Hosana na Haleluya—Yesu Kristo Aliye Hai: Kiini cha Urejesho na Pasaka
Katika kipindi hiki cha hosana na haleluya, imba haleluya—kwani Atatawala milele na milele!
Wapendwa akina kaka na akina dada: kwa hosana na haleluya, tunamsherehekea Yesu Kristo aliye hai katika kipindi hiki cha mwendelezo wa Urejesho na Pasaka. Kwa upendo mkamilifu, Mwokozi wetu anatuhakikishia: “mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”1
Miaka kadhaa iliyopita, wakati Dada Gong na mimi tulipokutana na familia pendwa, binti yao mdogo, Ivy, kwa aibu alileta sanduku la fidla. Aliinua upinde wa fidla, akaukaza na kutia ulimbo. Kisha akaurudisha ulimbo ndani ya sanduku, akatabasamu, na akakaa chini. Mwanafunzi mpya, alikuwa ameshiriki yote aliyoyajua kuhusu fidla. Sasa, miaka kadhaa baadaye, Ivy anapiga fidla vizuri sana.
Katika kipindi hiki cha maisha ya kufa, sisi sote kidogo ni kama Ivy na fidla yake. Tunaanzia mwanzo. Kwa mazoezi na uvumilivu, tunakua na kuendelea. Kadiri muda unavyopita, uhuru wa maadili na uzoefu wa kibinadamu hutusaidia sisi kuwa zaidi kama Mwokozi wetu tunapofanya kazi pamoja Naye katika shamba Lake la mizabibu2 na kufuata njia Yake ya agano.
Sherehe za kumbukumbu, ikiwemo hii ya miaka mia mbili, zinaonesha mpangilio wa urejesho.3 Katika kusherehekea mwendelezo wa Urejesho wa injili ya Yesu Kristo, pia tunajiandaa kwa Pasaka. Katika yote, tunafurahia kurudi kwa Yesu Kristo. Anaishi—siyo tu hapo kale, bali sasa; si kwa wachache, lakini kwa wote. Alikuja na anakuja kuwaponya waliovunjika mioyo, kuwakomboa mateka, kuwaponya vipofu, na kuwaweka huru wale walioumia.4 Hao ni kila mmoja wetu. Ahadi zake za ukombozi zinatumika, bila kujali mambo yetu ya zamani, ya sasa, au wasiwasi wetu kwa ajili ya baadaye.
Kesho ni Jumapili ya Mitende. Kwa utamaduni, mitende ni ishara takatifu ya kuelezea shangwe katika Bwana wetu, kama ilivyo katika Kristo Kuingia kwa shangwe Yerusalemu, ambapo “watu wengi … walichukua matawi ya mitende, na wakatoka kwenda kumlaki.”5 (Unaweza kuvutiwa kujua uhalisia wa mchoro huu wa Harry Anderson unaoning’inia kwenye ofisi ya Rais Russell M. Nelson, nyuma tu ya meza yake.) Katika kitabu cha Ufunuo, wale wanaomsifu Mungu na Mwana Kondoo wanafanya hivyo kwa “kuvaa majoho meupe, na mitende mikononi mwao.”6 Pamoja na “majoho ya wema” na “mataji ya utukufu,” mitende imejumuishwa katika sala ya kuweka wakfu Hekalu la Kirtland.7
Kwa kweli, umuhimu wa Jumapili ya Mitende unakwenda zaidi ya umati kumpokea Yesu kwa mitende. Siku ya Jumapili ya Mitende, Yesu aliingia Yerusalemu kwa njia inayotambuliwa na waaminifu kama utimilifu wa unabii. Kama Zekaria8 na Mtunga Zaburi walivyotabiri kinabii, Bwana wetu aliingia Yerusalemu akipanda mwana punda huku umati wa watu wakipaaza sauti, “Hosana kwa aliye juu zaidi.”9 Hosana maana yake “okoa sasa.”10 Kisha, kama sasa, tunafurahia, “Abarikiwe yule ajaye katika jina la Bwana.”11
