Mkutano Mkuu
Sala za Imani
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Sala za Imani

Tunaposali kwa imani, tutakuwa sehemu muhimu katika kazi ya Bwana wakati Yeye anapoandaa ulimwengu kwa Ujio Wake wa Pili.

Sala ya mzee Maynes mwanzoni mwa kikao hiki cha kwanza cha mkutano mkuu inajibiwa. Msukumo umekuja kwetu kupitia jumbe nzuri na muziki mzuri. Ahadi ya Rais Russell M. Nelson kwamba mkutano huu utakuwa wa kukumbukwa tayari imeanza kutimia.

Rais Nelson ameteua mwaka huu kama “kipindi cha kumbukumbu ya miaka 200 tangu Mungu Baba na Mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo, walipomtokea Joseph Smith katika ono.” Rais Nelson alitualika kuweka mpango binafsi wa kujiandaa wenyewe kwa mkutano huu wa kihistoria, ambao kumbukumbu yake alisema itakuwa “sehemu ya kiunganishi katika historia ya Kanisa, na sehemu yako ni muhimu.”1

Kama mimi, labda ulisikia ujumbe wake na ukajiuliza, “Je! Sehemu yangu ni muhimu kwa njia ipi? Labda ulisoma na kusali kujua matukio ya Urejesho. Labda, zaidi kuliko hapo awali, ulisoma simulizi za nyakati hizo chache wakati Mungu Baba alipomtambulisha Mwanaye Mpendwa. Labda ulisoma mifano ya nyakati Mwokozi alipozungumza na watoto wa Baba yetu wa Mbingu. Ninajua nilifanya vitu hivyo vyote na zaidi.

Nilipata marejeleo katika kusoma kwangu ukuhani wa Mungu na ufunguzi wa vipindi vya maongozi ya Mungu. Nilinyenyekezwa wakati nilipogundua kwamba maandalizi yangu kwa ajili ya mkutano huu yalikuwa ni kiunganishi katika historia yangu binafsi. Nilihisi mabadiliko moyoni mwangu. Nilihisi shukrani mpya. Nilihisi kujawa na furaha kwa matarajio ya kualikwa kushiriki katika sherehe hii ya Urejesho unaoendelea.

Nadhani kwamba wengine wanahisi, kwa sababu ya maandalizi ya uangalifu, furaha zaidi, matumaini zaidi, na wameazimia zaidi kuhudumu kwa uwezo wowote unaohitajika na Bwana.

Matukio ya kustaajabisha ambayo tunayaheshimu yalikuwa ni mwanzo wa kipindi cha mwisho kilichotabiriwa, ambapo Bwana anaandaa Kanisa Lake na watu Wake, wale wanaobeba jina Lake, ili kumpokea Yeye. Kama sehemu ya maandalizi yetu kwa ujio Wake, Atamwinua kila mmoja wetu ili tuweze kuinuka juu ya changamoto na fursa za kiroho tofauti na vyoyote vile ilivyowahi kuonekana kwenye historia ya ulimwengu huu.

Mnamo Septemba 1840, Nabii Joseph Smith na washauri wake katika Urais wa Kwanza walitangaza yafuatayo: “Kazi ya Bwana katika siku hizi za mwisho, ni jambo kubwa na pana lililozidi uelewa wa kibinadamu. Utukufu wake hauelezeki, na ukuu wake hauwezi kufikika. Ni mada ambayo imesisimua nafsi za manabii na wenye haki tangu kuumbwa kwa ulimwengu kupitia vizazi hadi sasa; na hakika ni wakati wa utimilifu wa nyakati, wakati vitu vyote vilivyo katika Kristo Yesu, iwe mbinguni au duniani, vitakusanywa pamoja Kwake, na wakati vitu vyote vitakaporejeshwa, kama ilivyosemwa na manabii wote watakatifu tangu ulimwengu kuanza; kwani katika hiyo kutakuwa na utimizwaji mtukufu wa ahadi zilizotolewa kwa mababu, wakati udhihirisho wa nguvu za aliye Juu Zaidi zitakuwa kuu, zenye utukufu, na za kushangaza.”

