uwepo wa Mungu … na kwamba jina lake lilikuwa Moroni.”3 Alimwelekeza Joseph juu ya ujio wa Kitabu cha Mormoni.

Na kisha Moroni alinukuu kutoka kitabu cha Malaki katika Agano la Kale, pamoja na tofauti ndogo katika lugha iliyotumika kwenye toleo la King James:

“Tazama, nitakufunulieni Ukuhani, kwa mkono wa Eliya nabii, kabla ya kuja kwa siku ile iliyo kuu na ya kuogofya ya Bwana. …

“Naye atapanda katika mioyo ya watoto ahadi zilizofanywa kwa baba, na mioyo ya watoto itawageukia baba zao. Kama haingekuwa hivyo, dunia yote ingeliharibiwa kabisa wakati wa kuja kwake.”4

Muhimu zaidi, maelekezo ya Moroni kwa Joseph Smith juu ya misheni ya Eliya yalianzisha kazi ya hekalu na historia ya familia katika siku za mwisho na ilikuwa jambo muhimu katika kurejesha “vitu vyote, vilivyonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu.5

Ninasali kwa ajili ya usaidizi wa Roho Mtakatifu tunapojifunza pamoja kuhusu maagano, ibada, na baraka ambazo zipo kwa ajili yetu katika mahekalu ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Kurudi kwa Eliya

Ninaanza kwa kuuliza swali la msingi: Kwa nini kurudi kwa Eliya kulikuwa muhimu?

“Tunajifunza kutokana na ufunuo wa siku za mwisho kwamba Eliya alishikilia nguvu za kuunganisha za Ukuhani wa Melkizedeki”6 na “alikuwa nabii wa mwisho kufanya hivyo kabla ya wakati wa Yesu Kristo.”7

Nabii Joseph Smith alielezea: “Roho, nguvu, na wito wa Eliya ni, kwamba muwe na nguvu za kushikilia ufunguo wa … utimilifu wa Ukuhani wa Melkizedeki … ; na … kupata … ibada zote zilizo mali ya ufalme wa Mungu, hata kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, hata wale waliopo mbinguni.”8

Mamlaka haya matakatifu ya kuunganisha ni muhimu ili kwamba “lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni: na lolote utakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni”9

Joseph alifafanua zaidi: “Mungu atawezaje kuja kukiokoa kizazi hiki? Atamtuma nabii Eliya. … Eliya atafunua maagano ya kuiunganisha mioyo ya akina baba kwa watoto, na mioyo ya watoto kwa akina baba.”10

Eliya alijitokeza pamoja na Musa kwenye mlima wa kugeuka sura na kutunuku mamlaka haya kwa Petro, Yakobo, na Yohana.11 Eliya pia alijitokeza pamoja na Musa na Elia mnamo Aprili 3, 1836, katika Hekalu la Kirtland na kutunuku funguo zile za ukuhani kwa Joseph Smith na Oliver Cowdery.12

Urejesho wa mamlaka ya kuunganisha uliofanywa na Eliya mwaka 1836 ulikuwa muhimu kwa ajili ya kuuandaa ulimwengu kwa ujio wa pili wa Mwokozi na kuanzisha shauku kubwa na ya ulimwenguni kote katika utafiti wa historia ya familia.

Kubadilisha, Kugeuza, na Kuitakasa Mioyo

Neno moyo limetumika zaidi ya mara 1,000 katika vitabu vitakatifu vya Kanisa. Neno hili rahisi lakini muhimu mara nyingi huashiria hisia za ndani za mtu. Mioyo yetu—jumla ya matamanio yetu, hisia, nia, dhamira, na mitazamo yetu—hufafanua sisi ni nani na kuamua kile tutakachokuwa. Na kiini cha kazi ya Bwana ni kubadilisha, kugeuza, na kutakasa mioyo kupitia maagano ya injili na ibada za ukuhani.

Hatujengi au hatuingii kwenye mahekalu matakatifu ili tu kupata tukio la kumbukumbu binafsi au ya kifamilia. Badala yake, maagano yanayopokelewa na ibada zinazofanywa katika mahekalu ni muhimu katika kutakasa mioyo yetu na kwa ajili ya hatima ya kuinuliwa kwa wana na mabinti za Mungu.

Kupandikiza katika mioyo ya watoto ahadi zilizofanywa na mababu—hata Ibrahimu, Isaka, na Yakobo—kuigeuza mioyo ya watoto iwageukie baba zao wenyewe, kufanya utafiti wa historia ya familia, na kutekeleza ibada za uwakilishi hekaluni ni kazi ambazo hubariki watu katika pande zote mbili za pazia. Tunapojishughulisha kwa shauku katika kazi hii takatifu, tunatii amri za kumpenda na kumtumikia Mungu na majirani zetu.13 Na huduma hii isiyo ya ubinafsi inatusaidia sisi kwa hakika “Kumsikiliza Yeye!”14 na kuja kwa Mwokozi.15

Maagano na ibada takatifu zaidi za ukuhani zinapokelewa hekaluni tu—Nyumba ya Bwana. Kila kitu ambacho unajifunza na yote yanayofanyika katika hekalu yanasisitiza utukufu wa Yesu Kristo na nafasi Yake katika mpango mkuu wa furaha wa Baba wa Mbinguni.

