Njoo, Unifuate
Oktoba 14–20: “Ninyi ni Watoto wa Agano.” 3 Nefi 20–26


“Oktoba 14–20: ‘Ninyi ni Watoto wa Agano.’ 3 Nefi 20–26,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2023)

“Oktoba 14–20. 3 Nefi 20–26,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2023)

Kristo akiwatokea Wanefi

Kielelezo cha Kristo akiwatokea Wanefi, na Andrew Bosley

Oktoba 14–20: “Ninyi ni Watoto wa Agano”

3 Nefi 20–26

Wakati unaposikia watu wakitumia istilahi kama nyumba ya Israeli, je unahisi kana kwamba wanazungumza kukuhusu wewe? Wanefi na Walamani walikuwa wazao halisi wa Israeli, “tawi la mti wa Israeli,” lakini pia walikuwa “wamepotea kutoka kwenye kiwiliwili chake” (Alma 26:36; ona pia 1 Nefi 15:12). Lakini Mwokozi aliwataka wajue kwamba hawakuwa wamepotea Kwake. “Ninyi ni wa nyumba ya Israeli,” Alisema, “na ni wa agano” (3 Nefi 20:25). Yeye angeweza kusema kitu sawa na hicho kwako leo hii, kwa yeyote ambaye anabatizwa na kufanya maagano Naye pia ni wa nyumba ya Israeli, “wa agano.” Kwa maneno mengine, wakati Yesu anapozungumza kuhusu nyumba ya Israeli, Yeye anazungumza kukuhusu wewe. Maelekezo ya kubariki “jamaa yote ya dunia” ni kwa ajili yako (3 Nefi 20:27). Mwaliko wa “amka tena, na jivike nguvu yako” ni kwa ajili yako (3 Nefi 20:36). Na ahadi Yake ya thamani, “Wema wangu hautaondoka kutoka kwako, wala agano langu la amani kuondolewa,” ni kwa ajili yako (3 Nefi 22:10).

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

3 Nefi 20–22

Katika siku za mwisho, Mungu atafanya kazi ya ajabu.

Katika 3 Nefi 20–22, Mwokozi alitoa unabii kuhusu siku za baadaye za watu Wake wa agano (ona hasa 3 Nefi 20:30–32, 39–41; 21:9–11, 22–29). Unaposoma mistari hii, kumbuka kitu ambacho Rais Russell M. Nelson alikisema: “Sisi ni miongoni mwa watu wa agano wa Bwana. Yetu sisi ni fursa ya kushiriki binafsi katika utimizwaji wa ahadi hizi. Wakati wa kusisimua ulioje kuwa hai!” (“Kukusanywa kwa Israeli Iliyotawanyika,” Liahona, Nov. 2006, 79). Unabii upi ni wa kusisimua zaidi kwako? Unaweza kufanya nini ili kusaidia kuutimiza?

Tafuta maneno na virai vyenye mwongozo wa kiungu. Unaweza kukuta kwamba maneno na virai fulani katika maandiko vinakugusa wewe, kana kwamba viliandikwa mahususi kwa ajili yako. Fikiria kuviwekea alama katika maandiko yako au kuviandika katika shajara ya kujifunzia.

3 Nefi 2224

Mungu ni mwenye rehema kwa watu wanaorudi Kwake.

Katika 3 Nefi 22 na 24, Mwokozi ananukuu maneno kutoka kwa Isaya na Malaki ambayo yamejaa picha dhahiri na ulinganifu—makaa ya mawe katika moto, fedha iliyosafishwa, madirisha ya mbinguni (ona hasa 3 Nefi 22:7–8, 10–17; 24:10–12, 17–18). Je, ulinganifu huu unakufundisha nini kuhusu uhusiano kati ya Mungu na watu Wake—na uhusiano Wake na wewe? Ni kwa jinsi gani ahadi katika sura hizi zimetimizwa katika maisha yako au ya familia yako?

Ona pia “The Refiner’s Fire” (video), Maktaba ya Injili.

3 Nefi 23:6–13

Kuandika uzoefu wa kiroho kunaweza kuibariki familia yako.

Ni kipi kinakutia msukumo kuhusu mchangamano wa Mwokozi na Wanefi katika 3 Nefi 23: 6–13? Kama Mwokozi angechunguza kumbukumbu ambayo wewe umeiweka, ni maswali gani Yeye angeweza kukuuliza? Je, ni matukio yapi muhimu au uzoefu wa kiroho ambao unapaswa kuuandika? Kwa nini ni muhimu kufanya hivyo? (ona 3 Nefi 26:2).

3 Nefi 23; 26:1–12

Mwokozi ananitaka niyachunguze maandiko.

Unaposoma 3 Nefi 20:10–12; 23; 26:1–12, tafakari jinsi Mwokozi anavyohisi kuhusu maandiko. Je, kuna tofauti ipi kati ya kuyachunguza maandiko na kuyasoma tu? (ona 3 Nefi 23:1).

3 Nefi 24:7–12

ikoni ya seminari
Kulipa zaka hufungua madirisha ya mbinguni.

Watu wa Mungu daima wameamriwa kulipa zaka (ona Mwanzo 14:17–20; Malaki 3:8–11). Unapojifunza 3 Nefi 24:1–12, fikiria kuhusu kwa nini Mungu anawaomba watu Wake walipe zaka. Maswali haya yanaweza kuongoza kujifunza kwako:

  • Sheria ya zaka ni nini? (Ona Mafundisho na Maagano 119. “Mapato” katika ufunuo huu humaanisha kipato. Waumini wote ambao wana kipato wanapaswa kulipa zaka.) Je, Ni kwa jinsi gani zaka ni tofauti na aina nyingine ya michango?

