Mkutano Mkuu
Je, Hatuna Budi Kuendelea Katika Kazi Hii Iliyo Kuu?
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Je, Hatuna Budi Kuendelea Katika Kazi Hii Iliyo Kuu?

Tunapaswa daima kukumbuka gharama ambayo Joseph na Hyrum Smith walilipa, sambamba na wanaume wengine wengi, wanawake na watoto waaminifu, kwenye kuanzisha Kanisa.

Asante sana, Rais, kwa ufunguzi huo wa kupendeza. Akina kaka na akina dada, miaka 215 iliyopita, mtoto mdogo alizaliwa kwa Joseph na Lucy Mack Smith huko Vermont katika mkoa uliojulikana kama New England huko kaskazini mashariki mwa Marekani.

Joseph na Lucy Mack waliamini katika Yesu Kristo, walijifunza maandiko matakatifu, waliomba kwa dhati, na walitembea kwa imani katika Mungu.

Walimwita mtoto wao wa kiume Joseph Smith Jr.

Juu ya familia ya Smith, Brigham Young alisema: “Bwana aliweka macho yake wazi juu ya [Joseph Smith], na juu ya baba yake, na juu ya babu yake, na juu ya waasisi wao kurudi nyuma mpaka kwa Ibrahimu, na kutoka kwa Ibrahimu mpaka kwenye mafuriko, kutoka kwenye mafuriko mpaka kwa Henoko na kutoka kwa Henoko mpaka kwa Adamu. Ametazama familia hiyo na damu hiyo kama ilivyosambaa kutoka kwenye chemchemi yake mpaka kuzaliwa kwa mtu huyo. [Joseph Smith] alitawazwa tangu mwanzo.”1

Akiwa kipenzi cha familia yake, Joseph Jr. alikuwa hasa karibu sana na kaka yake mkubwa Hyrum, ambaye alikuwa na miaka sita wakati Joseph alipozaliwa.

Oktoba iliyopita, nilikaa pembeni ya jiwe kwenye ardhi ambalo lilikuwa ndani ya nyumba ndogo ya Smith huko Sharon, Vermont, ambapo Joseph alizaliwa. Nilihisi upendo wa Hyrum kwa Joseph na kumfikiria akiwa amembeba mdogo wake mikononi mwake na kumfundisha jinsi ya kutembea.

Baba na mama Smith walipitia vipingamizi binafsi, vilivyowalazimu kuihamisha familia yao mara kadhaa kabla ya hatimaye kukata tamaa huko New England na kufanya uamuzi wa kijasiri wa kusonga zaidi magharibi, huko Jimbo la New York.

Kwa sababu familia ilikuwa na umoja, walihimili changamoto hizi na kwa pamoja walikabiliana na jukumu la kukatisha tamaa la kuanza upya tena kwenye eneo lenye miti la ekari mia (0.4 km2) la huko Manchester, karibu na Palmyra, New York.

Sina hakika kwamba wengi wetu wanatambua changamoto za kimwili na kihisia ambazo kuanza upya kulileta kwa familia ya Smith—kusafisha ardhi, kupanda matunda na mashamba, kujenga nyumba ndogo ya magogo na maumbo mengine ya shamba, kufanya vibarua vya siku na kutengeneza bidhaa za nyumbani ili kuziuza mjini.

Wakati familia ilipowasili western New York, eneo lilikuwa likiwaka kwa hamasa ya kidini—iliyojulikana kama Uamsho Mkuu wa Pili.

Wakati wa kipindi hiki cha mdahalo na mzozo kati ya makundi ya dini, Joseph alipata ono la kupendeza, linalojulikana leo kama Ono la Kwanza. Tumebarikiwa kuwa na maelezo ya aina nne ya msingi ambayo kwayo nitajikita.2

Joseph aliandika: “Wakati huu wa msisimko mkubwa [wa kidini] akili yangu ilizinduliwa na tafakuri nzito na yenye mashaka makubwa; lakini ingawa hisia zangu zilikuwa nzito na daima kali, hata hivyo nilijiweka mbali na dini hizi, ingawa nilikuwa nimehudhuria mikutano yao kadha wa kadha kadiri nafasi ilivyoniruhusu. … [Bado] mchafuko mkubwa na mzozo ulikuwepo miongoni mwa madhehebu mbali mbali, kwamba ilikuwa vigumu kwa mtu kijana mdogo kama mimi nilivyokuwa, na kwa jinsi nisivyowafahamu watu na mambo yao, kuweza kufikia uamuzi wa nani ni sahihi na nani si sahihi.”3

Joseph aligeukia Biblia ili kupata majibu ya maswali yake na alisoma Yakobo 1:5: “Mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.”4

Alikumbuka: “Kamwe kifungu chochote cha maandiko hakijawahi kumwingia mtu moyoni kwa nguvu nyingi kuliko hiki kilivyofanya kwangu wakati huu. Kilionekana kuniingia kwa nguvu nyingi katika kila hisia za moyo wangu. Nilitafakari tena na tena.”5

Joseph alikuja kugundua kwamba Biblia haikuwa na majibu yote ya maswali ya maisha; bali, iliwafundisha wanaume na wanawake jinsi wanavyoweza kupata majibu ya maswali yao kwa kuwasiliana moja kwa moja na Mungu kupitia sala.

Aliongeza: “Hivyo, kufuatana na dhamira yangu ya kuomba dua kwa Mungu, nilienda msituni kufanya jaribio. Ilikuwa asubuhi nzuri, ya siku angavu, mapema katika majira ya kuchipua ya mwaka elfu moja mia nane na ishirini.”6

Punde baada ya hapo, Joseph alisema “[nguzo ya] mwanga ilitua juu yangu [na] nikawaona Viumbe wawili, ambao mng’aro na utukufu wao wapita maelezo yote, wakiwa wamesimama juu yangu angani. Mmoja wao akaniambia, akiniita mimi kwa jina na kusema, huku akimwonyesha yule mwingine—[Joseph,] Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!7

Mwokozi kisha alizungumza, “Joseph, mwanangu, dhambi zako zimesamehewa. Enenda zako, enenda katika hukumu zangu, na ukazishike amri zangu. Tazama, mimi ni Bwana wa utukufu. Nilisulubiwa kwa ajili ya ulimwengu, ili wote watakaoliamini jina langu waweze kupata uzima wa milele.”8

Joseph aliongeza, “Mara niliporejewa na fahamu zangu, ili kwamba niweze kuzungumza, ndipo nilipowauliza wale viumbe waliosimama juu yangu katika mwanga, ni lipi kati ya madhehebu yale yote lilikuwa sahihi.”9

Alikumbuka: “Waliniambia kwamba madhehebu yote ya dini yalikuwa yakiamini katika mafundisho ya uongo, na kwamba hakuna kati yao lililotambulika kwa Mungu kama kanisa na ufalme wake. Na … wakati huo huo [mimi] [nili]pokea ahadi kwamba utimilifu wa injili katika wakati fulani ujao utajulishwa kwangu.”10

Joseph pia alikumbuka, “niliwaona malaika wengi katika ono hili.”11

Kufuatia ono hili tukufu, Joseph aliandika: “Nafsi yangu ilijazwa na upendo, na kwa siku nyingi ningeweza kufurahi kwa furaha kuu. … Bwana alikuwa pamoja nami.”12

Aliibuka kutoka kwenye Kijisitu Kitakatifu kuanza matayarisho yake kuwa nabii wa Mungu.

Joseph pia alianza kujifunza kile manabii wa kale walichopitia—kukataliwa, upinzani na mateso. Joseph anakumbuka kushiriki kile alichokuwa ameona na kusikia na mmoja wa watumishi ambaye alikuwa hai katika uamshaji wa kidini.

“Nilishangazwa sana na tabia yake; siyo tu hakuipa uzito taarifa yangu, bali kwa dharau kubwa, alisema hii yote ilikuwa ni ibilisi, kwamba hakuna kitu cha jinsi hiyo kama maono au mafunuo katika siku hizi; kwamba mambo ya jinsi hiyo yamekoma pamoja na mitume, na kwamba kamwe hayatakuwepo tena.

“Mara niligundua, hata hivyo, kwamba kuzungumza kwangu juu ya hadithi hii kumeamsha mateso makubwa dhidi yangu kutoka miongoni mwa watangaza imani za dini, na ilikuwa chanzo cha mateso makubwa, ambayo yaliendelea kuongezeka; … na hii ilikuwa jambo la kawaida miongoni mwa madhehebu yote—yote yaliungana ili kunitesa mimi.”13

Miaka mitatu baadaye, mnamo 1823, mbingu zilifunguka tena kama sehemu ya Urejesho unaoendelea wa injili ya Yesu Kristo katika siku za mwisho. Joseph alikumbuka kwamba malaika, aliyeitwa Moroni, alimtokea na kusema “kwamba Mungu alikuwa na kazi ya kufanywa na mimi … [na kwamba] kulikuwepo na kitabu kilichohifadhiwa, kilichoandikwa kwenye mabamba ya dhahabu” ambacho kilikuwa na “utimilifu wa Injili isiyo na mwisho … kama ilivyoletwa na Mwokozi kwa wakazi hao wa kale [wa Amerika].”14

Hatimaye, Joseph alipokea, kutafsiri na kuchapisha kumbukumbu ya kale, inayojulikana leo kama Kitabu cha Mormoni.

Kaka yake Hyrum, ambaye alimuunga mkono daima, hasa kufuatia upasuaji wake wenye maumivu na wa kutishia maisha mnamo 1813, alikuwa mmoja wa mashahidi wa bamba za dhahabu. Alikuwa pia mmoja wa waumini sita wa Kanisa la Yesu Kristo wakati lilipoundwa mnamo 1830.

Wakati wa maisha yao, Joseph na Hyrum walikabiliana na wavamizi na mateso mengi. Kwa mfano, walidhoofika katika hali mbaya zaidi ndani ya gereza la Liberty huko Missouri kwa miezi mitano wakati wa baridi ya 1838–39.

Mnamo Aprili 1839, Joseph alimwandikia mke wake Emma akielezea hali yao katika Gereza la Liberty: “Ninaamini sasa ni takriban miezi mitano na siku sita tangu niwe chini ya uso uliokunjamana wa mlinzi, usiku na mchana, na ndani ya kuta, viunzi na milango ya chuma yenye kukwaruza, ya gereza lenye upweke wa giza na uchafu. … Tutahamishwa kutoka [mahali] hapa kwa kiwango chochote, na tunafurahia hilo. Bila kujali kile kitakachotupata, hatuwezi kuwa katika shimo baya kuliko lilivyo hili. … Hatuwezi kamwe kuwa na tamanio la kurudi baada ya Liberty katika kaunti ya Clay, Missouri. Tumechoshwa na gereza hilo milele.”15

Wakati wakipitia mateso, Hyrum alionesha imani katika ahadi za Bwana, ikiwa ni pamoja na hakikisho la kuwaponyoka maadui zake ikiwa angechagua hilo. Katika baraka Hyrum aliyopokea mnamo 1835 chini ya mikono ya Joseph Smith, Bwana alimuahidi, “Nawe utakuwa na uwezo wa kuponyoka mikono ya maadui zako. Maisha yako yatawindwa kwa ari isiyokoma, lakini utaponyoka. Ikiwa itakupendeza, na unatamani, utakuwa na uwezo kwa hiyari yako kuyatoa maisha yako ili kumtukuza Mungu.”16

Mnamo June 1844, Hyrum alipewa uchaguzi wa kuishi au kuyatoa maisha yake ili kumtukuza Mungu na “kutia muhuri ushuhuda wake kwa damu yake”—bega kwa bega pamoja na kaka yake mpendwa Joseph.17

Wiki moja kabla ya safari ya majaaliwa ya Carthage ambapo waliuwawa kwa kukusudia na wavamizi waoga wenye silaha ambao walijipaka rangi nyuso zao kuepuka kugundulika, Joseph aliandika kwamba “nilimshauri kaka yangu Hyrum kuichukua familia yake kwenye boti ya mvuke iliyofuata na kwenda Cincinnati.”

Bado nahisi hisia kuu wakati nikikumbuka jibu la Hyrum: “Joseph, siwezi kukuacha.’’18

Hivyo Joseph na Hyrum walikwenda Carthage, ambapo waliuwawa kwa ajili ya kusudi na jina la Kristo.

Tangazo rasmi la mauaji lilisema yafuatayo: “Joseph Smith, Nabii na Mwonaji wa Bwana, … amekileta Kitabu cha Mormoni, ambacho amekitafsiri kwa kipawa na uweza wa Mungu, na amekuwa njia ya kukichapisha katika mabara mawili; amepeleka utimilifu wa injili isiyo na mwisho, ambayo imo ndani yake, kwenye pande nne za dunia; ameleta mafunuo na amri ambazo zinaunda kitabu hiki cha Mafundisho na Maagano, na maandishi mengine mengi ya busara na maelekezo kwa manufaa ya watoto wa watu; amewakusanya maelfu mengi ya Watakatifu wa Siku za Mwisho, ameanzisha mji mkubwa, na ameacha sifa na jina ambalo haliwezi kuuawa. … na kama wengi wa wapakwa mafuta wa Bwana katika siku za kale, [Joseph] ametia muhuri huduma yake na kazi zake kwa damu yake yeye mwenyewe; na ndivyo ilivyo kwa kaka yake Hyrum. Katika maisha hawakugawanyika, na katika mauti hawakutenganishwa!19

Kufuatia mauaji, miili ya Joseph na Hyrum ilirejeshwa Nauvoo, ikaoshwa na kuvishwa ili familia ya Smith iweze kuwaona wapendwa wao. Mama yao mpendwa alikumbuka: “Kwa muda mrefu nilijiandaa kiroho na kimwili, nikiinua kila nguvu ya nafsi yangu, na kumlilia Mungu aniimarishe; lakini nilipoingia chumbani, na kuwaona wana wangu waliouwawa wamewekwa wote kwa mara moja mbele ya macho yangu, na kusikia huzuni na kwikwi za familia yangu [na] vilio kutoka kwenye midomo ya wake zao, watoto, kaka zao na dada zao, ilikuwa ya kuchosha. Nilizama tena kumlilia Bwana katika maumivu ya nafsi yangu, ‘Mungu wangu! Mungu wangu! Mbona umeiacha familia hii!’”20

Katika wasaa ule wa huzuni na kukata tamaa, alikumbuka wakimwambia, “Mama, usilie kwa ajili yetu; sisi tumeushinda ulimwengu kwa upendo.”21

Wao kwa hakika waliushinda ulimwengu. Joseph na Hyrum Smith, sawa na wale Watakatifu waaminifu walioelezewa katika kitabu cha Ufunuo, “wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo [na] wako … mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake: na yeye aketiye katika kiti cha enzi atakaa miongoni mwao.

“Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena; wala jua halitawapiga, wala joto lolote.

“Kwa maana huyo Mwana-Kondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemichemi za maji yenye uhai: na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.”22

Tunaposherehekea tukio hili la furaha, kumbukumbu ya miaka 200 ya Ono la Kwanza, tunapaswa daima kukumbuka gharama ambayo Joseph na Hyrum Smith walilipa, sambamba na wanaume wengine wengi, wanawake na watoto waaminifu, kwenye kuanzisha Kanisa ili mimi na wewe tuweze kufurahia baraka nyingi na kweli hizi zote zilizofunuliwa tulizonazo leo. Uaminifu wao haupaswi kamwe kusahaulika!

Mara nyingi nimejiuliza kwa nini Joseph na Hyrum pamoja na familia zao walipaswa kuteseka kiasi hicho. Yaweza kuwa kwamba walipata kumjua Mungu kupitia mateso yao katika njia ambazo wasingeweza kumjua bila hayo. Kupitia mateso, walitafakari juu ya Gethsemane na msalaba wa Mwokozi. Kama Paulo alivyosema “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake.”23

Kabla ya kifo chake mnamo 1844, Joseph aliandika barua iliyojaa ujasiri kwa Watakatifu. Ulikuwa ni mwito wa kutenda, ambao unaendelea katika Kanisa leo:

“Ndugu [na akina dada], je, si lazima sisi tuendelee katika kazi hii iliyo kuu? Twende mbele na siyo nyuma. Ujasiri, ndugu [na akina dada]; na mbele, mbele kwenye ushindi! …

“… Kwa hiyo, sisi, kama kanisa na watu, na kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, tumtolee Bwana dhabihu katika haki.”24

Tunapomsikiliza Roho wakati wa kumbukumbu ya sherehe hii ya miaka 200 wikiendi hii, fikiria ni dhabihu ipi utaitoa kwa Bwana katika haki katika siku zijazo. Vaa ujasiri—ishiriki na mtu unayemwamini na muhimu zaidi, tafadhali tenga muda kuitimiza!

Ninajua kwamba Mwokozi anapendezwa tunapomtolea Yeye dhabihu kutoka mioyoni mwetu katika haki, kama vile Yeye alivyopendezwa na dhabihu ya uaminifu ya wale akina kaka wa kupendeza, Joseph na Hyrum Smith, na Watakatifu wengine wote waaminifu. Juu ya hili ninashuhudia kwa heshima katika jina takatifu la Bwana wetu Yesu Kristo, amina.

Chapisha