Mkutano Mkuu
Kushiriki Ujumbe wa Urejesho na Ufufuko
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Kushiriki Ujumbe wa Urejesho na Ufufuko

Urejesho ni kwa ajili ya Ulimwengu, na ujumbe wake ni muhimu hasa hivi leo.

Katika kipindi chote cha mkutano huu mkuu tumezungumza na kuimba kwa furaha juu ya utimizwaji wa unabii uliotabiriwa hapo zamani “kufanywa upya vitu vyote,”1 kuhusu kuvileta “pamoja vitu vyote katika Kristo,”2 kuhusu kurejeshwa kwa utimilifu wa injili, ukuhani, na Kanisa la Yesu Kristo duniani, ambayo yote tunayapata katika kichwa cha habari “Urejesho.”

Lakini Urejesho si tu kwa ajili yetu wale ambao tunaufurahia leo hii. Ufunuo wa Ono la Kwanza haukuwa kwa ajili ya Joseph Smith peke yake bali ulitolewa kama nuru na ukweli kwa yeyote “aliyepungukiwa hekima.”3 Kitabu cha Mormoni ni kwa ajili ya wanadamu. Ibada za ukuhani za wokovu na kuinuliwa ziliandaliwa kwa ajili ya kila mmoja, ikijumuisha wale ambao hawaishi tena katika mwili. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa siku za mwisho na baraka zake zimekusudiwa kwa ajili ya wote wanaozihitaji. Kipawa cha Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya kila mmoja. Urejesho ni kwa ajili ya Ulimwengu, na ujumbe wake ni muhimu hasa hivi leo.

“Kwa hivyo, ni muhimu sana kuwajulisha wakazi wa dunia kuhusu vitu hivi, ili wajue hakuna binadamu anayeweza kuishi karibu na Mungu, bila fadhili, na rehema, na neema za Masiya Mtakatifu, ambaye anatoa maisha yake katika mwili, na kuyachukua tena kwa uwezo wa Roho, ili alete ufufuo wa wafu.”4

Tangu siku ambayo kaka yake Nabii, Samuel Smith, alipojaza mkoba wake kwa nakala mpya zilizochapishwa za Kitabu cha Mormoni na kutembea kwenda kushiriki maandiko mapya, Watakatifu wamefanya kazi kwa nguvu bila kukoma “kufanya mambo haya yote yajulikane kwa wakazi wa dunia.”

Mnamo 1920, Mzee David O. McKay wa Akidi ya Mitume kumi na wawili wakati huo alianza ziara ya mwaka mzima kwenye misheni za Kanisa. Mnamo Mei 1921, alikuwa amesimama katika sehemu ndogo ya makaburi katika Fagali’i, Samoa, mbele ya makaburi yaliyotunzwa vizuri ya watoto wadogo watatu, binti na wana wawili wa Thomas na Sarah Hilton. Wadogo hawa—mkubwa akiwa wa miaka miwili—walifariki wakati Thomas na Sarah wakihudumu kama wamisionari vijana wanandoa mwishoni mwa miaka ya 1800.

Kabla ya kuondoka Utah, Mzee McKay alimuahidi Sarah, kwa sasa ni mjane, kwamba angetembelea makaburi ya watoto wake huko Samoa kwani Sara hakuwahi kurudi huko. Mzee McKay alimuandikia barua, “Watoto wako wadogo watatu, Dada Hilton, katika ukimya wenye ufasaha … wanaendeleza kazi yako nzuri ya umisionari uliyoianza karibu miaka thelathini iliyopita.” Baadaye aliongeza ubeti alioutunga mwenyewe:

Kwa mikono ya upendo macho yao ya kufa yalifumbwa,

Kwa mikono ya upendo miguu yao midogo iliwekwa vizuri,

Kwa mikono ya ugenini makaburi yao yalirembeshwa,

Kwa wageni waliheshimiwa, na wageni waliomboleza.5

Hadithi hii ni mojawapo ya maelfu, mamia kwa maelfu, inayoongelea muda, mali, na maisha yaliyotolewa dhabihu zaidi ya miaka 200 ilyopita ili kushiriki ujumbe wa Urejesho. Hamasa yetu kufikia kila taifa, koo, ndimi, na watu haizuiliki leo, kama inavyodhihirishwa kwa makumi elfu ya vijana wa kiume, wa kike, na wanandoa ambao kwa sasa wanatumikia miito yao kama wamisionari; kwa waumini wa Kanisa kwa ujumla, wanaoitikia wito wa Filipo wa kuja na kuona;6 na kwa mamilioni ya dola yanayotumika kila mwaka kuidhinisha juhudi hii duniani kote.

