Mkutano Mkuu
Msingi Mzuri kwa Wakati Ujao
Mkutano mkuu wa Aprili 2020


Msingi Mzuri kwa Wakati Ujao

Katika miaka ijayo, acha turuhusu maboresho yaliyofanywa kwenye Hekalu la Salt Lake yatupe msukumo na mwongozo wa kiungu.

Historia ya Hekalu la Salt Lake

Acha turudi nyuma alasiri yenye joto mnamo Julai 24, 1847 karibu saa 8:00 alasiri. Kufuatia safari ngumu ya siku 111 pamoja na washiriki 148 wa Kanisa ambao waliunda kikundi cha kwanza kuelekea magharibi, Brigham Young, wakati huo akiwa Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, mgonjwa na dhaifu kutokana na homa ya mlimani, waliingia kwenye Bonde la Salt Lake.

Siku mbili baadaye, alipokuwa akipata nafuu kutokana na ugonjwa wake, Brigham Young aliwaongoza washiriki kadhaa wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili na wengine kwenye safari ya kufanya uchunguzi. William Clayton alirekodi: “Karibu robo tatu ya maili kaskazini mwa kambi hiyo, tulifika kwenye ardhi nzuri iliyo sawa, iliyolala mtambaa na iliyoteremka vizuri kuelekea magharibi.”1

Picha
Brigham Young kwenye eneo la hekalu
Picha
Brigham Young akiweka alama mahali pa kujenga hekalu.
Picha
Kuwekea alama mahali pa kujenga hekalu

Wakati akikagua mahali hapo na kikundi hicho, Brigham Young ghafla akasimama na kuchomeka mkongojo wake ardhini, akisema, “Hapa ndipo patasimama Hekalu la Mungu wetu.” Mmoja wa wenzake alikuwa Mzee Wilford Woodruff, ambaye alisema kwamba taarifa hiyo “ilimpitia [yeye] kama umeme,” na akaingiza tawi ardhini kuweka alama mahali palipotengenezwa kwa mkongojo wa Rais Young. Ekari 40 (16 ha) zilichaguliwa kwa ajili ya hekalu, na iliamuliwa kwamba mji unapaswa kuwekwa “mraba mzuri kabisa Kaskazini & Kusini, mashariki & magharibi” na hekalu likiwa mahali pa katikati.2

Katika mkutano mkuu wa Aprili 1851, washiriki wa Kanisa walichagua kwa sauti moja kuidhinisha hoja ya kujenga hekalu “kwa jina la Bwana.”3 Miaka miwili baadaye, mnamo Februari 14, 1853, mahali pale paliwekwa wakfu na Heber C. Kimball katika ibada ya umma iliyohudhuriwa na Watakatifu elfu kadhaa, na ardhi ilitengwa kwa ajili ya msingi wa hekalu la Salt Lake. Miezi michache baadaye, mnamo Aprili 6, mawe makubwa ya pembeni ya hekalu yaliwekwa na kuwekwa wakfu katika sherehe zilizojumuisha tamasha la walinzi wenye sare na bendi na maandamano yaliyoongozwa na viongozi wa Kanisa kutoka kwenye hema la zamani hadi kwenye sehemu ya hekalu, ambapo hotuba na sala zilikuwa zinatolewa kwenye kila moja ya mawe manne.4

Picha
Msingi wa Hekalu la Salt Lake
Picha
Brigham Young

Katika hafla kuu ya kuweka jiwe la msingi, Rais Young alikumbuka kwamba alikuwa amepata maono wakati alipoweka mguu wa kwanza juu ya ardhi walipokuwa wakikagua mtambaa wa bonde, na kusema, “Nilijua [wakati ule], kama ninavyojua sasa, kwamba hii ilikuwa ardhi ya kujenga hekalu—ilikuwa mbele yangu.”5

Miaka kumi baadaye, Brigham Young alitoa utambuzi ufuatao wa kinabii kwenye mkutano mkuu wa Oktoba 1863: “Ninataka kuona hekalu linajengwa kwa njia ambayo litahimili hadi Milenia. Hili siyo hekalu pekee tutakalojenga; yatakuwepo mamia ya haya yatakayojengwa na kuwekwa wakfu kwa Bwana. Hekalu hili litajulikana kama hekalu la kwanza lililojengwa ndani ya milima na Watakatifu wa Siku za Mwisho. … Ninataka hekalu … hilo libaki limesimama kama jengo la ukumbusho wa kujivunia wa imani yetu, uvumilivu na utenda kazi wa Watakatifu wa Mungu kwenye milima.”6

Picha
Hekalu la Salt Lake kwenye ujenzi
Picha
Hekalu la Salt Lake kwenye ujenzi

Katika kurejea historia hii fupi, ninapata mshangao juu ya uonaji wa Brigham Young—kwanza, hakikisho lake kwamba, kadiri inavyowezekana na, kwa kutumia njia za ujenzi zilizopatikana wakati na mahali pale, Hekalu la Salt Lake lingejengwa kwa njia ya kuhimili mpaka milenia yote na, pili, unabii wake juu ya ukuaji wa mahekalu ya baadaye ulimwenguni, hata kufikia idadi ya mamia.

Ukarabati wa Hekalu la Salt Lake

Kama Brigham Young, manabii wetu wa hivi leo wanaangalia Hekalu la Salt Lake na mengine yote kwa uangalifu mkubwa. Katika miaka yote, Urais wa Kwanza umekuwa, kila mara, ukiushauri Uaskofu Simamizi kuhakikisha kuwa msingi wa Hekalu la Salt Lake ni thabiti. Wakati nilipohudumu katika Uaskofu Simamizi, kwa ombi la Urais wa Kwanza, tulifanya tathmini ya ujenzi wa Hekalu la Salt Lake, ikiwa ni pamoja na tathmini ya maendeleo ya hivi karibuni katika ubunifu wa tetemeko na mbinu za ujenzi.

Hapa ni baadhi ya sehemu za marejeo yaliyotolewa kwa Urais wa Kwanza wakati huo: “Katika muundo na ujenzi wa Hekalu la Salt Lake, uhandisi bora zaidi, kazi ya ustadi, vifaa vya ujenzi, samani, na nyenzo zingine zilizopatikana zilitumika. Tangu lilipowekwa wakfu mnamo 1893, hekalu limesimama kidete na kutumika kama mnara wa imani [na] tumaini na kama nuru kwa watu. Uangalifu mkubwa umefanywa kwenye kutumia, kusafisha, na kudumisha hekalu katika hali nzuri. Viunga vya sakafu ya mawe ya nje na ndani na mihimili ya boriti viko katika hali nzuri. Uchunguzi wa hivi karibuni unathibitisha kwamba eneo lililochaguliwa na Brigham Young kwa ajili ya hekalu lina mchanga mzuri na sifa za uimara.”7

Tathmini ilihitimisha kuwa matengenezo ya kawaida na maboresho yalihitajika ili kufanya upya na kufanya hekalu kuwa la kisasa, ikiwa ni pamoja na eneo la nje na maeneo ya juu, mifumo ya huduma iliyochakaa, maeneo ya Ubatizo. Hata hivyo, mapendekezo ya kuongeza upana zaidi unaojitegemea, kuzuia tetemeko kuanzia msingi wa hekalu kwenda juu yalipendekezwa pia.

Msingi wa Hekalu

Kama unavyoweza kukumbuka, Rais Brigham Young mwenyewe alihusika pakubwa katika ujenzi wa msingi wa hekalu la kwanza, ambao umehimili hekalu vizuri tangu kukamilika kwake miaka 127 iliyopita. Kifurushi kipya cha kuzuia tetemeko kilichopendekezwa kwa ajili ya hekalu kitatumia teknolojia ya kutenga msingi, ambayo haikufikiriwa wakati wa ujenzi wake. Hii inachukuliwa kuwa ya kisasa, sanaa ya hali ya juu ya uhandisi kwa ulinzi wa tetemeko la ardhi.

Picha
Mpango wa ukarabati wa hekalu
Picha
Mpango wa ukarabati wa hekalu

Teknolojia hii, ya hivi karibuni katika maendeleo yake, huanza katika msingi hasa wa hekalu, ikitoa ulinzi mkali dhidi ya uharibifu kutokana na tetemeko la ardhi. Kwa asili, inaimarisha hekalu kusimama kidete, hata wakati dunia na mazingira yanayolizunguka yanapitia tukio lenye kutetemesha ardhi.

Ukarabati wa hekalu ambao ungetumia teknolojia hii ulitangazwa na Urais wa Kwanza mwaka jana. Chini ya maelekezo ya Uaskofu Simamizi, ujenzi ulianza miezi michache iliyopita, mnamo Januari 2020. Unakadiriwa kukamilika katika takribani miaka minne.

Kuhakikisha Msingi wako Binafsi

Ninapofikiria miaka minne ijayo ya maisha ya Hekalu hili zuri, tukufu, lililoinuliwa, na la kushangaza la Salt Lake, ninaliona zaidi kama wakati wa kufanywa upya badala ya wakati wa kufungwa! Kwa njia hiyo hiyo, tunaweza kujiuliza, “Je, ni kwa jinsi gani kufanywa upya huku kwa Hekalu la Salt Lake kunaweza kutupa sisi msukumo wa kiungu kufanya upya, kurekebisha upya, kuzaliwa upya, au kurejeshwa kwetu kiroho?”

Kujitathmini kwa kina kunaweza kudhihirisha kwamba sisi pia pamoja na familia zetu tunaweza kufaidika kutokana na kufanya kazi fulani inayohitajika ya matengenezo na ukarabati, hata kufanywa upya dhidi ya matetemeko ya ardhi! Tunaweza kuanza mchakato kama huo kwa kuuliza:

“Je! Msingi wangu unaonekanaje?”

“Je! ni nini kinachounda ukuta mnene, mawe thabiti ya pembeni, yaliyo na nguvu, ambayo ni sehemu ya msingi wangu binafsi, ambapo ushuhuda wangu upo?”

“Je! ni mambo gani ya msingi ya tabia yangu ya kiroho na kihisia ambayo yataniruhusu mimi na familia yangu kubaki thabiti na bila kusonga, hata kuhimili matukio na ghasia za kutetemesha ambayo hakika yatatokea katika maisha yetu?”

Matukio haya, ambayo ni sawa na tetemeko la ardhi, mara nyingi ni ngumu kuyatabiri na huja kwa viwango tofauti vya nguvu—kupambana na maswali au shaka, kukabiliwa na shida au majaribu, kujaribu kushinda chuki binafsi kwa viongozi wa Kanisa, washiriki, mafundisho, au sera. Ulinzi bora dhidi ya haya upo kwenye msingi wetu wa kiroho.

Je! ni nini mawe ya pembeni ya kiroho ya maisha yetu binafsi na ya familia? yanaweza kuwa kanuni rahisi, za wazi, na za thamani za kuishi injili—sala ya familia; kusoma maandiko, ikiwa ni pamoja na Kitabu cha Mormoni; uhudhuriaji hekaluni; na kujifunza injili kupitia Njoo Unifuate na jioni ya nyumbani. Nyenzo zingine za kusaidia kuimarisha msingi wako wa kiroho zinaweza kujumuisha Makala za Imani, tangazo kwa familia, na “Kristo Aliye hai.”

Kwangu mimi, kanuni zilizojumuishwa kwenye maswali yaliyojadiliwa kama sehemu ya kupokea kibali cha hekaluni hutumika kama msingi madhubuti wa msingi wa kiroho—hasa maswali manne ya mwanzo. Ninayaona kama mawe ya pembeni ya kiroho.

Sisi, bila shaka, tunafahamu maswali haya, kama Rais Russell M. Nelson alivyotusomea moja baada ya jingine katika mkutano mkuu uliopita.

  1. Je, una imani katika, na ushuhuda wa Mungu, Baba wa Milele; Mwanaye, Yesu Kristo; na Roho Mtakatifu?

    Picha
    Uungu
  2. Je, una ushuhuda wa Upatanisho wa Yesu Kristo na wa jukumu Lake kama Mwokozi na Mkombozi wako?

    Picha
    Upatanisho wa Yesu Kristo
  3. Je, una ushuhuda wa Urejesho wa injili ya Yesu Kristo?

    Picha
    Urejesho
  4. Je, unamuidhinisha Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kama nabii, mwonaji, na mfunuzi na kama mtu pekee duniani aliyepewa mamlaka ya kutumia funguo zote za ukuhani?8

    Picha
    Manabii

Je! unaweza kuona jinsi unavyoweza kuzingatia maswali haya kama vipengele vya msingi katika msingi wako binafsi kukusaidia kuujenga na kuuimarisha? Paulo aliwafundisha Waefeso juu ya kanisa ambalo “lilijengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, Yesu Kristo mwenyewe akiwa jiwe kuu la pembeni; katika yeye majengo yote yaliyowekwa vizuri pamoja yanakua hekalu takatifu katika Bwana.”9

Picha
Hekalu lenye msingi imara

Moja ya furaha kubwa maishani mwangu ni kufahamiana na kuhamasishwa na washiriki wa Kanisa ulimwenguni kote ambao wanaishi mfano wa imani katika Yesu Kristo na injili yake. Wamejenga misingi binafsi madhubuti ambayo inawaruhusu kuhimili matukio ya tetemeko kwa uelewa thabiti, licha ya maumivu yao ya moyo na uchungu.

Ili kuonesha hili kwa kiwango binafsi zaidi, hivi karibuni nilizungumza kwenye mazishi ya mke na mama mwema, mwenye nguvu (pia rafiki wa familia yetu). Alikuwa mchezaji wa soka mwenye nguvu na kiwango cha juu wakati alipokutana na kuolewa na mume wake mwanafunzi wa udaktari wa meno. Walibarikiwa kwa binti mzuri, mwenye busara. Alipambana vikali na aina mbali mbali za saratani kwa miaka sita yenye changamoto. Licha ya shida ya kihisia na ya kimwili ambayo alipata, alimwamini Baba yake wa Mbinguni mwenye upendo na mara nyingi alinukuliwa na wafuasi wake wa mitandao ya kijamii kwa msemo wake maarufu: “Mungu yuko kwenye kila kitu.”

Kwenye moja ya machapisho yake ya mitandao ya kijamii, aliandika kwamba kuna mtu alikuwa amemwuliza, “Ni kwa jinsi gani bado una imani licha ya maumivu yote ya moyo yanayokuzunguka?” Alijibu kwa uimara kwa maneno haya: “Kwa sababu imani ndiyo inanipitisha katika nyakati hizi za giza. Kuwa na imani haimaanishi kuwa kitu kibaya hakitatokea. Kuwa na imani kunaniruhusu kuamini kuwa kutakuwa na nuru tena. Na nuru hiyo itakuwa angavu hasa kwa sababu nimepitia giza. Kadiri ya giza nene nililoshuhudia kwa miaka mingi, ndivyo nilivyoshuhudia nuru zaidi. Nimeona miujiza. Nimewahisi malaika. Nimejua kuwa Baba yangu wa Mbinguni alikuwa ananibeba. Nisingepata uzoefu wa yote hayo kama maisha yangekuwa rahisi. Wakati ujao wa maisha haya unaweza kuwa haujulikani, lakini si imani yangu. Nikichagua kutokuwa na imani basi nimechagua kutembea gizani tu. Kwa sababu bila imani, giza pekee ndilo limesalia.”10

Ushuhuda wake usiotikisika wa imani katika Bwana Yesu Kristo—katika maneno yake na vitendo vyake—ulikuwa msukumo kwa wengine. Hata ingawa mwili wake ulikuwa mdhaifu, aliwainua wengine kuwa na nguvu.

Ninawafikiria washiriki wengine wengi wa Kanisa, mashujaa kama dada huyu, ambao hutembea kila siku kwa imani, wakijitahidi kuwa wanafunzi wa kweli na wasio na hofu wa Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Wanajifunza juu ya Kristo. Wanahubiri juu ya Kristo. Wanajitahidi kufuata mfano Wake. Iwe siku za maisha yao ziko kwenye ardhi thabiti au ya kutikisika, msingi wao ni imara na usioondoshwa.

Hawa ndio nafsi ambazo zinaelewa maana kubwa ya maneno “Msingi imara, enyi Watakatifu wa Bwana” na “ambazo kwa Mwokozi wamekimbilia kwa ajili ya pumziko.”11 Ninashukuru kupita kiasi kutembea kati ya wale ambao wameandaa msingi wa kiroho unaostahili jina la Watakatifu na walio na nguvu na imara vya kutosha kukabiliana na mishtuko mingi ya maisha.

Sidhani kama tunaweza kuelezea vya kutosha umuhimu wa msingi imara kama huu katika maisha yetu binafsi. Hata katika umri mdogo, watoto wetu wa Msingi hufundishwa wanapokuwa wakiimba juu ya ukweli huu:

Mtu mwenye busara alijenga nyumba yake juu ya mwamba,

Na mvua ikanyesha. …

Mvua ikanyesha, na mafuriko yakaja juu,

Na nyumba juu ya mwamba ikasimama imara.12

Maandiko yanaimarisha fundisho hili la kimsingi. Mwokozi aliwafundisha watu wa Amerika:

“Na ikiwa mtafanya hivi vitu daima mna baraka, kwani mmejengwa juu ya mwamba wangu.

“Lakini yeyote miongoni mwenu ambaye atafanya ndogo kuliko hawa hajajengwa juu ya mwamba wangu, lakini wamejengwa kwenye msingi wa mchanga; na wakati mvua itateremka, na mafuriko kuja, na upepo kuvuma, na kujipigisha juu yao, wataanguka.”13

Ni tumaini la dhati la viongozi wa Kanisa kwamba ukarabati muhimu katika Hekalu la Salt Lake utachangia kutimiza hamu ya Brigham Young ya kuona “Hekalu likijengwa kwa njia ambayo litaweza kuhimili hadi milenia.” Katika miaka ijayo, na turuhusu maboresho haya yanayofanywa kwenye Hekalu la Salt Lake yatupe msukumo na mwongozo wa kiungu, kama watu binafsi na familia, kwamba sisi pia—kimafumbo—“tujengwe katika njia ambayo itahimili hadi milenia.”

Tutafanya hivyo tunapotimiza agizo la mtume Paulo la “[kujiwekea] akiba [wenyewe] msingi mzuri kwa wakati ujao, ili [sisi] tupate uzima ulio kweli kweli.”14 Ni maombi yangu ya dhati kwamba msingi wetu wa kiroho utakuwa wa uhakika na imara, kwamba ushuhuda wetu wa Upatanisho wa Yesu Kristo na wa jukumu Lake kama Mwokozi na Mkombozi wetu utakuwa jiwe letu kuu la pembeni, ambalo juu yake ninashuhudia katika jina Lake, hata Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. William Clayton journal, July 26, 1847, Maktaba ya Historia ya Kanisa, Jiji la Salt Lake.

  2. Ona “Kwenye Hema, Marais Woodruff na Smith Wanahutubia Watakatifu Jana Alasiri,” Deseret Evening News, Aug. 30, 1897, 5; “Pioneers’ Day,” Deseret Evening News, Julai 26, 1880, 2; Wilford Woodruff journal, Julai 28, 1847, Church History Library, Salt Lake City.

  3. “Kumbukumbu za Mkutano Mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho uliofanyika kwenye Jiji Kuu la Salt Lake, Jimbo la Deseret, Aprili 6, 1851,” Deseret News, Apr. 19, 1851, 241.

  4. Ona “Hekalu,” Deseret News, Feb. 19, 1853, 130; “Minutes of the General Conference,” Deseret News, Apr. 16, 1853, 146; “Minutes of the General Conference,” Deseret News, Apr. 30, 1853, 150.

  5. “Hotuba ya Rais Brigham Young,” Millennial Star, Apr. 22, 1854, 241.

  6. “Maneno ya Rais Brigham Young,” Deseret News, Okt. 14, 1863, 97.

  7. Wasilisho la Uaskofu Simamizi kwenye Hekalu la Salt Lake Kwa Urais wa Kwanza, Okt. 2015.

  8. Ona Russell M. Nelson, “Hotuba ya Kufunga,” Liahona, Nov. 2019, 121.

  9. Waefeso 2:20–21.

  10. Chapisho la mtandao wa kijamii na Kim Olsen White.

  11. “How Firm a Foundation,” Nyimbo za Kanisa, na. 85.

  12. “The Wise Man and the Foolish Man,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 281; msisitizo katika nakala halisi uliondolewa katika hali hii.

  13. 3 Nefi 18:12–13; msisitizo umeongezwa.

  14. 1 Timotheo 6:19; msisitizo umeongezwa.

Chapisha