Madirisha ya Mbinguni
Nashuhudia kwamba baraka za kiroho na kidunia huja katika maisha yetu tunapoishi sheria ya zaka.
Ningependa kuelezea masomo mawili muhimu niliojifunza kuhusu sheria ya zaka. Somo la kwanza linazingatia baraka ambazo zinakuja kwa watu binafsi na familia wanapotii kwa uaminifu amri hii. Somo la pili linasisitiza umuhimu wa zaka katika ukuaji wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho katika ulimwengu wote. Naomba Roho Mtakatifu atathibitisha kwa kila mmoja wetu ukweli wa kanuni ninazojadili.
Somo Nambari 1---Baraka Muhimu lakini Zisizotambulika Virahisi
Mama ya Dada Bednar ni mwanamke mwaminifu na mtunza nyumba wa kufana. Kutoka siku za mapema za ndoa yake, yeye ameweka kumbukumbu za matumizi ya kifedha ya nyumbani. Kwa miongo yeye amehesabu kwa makini mapato ya familia na matumizi akitumia daftari ya hesabu rahisi sana. Habari ambazo amekusanya katika miaka mingi ni pana na ina taarifa nyingi.
Dada Bednar alipokuwa msichana, mama yake alitumia habari zilizo katika daftari za hesabu kusisitiza kanuni za kimsingi za kuishi kwa uwekevu na usimamizi wa busara wa nyumbani, Siku moja walipokuwa wakirejelea pamoja sehemu kadhaa za matumizi, mama yake aligundua mwelekeo wa kuvuta hisia. Gharama ya daktari na dawa kwa familia yake ilikuwa chini sana kuliko vile ingetarajiwa. Basi yeye alilinganisha uvumbuzi huu na injili ua Yesu Kristo na kumwelezea bintiye ukweli wa nguvu sana: kadiri tunavyoishi sheria ya zaka, kila mara tunapokea baraka muhimu lakini zisizotambulika virahisi ambazo kwa kawaida si zile tulizotarajia na ni rahisi kukosa kuzitambua, Familia haikupokea ghafula mapato ya ziada ya nyumba au yaliyo wazi. Badala yake, Baba wa Mbinguni alitoa baraka rahisi katika njia zilizoonekana kuwa za kawaida. Dada Bednar daima atakumbuka hili somo muhimu kutoka kwa mama yake kuhusu msaada ambao huja kwetu kupitia madirisha ya mbinguni, kama ilivyoahidiwa na Malaki katika Agano la Kale (ona Malaki 3:10).
Kila mara tunapofundisha na kushuhudia kuhusu sheria ya zaka, sisi huhimiza baraza za muda za mara moja, za kusisimua, zinazotambulikana kwa uwazi tunazopokea. Na hakika baraka kama hizo hutokea. Hali baadhi ya baraka tofauti tofauti tunazopokea tunapokuwa watiifu kwa amri hii ni muhimu na ni ngumu kuelezea. Baraka kama hizo zinaweza kutambulika kama sisi tu wasikivu kiroho na tuko macho (ona 1 Wakorintho 2:14).
Taswira ya “madirisha” ya mbinguni iliyotumiwa na Malaki inafaa sana. Madirisha huruhusu mwanga wa asili kuingia katika jengo. Vivyo hivyo, mwangaza na mtazamo wa kiroho humwangwa kupitia madirisha ya mbinguni na hata ndani ya maisha yetu kadiri tunavyoheshimu sheria ya zaka.
Kwa mfano, baraka muhimu lakini isiyorahisi kutambua tunayopokea ni karama ya kiroho ya shukrani ambayo inawezesha ufahamu wetu wa kile tunachofaa kuzia hamu kwa ajili ya kile tunachotaka. Mtu mwenye shukrani ni tajiri katika kuridhika. Mtu asiye na shukrani huteseka katika dhiki ya kutoridhika kusikoisha. (ona Luka 12:15).
Tunaweza kuhitaji na kuomba ili tupate ajira ya kufaa. Macho na masikio ya imani (ona Etheri 12:19) yanahitajika, hata hivyo, kutambua kipawa cha kiroho cha utambuzi wa juu ambao unaweza kutupatia uwezo wa kutambua nafasi za kazi ambazo watu wengi wanaweza kukosa kuziona au baraka za azimio kuu la kibinafsi ili kutafuta sana na zaidi nafasi kuliko watu wengine wanavyoweza au walivyo tayari kufanya. Tunaweza kutaka na kutarajia kuitiwa kazi, lakini baraka ambazo huja kwetu kupitia madirisha ya mbimguni zinaweza kuwa uwezo mkuu wa kutenda na kubalisha hali zetu wenyewe badala ya kutarajia hali zetu kubadilishwa na mtu au kitu kingine.
Tunaweza kwa kufaa kuwa na hamu na kufanya kazi ili kupokea ongezeko la mshahara katika ajira yetu ili kukithi vyema mahitaji ya maisha. Macho na masikio ya imani yanahitajika, hata hivyo, na kutambua ndani yetu ongezeko la uwezo wa kiroho na kimwili (ona Luka 2:52) wa kufanya mengi kwa kutumia kidogo, uwezo makini wa kuweka kipaumbele na kurahisisha, na uwezo wa juu wa kutunza mali tuliyonayo tayari. Tunaweza kutaka na kutarajia hundi nono ya mshahara, lakini baraka ambao huja kwetu kupitia kwa madirisha ya mbinguni inaweza kuwa uwezo mkubwa wa kubadilisha hali zetu wenyewe badala ya kutarajia hali zetu kubadishwa na mtu au kitu kingine.
Askari vijana katika Kitabu cha Mormoni (ona Alma 53; 56–58) waliomba kwa dhati kwamba Mungu angewaimarisha na kuwakomboa kutoka kwenye mikono ya maadui zao. Cha kushangaza, majibu ya maombi haya hayakuzaa zana zaidi au ongezeko la majeshi. Badala yake, Mungu aliwapatia askari hawa waaminifu hakikisho kwamba Yeye angewakomboa wao, amani katika nafsi zao, na imani kuu na tumaini la ukombozi katika Yeye (ona Alma 58:11). Basi, wana wa Helamani walihamasika, wakaweka azimio lao la kushinda, na kwenda mbele kwa nguvu zao zote dhidi ya Walamani (ona Alma 58:12–13). Hakikisho, amani, imani, na tumaini hapo awali ingeweza kuonekana kama kwamba si zile baraka askari wangetaka, bali zilikuwa hasa ndio zile baraka hawa wavulana jasiri walihitaji kusonga mbele na kushinda kimwili na kiroho.
Wakati mwingine tunaweza kumwomba Mungu ufanisi, na Yeye hutupatia sisi uthabiti wa kimwili na kiroho. Tunaweza kusihi tupate ustawi, na tupokee mtazamo mkubwa na ongezeko la uvumilivu, au tunaomba tupate ukuaji na tunabarikiwa na kipawa cha neema. Yeye anaweza kututunukia sisi na msimamo na imani tunavyojitahidi kupata malengo yanayostahili. Na tunaposihi tupate msaada kutokana na ugumu wa kimwili, kiakili, na kiroho, Yeye anaweza kuongezea azma na uthabiti.
Mimi naahidi kwamba wewe nami tumaposhika na kuweka sheria ya zaka, kwa kweli madirisha ya mbinguni yatafunguliwa na baraka za kimwili na kiroho zitamwangwa hata kwamba hakutakuwa na nafasi ya kutosha ya kuzipokelea (ona Malaki 3:10). Pia tutakumbuka tamko la Bwana:
“Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.
“Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu” (Isaya 55:8–9).
Mimi nashuhuhdia kwamba sisi tunapokuwa wasikivu na watiifu, sisi tutabarikiwa na macho ambayo yanaona kwa uwazi zaidi, na masikio ambayo yanasikia vizuri, na mioyo ambayo inayoelewa kikamilifu umuhimu na ugumu wa kueleweka wa njia Zake, mawazo Yake, na baraka Zake katika maisha yetu.
Somo Nambari 2---Urahisi wa Njia ya Bwana
Kabla ya wito wangu kuhudumu kama mshiriki wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili, nilisoma mara nyingi katika Mafundisho na Maagano kuhusu baraza lililoteuliwa kusimamia na kugawa hazina ya zaka takatifu. Baraza la Matumizi ya Zaka liliundwa kwa ufunuo na linajumuisha Urais wa Kwanza, Jamii ya Mitume Kumi na Wawili, na Uaskofu Simamizi (ona M&M 120).. Nilipojitayarisha Desemba 2004 kuhudhuria mkutano wa kwanza wa baraza hili, nilitazamia kwa furaha fursa kuu ya kujifunza.
Bado ninakumbuka mambo niliyopitia na kuhisi katika lile baraza. Nilipata ufahamu mkubwa na staha kwa sheria ya Bwana ya fedha kwa watu, familia, na kwa Kanisa Lake. Mpango wa kifedha wa msingi wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho---kwa yote mapato na mgawo---umeelezewa katika sehemu ya 119 na 120 ya Mafundisho na Maagano. Taarifa mbili zinazopatikana katika funuo hizi zinapatiana msingi wa mambo ya Kanisa ya mwaka wa fedha.
Sehemu ya 119 kwa urahisi inasema kwamba washiriki wote “watalipa sehemu moja ya kumi ya mapato yao ya kila mwaka; na hii itakuwa sheria ya kudumu kwao milele, ... asema Bwana. (mstari wa 4).
Basi, kuhusu mgawo ulioidhinishwa wa zaka, Bwana alisema, “Bwana asema hivi, wakati sasa umefika, ambao itatolewa na baraza, linaloundwa la Urais wa Kwanza wa Kanisa langu, na askofu na baraza lake, na baraza langu kuu; na kwa sauti yangu mwenyewe kwao, asema Bwana” (M&M 120:1). “Askofu na baraza lake” na “baraza kuu langu” ilivyorejelewa katika huu ufunuo inajulikana siku hizi kama Uaskofu Simamizi na Jamii ya Mitume Kumi Wawili, mtawalia. Hizi hazina takatifu hutumika katika ukuaji wa haraka wa kanisa kiroho kubariki watu na familia kwa kujenga na kugharamia mahekalu na nyumba za ibada, kugharamia kazi ya umisionari, kutafsiri na kuchapisha maandiko, kuendeleza utafiti wa historia ya familia, kufadhili shule na elimu ya dini, na kutimiza madhumuni mengine mengi ya Kanisa kama inavyoelekezwa na watumishi wa Bwana wateule.
Mimi hushangazwa na uwazi na ufupi wa maneno ya hizi funuo mbili katika kulinganishwa na utaratibu wa mwongozo na usimamizi wa kifedha unaotumiwa katika taasisi nyingi sana na serikali kote ulimwenguni. Je! Inawezekaje shughuli za shirika kubwa hivi kama Kanisa la Yesu Kristo la urejesho linaweza kuendeshwa kote ulimwenguni likitumia maelekezo mafupi kama hayo? Kwangu mimi jibu ni wazi kabisa: hii ni kazi ya Bwana, Yeye anaweza kufanya kazi Yake mwenyewe (ona 2 Nefi 27:20), na Mwokozi huvuvia na kuelekeza watumishi Wake wanapotumia maelekezo Yake na kufanya katika kazi Yake.
Katika huo mkutano wa kwanza wa baraza nilipendezwa na urahisi wa kanuni ambayo iliongoza majadiliano na uamuzi wetu. Katika usimamizi wa kifedha wa Kanisa, kanuni mbili na thabiti za msingi hutimizwa. Kwanza, Kanisa hutumia kulingana na uwezo wake na huwa halitumii zaidi ya vile linavyopokea. Pili, sehemu ya mapato ya mwaka huwekwa kando kama akiba ya dharura na mahitaji yasiyotarajiwa. Kwa miongo, Kanisa limefunza washiriki wake kanuni ya kuweka kando chakula cha ziada, fueli, na pesa za kushughulikia dharura zinazoweza kutokea. Kanisa kama taasisi kwa urahisi hufuata kanuni hizo hizo ambazo washiriki hufunzwa kila mara.
Mkutano ulipoendelea, nilijipata nikitamani kwamba washiriki wote wa Kanisa wangeweza kuona urahisi, uwazi, utaratibu, hisani, na uwezo wa njia ya Bwana (ona M&M 104:16) kwa kuendesha shughuli za Kanisa Lake. Mimi sasa nishashiriki katika Baraza la Matumizi ya Zaka kwa miaka mingi. Shukrani na staha yangu kwa mpangilio wa Bwana imeongezeka kila mwaka, na mafunzo niliyojifunza yamepata hata kuwa ya kina zaidi.
Moyo wangu unajawa na upendo na kuvutiwa na washiriki waaminifu na watiifu wa Kanisa hili kutoka kila taifa, ukoo, ndimi, na watu. Ninaposafiri duniani, nimejifunza kuhusu matumaini na ndoto zenu, mazingira yenu tofauti ya kuishi na hali na kujizatiti kwenu. Nimehudhuria mikutano ya Kanisa pamoja nanyi na kutembelea baadhi ya nyumba zenu. Imani yenu huimarisha imani yangu. Uchaji wako hunifanya mimi kuwa mchaji zaidi. Na wema wenu na utiifu wenu wa hiari kwa sheria ya zaka huniongoza kuwa mtu bora, mume, na kiongozi wa Kanisa. Mimi huwakumbuka na kuwafikiria ninyi kila mara ninaposhiriki katika Baraza la Matumizi ya Zaka. Asanteni kwa wema na uaminifu wenu mnapoyashika maagano yenu.
Viongozi wa Kanisa la Bwana la Urejesho wanahisi jukumu kubwa la kutunza ifaavyo matoleo wakfu ya washiriki wa Kanisa. Tunajua vyema asili takatifu ya kimchango cha mjane.
“Naye [Yesu] akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi.
“Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa.
“Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina;
“ Maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia” (Marko 12:41–44).
Najua mwenyewe binafsi kwamba Baraza la Matumizi ya Zaka liko makini katika kutunza kimchango cha mjane. Natoa shukurani kwa Rais Thomas S.Monson na washauri wake kwa uongozi bora katika kutekeleza wakala huu mtakatifu. Na mimi ninakiri sauti (ona M&M 120:1) na mkono wa Bwana anaowahimili watumishi Wake katika kutimiza wajibu wa kumwakilisha Yeye.
Mwaliko na Ushuhuda
Ulipaji kwa uaminifu wa zaka ni zaidi ya wajibu kabisa; ni hatua muhimu katika mfanyiko wa kutakaswa kibnafsi. Kwa wale wenu ambao mnalipa zaka yenu, nawapa hongera.
Kwa wale wenu ambao kwa sasa hamtii sheria ya zaka, nawaalika ninyi mfikirie njia zenu na mtubu. Mimi nashuhudia kwamba utiifu wenu wa hii sheria ya Bwana, madirisha ya mbinguni yatafunguliwa kwenu. Tafadhali usihairishe siku yako ya toba.
Mimi nashuhudia baraka za kiroho na kimwili huja katika maisha yetu tunapoishi sheria ya zaka. Natoa ushahidi kwamba baraka kama hizo mara nyingi ni muhimu lakini zisizotambulika virahisi. Mimi pia natangaza kwamba urahisi wa njia ya Bwana ambao ni wazi kabisa katika shughuli za Kanisa Lake hupatiana mpangilio ambao unaweza kutuongoza sisi kama watu binafsi na kama familia. Naomba kila mmoja wetu aweze kujifunza na kufaidi kutokana na haya masomo muhimu, ni katika jina la takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.