Kutoka Ndani kwenda Nje

Rais Ezra Taft Benson alielezea mpangilio muhimu ambao Mkombozi aliuweka katika kuleta “kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.”16 Alisema: “Bwana hufanya kazi kutoka ndani kwenda nje. Ulimwengu unafanya kazi kutoka nje kwenda ndani. Ulimwengu utawaondoa watu kutoka kwenye makazi duni. Kristo huondoa makazi duni kutoka kwa watu, na kisha wao wanajiondoa wenyewe kutoka kwenye makazi duni. Ulimwengu utawabadilisha watu kwa kubadilisha mazingira yao. Kristo hubadilisha watu, ambao kisha hubadilisha mazingira yao. Ulimwengu utajenga tabia ya binadamu, bali Kristo anaweza kubadili asili ya binadamu.”17

Maagano na ibada za ukuhani ni kitovu katika mchakato huu endelevu wa kuzaliwa upya kiroho na wa badiliko; ni njia ambayo kwayo Bwana anafanya kazi na kila mmoja wetu kutoka ndani kwenda nje. Maagano ambayo yanaheshimiwa kwa dhati, yanakumbukwa daima, na kuandikwa “na Roho wa Mungu aliye hai … katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama”18 hutupa kusudi na uhakika wa baraka duniani na milele. Ibada ambazo zinapokelewa kwa kustahili na kukumbukwa daima hufungua njia za mbinguni ambazo kupitia hizo nguvu za uchamungu zinaweza kumiminika katika maisha yetu.

Hatuendi hekaluni ili kujificha au kuyatoroka maovu ya ulimwengu. Badala yake, tunakwenda hekaluni kuushinda ulimwengu wenye uovu. Tunapoalika ndani ya maisha yetu “nguvu za uchamungu”19 kwa kupokea ibada za ukuhani na kufanya na kushika maagano matakatifu, tunabarikiwa kwa nguvu zaidi ya zetu wenyewe20 ili kushinda majaribu na changamoto za mwili wenye kufa na kufanya mema na kuwa wema.

Umaarufu wa Nyumba Hii Utaenea

Hekalu la kwanza katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu lilijengwa huko Kirtland, Ohio, na kuwekwa wakfu mnamo Machi 27, 1836.

Katika ufunuo kwa Nabii Joseph Smith wiki moja baada ya kuwekwa wakfu, Bwana alitamka:

“Na acha mioyo ya watu wangu wote ifurahi, ambao, kwa nguvu zao, wameijenga nyumba hii kwa ajili ya jina langu.

“Ndiyo mioyo ya maelfu na makumi ya elfu itafurahia kwa furaha kuu kwa matokeo ya baraka zitakazomwagwa, na kwa endaomenti ambayo watumishi wangu wamepewa katika nyumba hii.

“Na umaarufu wa nyumba hii utaenea hadi nchi za kigeni; na huu ni mwanzo wa baraka ambazo zitamwagwa juu ya vichwa vya watu wangu.”21

Tafadhali kumbuka vifungu, mioyo ya maelfu na makumi ya elfu itafurahi kwa furaha kuu na umaarufu wa nyumba hii utaenea hadi nchi za kigeni. Haya yalikuwa matamko ya kushangaza mnamo Aprili 1836 wakati Kanisa lilikuwa na waumini wachache tu na hekalu moja.

Leo mwaka 2020, tuna mahekalu 168 yanayofanya kazi. Mahekalu mengine arobaini na tisa yapo kwenye ujenzi au yametangazwa kujengwa. Nyumba za Bwana zinajengwa “juu ya visiwa vya bahari”22 na katika nchi na maeneo ambayo awali yalidhaniwa na wengi yasingekuwa na hekalu.

Sherehe za endaomenti kwa sasa zinatolewa katika lugha 88 na zitapatikana katika lugha nyingine nyingi kadiri mahekalu yanavyoendelea kujengwa ili kuwabariki watoto wa Mungu. Katika miaka 15 ijayo, idadi ya lugha ambazo kwazo ibada za hekaluni zitapatikana zitaongezeka mara mbili.

Mwaka huu tutavunja ardhi na kuanza ujenzi wa mahekalu 18. Kinyume chake, ilichukua miaka 150 kujenga mahekalu 18 ya kwanza, toka kuanzishwa kwa Kanisa mwaka 1830 hadi kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Tokyo Japan na Rais Spencer W. Kimball mwaka 1980.