  • Zaka hutumiwa kwa ajili gani? Unaweza kupata sehemu ya orodha katika Mada za Injili, “Zaka” (Maktaba ya Injili). Ni kwa njia zipi umebarikiwa kwa sababu waumini wa Kanisa hulipa zaka?

  • Ni baraka zipi huja kwa watu wanaoishi sheria ya zaka? (Ona 3 Nefi 24:7–12.) Unaweza kupata baadhi ya baraka hizo katika ujumbe wa Mzee David A. Bednar “Madirisha ya Mbinguni” (Liahona, Nov. 2013, 17–20). Tafuta, hasa, kwa ajili ya baraka ambazo si lazima ziwe pesa. Ni kwa jinsi gani umeona baraka hizo katika maisha yako?

Unaweza pia kutaka kuangalia video “Jesus Teaches about the Widow’s Mite” (Mada za Injili), au kusoma Marko 12:41–44. Je, hadithi hii inakufundisha nini?

3 Nefi 25:5–6

Bwana alimtuma Eliya kuugeuza moyo wangu uwaelekee mababu zangu.

Katika siku yetu, mioyo yetu “inageuzwa kuwaelekea mababu [zetu]” kupitia kazi ya hekaluni na historia ya familia. Ni kwa jinsi gani hii inatokea kwako? Unaposoma 3 Nefi 25:5–6 na Mafundisho na Maagano 110:13–16, tafakari kwa nini ni sehemu muhimu ya mpango wa Mungu.

Ona pia: “Families Can Be Together Forever,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto,188.

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la Liahona na magazeti ya Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana.

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

3 Nefi 23:1, 5

Ninaweza kuyachunguza maandiko kwa bidii.

  • Maelekezo ya Mwokozi katika 3 Nefi 23 yanaonesha jinsi maandiko yalivyo muhimu Kwake. Ili kuwasaidia watoto wako wagundue hili, ungeweza kusoma 3 Nefi 23:1, 5 na uwaombe wasikilize neno ambalo limerudiwa mara tatu. Ni kwa jinsi gani kuchunguza ni tofauti na kusoma tu?

  • Pengine wewe na watoto wako mngeweza kuandika mstari pendwa wa maandiko na kuuficha. Kisha mngeweza kufanya zamu kutafuta maandiko ya mmoja na mwingine yaliyofichwa, yasomeni pamoja, na mzungumze kuhusu kwa nini mistari hii ina maana sana.

3 Nefi 24:8–12

Kulipa zaka hufungua madirisha ya mbinguni.

  • Wasaidie watoto wako wachunguze 3 Nefi 24:8–12 ili kupata njia za kukamilisha sentensi hii: Kama ukilipa zaka, Bwana ata …. Ungeweza pia kushiriki uzoefu ambapo ulibarikiwa kwa sababu ulilipa zaka. Kama itakuwa yenye msaada, fikiria kuandika kiasi kidogo cha pesa ubaoni na wasaidie watoto wakokotoe ni kiasi gani cha zaka (asilimia 10) tunapaswa kutoa kwa kila kiasi.

  • Ukurasa wa shughuli ya wiki hii unaweza kuwasaidia watoto wako wazungumze kuhusu baadhi ya njia ambazo Bwana hutumia zaka kuwabariki waumini wa Kanisa Lake. Pengine wangeweza kuchora picha (au kutafuta picha kwenye magazeti ya Kanisa) za njia ambazo zaka huwabariki wao.

3 Nefi 25:5–6

Baba wa Mbinguni ananitaka nijifunze kuhusu mababu zangu.

  • Ni kwa jinsi gani utawatia moyo watoto wako wachunguze na kujifunza kuhusu mababu zao? Ni kwa jinsi gani unaweza kuwatia moyo watoto wako wafanye ibada kwa ajili ya mababu zao pale watakapokuwa wakubwa? Fikiria kuwasaidia wachunguze 3 Nefi 25:5–6 ili kupata kitu fulani ambacho kitatokea katika siku za mwisho. Watoto wadogo wangeweza kuweka mkono wao kwenye moyo wao kila mara wanaposikia neno “moyo” unaposoma mistari hii. Ungeweza pia kusoma kuhusu jinsi unabii huu ulivyotimizwa katika Mafundisho na Maagano 110:13–16 (ona pia Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 95). Waambie watoto wako kuhusu jinsi ambavyo moyo wako umewageukia mababu zako. Kwa mfano, ungeweza kushiriki uzoefu wowote uliopata wakati ukijifunza kuhusu mababu zako na kufanya ibada za hekaluni kwa niaba yao.

  • Wasaidie watoto wako wajaze mti wa familia kwa majina ya wazazi wao na babu na bibi zao. Ni hadithi ipi ungeweza kuishiriki kuhusu mmoja wa mababu zako? Onesha picha ikiwezekana. Mngeweza pia kuimba pamoja “Families Can Be Together Forever” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 188) na kuzungumza na watoto wako kuhusu kwa nini familia ni muhimu katika mpango wa Baba wa Mbinguni.

Kwa ajili ya mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

Yesu akisoma kumbukumbu za Wanefi pamoja na Nefi

Leta Hapa Kumbukumbu, na Gary L. Kapp