Wakati mialiko yetu si ya kulazimisha, tunatumaini watu wataiona ni ya ulazima. Kwa hilo kufanyika, ninaamini angalau vitu viitatu vinahitajika: kwanza, upendo wako; pili, mfano wako; na tatu, utumiaji wako wa Kitabu cha Mormoni.

Mialiko yetu haiwezi kuwa jambo la matakwa binafsi; bali, lazima iwe kielelezo cha upendo usio na choyo.7 Upendo huu, ujulikanao kama hisani, upendo msafi wa Kristo, ni wetu kwa wanaouomba. Tunaalikwa, hata kuamriwa “kuomba kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba [sisi] tujazwe na upendo huu.”8

Kama mfano, nashiriki uzoefu ulioelezwa na Dada Lanett Ho Ching, ambaye kwa sasa anahudumu na mume wake, Rais Francis Ho Ching, anayesimamia Misheni ya Samoa Apia. Dada Ho Ching anaeleza:

“Miaka mingi iliyopita, familia yetu changa ilihamia katika nyumba ndogo huko Laie, Hawaii. Banda la gari la nyumba yetu lilikuwa limegeuzwa kuwa chumba cha studio, ambamo mwanaume aliyeitwa Jonathan aliishi. Jonathan aliwahi kuwa jirani yetu sehemu nyingine. Tukihisi kuwa haikuwa bahati mbaya kwamba Bwana ametuweka pamoja, tuliamua kuwa wazi kuhusu shughuli zetu na uumini wetu Kanisani. Jonathan alifurahia urafiki wetu na alipenda kutumia muda kuwa na familia yetu. Alipenda kujifunza kuhusu injilli, ila hakupendelea kuja Kanisani.

“Kwa muda, Jonathan alipata jina la utani ‘Mjomba Jonathan’ kwa watoto wetu. Kadiri familia yetu ilivyoendelea kukua, ndivyo kuvutiwa kwa Jonathan kulivyokuwa katika matukio yetu. Mialiko yetu kwenye shughuli za sikukuu, siku za kuzaliwa, shughuli za shule, na shughuli za Kanisa zilipelekea kwenye jioni ya familia na kwenye ubatizo wa watoto.

“Siku moja nilipokea simu kutoka kwa Jonathan. Alihitaji msaada. Alikuwa anaumwa kisukari na alikuwa amepata maambukizi makubwa ya mguu ambao ulihitajika kukatwa. Familia yetu na waumini majirani wa kata tulikuwa naye kwenye kipindi hicho kigumu. Tulibadilishana kumtembelea hosipitalini, na baraka za ukuhani zilitolewa. Wakati Jonathan akiwa anaendelea kuimarika, kwa msaada wa akina dada wa Muungano wa Usaidizi wa Akina mama, tulisafisha makazi yake. Akina kaka wa ukuhani walijenga njia ya mteremko kuelekea mlango wake na vyuma vya kushikilia bafuni kwake. Wakati Jonathan aliporudi nyumbani, alizidiwa kwa hisia.

“Jonathan alianza mafundisho ya wamisionari tena. Wiki moja kabla ya Mwaka Mpya, aliniita na kuniuliza, ‘Utafanya nini jioni kabla ya Mwaka Mpya?’ Nilimkumbusha kuhusu sherehe yetu ya mwaka. Badala yake, alijibu, ‘Nataka uje kwenye ubatizo wangu! Nataka kuanza mwaka mpya huu vizuri.’ Baada ya miaka 20 ya ‘njoo uone,’ ‘njoo usaidie,’ na ‘njoo ukae,’ nafsi hii ya thamani ilikuwa tayari kubatizwa.

“Mwaka 2018, tulipoitwa kuwa rais wa misheni na mwenza wake, afya ya Jonathan ilikuwa ikidhoofika. Tulimwomba abaki imara akisubiri kurejea kwetu. Aliendelea karibu mwaka mzima, lakini Bwana alikuwa anamuandaa kurudi nyumbani. Alifariki kwa amani mnamo Aprili 2019. Mabinti zangu walihudhuria mazishi ya ‘Mjomba Jonathan’ na kuimba wimbo ule tulioimba siku ya ubatizo wake.”

Natambulisha hitaji la pili kwa ajili ya kushiriki ujumbe wa Urejesho kikamilifu kwa swali hili: ni nini ambacho kitafanya mwaliko wako uvutie kwa mtu? Je si wewe, mfano wa maisha yako? Wengi waliosikia na kupokea ujumbe wa Urejesho mwanzo walivutiwa na kile walichoona kwa muumini au waumini wa Kanisa la Yesu Kristo. Yawezekana ni kutokana na jinsi walivyowatendea wengine, mambo ambayo walisema au hawakusema, uthabiti waliouonesha kwenye nyakati ngumu, ama tu mwonekano wao.9

Iwe ni sababu yoyote ile, hatuwezi kuepuka ukweli kwamba tunahitaji kuelewa na kuishi misingi ya injili ya urejesho vizuri kadiri tuwezavyo kwa ajili ya mialiko yetu kuwa ya kuvutia. Ni jambo linalorejelewa mara kwa mara leo kama uhalisia. Kama upendo wa Kristo upo ndani yetu, wengine watajua upendo wetu kwao ni wa kweli. Kama nuru ya Roho Mtakatifu ina mwako ndani yetu, itaamsha Nuru ya Kristo ndani yao.10 Vile ulivyo hutoa uhalisia katika mwaliko wako wa njoo upate uzoefu wa shangwe ya utimilifu wa injili ya Yesu Kristo.

Hitaji la tatu ni matumizi huru ya zana ya uongofu ambayo Bwana aliitengeneza kwa ajili ya injili ya nyakati za mwisho, Kitabu cha Mormoni. Ni ushahidi dhahiri wa wito wa kinabii wa Joseph Smith na ushahidi wenye ushawishi juu ya uungu na Ufufuko wa Yesu Kristo. Uwazi wake juu ya mpango wa Baba yetu wa Mbinguni kuhusu ukombozi hauna kifani. Unaposhiriki Kitabu cha Mormoni, unashiriki Urejesho.

Wakati Jason Olsen alipokuwa kijana, alionywa kila mara na wanafamilia pamoja na wengine dhidi ya kuwa Mkristo. Alikuwa na marafiki wawili wazuri, hata hivyo, ambao walikuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, na mara kwa mara walijadili kuhusu dini. Rafiki zake, Shea na Dave, kwa heshima walipinga mawazo ambayo wengine walikuwa wamempa Jason dhidi ya imani katika Yesu Kristo. Hatimaye, walimpa nakala ya Kitabu cha Mormoni, wakisema, “Kitabu hiki kitajibu maswali yako. Tafadhali kisome.” Kwa kusita alikipokea kitabu na kukiweka katika begi lake, ambapo kilikaa kwa miezi mingi. Hakupenda kukiacha nyumbani ambako familia yake ingeweza kukiona, na hakupenda kuwakatisha tamaa Shea na Dave kwa kukirudisha. Mwishowe, alifikia uamzi wa kukichoma kitabu.

