2010–2019
Funguo ya Ulinzi wa Kiroho
Oktoba 2013


14:35

Ufunguo wa Ulinzi wa Kiroho

Amani inaweza kutua katika moyo wa kila mmoja ambaye anageukia maandiko na kufungua ahadi za ulindi na ukombozi.

Kipindi kifupi kilichopita, niliwaunganisha wanandoa vijana kwenye hekalu. Wanandoa hawa walijiweka wasafi kuifikia siku ya ajabu wakati mwana na binti waliziacha nyumba za ujana wao na kuwa mume na mke. Katika kipindi hiki kitakatifu, walikuwa halisi na wasafi. Hapo baadaye, wataanza kuwa na watoto wao wenyewe, katika mpango wa makubaliano uliowekwa na Baba yetu wa mbinguni. Furaha yao, na furaha ya vizazi vijavyo, itategemea vile viwango vilivyowekwa na Mwokozi na kuelezewa katika maandiko Yake.

Wazazi leo wanastaajabu kama kuna sehemu salama ya kuwalea watoto wao. Kuna sehemu salama. Ni katika nyumba zetu ambazo injili inafundishwa. Tunazingatia familia kwenye Kanisa, na tunawashauri wazazi popote pale kuwalea watoto wao katika haki.

Mtume Paulo alitoa unabii na kuonya kwamba “siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.

“Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,

“Wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,

“Wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;

“Wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.”1

Paulo pia alitoa unabii, “lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.”2

Mistari hii inatoa onyo, ikionyesha ni mipango gani ya kuepuka. Lazima daima tuwe macho na wenye bidii. Tunaweza kurejelea kila unabii na kuuwekea alama karibu yake kuonyesha kwamba upo na ni tahadhari katika ulimwengu wa leo:

Nyakati za Hatari sasa. Tunaishi katika nyakati za hatari sana.

Wenye tamaa, wenye kujisifu, wenye kiburi—wote wapo na wapo miongoni mwetu.

Wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao —wote hawa wameelezewa vyema.

Wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, na mengine mengi---yote yanaweza kuwekewa alama kama ushahidi kwamba wapo miongoni mwetu.

Moroni pia aliongea kuhusu uovu wa siku zetu pale alipotuonya:

“Wakati mtakapoona vitu hivi vikija miongoni mwenu … kwamba mtaamka kwa ufahamu wa hali yenu ya kutisha. …

Kwa hivyo, mimi, Moroni, nimeamriwa kuandika vitu hivi ili uovu ungeondolewa mbali, na ili wakati ungekuja ambapo Shetani hawezi kuwa na uwezo kwa mioyo ya watoto wa watu, lakini kwamba wangeshawishiwa kutenda mema siku zote, kwamba wangekuja kwenye chemichemi ya ukweli wote na kuokolewa. ”3

Maelezo ambayo Paulo na Moroni waliutoa kuhusu siku hizi ni sahihi sana kwamba hayawezi kupuuzwa. Kwa walio wengi inaweza kuwa usumbufu, na hata kukatisha tamaa. Hata hivyo, ninapofikiria kuhusu siku za usoni, ninazidiwa na matumaini chanya.

Katika ufunuo wa Paulo, kama ziada ya orodha ya changamoto na shida, yeye pia anatueleza kile tunachoweza kufanya ili kujikinga wenyewe.

“Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao;

“Na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.”4

Maandiko yanafunguo za ulinzi wa kiroho. Yanachukua mafundisho na sheria na ibada ambazo zinaweza kumleta kila mtoto wa Mungu kwenye ushuhuda wa Yesu kristo kama Mwokozi na Mkombozi wao.

Pamoja na miaka mingi ya maandalizi, pamekuwepo na juhudi kubwa za kuchapisha maandiko katika kila lugha yakiwa na tanbihi na marejeo tambuko. Tunataka yapatikane kwa wale wote wanaotaka kujifunza. Yanatufundisha wapi pa kwenda na nini cha kufanya. Yanatoa tumaini na maarifa.

Miaka kadhaa iliyopita, Mzee S. Dilworth Young wa Wale Sabini alinifundisha somo juu ya kusoma maandiko. Kigingi kilikuwa kinasumbuliwa na mvutano na shida miongoni mwa washiriki, na ushauri ilibidi utolewe.

Nikamwuliza Rais Young, “Ninapaswa kusema nini.”

Kwa urahisi alijibu, “Waambie wasome maandiko.”

Nikauliza, “Maandiko gani?”

Alisema, “Hakika haijalishi. Waambie wafungue Kitabu cha Mormoni, kwa mfano, na kuanza kusoma. Mara moja hali ya amani na maongozi itakuja, na suluhisho litakuja lenyewe.”

Fanya kusoma maadiko kuwa sehemu ya maisha yako, na baraka zitafuata. Katika maandiko kuna sauti ya kuonya, lakini pia kuna lishe kubwa sana.

Kama lugha ya maandiko kwanza inaonekana geni kwako, endelea kusoma. Punde utakuja kugundua uzuri na nguvu zinapotatikana kwenye hizo kurasa.

Paulo alisema, “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki.”5

Unaweza kujaribu ahadi hii wewe mwenyewe.

Tunaishi katika nyakati za hatari; hata hivyo, tunaweza kutafuta tumaini na amani kwa ajili yetu na familia zetu. Wale waishio kwa huzuni, bila tumaini la uwezekano wa kuokolewa kwa watoto toka kwa ulimwengu uliowachukua, naomba msikate tamaa. “Usiogope, amini tu.”6 Wema una nguvu zaidi kuliko uovu.

Watoto waliofundishwa kuyaelewa maandiko mapema katika maisha wanayopaswa kutembelea na watapendelea kubaki kwenye njia hiyo. Wale waliopotoka watakuwa na uwezo wa kurudi na, kwa msaada, wanaweza kuipata njia yao ya kurudi.

Wana wa Mosia, walipigana dhidi ya Kanisa kwa muda lakini baadaye walitubu na wakapitia mageuzi makubwa. Katika Alma tunasoma, “Hawa wana wa Mosia walikuwa … wameongezwa nguvu kwa ufahamu wa ukweli; kwani walikuwa watu ambao wana ufahamu mwema na walikuwa wameyapekua maandiko kwa bidii, ili wajue neno la Mungu.”7

Rais Joseph {nb F. Smith alikuwa na miaka mitano wakati baba yake, Hyrum, alipouawa kwenye gereza la Carthage. Baadaye, Joseph alivuka nyika akiwa na mama yake mjane.

Akiwa na miaka 15, aliitwa kutumikia misheni huko Hawaii. Alijiona kama amepotea na mpweke na akasema: “Nilikuwa kama nimeonewa. … Nilijiona kama mnyonge katika hali yangu ya ufukara, mkosefu wa akili na maarifa, kijana mdogo, ambaye ni vigumu hata kujaribu kumtazama [mtu yeyote] usoni.”

Akiwa anatafakari matatizo yake usiku mmoja, kijana Joseph aliota alikuwa safarini, akisafiri kwa kasi kadiri awezavyo. Alikuwa amebeba kifurushi kidogo. Mwishowe, akawasili kwenye nyumba kubwa nzuri ambapo ndiyo ilikuwa mwisho wa safari yake. Alipokaribia, aliona bango lililosomeka, “Kuoga.” Haraka akaingia na kuoga. Akafungua kifurushi na kukuta nguo safi nyeupe. Nguo nyeupe alisema, “sijawahi kuziona kwa muda mrefu.” Akazivaa na kwenda kasi kwenye mlango wa jumba.

“Nikabisha hodi,” alisema, “na mlango ukafunguliwa, na mtu aliyesimama pale alikuwa ni Nabii Joseph Smith. Aliniangalia kidogo kwa kunikaripia, na maneno ya kwanza aliyosema: ‘Joseph, umechelewa.’ Hata hivyo nikawa na ujasiri na kusema:

“Ndiyo, lakini mimi ni msafi----mimi ni msafi! ’”8

Na hivyo itakuwa kwa kila mmoja wetu.

Kama umeingia kwenye njia ya imani na utumishi wa Kanisani, endelea hivyo na utii maagano. Endelea mbele hadi muda ambao Baraka za Bwana zitakapokuja kwako na Roho Mtakatifu atafunuliwa kama nguvu ya msukumo katika maisha yako.

Kama upo kwenye njia isiyo sahihi ambayo nitofauti na iliyoandikwa kwenye maandiko, ngoja niwahakikishieni kuwa kuna njia ya kurudi.

Yesu Kristo alielezea njia nzuri ya sisi kutubu na kutafuta kuponywa katika maisha yetu. Tiba ya makosa yetu yaweza kupatikana kwa kuomba msamaha kupitia sala binafsi. Hata hivyo, kuna baadhi ya matatizo ya kiroho, hususani yale yahusuyo ukiukwaji wa maadili ya kimwili, ambayo kwa hakika yanahitaji msaada na tiba ya mtu mwenye ukuhani.

Miaka kadhaa iliyopita, msichana alikuja ofisini kwangu akiwa na baba yake mzee. Alimleta toka umbali wa maili mia na kadhaa ili kuja kutafuta dawa ya makosa yake. Akiwa kijana alifanya makosa makubwa sana, na uzeeni mwake kumbukumbu zikamrudia. Asingeweza kusahau hisia ya hatia. Hakuweza kwenda na kusahihisha makosa ya ujana wake yeye mwenyewe, lakini angeweza kuanza pale alipokuwa na, kwa usaidizi, kufuta makosa yaliyokuwa yakimzonga kwa miaka yote ile.

Nilikuwa na shukrani kwamba kwa kumfundisha kanuni toka kwenye Kitabu cha Mormoni ilikuwa kama vile mzigo mzito ulikuwa umetolewa toka mabegani mwake. Wakati yeye na binti wake walipokuwa wakisafiri maili nyingi kurudi, yule mzee alikuwa ameyaacha makosa yake ya kale.

Kama “utakuwa umeona ulikuwa na tatizo kubwa”9 na unatamani kurudi kwenye hali kamilifu, muone askofu wako. Yeye anafunguo na anaweza kukusaidia katika njia ya toba.

Toba ni ya mtu binafsi, na pia kusamehe. Bwana anahitaji mmoja tu kugeuka toka dhambini, na “[Yeye] atausamehe uovu wao, wala  …dhambi yao sitaikumbuka tena.”10

Wakati mchakato wa toba umemalizika, utakuja kujua maana ya ahadi za Isaya juu ya Urejesho: “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” 11

Kama ilivyo na chaki kuwa yaweza kufutwa toka ubaoni, kwa njia ya toba ya kweli madhara ya makosa yetu yanaweza kufutwa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo. Ahadi hiyo inatumika kwa kila jambo.

Injili inatufundisha kuwa na furaha, kuwa na imani ni bora kuliko kuwa na woga, kupata tumaini na kushinda tamaa, kuacha giza na kuukimbilia nuru ya injili ya milele.

Paulo na wengine walionya kuhusu majaribu wa nyakati zetu na siku zijazo. Lakini amani inaweza kuwa moyoni mwa kila mtu apendaye maandiko na kufungua ahadi ya ulinzi na ukombozi ambao unafundishwa. Tunawaalika wote kumgeukia Mwokozi Yesu Kristo, kwenye mafundisho Yake yapatikanayo kwenye Agano la Kale, Agano Jipya, Kitabu cha Mormoni, Mafundisho na Maagano na Lulu ya Thamani Kuu.

Ninatoa ushahidi wa kweli wa maandiko kama funguo ya ulinzi wa kiroho. Pia ninatoa ushahidi wa nguvu za uponyaji za Upatanisho wa Yesu Kristo, kwamba kwa kupitia yeye sote tunaweza kuokoka.12 Kanisa la Bwana limeanzishwa tena hapa duniani. Kwa ukweli wa injili ninatoa ushahidi. Kwa ajili yake mimi ni shahidi. Katika jina la Yesu Kristo, amina.