Wiki moja baada ya Jumapili ya Mitende ni Jumapili ya Pasaka. Rais Russell M. Nelson anafundisha kwamba Yesu Kristo “alikuja kulipa deni ambalo si Lake kwa sababu tulikuwa na deni ambalo tusingeweza kulipa.”12 Hakika, kupitia Upatanisho wa Kristo, watoto wote wa Mungu “wanaweza kuokolewa, kwa kutii sheria na ibada za Injili.”13 Wakati wa Pasaka, tunaimba haleluya. Haleluya maana yake “usifiwe wewe Bwana Yehova.”14 “Kibwagizo cha Haleluya” katika Handel Masiya ni tamko linalopendwa la Pasaka kwamba Yeye ni “Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.”15
Matukio matakatifu kati ya Jumapili ya Mitende na Jumapili ya Pasaka ni hadithi ya hosana na haleluya. Hosana ni ombi letu kwa Mungu kuokoa. Haleluya inatoa sifa yetu kwa Bwana kwa tumaini la wokovu na kuinuliwa. Katika hosana na haleluya tunamtambua Yesu Kristo aliye hai kama kiini cha Pasaka na urejesho wa siku za mwisho.
Urejesho wa siku za mwisho huanza na theofani—mwonekano halisi wa Mungu Baba na Mwana Wake, Yesu Kristo, kwa nabii kijana Joseph Smith. Nabii Joseph alisema, “Ungeweza kutazama mbinguni dakika tano, ungejua zaidi ya unavyojua kwa kusoma yote ambayo yamewahi kuandikwa juu ya mada hiyo.”16 Kwa sababu mbingu zimefunguka tena, tunajua na “kuamini katika Mungu, Baba wa Milele, na katika Mwanae, Yesu Kristo, na katika Roho Mtakatifu”17—Uungu mtakatifu.
Siku ya Jumapili ya Pasaka, Aprili 3, 1836, mwanzoni mwa miaka ya Urejesho, Yesu Kristo aliye hai alionekana wakati wa kuweka wakfu Hekalu la Kirtland. Wale waliomuona Yeye huko walimshuhudia katika tofauti zinazoambatana na moto na maji: “Macho yake yalikuwa kama mwale wa moto; nywele za kichwa chake zilikuwa nyeupe kama theluji safi; uso wake ulinga’ra kupita mng’aro wa jua; na sauti yake ilikuwa kama sauti ya maji mengi yakimbiayo, hata sauti ya Yehova.”18
Kwenye tukio hilo, Mwokozi wetu alitangaza, “Mimi ni mwanzo na mwisho; Mimi ni yeye aliye hai, Mimi ni yule aliyeuawa; Mimi ni Mwombezi wenu kwa Baba.”19 Tena, tofauti zinazoambatana—mwanzo na mwisho, hai na kuuwawa. Yeye ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho,20 mwanzilishi na mtimizaji wa imani yetu.21
Baada ya kutokea kwa Yesu Kristo, Musa, Elia, na Eliya pia walikuja. Kwa mwongozo mtakatifu, manabii hawa wakuu wa kale walirejesha funguo na mamlaka ya ukuhani. Kwa hivyo, “funguo za kipindi hiki cha nyakati zimewekwa”22 ndani ya Kanisa Lake lililorejeshwa kuwabariki watoto wote wa Mungu.
Kuja kwa Eliya katika Hekalu la Kirtland pia kulitimiza unabii wa Malaki wa Agano la Kale kwamba Eliya atarudi “kabla ya kuja kwa siku ile kuu na ya kutisha ya Bwana.”23 Kwa kufanya hivyo, muonekano wa Eliya uliendana, ingawa sio kwa bahati mbaya, na msimu wa Pasaka ya Kiyahudi, ambapo mila hiyo hutegemea kurudi kwa Eliya kwa heshima.