Waliendelea kusema: “Tunajisikia nia ya kusonga mbele na kuunganisha nguvu zetu kwenye kujenga Ufalme, na kuanzisha Ukuhani katika ukamilifu na utukufu wake. Kazi ambayo inastahili kutekelezwa katika siku za mwisho ni yenye umuhimu mkubwa, na itahitaji kuweka katika vitendo nguvu, ustadi, vipaji, na uwezo wa Watakatifu, ili iweze kusonga mbele kwa utukufu huo na ukuu ulioelezewa na nabii [Danieli] [ona Danieli 2:34–35, 44–45]; na kwa hivyo itahitaji umakini wa Watakatifu, ili kukamilisha kazi za ukuu na utukufu kama hiyo.”2

Maelezo mengi ya yale tutakayofanya na lini tutayafanyia kazi katika Urejesho unaojifunua bado hayajafunuliwa. Walakini Urais wa Kwanza hata katika siku zile za mwanzo ulijua upana na kina cha kazi ambayo Bwana ameweka mbele yetu. Hii ni mifano michache tu ya kile tunachojua kitatokea:

Kupitia Watakatifu Wake, Bwana atatoa zawadi ya injili Yake “kwa kila taifa, jamaa, lugha, na watu.”3 Teknolojia na miujiza vitaendelea kuchukua nafasi—kama vile itakavyokuwa kwa “wavuvi wa watu”4 ambao hutumikia kwa nguvu na imani inayoongezeka.

Sisi kama watu tutakuwa na umoja zaidi wakati wa migogoro inayoongezeka. Tutakusanywa kwa nguvu ya kiroho ya vikundi na familia zilizojazwa na nuru ya injili.

Hata ulimwengu usioamini utalitambua Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na kutambua nguvu ya Mungu juu yake. Wafuasi waaminifu na hodari bila woga, kwa unyenyekevu, na kwa uwazi watajichukulia wenyewe jina la Kristo katika maisha yao ya kila siku.

Basi, ni vipi, kila mmoja wetu anaweza kushiriki katika kazi ya ukuu na utukufu kama hii? Rais Nelson ametufundisha jinsi ya kukua katika nguvu za kiroho. Tunapochukua toba kama fursa ya kufurahisha kwa sababu ya imani yetu inayokua kwamba Yesu ndiye Kristo, tunapoelewa na kuamini kuwa Baba wa Mbinguni anasikia kila sala yetu, tunapojitahidi kutii na kuishi kulingana na amri, tunakua katika uwezo wetu ya kupokea ufunuo endelevu. Roho Mtakatifu anaweza kuwa mwenzi wetu daima. Hisia ya nuru itakaa nasi hata kama ulimwengu unaotuzunguka unapozidi kuwa na kiza.

Joseph Smith ni mfano wa jinsi ya kukua katika uwezo huo wa kiroho. Alituonesha kwamba sala ya imani ndio ufunguo wa ufunuo kutoka kwa Mungu. Alisali kwa imani, akiamini kwamba Mungu Baba angejibu sala yake. Alisali kwa imani, akiamini kwamba kupitia Yesu Kristo pekee angeweza kuachiliwa kutoka kwenye hatia aliyohisi kwa sababu ya dhambi zake. Na alisali kwa imani, akiamini kwamba alihitaji kupata Kanisa la kweli la Yesu Kristo ili kupata msamaha huo.

Katika huduma yake yote ya unabii, Joseph Smith alitumia sala za imani ili kupata ufunuo unaoendelea. Tunapokabiliwa na changamoto za leo na zile zitakazokuja, sisi pia tutahitaji kufanyia mazoezi mpangilio sawa na huo. Rais Brigham Young alisema, “Sijui njia nyingine yoyote kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho kuliko kila pumzi kuwa ombi kwa Mungu ili awaongoze na kuwaelekeza watu wake.”5

Maneno haya kutoka kwenye sala ya sakramenti yanapaswa kuwa maelezo ya maisha yetu ya kila siku: “kumkumbuka Yeye daima.” “Yeye” ina maana Yesu Kristo. Maneno yanayofuata, “na kushika amri zake,” yanapendekeza kile inachomaanisha kwetu kwa kumkumbuka Yeye.6 Tunapomkumbuka Yesu Kristo kila wakati, tunaweza kuuliza katika sala ya kimya kimya, “Je, Yeye angetaka mimi nifanye nini?”

Sala kama hii, iliyotolewa kwa imani katika Yesu Kristo, ilikaribisha kipindi hiki cha mwisho cha maongozi ya Mungu. Na itakuwa kwenye kiini cha kila sehemu ya mmoja wetu ambayo ataifanya katika mwendelezo wa kujifunua kwake. Nimegundua, kama ilivyo kwenu, mifano mizuri ya sala ya namna hiyo.

Kwanza ni Joseph Smith. Aliuliza kwa imani kama ya mtoto kile ambacho Bwana angetaka afanye. Jibu lake lilibadilisha historia ya ulimwengu.

Kwangu, somo muhimu zaidi linatokana na mwitikio wa Joseph dhidi ya mashambulizi ya Shetani wakati Joseph alipopiga magoti kusali.

Ninajua kutokana na uzoefu kwamba Shetani na watumishi wake wanajaribu kutufanya tuhisi kwamba hatupaswi kusali. Wakati Joseph Smith alipotumia nguvu zake zote kumwomba Mungu amwokoe kutoka kwa nguvu iliyojaribu kumfunga, sala yake kwa ajili ya msaada ilijibiwa na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo walitokea.