Mahekalu sita

Fikiria kuharakishwa kwa kazi ya hekalu ambako kumetokea wakati wa uhai wa Rais Russell M. Nelson. Wakati Rais Nelson alipozaliwa mnamo Septemba 9, 1924, Kanisa lilikuwa na mahekalu sita yaliyokuwa yanafanya kazi.

Mahekalu 26

Alipotawazwa kuwa Mtume mnamo Aprili 7, 1984, miaka 60 baadaye, mahekalu 26 yalikuwa yanafanya kazi, ongezeko la mahekalu 20 katika miaka 60.

Mahekalu 159

Wakati Rais Nelson alipoidhinishwa kama Rais wa Kanisa, mahekalu 159 yalikuwa yanafanya kazi, ongezeko la mahekalu 133 katika miaka 34 ya kipindi ambacho alihudumu kama mshiriki wa Akidi ya Kumi na Wawili.

Mahekalu yanayotumika na yaliyotangazwa

Toka amekuwa Rais wa Kanisa mnamo Januari 14, 2018, Rais Nelson ametangaza mahekalu mapya 35.

Asilimia tisini na sita ya mahekalu yaliyopo yamewekwa wakfu wakati wa uhai wa Rais Nelson; asilimia 84 yamewekwa wakfu tangu alipotawazwa kuwa Mtume.

Mara Zote Fokasi Kwenye Mambo Yaliyo Muhimu Zaidi

Kama waumini wa Kanisa la Bwana lililorejeshwa, sisi sote tunashangaa kasi ya kazi Yake katika siku za mwisho. Na mahekalu zaidi yanakuja.

Brigham Young alitoa unabii, “Ili kukamilisha kazi hii panatakiwa kuwa na si hekalu moja pekee bali maelfu, na maelfu na makumi elfu ya wanaume na wanawake watakwenda kwenye mahekalu hayo na kufanya kazi kwa ajili ya watu walioishi huko nyuma kadiri Bwana atakavyofunua.”23

Kwa uelewa, tangazo la kila hekalu jipya ni chanzo cha furaha kubwa na sababu ya kutoa shukrani kwa Bwana. Hata hivyo, fokasi yetu ya msingi inatakiwa kuwa kwenye maagano na ibada ambazo zinaweza kubadilisha mioyo yetu na kuongeza kujitoa kwetu kwa Mwokozi na siyo tu mahali au uzuri wa jengo.

Wajibu wa msingi ambao upo kwetu sisi kama waumini wa Kanisa lililorejeshwa la Bwana ni (1) “Kumsikiliza Yeye!”24 na kuifanya mioyo yetu ibadilike kupitia maagano na ibada na (2) kutimiza kwa furaha jukumu lililowekwa la kutoa baraka za hekalu kwa familia yote ya wanadamu pande zote za pazia. Kwa mwongozo na msaada wa Bwana, hakika tutatimiza kazi hizi takatifu.

Ujenzi wa Sayuni

Nabii Joseph Smith alitangaza:

“Ujenzi wa Sayuni ni kazi ambayo imewapendeza watu wa Mungu wa kila zama; ni kauli mbiu ambayo juu yake manabii, makuhani na wafalme wamekuwa wakiisubiri kwa furaha ya kipekee; wameitazamia kwa matarajio ya furaha siku hii ambayo sisi tunaishi; wakisukumwa na matarajio ya kimbingu na kwa furaha wameimba na kuandika na kutoa unabii juu ya siku yetu hii; lakini walikufa bila kuiona; … imebaki kwetu sisi kuiona, kushiriki na kusaidia kusukuma mbele utukufu wa siku za Mwisho.”25

“Ukuhani wa kimbingu utaungana na wa kidunia, ili kutimiza madhumuni hayo makuu; … kazi ambayo Mungu na malaika wameitazamia kwa furaha kwa vizazi vilivyopita; ambayo ilichochea nafsi za mapatriaki na manabii wa kale; kazi ambayo ilikusudiwa kuleta angamizo la nguvu za giza, kufanya upya dunia, utukufu wa Mungu, na wokovu wa familia ya mwanadamu.”26

Ninashuhudia kwa dhati kwamba Baba na Mwana walimtokea Joseph Smith, na Eliya alirejesha mamlaka ya kuunganisha. Maagano na ibada takatifu za hekaluni zinaweza kuimarisha na kutakasa mioyo yetu kama “Tunamsikiliza Yeye!”27 na kupokea nguvu za uchamungu katika maisha yetu. Na ninashuhudia kwamba kazi hii ya siku za mwisho itaangamiza nguvu za giza na kuleta wokovu wa familia ya mwanadamu. Juu ya kweli hizi ninashuhudia kwa furaha katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.