Familia nyingi za Kiyahudi zilizomcha Mungu zilitenga sehemu ya Eliya kwenye meza yao ya Pasaka. Wengi hujaza kikombe hadi juu ili kumwalika na kumkaribisha. Na wengine, wakati wa Sherehe ya Jadi ya Pasaka, wanamtuma mtoto mlangoni, wakati mwingine waliacha mlango wazi kidogo ili kuona kama Eliya yuko nje akisubiri kualikwa.24
Katika utimizwaji wa unabii na kama sehemu ya ahadi ya kurejesha vitu vyote,25 Eliya alikuja kama ilivyoahidiwa, wakati wa Pasaka na baada ya Pasaka. Alileta mamlaka ya kuunganisha ya kuzifunga familia duniani na mbinguni. Kama Moroni alivyomfundisha Nabii Joseph, Eliya “atapanda katika mioyo ya watoto ahadi zilizofanywa kwa baba, na mioyo ya watoto itawageukia baba zao. Kama si hivyo,” Moroni anaendelea, “dunia yote ingeliangamia kabisa wakati wa kuja Kwake [Bwana].”26 Roho ya Eliya, udhihirisho wa Roho Mtakatifu, inatuvuta kwa vizazi vyetu—vya zamani, vya sasa, na vijavyo—katika koo zetu, historia, na huduma ya hekalu.
Acha tukumbuke kwa ufupi pia maana ya Pasaka. Pasaka inakumbuka ukombozi wa wana wa Israeli kutoka miaka 400 ya utumwa. Kitabu cha Kutoka kinasimulia jinsi ukombozi huu ulivyokuja baada ya mapigo ya vyura, chawa, inzi, vifo vya ng’ombe, majipu, upele, mvua ya mawe na moto, nzige na giza nene. Pigo la mwisho lilitishia kifo cha mzaliwa wa kwanza katika nchi, lakini si katika nyumba za Israeli ikiwa—ikiwa kaya hizo zingeweka damu ya mwanakondoo asiye na lawama kwenye miimo ya milango yao.27
Malaika wa kifo alipita karibu na nyumba zilizowekwa alama ya damu ya kondoo wa mfano.28 Kupita huko, au kuwapita, kunawakilisha Yesu Kristo hatimaye kushinda kifo. Kwa kweli, damu ya upatanisho ya Mwanakondoo wa Mungu inampa Mchungaji wetu Mwema nguvu ya kukusanya watu Wake katika maeneo yote na hali zote katika usalama wa zizi Lake kwenye pande zote za pazia.
Kwa kweli, Kitabu cha Mormoni kinaelezea “nguvu na ufufuko wa Kristo”29—kiini cha Pasaka—katika rejesho mbili.
Kwanza, ufufuo unajumuisha urejesho wa kimwili wa “umbo sahihi na kamilifu”; “kila sehemu na kiungo,” “hata nywele ya kichwa haitapotea.”30 Ahadi hii inatoa tumaini kwa wale waliopoteza viungo; wale waliopeteza uwezo wa kuona, kusikia, au kutembea; au wale wanaosumbuka na tatizo la kimwili, ugonjwa wa akili, au uwezo mwingine hafifu. Anatutafuta sisi. Anatufanya tuwe wazima.