Jaribio la Shetani la kuharibu mwanzo wa Urejesho lilikuwa kali sana kwa sababu sala ya Joseph ilikuwa muhimu sana. Wewe na mimi tutakuwa na sehemu ndogo ndogo za kufanya katika Urejesho unaoendelea. Bado adui wa Urejesho atajaribu kutuzuia tusisali. Mfano wa imani ya Joseph na azimio lake vinaweza kututia nguvu katika azimio letu. Hii ni moja ya sababu nyingi za kwa nini sala zangu ni pamoja na kumshukuru Baba wa Mbinguni kwa ajili ya Nabii Joseph.

Enoshi kwenye Kitabu cha Mormoni ni mfano mwingine wa sala yangu ya imani ninapojaribu kufanya sehemu yangu katika Urejesho unaoendelea. Sehemu yoyote ile utakayokuwa, ungeweza kumchukua yeye kama mshauri wako binafsi.

Kama Joseph, Enoshi alisali kwa imani. Alielezea uzoefu wake kwa njia hii:

“Na nafsi yangu ikapata njaa; na nikapiga magoti mbele ya Muumba wangu, na nikamlilia kwa sala kuu na nikamsihi kwa nafsi yangu; na kwa siku nzima nikamlilia; ndiyo, na wakati usiku ulipofika bado nilipaza sauti yangu na hata ikafika mbinguni.

“Na sauti ikanijia, ikisema: Enoshi, umesamehewa dhambi zako, na wewe utabarikiwa.

“Na mimi, Enoshi, nilijua kwamba Mungu hawezi kusema uwongo; kwa hivyo, hatia yangu iliondolewa mbali.

“Na nikasema: Bwana, je, inafanywa vipi?

“Na akaniambia: Kwa sababu ya imani yako katika Kristo, ambaye wewe hujamwona kamwe wala kumsikia. Na miaka mingi itapita kabla yeye hajajidhihirisha katika mwili; kwa hivyo, nenda, imani yako imekufanya mkamilifu.”7

Somo ambalo limenibariki mimi lipo katika maneno haya: “Kwa sababu ya imani yako katika Kristo, ambaye wewe hujamwona kamwe wala kumsikia.”

Joseph alikuwa na imani katika Kristo kwenda kwenye msitu na pia kusali kwa ajili ya kuondolewa nguvu za Shetani. Alikuwa bado hajamwona Baba na Mwana, lakini alisali kwa imani na kwa nguvu zote za moyo wake.

Uzoefu wa Enoshi umenifundisha somo hilo la thamani kuu. Wakati ninaposali kwa imani, ninaye Mwokozi kama mtetezi wangu kwa Baba na ninaweza kuhisi kwamba sala zangu zinafika mbinguni. Majibu yanakuja. Baraka zinapokelewa. Kuna amani na furaha hata katika nyakati ngumu.

Nakumbuka wakati, kama mshiriki mpya zaidi wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, nilipiga magoti kwa ajili ya sala nikiwa na Mzee David B. Haight. Alikuwa na umri nilionao sasa, na changamoto ambazo mimi mwenyewe ninazipitia sasa. Ninakumbuka sauti yake wakati aliposali. Sikufumbua macho yangu kuangalia, lakini ilisikika kwangu kama alikuwa akitabasamu. Aliongea na Baba wa Mbinguni kwa sauti ya furaha

Ninaweza kusikia akilini mwangu furaha yake wakati aliposema, “Katika jina la Yesu Kristo.” Ilionekana kwangu mimi kana kwamba Mzee Haight alihisi Mwokozi alikuwa akithibitisha wakati ule ujumbe aliokuwa akisali kwa Baba. Na nilikuwa na uhakika ungepokelewa kwa tabasamu.

Uwezo wetu wa kutoa mchango wetu muhimu katika Urejesho mzuri unaoendelea utaongezeka wakati tunapokua katika imani yetu kwa Yesu Kristo kama Mwokozi wetu na Baba yetu wa Mbingu kama Baba yetu mwenye upendo. Tunaposali kwa imani, tutakuwa sehemu muhimu katika kazi ya Bwana wakati Yeye anapoandaa ulimwengu kwa Ujio Wake wa Pili. Ninasali kwamba sote tuweze kupata furaha katika kufanya kazi ambayo Yeye anatualika kila mmoja wetu kuitekeleza.

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo yu hai. Hili ni Kanisa Lake na ufalme Wake hapa duniani. Joseph Smith ni nabii wa Urejesho. Rais Russell M. Nelson ni nabii wa Bwana duniani leo. Anashikilia funguo zote za ukuhani katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha