Njoo na Ustahili Kuwa
Tunawaalika watoto wote wa Mungu ulimwenguni kote kujiunga nasi katika jitihada hizi kubwa.
Wapendwa kaka zangu na dada zangu, rafiki zangu wapendwa, kila wiki waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ulimwenguni kote wanamwabudu Baba yetu mpendwa wa Mbinguni, Mungu na Mfalme wa ulimwengu wote, na Mwanaye mpendwa,Yesu Kristo. Tunatakafari maisha na mafundisho ya Yesu Kristo—nafsi pekee isiyo na dhambi ambayo iliwahi kuishi, Mwanakondoo wa Mungu asiye na mawaa. Mara nyingi tuwezavyo, tunashiriki sakramenti kwa kukumbuka juu ya dhabihu Yake na kutambua kwamba Yeye ni kiini katika maisha yetu.
Tunampenda na Kumheshimu. Kwa sababu ya upendo Wake mkuu na wa milele, Yesu Kristo aliteseka na kufa kwa ajili yako na mimi. Alivunja milango ya kifo, akavunja vizuizi ambavyo vilitenganisha marafiki na wapendwa wao,1 na kuleta matumaini kwa waliokata tamaa, uponyaji kwa wagonjwa, na uhuru kwa mateka.2
Kwake tunatoa mioyo yetu, maisha yetu, na kujitoa kwetu kila siku. Kwa sababu hii, “tunazungumza kuhusu Kristo, tunafurahia katika Kristo, [na] tunahubiri kuhusu Kristo, … ili watoto wetu wajue asili ya kutegemea kwa msamaha wa dhambi zao.”3
Kufanyia kazi Ufuasi
Hata hivyo, Kuwa mfuasi wa Yesu Kristo kunahusisha mengi zaidi ya kuzungumza na kuhubiri juu ya Kristo. Mwokozi Mwenyewe alirejesha Kanisa Lake kutusaidia kwenye njia ya kuwa zaidi kama Yeye. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho limeundwa kutoa fursa za kufanyia kazi misingi ya ufuasi. Kupitia ushiriki wetu katika Kanisa, tunajifunza kutambua na kufanyia kazi misukumo ya Roho Mtakatifu. Tunakuza tabia ya kuwafikia wengine kwa upendo na ukarimu.
Hii ni juhudi ya maisha yote, na huitaji kufanyiwa kazi.
Wanariadha hodari wanatumia masaa yasiyo hesabika wakifanyia kazi misingi ya mchezo wao. Manesi, wanamitandao, wahandisi wa nyuklia, na hata mimi mpishi hodari katika jiko la Harriet huwa na uwezo na ujuzi pale tu tunapofanyia mazoezi ufundi wetu kwa bidii.
Kama rubani wa ndege, mara kwa mara niliwafunza marubani kwa kutumia chombo kinachoonesha hali bandia—mashine ya kisasa ambayo inarudufu uzoefu wa kuruka. Chombo kinachoonesha hali bandia sio tu kinasaidia marubani kujifunza misingi ya kuruka; pia kinawaruhusu kupata uzoefu na kujibu matukio yasiyotegemewa wanayoweza kukabiliana nayo wakati watakapoongoza ndege ya kweli.
Kanuni hizohizo hufanya kazi kwa wafuasi wa Yesu Kristo.
Kushiriki kiutendaji katika Kanisa la Yesu Kristo na katika fursa zake tofauti tofauti kutatusaidia kujiandaa vyema kwa ajili ya hali za maisha zinazobadilika, kwa vyovyote vile zitakavyokuwa. Kama waumini wa Kanisa, tunahamasishwa kuchunguza kwa kina maneno ya Mungu kupitia manabii Wake, wa kale na wa sasa. Kupitia sala za kweli na za unyenyekevu kwa Baba yetu wa Mbinguni, tunajifunza kutambua sauti ya Roho Mtakatifu. Tunakubali miito ya kuhudumu, kufundisha, kupanga, kutumikia, na kusimamia. Fursa hizi zinaturuhusu kukua kiroho, kimawazo, na kitabia.
Zitatusaidia kujiandaa kufanya na kutunza maagano matakatifu ambayo yatatubariki katika maisha haya na katika maisha yajayo.
Njoo, Ujiunge Nasi!
Tunawaalika watoto wote wa Mungu ulimwenguni kote kujiunga nasi katika jitihada hizi kubwa. Njoo na uone! Hata wakati wa changamoto hii ya Virusi vya Corona, kutana nasi mtandaoni. Kutana na wamisionari wetu mtandaoni. Tafuteni kujua wenyewe Kanisa hili linahusu nini! Kipindi hiki kigumu kitakapopita, kutana nasi nyumbani kwetu na sehemu zetu za kuabudia!
Tunawaalika kuja na kusaidia! Njooni na hudumia pamoja nasi, kuhudumia watoto wa Mungu, kufuata nyayo za Mwokozi, na kufanya ulimwengu huu kuwa mahali pazuri sana.
Njoo na ustahili kuwa! Utatufanya imara. Na utakuwa bora, mwema, na vile vile mwenye furaha zaidi. Imani yako itaongezeka kwa kina na kuwa thabiti zaidi—kuwa na uwezo zaidi wa kuhimili fujo na majaribu yasiyotegemewa ya kimaisha.
Na je, tunaanzaje? Kuna njia yingi zinazowezekana.
Tunawaalika kusoma Kitabu cha Mormoni. Kama huna nakala, unaweza kukisoma kwenye ChurchofJesusChrist.org4 au pakua programu ya Kitabu cha Mormoni. Kitabu cha Mormoni ni ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo na mwenza kwa Agano la Kale na Jipya. Tunayapenda maandiko yote haya matakatifu na kujifunza kutoka kwayo.
Tunawaalika kutumia muda kiasi kwenye ComeuntoChrist.org kungudua kile waumini wa Kanisa wanachofundisha na kuamini.
Waalike wamisionari kukutembelea kimtandao au katika faragha ya nyumba yako kule ambako hii inawezekana—wana ujumbe wa matumaini na uponyaji. Wamisionari hawa ni wana na mabinti zetu wa thamani wanaohudumu katika sehemu nyingi ulimwenguni kote kwa muda na pesa zao wenyewe.
Katika Kanisa la Yesu Kristo, utakuta familia ya watu ambao siyo tofauti na wewe. Utawakuta watu wanaohitaji msaada wako na wanaotaka kukusaidia wewe pale unapojitahidi kuwa toleo bora la wewe mwenyewe—mtu ambaye Mungu amekuumba kuwa.
Kumbatio la Mwokozi ni kwa Wote
Unaweza kuwa unafikiria, “Nimefanya makosa katika maisha yangu. Sina hakika ningeweza hata kujisikia kama nastahili kuwa katika Kanisa la Yesu Kristo. Mungu asingeweza kupendezwa na mtu kama mimi.”
Yesu Kristo, ingawa ni “Mfalme wa Wafalme,”5 Masiya, “Mwana wa Mungu aliye hai,”6 hujali kwa undani kuhusu kila mmoja na kila mtoto wa Mungu. Anawajali bila kujali nafasi ya mtu—jinsi gani alivyo masikini au tajiri, jinsi gani asivyo mkamilifu au alivyochukuliwa kuwa. Wakati wa maisha Yake duniani, Mwokozi aliwahudumia wote: kwa wenye furaha na waliofikia malengo, kwa wenye kukata tamaa na kupotea, na kwa wale wasio na matumaini. Mara nyingi, watu aliowatumikia na kuwahudumia hawakuwa watu mashuhuri, wa kupendeza, au matajiri. Mara nyingi, watu Aliowainua hawakuwa na kingi cha kutoa kama malipo isipokuwa shukrani, moyo wa unyenyekevu, na hamu ya kuwa na imani.
Kama Yesu alitumia maisha yake ya duniani kuwahudumia “wadogo wa hawa,”7 je, asingewapenda hivi leo? Je, hakuna nafasi katika Kanisa Lake kwa ajili ya watoto wote wa Mungu? Hata kwa wale wanaojiona hawastahili, wamesahauliwa, au wapweke?
Hakuna kiwango cha juu cha ukamilifu ambacho lazima ufikie ili uweze kustahili neema ya Mungu. Sala zako hazipaswi kuwa za kelele au za kushawishi au sahihi kisarufi ili zifike mbinguni.
Kiukweli, Mungu haoneshi upendeleo8—Vitu ulimwengu unavyovithamini havina maana yoyote Kwake. Anajua moyo wako, na Anakupenda bila kujali cheo chako, uwezo wako wa kifedha, au nambari ya wafuasi wako wa Instagram.
Tunaponyenyekeza mioyo yetu kwa Baba wa Mbinguni na kumkaribia Yeye, tutamhisi Yeye akija karibu nasi.9
Sisi ni watoto Wake wapendwa.
Hata wale wanaomkataa.
Hata hao ambao, kama mtoto mkaidi, mtukutu, awavyo na hasira na Mungu na Kanisa Lake, wakifungasha mabegi yao, na kuondoka kwa hamaki nje ya mlango wakitangaza kwamba wanakimbilia mbali na kamwe hawatarudi.
Wakati mtoto anapokimbia mbali na nyumbani, anaweza asiwaone wazazi wanaosikitika wakiangalia kutokea dirishani. Pamoja na mioyo ya huruma, wanawaangalia wana na mabinti zao wakiondoka—wakitegemea watoto wao wa thamani watajifunza kitu fulani kutokana na uzoefu huu wa kuhuzunisha sana na pengine kuyaona maisha kwa macho mapya—na hatimaye kurudi nyumbani.
Ndivyo ilivyo kwa Baba yetu mpendwa wa Mbinguni. Anangojea kurudi kwetu.
Mwokozi wako, kwa machozi ya upendo na huruma katika macho yake, anangojea kurudi kwako. Hata wakati unapojiona uko mbali kutoka kwa Mungu, Atakuona; atakuwa na huruma kwa ajili yako na kukimbia kukukumbatia.10
Njoo na ustahili kuwa.
Mungu Anaturuhusu Kujifunza kutokana na makosa yetu.
Sisi ni mahujaji tunaotembea katika njia ya duniani katika kutafuta maana na ukweli wa msingi. Mara nyingi, vyote tuonavyo ni barabara mbele yetu—hatuwezi kuona zitakakoelekea kona kwenye barabara. Baba yetu wa Mbinguni Anayetupenda hajatupatia kila jibu. Yeye anatutarajia sisi kuelewa vitu vingi sisi wenyewe. Yeye anatutarajia sisi kuamini—hata inapokuwa vigumu kufanya hivyo.
Yeye anatutarajia sisi kuimarisha mabega yetu na kuanzisha uamuzi mdogo—ujasiri kidogo—na kuchukua hatua nyingine mbele.
Hivyo ndivyo tunavyojifunza na kukua.
Je, ungetaka kwa dhati kila kitu kielezewe kinagaubaga? Je, ungetaka kwa dhati kila swali lijibiwe? Kila mwisho wa safari kuwa na ramani?
Ninaamini wengi wetu tungechoka mapema sana na aina hii ya utawala mdogo wa kimbingu. Tunajifunza masomo muhimu ya maisha kupitia uzoefu. Kupitia kujifunza kutokana na makosa yetu. Kupitia kutubu na kutambua sisi wenyewe kwamba “uovu kamwe haujawahi kuwa furaha.”11
Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, alikufa ili kwamba makosa yetu yasiweze kutuhukumu na milele kusimamisha maendeleo yetu. Kwa sababu Yake, tunaweza kutubu, na makosa yetu yanaweza kuwa matukio yanayochangia kuleta mafanikio kwa utukufu mkuu.
Huna haja ya kutembea njia hii peke yako. Baba yetu wa Mbinguni hajatuacha kutangatanga katika giza.
Hii ndiyo sababu, katika majira ya kuchipua ya mwaka 1820, alitokea Yeye pamoja na Mwanaye, Yesu Kristo, kwa kijana, Joseph Smith.
Fikiria kuhusu hilo kwa muda mfupi! Mungu wa ulimwengu alimtokea binadamu!
Hili lilikuwa tukio la kwanza kati ya mengi aliyokuwa nayo Joseph juu ya Mungu na viumbe wengine wa mbinguni. Mengi ya maneno hawa viumbe watakatifu waliyoyasema kwake yameandikwa katika maandiko ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Yanapatikana kwa urahisi. Yoyote anaweza kuyasoma na kujifunza wao wenyewe ujumbe Mungu alionao kwa ajili yetu katika siku hizi.
Tunawaalika mjifunze ninyi wenyewe.
Joseph Smith alikuwa bado mdogo wakati alipopokea mafunuo haya. mengi ya mafunuo haya yalikuja kabla hajafikisha umri wa miaka 30.12 Alikosa uzoefu, na kwa baadhi ya watu, labda alionekana hakustahili kuwa nabii wa Bwana.
Na bado Bwana alimwita vivyo hivyo—kufuatia mpangilio tunaoupata katika maandiko yote matakatifu.
Mungu hakungoja kupata mtu mkamilifu ili kurejesha injili.
Kama Angefanya hivyo, angekuwa bado Anangojea.
Joseph alikuwa sawa na wewe na mimi. Ingawa Joseph alifanya makosa, Mungu alimtumia kukamilisha makusudi Yake makuu.
Rais Thomas S. Monson mara kadhaa alirudia maneno haya ya ushauri: “Yule ambaye Bwana humwita, Bwana humstahilisha.”13
Mtume Paulo aliwashawishi Watakatifu wa Korintho: “Angalieni mwito wenu, akina kaka na akina dada: si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa.”14
Mungu hutumia walio dhaifu na wa kawaida kutekeleza makusudi Yake. Ukweli huu unasimama kama ushuhuda kwamba ni nguvu ya Mungu, si ya mwanadamu, ambayo inakamilisha kazi Yake duniani.15
Msikilizeni yeye, Mfuateni Yeye
Wakati Mungu alipomtokea Joseph Smith, Alimtambulisha Mwanaye, Yesu Kristo, na alisema, “Msikilize Yeye.”16
Joseph alitumia maisha yake yote yaliyosalia akimsikiliza Yeye na kumfuata Yeye.
Kama ilivyokuwa kwa Joseph, ufuasi wetu unaanza na uamuzi wetu wa kumsikiliza na kumfuata Mwokozi Yesu Kristo.
Kama unatamani kumfuata Yeye, kusanya imani yako na jitwike mwenyewe msalaba Wake.
Utaona kwamba wewe kweli unastahili kuwa katika Kanisa Lake—sehemu ya wema mwingi na ukaribishaji ambapo unaweza kujiunga katika utafutaji mkuu wa ufuasi na furaha.
Ni matumaini yangu kwamba, katika mwaka huu wa mia mbili wa Ono la Kwanza, tunapotafakari na kujifunza juu ya Urejesho wa Kanisa la Yesu Kristo, tutatambua kwamba si tu tukio la kihistoria. Wewe na mimi tuna sehemu muhimu sana kwenye hii hadithi kuu, inayoendelea.
Ni ipi, basi, sehemu yako na yangu?
Ni kujifunza juu ya Yesu Kristo. Kusoma maneno Yake. Kumsikiliza Yeye na kumfuata Yeye kwa kushiriki kiutendaji katika kazi hii kuu. Ninakualika kuja na kustahili kuwa!
Huhitaji kuwa mkamilifu. Unatakiwa tu uwe na hamu ya kukuza imani yako na kumkaribia Yeye kila siku.
Sehemu yetu ni kumpenda na kumtumikia Mungu na kuwapenda na kuwatumikia watoto wa Mungu.
Unapofanya hivyo, Mungu atakuzingira kwa upendo wake, furaha, na mwongozo fulani kupitia maisha haya, hata katika hali ngumu mno na zaidi ya hapo.
Juu ya hili ninashuhudia, na ninawaachia baraka zangu katika shukrani ya dhati na upendo kwa kila mmoja wenu, katika jina takatifu la Mwokozi wetu, Bwana wetu—katika jina la Yesu Kristo, amina.