Ahadi ya pili ya Pasaka na Upatanisho wa Bwana wetu ni kwamba, kiroho, “vitu vyote vitarudishwa kwenye hali yake ya kawaida.”31 Urejesho huu wa kiroho, unaangazia kazi zetu na matamanio yetu. Kama vile mkate katika maji,32 unarejesha “kile kilicho chema,” “adilifu,” “haki,” na “chenye rehema.”33 Haishangazi kwa nabii Alma kutumia neno rejesha mara 2234 anapotutaka sisi “kutenda haki, kuhukumu kwa haki, na kutenda mema daima.”35
Kwa sababu “Mungu mwenyewe alimwaga damu kwa dhambi za ulimwengu,”36 Upatanisho wa Bwana unaweza kurejesha si tu kilichokuwepo, bali pia kile kinachoweza kuwa. Kwa sababu anajua maumivu yetu, mateso, magonjwa, “majaribu yetu ya kila aina,”37 Anaweza, kwa rehema, kutusaidia kulingana na unyonge wetu.38 Kwa sababu Mungu ni “mkamilifu, Mungu wa haki, na pia Mungu wa rehema,” mpango wa rehema unaweza “kutimiza matakwa ya haki.”39 Tunatubu na kutenda yote tunayoweza. Anatuzingira milele “katika mikono ya upendo wake.”40
Leo tunasherehekea urejesho na ufufuko. Pamoja nanyi, ninafurahia katika Urejesho unaoendelea wa utimilifu wa injili ya Yesu Kristo. Kama ulivyoanza miaka mia mbili katika majira haya ya kuchipua, nuru na ufunuo vinaendelea kutokea kupitia nabii aliye hai wa Bwana na Kanisa Lake linaloitwa kwa jina Lake—Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho—na kupitia ufunuo binafsi na msukumo na zawadi kuu ya Roho Mtakatifu.
Pamoja nanyi, msimu huu wa Pasaka, ninatoa ushuhuda wa Mungu, Baba yetu wa Milele, na Mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo aliye hai. Wanadamu walisulubiwa kikatili na baadaye wakafufuliwa. Lakini Yesu Kristo aliye hai pekee katika hali Yake kamilifu ya ufufuko bado ana alama za vidonda mikononi, miguuni, na ubavuni mwake. Ni Yeye tu Anayeweza kusema, “Nimewachora kwenye viganja vya mikono yangu.”41 Ni yeye tu Anayeweza kusema: “Mimi ni yule aliyeinuliwa. Mimi ni Yesu aliyesulibiwa. Mimi ni Mwana wa Mungu.”42
Kama Ivy mdogo na fidla yake, sisi kwa namna fulani bado tunaanza. Kwa kweli, “jicho halijapata kuona wala sikio kusikia, wala havijawahi kuingia kwenye moyo wa mwanadamu, vile vitu Mungu ameviandaa kwa wale wanaompenda.”43 Katika nyakati hizi, tunaweza kujifunza mengi juu ya wema wa Mungu na uwezekano wetu mtakatifu kwa upendo wa Mungu kukua ndani yetu pale tunapomtafuta Yeye na kumfikia kila mmoja. Katika njia mpya na maeneo mapya, tunaweza kufanya na kuwa, mstari juu ya mstari, ukarimu juu ya ukarimu, kama watu binafsi na kwa pamoja.
Wapenda akina kaka na akina dada kila mahali, tunapokutana na kujifunza pamoja, imani na wema wenu unanijaza kwa hisia ya ujasiri na shukrani. Ushuhuda wenu na safari ya kiinjili vinakuza ushuhuda wangu na safari yangu ya kiinjili. Kujali kwenu na furaha yenu, upendo wenu kwa jamii yetu ya Watakatifu na nyumba ya Mungu, na ufahamu wenu wa kweli iliyorejeshwa na nuru huongeza utimilifu wangu wa injili iliyorejeshwa, na Yesu Kristo aliye hai akiwa kiini chake. Kwa pamoja tunaamini, “kwenye Mawingu na Jua, Bwana, Kaa Nami.”44 Kwa pamoja tunajua, katikati ya mizigo na majukumu, tunaweza kuhesabu baraka zetu nyingi.45 Katika mambo ya kila siku na mambo madogo na rahisi, tunaweza kuona mambo makubwa yakitokea katika maisha yetu.46
“Na itakuwa kwamba wenye haki watakusanywa kutoka miongoni mwa mataifa yote, nao watakuja Sayuni, wakiimba nyimbo za shangwe isiyo na mwisho.”47 Katika kipindi hiki cha hosana na haleluya, imba haleluya—kwani Atatawala milele na milele! Paza sauti ya hosana, kwa Mungu na Mwanakondoo! Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.