Usiku mmoja, akiwa na kiberiti mkono mmoja na mwingine Kitabu cha Mormoni, alikuwa anakaribia kuwasha moto kwenye kitabu wakati aliposikia sauti kwenye akili yake iliyosema, “Usichome Kitabu changu.” Aligutuka, na kusubiria kwa muda. Baadae, akifikiri kuwa alikuwa amepata dhana ya sauti, alijaribu tena kuwasha moto. Kwa mara nyingine, sauti ilikuja akilini mwake: “Nenda chumbani kwako na usome kitabu changu.” Jason aliweka kiberiti pembeni, alirudi chumbani kwake, alifungua Kitabu cha Mormoni, na kuanza kukisoma. Aliendelea siku hadi siku, mara nyingi katika masaa ya mapema asubuhi. Wakati Jason alipofika mwisho na kusali, alieleza, “Nilijazwa na Roho kuanzia utosi wa kichwa changu hadi kwenye nyayo za miguu yangu. … Nilihisi kujawa nuru. … Ulikuwa uzoefu wa furaha tele ambayo sijawahi kuwa nayo maishani mwangu.” Alitafuta ubatizo na baadaye alikuwa mmisionari yeye mwenyewe.

Labda inawezekana isisemwe kwamba licha ya upendo wa dhati na uwazi, mingi ya mialiko yetu, kama si karibu yote, ya kushiriki ujumbe wa Urejesho itakataliwa. Lakini kumbuka hili: kila mtu anastahili mwaliko huo—“wote ni sawa kwa Mungu”;11 Bwana anafurahishwa na kila bidii tunaiyofanya, bila kujali matokeo; mwaliko uliokataliwa si sababu ya kusitisha mahusiano yetu; na kutopendelea leo kunaweza kubadilika kuwa kupendelea katika siku zijazo. Bila kujali, upendo wetu hubaki palepale.

Na kamwe tusisahau kwamba Urejesho umekuja kutokana na majaribu makali na dhabihu kubwa. Hiyo ni mada kwa ajili ya siku nyingine. Leo tunafurahia katika matunda ya Urejesho, moja kati ya vitu vikuu kikiwa ni nguvu ya kuunganisha tena hapa duniani na mbinguni.12 Kama ilivyoelezwa miaka mingi iliyopita na Rais Gordon B. Hinckley, “Kama hakuna kingine chochote kilichokuja kutokana na majonzi yote na masumbuko na maumivu ya urejesho kuliko nguvu za ukuhani mtakatifu za kuunganisha familia pamoja milele, kingekuwa ndicho cha thamani kwa gharama yake yote.”13

Ahadi ya juu ya Urejesho ni ukombozi kupitia Yesu Kristo. Ufufuko wa Yesu Kristo ni ushahidi kwamba Yeye, kimsingi, anazo nguvu za kuwakomboa wote watakaokuja Kwake—kuwaokoa kutoka katika majonzi, uonevu, majuto, dhambi, na hata kifo. Leo ni Jumapili ya Matawi; wiki moja kutoka sasa ni Pasaka. Tunakumbuka, kila mara tunakumbuka, mateso na kifo cha Kristo kulipia dhambi zetu, na tunasherehekea Jumapili ile ya ajabu, siku ya Bwana, Aliyoinuka kutoka wafu. Kwa sababu ya Ufufuko wa Yesu Kristo, Urejesho una maana, maisha yetu ya duniani yana maana, na hatimaye uwepo wetu hasa una maana.

Joseph Smith, nabii mkuu wa Urejesho, anatoa ushuhuda mkuu kwa nyakati zetu juu ya Kristo aliyefufuka: “Kwamba anaishi! Kwani tulimwona, hata mkono wa kuume wa Mungu.”14 Kwa unyenyekevu naongeza ushuhuda wangu kwenye ule wa Joseph na kwa ule wa mitume na manabii waliomtangulia na mitume na manabii waliofuatia baada yake, kwamba Yesu wa Nazareti ndiye Masiya aliyetabiriwa, Mwana Pekee wa Mungu, na Mwokozi aliyefufuka wa watu wote.

“Tunashuhudia kwamba wale wote ambao kwa sala wanajifunza ujumbe wa Urejesho na kutenda kwa imani watabarikiwa kupata ushahidi wao wenyewe wa utakatifu wake na wa lengo lake la kuuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili ulioahidiwa wa Bwana wetu na Mwokozi, Yesu Kristo.”15 Ufufuko wa Kristo unafanya ahadi zake kuwa za kweli. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha