Mkutano Mkuu
Kufungua Mbingu kwa Ajili ya Msaada
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


2:3

Kufungua Mbingu kwa Ajili ya Msaada

Acha tuweke imani yetu katika Bwana Yesu Kristo kwenye matendo!

Kikao hiki kimekuwa cha kipekee na kizuri kiasi gani! Asanteni, wapendwa Laudy na Enzo. Mmewawakilisha wasichana na wavulana wa kupendeza wa Kanisa vizuri sana.

Wapendwa kaka na dada zangu, tumesikia mengi leo kuhusu Urejesho wa Kanisa—Kanisa lilelile ambalo Mwokozi wetu, Yesu Kristo, alilianzisha wakati wa huduma Yake ya kidunia. Urejesho huo ulianza miaka 200 iliyopita wakati huu wa majira ya kuchipua wakati Mungu Baba na Mwanae, Yesu Kristo, walimtokea kijana Joseph Smith.

Miaka Kumi baada ya ono hili linalopita uwezo wa binadamu, Nabii Joseph Smith na wengine watano waliitwa kama waumini waanzilishi wa Kanisa la urejesho la Bwana.

Kutoka kundi lile dogo lililokusanyika pamoja Aprili 6,1830, limekuja shirika la kiulimwengu la zaidi ya waumini millioni 16. Mazuri Kanisa hili linayoyakamilisha ulimwenguni kote kupunguza mateso ya binadamu na kutoa msaada kwa wanadamu yanajulikana sana. Lakini kusudi lake kuu ni kuwasaidia wanaume, wanawake, na watoto kumfuata Bwana Yesu Kristo, kutii amri Zake, na kustahili baraka kuu kuliko zote—ile ya uzima wa milele pamoja na Mungu na wapendwa wao.

Tunapoadhimisha tukio ambalo lilizindua Urejesho mnamo 1820, ni muhimu kukukumbuka kwamba wakati tunamheshimu Joseph Smith kama nabii wa Mungu, hili siyo kanisa la Joseph Smith, wala si kanisa la Mormoni. Hili ni Kanisa la Yesu Kristo. Alitoa amri mahususi kwenye jina ambalo Kanisa Lake lilipaswa kuitwa: “Kwani hivyo ndivyo kanisa langu litakavyoitwa katika siku za mwisho, hata Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.”

Nilizungumza kipindi cha nyuma kuhusu uelekeo uliohitajika wa kusahihisha katika jinsi tunavyotaja jina la Kanisa. Tangu wakati huo, mengi yamefanyika kukamilisha sahihisho hili. Ninawashukuru sana Rais M. Russel Ballard na Akidi nzima ya Mitume Kumi na Wawili, ambao wamefanya mengi sana kuongoza juhudi hizi vilevile na wale waliohusika katika juhudi nyingine ambayo nitaitangaza jioni hii.

Viongozi na idara za Kanisa, vitengo vinavyohusika, na mamilioni ya waumini—na wengine—sasa wanatumia jina sahihi la Kanisa. Mtindo wa mwongozo rasmi wa Kanisa umerekebishwa. Tovuti kuu ya Kanisa sasa ni ChurchofJesusChrist.org. Anwani kwa ajili ya barua pepe, umiliki wa majina, na chaneli za mitandao ya kijamii zimesahihishwa. Kwaya yetu tuipendayo sasa ni Kwaya ya Tabernacle huko Temple Square.

Tumekwenda kwenye juhudi hizi za kipekee kwa sababu tunapoliondoa jina la Bwana kutoka kwenye jina la Kanisa Lake, bila kukusudia tunamtoa Yeye kama fokasi kuu ya kuabudu kwetu na maisha yetu. Tunapojichukulia jina la Mwokozi juu yetu wakati wa ubatizo, tunaahidi kushuhudia, kwa maneno yetu, mawazo yetu, na matendo yetu, kwamba Yesu ni Kristo.

Kipindi cha nyuma, niliahidi kwamba kama “tutafanya bidii kurejesha jina sahihi la Kanisa la Bwana,” Yeye “angemimina chini nguvu Zake na baraka juu ya vichwa vya Watakatifu wa Siku za Mwisho, baraka ambazo hatujapata kuona.” Ninarejesha upya ahadi hiyo leo.

Kutusaidia kumkumbuka Yeye na kulitambua Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kama Kanisa la Bwana, tunafurahi kutambulisha alama ambayo itaonesha mahali pakuu pa Yesu Kristo katika Kanisa Lake.

Alama hii inajumuisha jina la Kanisa lililopo ndani ya jiwe la pembeni. Yesu Kristo ni jiwe kuu la pembeni.

Alama ya maneno pamoja na jiwe la pembeni

Katikati ya alama ni uwakilishi wa sanamu ya marumaru ya Thorvaldsen Christus. Inamuelezea Bwana aliyefufuka, aliye hai akinyoosha mikono kuwakumbatia wote ambao watamwendea Yeye.

Kama mfano, Yesu Kristo amesimama chini ya tao. Tao linatukumbusha juu ya Mwokozi aliyefufuka akiibuka kutoka kaburini siku ya tatu kufuatia Kusulibiwa Kwake.

Alama mpya ya Kanisa

Alama hii inapaswa kuwa iliyozoeleka kwa wengi, kama ambavyo kwa muda mrefu tumeitambua injili ya urejesho kwa Kristo aliye hai, aliyefufuka.

Alama sasa itatumika kama utambulisho wa kuonekana kwa ajili ya fasihi rasmi, habari, na matukio ya Kanisa. Itawakumbusha wote kwamba hili ni Kanisa la Mwokozi na kwamba yote tunayofanya kama waumini wa Kanisa Lake yamejikita juu ya Yesu Kristo na injili Yake.

Sasa, kaka na dada zangu wapendwa, kesho ni Jumapili ya Mitende, kama Mzee Gong alivyofundisha kwa ushawishi. Kisha tunaingia kwenye wiki maalum ambayo inafikia kilele kwa Pasaka. Kama wafuasi wa Yesu Kristo, kuishi katika siku ambayo ugonjwa wa kuambukiza wa COVID-19 umeweka ulimwengu katika vurugu, acha sisi tusizungumze tu juu ya Kristo au kuhubiri kuhusu Kristo au kutumia alama inayomwakilisha Kristo.

Acha tuweke imani yetu katika Bwana Yesu Kristo kwenye matendo!

Kama mnavyojua, waumini wa Kanisa wanashika sheria ya mfungo siku moja kila mwezi.

Kanuni ya kufunga ni ya kale. Ilikuwa ikifanywa na mashujaa wa kwenye biblia tokea siku za mwanzo kabisa. Musa, Daudi, Ezra, Nehemia, Esta, Isaya, Danieli, Yoeli, na wengine wengi walifunga na kuhubiri juu ya kufunga. Kupitia maneno ya Isaya, Bwana alisema: “Je saumu niliyoichagua siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa?”

Mtume Paulo aliwaonya Watakatifu wa Korintho “kujitoa wenyewe kwa kufunga na kuomba.” Mwokozi Mwenyewe alitangaza kwamba vitu fulani “haviondoki isipokuwa kwa sala na kufunga.”

Nilisema hivi karibuni katika video kwenye mtandao wa kijamii kwamba “kama daktari na mpasuaji, ninaheshima kubwa kwa ajili ya wataalamu wa afya, wanasayansi, na wote ambao wanafanya kazi masaa yote kudhibiti ueneaji wa COVID-19.”

Sasa, kama Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na Mtume wa Yesu Kristo, ninajua kwamba Mungu “ana nguvu zote, busara yote, na uelewa wote; anaelewa vitu vyote, na ni Kiumbe mwenye huruma, hata kwenye wokovu, kwa wale watakaotubu na kuamini kwenye jina lake.”

Kwa hiyo, katika kipindi cha huzuni kubwa, kama wakati ugonjwa unapofikia kuenea kwa kiasi kikubwa, Kitu cha asili kabisa kwa ajili yetu kufanya ni kumwomba Baba yetu wa Mbinguni na Mwanae—Mponyaji Mkuu—kuonesha mbele nguvu zao za ajabu kubariki watu wa duniani.

Katika ujumbe wangu wa video, niliwaalika wote kujiunga katika kufunga mnamo Jumapili ya Machi 29, 2020. Wengi wenu wanaweza kuwa wameona video na wamejiunga katika kufunga. Baadhi wanaweza kuwa hawajaiona. Sasa bado tunahitaji msaada kutoka mbinguni.

Kwa hiyo usiku huu, wapendwa akina kaka na dada zangu, katika roho ya wana wa Mosia, ambao walijitoa wenyewe kwa kufunga sana na sala, na kama sehemu ya mkutano wetu mkuu wa Aprili 2020, ninatoa mwito kwa ajili ya mfungo mwingine ulimwenguni kote. Kwa wale wote ambao afya zao zinaruhusu, na tufunge, tuombe, na tuunganishe imani zetu tena. Acha sote kwa maombi tusihi kwa ajili ya faraja dhidi ya ugonjwa huu ulioenea ulimwenguni pote.

Ninawaalika wote, ikiwa ni pamoja na wale ambao si wa imani yetu, kufunga na kusali siku ya Ijumaa Kuu, Aprili 10, ili ugonjwa ulioenea ulimwenguni uweze kudhibitiwa, watoa huduma walindwe, uchumi uimarishwe, na maisha yawe kawaida.

Tunafunga kwa namna gani? Milo miwili au kipindi cha saa 24 ni kawaida. Lakini unapaswa kuamua nini kingeanzisha dhabihu kwa ajili yako, wakati unapokumbuka dhabihu kubwa Mwokozi aliyofanya kwa ajili yako. Acha tuungane katika kuomba kwa ajili ya uponyaji ulimwenguni kote.

Ijumaa Kuu ingeweza kuwa siku sahihi kuwa na Baba wa Mbinguni na Mwanae kutusikia sisi!

Wapendwa akina kaka na dada zangu, ninaonesha kwa dhati upendo wangu wa kina, sambamba na ushuhuda wangu wa utakatifu wa kazi ambayo kwayo tumejiingiza. Hili ni Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Anasimama mwanzoni mwake na kuelekeza yote ambayo tunafanya. Ninajua kuwa atajibu maombi ya watu Wake. Nashuhudia hivyo, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.