Mkutano Mkuu
Ujio wa Kitabu cha Mormoni
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Ujio wa Kitabu cha Mormoni

Ukweli wa kihistoria na mashahidi maalum wa Kitabu cha Mormoni vinashuhudia kwamba ujio wake ulikuwa kweli wa kimuujiza.

Wakati akikutana na wazee wa Kanisa kipindi fulani, Nabii Joseph Smith alitangaza: “Toa kitabu cha Mormoni, na mafunuo, je dini yetu iko wapi? Hatuna chochote.”1 Wapendwa akina kaka na akina dada, kufuatia Ono la Kwanza, ujio wa kimuujiza wa Kitabu cha Mormoni ni tukio muhimu la pili la kihistoria la Urejesho unaojifunua wa injili ya Yesu Kristo katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu. Kitabu cha Mormoni kinashuhudia juu ya upendo wa Mungu kwa watoto Wake, juu ya dhabihu ya upatanisho usio na choyo wa Bwana Yesu Kristo, na juu ya kilele cha huduma Yake miongoni mwa Wanefi punde baada ya Ufufuko Wake.2 Kinashuhudia pia kwamba sazo la nyumba ya Israeli litakuwa moja kupitia kazi Yake ya siku za mwisho na kwamba hawajatupwa milele.3

Tunapojifunza ujio wa kitabu hiki kitakatifu cha maandiko katika siku hizi za mwisho, tunatambua kwamba kazi yote ilikuwa ya kimuujiza—kuanzia Nabii Joseph kupokea mabamba ya dhahabu kutoka kwa malaika mtakatifu mpaka tafsiri yake kwa “karama na nguvu ya Mungu,”4 utunzwaji wake, na uchapishwaji wake kwa mkono wa Bwana.

Ujio wa Kitabu cha Mormoni ulianza kitambo kabla ya Joseph Smith kupokea mabamba ya dhahabu kutoka kwenye mikono ya malaika Moroni. Manabii wa kale walitabiri kuhusu ujio wa kitabu hiki kitakatifu katika siku yetu.5 Isaya alizungumzia juu ya kitabu kilichofungwa, kwamba wakati ambapo kingetokea watu wangekuwa wakibishana juu ya neno la Mungu. Hali hii ingetoa muktadha ambapo Mungu angefanya “kazi yake ya ajabu na mwujiza,” akisababisha “akili za watu wao wenye akili [kupotea], na ufahamu wa wenye busara wao [kufichwa]” wakati wanyenyekevu “wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli.”6 Ezekieli alizungumza kuhusu kijiti cha Yuda (Bibilia) na kijiti cha Yusufu (Kitabu cha Mormoni) kuletwa pamoja kuwa kimoja. Wote Ezekieli (katika Agano la Kale) na Lehi (katika Kitabu cha Mormoni) wanaonesha kwamba “vitakua kwa pamoja” ili kuangamiza mafundisho ya uongo, kuimarisha amani, na kutuleta kwenye ufahamu wa maagano.7

Mnamo jioni ya Septemba 21, 1823, miaka mitatu na nusu baada ya tukio la Ono la Kwanza, Joseph alitembelewa mara tatu na malaika Moroni, nabii wa mwisho wa Wanefi katika Amerika ya kale, kama matokeo ya sala yake za dhati. Wakati wa mazungumzo yao ambayo yalidumu usiku kucha, Moroni alimwambia Joseph kwamba Mungu alikuwa na kazi ya ajabu kwa ajili yake kukamilisha—tafsiri yake na kuchapisha kwa ulimwengu maneno yenye mwongozo wa kiungu ya manabii wa kale wa bara la Amerika.8 Siku iliyofuata, Joseph alikwenda mahali pale, si mbali na nyumba yake, ambapo mabamba yalikuwa yamezikwa na Moroni kuelekea mwisho wa maisha yake, karne nyingi kabla. Hapo Joseph alimwona tena Moroni, ambaye alimwelekeza kujiandaa kuyapokea mabamba hayo katika siku za baadaye.

Kwa zaidi ya miaka minne iliyofuata, mnamo Septemba 22 ya kila mwaka, Joseph alipokea maelekezo ya ziada kutoka kwa Moroni juu ya ufahamu kuhusu jinsi ufalme wa Bwana unavyopaswa kuongozwa katika siku hizi za mwisho. Matayarisho ya Joseph pia yalijumuisha matembezi kutoka kwa malaika wa Mungu, hivyo kufunua ukuu na utukufu wa matukio ambayo yangetukia katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu.9

Ndoa yake na Emma Hale mnamo 1827 ilikuwa sehemu ya matayarisho hayo. Alibeba jukumu muhimu katika kumsaidia Nabii katika maisha yake yote na huduma yake. Kwa kweli, mnamo Septemba 1827, Emma alifuatana na Joseph kwenda mlimani ambapo mabamba yalikuwa yamefichwa, na alimsubiri wakati malaika Moroni alipoweka maandiko kwenye mikono ya Joseph. Joseph alipokea ahadi kwamba mabamba yangehifadhiwa ikiwa angefanya juhudi zake zote kuyaweka salama mpaka yatakaporejea kwenye mikono ya Moroni.10

Wenzangu wapendwa katika injili, ugunduzi mwingi wa leo tangu nyakati za kale hutokea wakati wa uchimbuaji wa vitu vya kale au hata kwa bahati mbaya wakati wa mradi wa ujenzi. Joseph Smith, hata hivyo, aliongozwa na malaika kwenye mabamba hayo. Hilo tu peke yake lilikuwa muujiza.

Mchakato wa kutafsiri Kitabu cha Mormoni ulikuwa pia muujiza. Kumbukumbu hii takatifu ya kale “haikutafsiriwa” katika njia ya kawaida ambayo wanazuoni wangetafsiri maandishi ya kale kwa kujifunza lugha ya kale. Tunapaswa kutazama mchakato zaidi kama “ufunuo” kwa usaidizi wa vifaa vya kushikika vilivyotolewa na Bwana, kinyume na “tafsiri” ya mtu mwenye ufahamu wa lugha. Joseph Smith alitamka kwamba kwa uwezo wa Mungu yeye “alitafsiri Kitabu cha Mormoni kutoka [silabi za kale], ufahamu ambao ulipotea ulimwenguni, ambamo tukio la kupendeza [yeye] alisimama peke yake, kijana asiye na elimu, kuikabili hekima ya ulimwengu na ujinga uliokithiri wa karne ya kumi na nane kwa ufunuo mpya.”11 Msaada wa Bwana katika kutafsiri mabamba—au ufunuo, inaweza kusemwa hivyo—pia ni uthibitisho pale unapozingatia muda mfupi wa kimuujiza Joseph Smith aliotumia kuyatafsiri.12

Waandishi wa Joseph walishuhudia juu ya nguvu ya Mungu ambayo ilidhihirishwa wakati wa kufanyia kazi tafsiri ya Kitabu cha Mormoni. Oliver Cowdery aliwahi kusema: “Hizi zilikuwa siku ambazo kamwe hazitasahaulika—kukaa chini ya sauti iliyotoa imla kwa mwongozo wa mbinguni, iliamsha hisia za shukrani za juu kabisa za moyo huu! Siku baada ya siku niliendelea, bila bugudha, kuandika kutoka katika kinywa chake, wakati alipotafsiri … ‘Kitabu cha Mormoni.’”13

Vyanzo vya kihistoria vinaonesha kwamba kutoka wakati ambao Joseph Smith alipata mabamba hayo mnamo 1827, majaribio yalifanywa ya kuyaiba kutoka kwake. Alikumbuka kwamba “matumizi ya nguvu nyingi yalitumika ili kuyapata [mabamba hayo] kutoka [kwake]” na kwamba “kila mkakati ambao ungebuniwa ulitumiwa kwa lengo hilo.”14 hatimaye Joseph na Emma walilazimika kuhama kutoka Manchester, New York, kwenda Harmony, Pennsylvania, kutafuta mahala salama ili kuendelea na kazi ya kutafsiri, mbali na wavamizi na watu waliotaka kuyaiba mabamba.15 Kama mwanahistoria mmoja anavyokumbuka: “Hiyo ilihitimisha kipindi kigumu cha kwanza cha ulinzi wa Joseph juu ya mabamba. … Bado kumbukumbu ilikuwa salama, na katika jitihada zake za kuyahifadhi Joseph bila shaka alikuwa amejifunza mengi kuhusu njia za Bwana na mwanadamu ambazo zingemhudumia vizuri katika nyakati zijazo.”16

Wakati akitafsiri Kitabu cha Mormoni, Joseph alijifunza kwamba Bwana angechagua mashahidi wa kuyaona mabamba.17 Hii ni sehemu ya kile Bwana mwenyewe alichoanzisha wakati Yeye aliposema, “Kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno litathibitishwa.”18 Oliver Cowdery, David Whitmer, na Martin Harris, ambao walikuwa baadhi ya wenza wa mwanzo wa Joseph katika uanzishwaji wa kazi ya maajabu ya Mungu katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu, walikuwa mashahidi wa kwanza kuitwa kutoa ushuhuda maalum juu ya Kitabu cha Mormoni kwa ulimwengu. Walishuhudia kwamba malaika, ambaye alikuja kutoka katika uwepo wa Mungu, aliwaonesha kumbukumbu hiyo ya kale na kwamba waliona maandishi yaliyochongwa kwenye mabamba. Walishuhudia pia kwamba walisikia sauti ya Mungu kutoka mbinguni ikitamka kwamba kumbukumbu hiyo ya kale ilikuwa imetafsiriwa kwa karama na nguvu ya Mungu. Kisha waliamriwa kushuhudia juu ya hilo kwa ulimwengu wote.19

Bwana kimiujiza aliwaita mashahidi wengine wanane ili wajionee wenyewe mabamba ya dhahabu na kuwa mashahidi maalum wa ukweli na utakatifu wa Kitabu cha Mormoni kwa ulimwengu. Walishuhudia kwamba waliona na kwa umakini waliyachunguza mabamba na herufi zilizochongwa humo. Hata katikati ya taabu, mateso, aina zote za magumu, na hata baadhi yao baadaye kuyumba katika imani yao, hawa mashahidi kumi na mmoja wa Kitabu cha Mormoni waliochaguliwa kamwe hawakukana shuhuda zao kwamba waliyaona mabamba. Joseph Smith hakuwa tena pekee yake mwenye ufahamu wa matembezi ya Moroni na mabamba ya dhahabu.

Lucy Mack Smith aliandika kwamba mwanaye aliwasili nyumbani akiwa amezidiwa na shangwe baada ya mashahidi kuwa wameoneshwa mabamba. Joseph aliwaelezea wazazi wake, “ninahisi kana kwamba nilikuwa nimepumzishwa mzigo ambao ulifikia kuwa mzito sana kwangu kuubeba, na inaleta shangwe nafsini mwangu, kwamba siko tena pekee yangu katika ulimwengu.”20

Joseph Smith alikabiliwa na upinzani mwingi katika kupiga chapa Kitabu cha Mormoni wakati tafsiri yake ilipokuwa ikifikia mwishoni. Aliweza kumshawishi mpiga chapa aliyeitwa B. Grandin huko Palmyra, New York, kukipiga chapa baada tu ya Martin Harris, katika tendo la imani na dhabihu kubwa, kuweka rehani shamba lake kama dhamana kwa ajili ya gharama za upigaji chapa. Kutokana kwa sehemu na kuendelea kwa upinzani baada ya uchapishwaji wa Kitabu cha Mormoni, Martin Harris kwa uaminifu aliuza ekari 151 (0.6 km2) za shamba lake ili kulipa gharama zote za uchapishaji. Kupitia ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith, Bwana alimwelekeza Martin Harris kutokutamani mali yake na kulipa gharama za kupiga chapa kitabu ambacho kina “ukweli na ni neno la Mungu.”21 Mnamo Machi 1830 nakala 5,000 za kwanza za Kitabu cha Mormoni zilichapishwa, na leo zaidi ya nakala milioni 180 zimechapishwa katika zaidi ya lugha mia moja.

Ukweli wa kihistoria na mashahidi maalum wa Kitabu cha Mormoni vinashuhudia kwamba ujio wake ulikuwa kweli wa kimuujiza. Hata hivyo, nguvu ya kitabu hiki haipo tu katika historia yake ya kupendeza bali kwenye ujumbe wake wenye nguvu, usioweza kulinganishwa ambao umebadili maisha yasiyo na idadi—ikijumuisha yangu!

Nilisoma Kitabu chote cha Mormoni kwa mara ya kwanza wakati nilipokuwa mwanafunzi mdogo wa seminari. Kama ilivyoshauriwa na walimu wangu, nilianza kukisoma nikianza na kurasa zake za utangulizi. Ahadi iliyopo katika kurasa za mwanzo za kitabu bado zinatoa mwangwi akilini mwangu: “Tafakari moyoni [mwako] … , na kisha … muulize Mungu [kwa imani] … katika jina la Kristo kama kitabu ni cha kweli. Wale ambao watafuata njia hii … watapata ushuhuda wa ukweli na utakatifu wake kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.”22

Kwa ahadi hiyo akilini, kwa uaminifu nikitafuta kujua zaidi ukweli wake, na kwa roho ya sala, nilisoma Kitabu cha Mormoni, kidogo kidogo, pale nilipokamilisha masomo ya seminari yaliyopangwa ya kila wiki. Ninakumbuka, kana kwamba ilikuwa jana, kwamba hisia nzuri taratibu ilianza kuvimba nafsini mwangu na kujaza moyo wangu, ikiangaza uelewa wangu, na ikiwa zaidi na zaidi ya kupendeza, kama ilivyoelezwa na Alma katika kuhubiri kwake neno la Mungu kwa watu wake.23 Hisia ile hatimaye iligeuka kuwa ufahamu ambao ulikita mizizi moyoni mwangu na kuwa msingi wa ushuhuda wangu wa matukio na mafundisho muhimu yanayopatikana katika kitabu hiki kitakatifu.

Kupitia uzoefu huu na uzoefu mwingine binafsi wenye thamani, Kitabu cha Mormoni hakika kimekuwa jiwe kuu ambalo linaendeleza imani yangu katika Yesu Kristo na ushuhuda wangu wa mafundisho ya injili Yake. Kimekuwa moja ya nguzo ambazo hushuhudia kwangu juu ya dhabihu takatifu ya upatanisho wa Kristo. Kimekuwa ngao kote katika maisha yangu dhidi ya majaribu ya adui ya kudhoofisha imani yangu na kuingiza kutokuamini katika akili yangu na kinanipa ujasiri wa kutangaza kwa ujasiri ushuhuda wangu wa Mwokozi kwa ulimwengu.

Rafiki zangu wapendwa, ushuhuda wangu wa Kitabu cha Mormoni ulikuja mstari juu ya mstari24 kama muujiza kwenye moyo wangu. Hadi leo, ushuhuda huu unaendelea kukua kadiri ninavyoendelea kutafuta, kwa moyo wa dhati, ili kuelewa kikamilifu neno la Mungu kama lilivyo ndani ya kitabu hiki cha ajabu cha maandiko.

Kwa nyote mnaosikia sauti yangu leo, ninawaalika muwe sehemu ya ujio wa kimuujiza wa Kitabu cha Mormoni katika maisha yako mwenyewe. Ninakuahidi kwamba kadiri unavyosoma maneno yake kwa sala na kwa uaminifu, unaweza kupokea ahadi zake na baraka tele katika maisha yako. Ninathibitisha kwa mara nyingine ahadi ambayo inatoa mwangwi kupitia kurasa zake: kwamba ikiwa “mtamwuliza Mungu, Baba wa Milele, katika jina la Kristo, ikiwa vitu hivi si vya kweli; na ikiwa mtauliza na moyo wa kweli, na kusudi halisi, mkiwa na imani katika Kristo,” Yeye kwa rehema “atawaonyesha ukweli wake kwenu, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.”25 Ninakuhakikishia kwamba Yeye atakupa jibu katika njia binafsi zaidi, kama Alivyofanya kwangu na kwa wengine wengi kote ulimwenguni. Uzoefu wako utakuwa mtukufu na mtakatifu kwako kama uzoefu wa Joseph Smith ulivyokuwa kwake, vilevile kama ilivyokuwa kwa mashahidi wa kwanza na kwa wote ambao wametafuta kupokea ushahidi wa uadilifu na uaminifu wa kitabu hiki kitakatifu.

Ninatoa ushahidi wangu kwamba Kitabu cha Mormoni hakika ni neno la Mungu. Ninashihudia kwamba kumbukumbu hii takatifu “inaeleza mafundisho ya injili, inadokeza juu ya mpango wa wokovu, na kuwaambia binadamu vitu vinavyo wapasa kufanya ili wapate amani katika haya maisha duniani na wokovu wa milele katika maisha yanayokuja.”26 Ninashuhudia kwamba Kitabu cha Mormoni ni chombo cha Mungu cha kuwezesha kukusanya Israeli katika siku yetu na kuwasaidia watu kumjua Mwana Wake, Yesu Kristo. Ninashuhudia kwamba Mungu yu hai na anatupenda sisi na Mwanaye, Yesu Kristo, ni Mwokozi wa ulimwengu, jiwe la katikati la teo la dini yetu. Ninasema mambo haya katika jina takatifu la Mkombozi wetu, Mwalimu wetu, na Bwana wetu, hata Yesu Kristo, amina.

Chapisha