2010–2019
Kuweni Waongofu
Oktoba 2013


11:29

Kuweni Waongofu

Uongofu wa kweli hutokea unapoendelea kutenda juu ya mafundisho unayojua kuwa ni kweli na kuweka amri, siku baada ya siku, mwezi baada ya mwezi. 

Kina ndugu na dada, ni tukio la kunyenyekeza kiasi gani kusimama katika mimbari hii ambapo wengi wa mashujaa wa maisha yangu walisimama. Ningependa kushiriki nanyi baadhi ya hisia za moyo wangu na kuzielekeza hasa kwa vijana.

Mojawapo wa mashujaa wakuu kutoka kwa Agano la Kale alikuwa nabii shujaa Yoshua. Aliendeleza mwaliko huu kwa wana wa Israeli, ambao aliongoza: “Chagueni hivi leo mtakayemtumikia; … lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.”1 Tangazo la Yoshua linaonyesha uongofu wa kweli kwa injili. Kwa Yoshua na sisi sote, uongofu kwa kanuni za injili huja kwa kuishi kanuni za injili kwa uadilifu na kuwa wakweli kwa maagano yetu na Bwana.

Napenda kushiriki hadithi ya uongofu kutoka historia ya familia yangu kuhusu mwingine wa mashujaa wangu. Jina lake ni Agnes Hoggan, na yeye na mumewe walijiunga na Kanisa huko Scotland mwaka 1861. Wakipitia mateso makali katika nchi yao, walihamia Marekani na watoto wao. Miaka kadhaa baadaye, Agnes alikuwa mjane na watoto wanane wa kukimu na alifanya kazi kwa bidii ili kuweza kuwalisha na kuwavisha. Bintiye wa miaka 12, Isabelle, alikuwa na bahati ya kupata ajira kama mtumishi kwa familia tajiri isiyokuwa ya WSM.

Isabelle aliishi katika nyumba yao kubwa na kusaidia kuangalia watoto wao wadogo. Kwa ajili ya huduma yake, mshahara kidogo kila wiki ulilipwa mama yake. Kwa haraka alikubalika kama mwanafamilia na kuanza kufurahia mengi ya fursa hizo, kama vile masomo ya dansi, mavazi mazuri, na kuhudhuria maonyesho. Utaratibu huu uliendelea kwa miaka minne, hadi wakati familia ambayo Isabelle aliifanyia kazi ilipohamishiwa kwa jimbo lingine. Walikuwa wamempenda sana Isabelle kiasi kwamba walimwendea mama yake, Agnes, na kumwomba ruhusa ya kisheria kumwasili. Waliahidi watampa elimu nzuri, kuona kwamba ameolewa vizuri, na kumfanya mrithi wa mali yao na watoto wao wenyewe. Wangeweza pia kuendelea kumtolea Agnes malipo.

Huyu mjane aliyekuwa akiteseka na mama alikuwa na uamuzi mgumu wa kufanya, lakini yeye hakusita hata kwa muda. Sikiliza maneno ya mjukuu wake, yaliyondikwa miaka mingi baadaye: “Kama upendo wake haukumlazimisha kusema la, alikuwa hata na sababu bora---alitokea huko kote Scotland na alikuwa amepitia shida na majaribu kwa ajili ya Injili, na hakutarajia, kwa njia yoyote, kuwezesha mtoto wake kupoteza kile alichoweza kupata.”2 Familia tajiri ilitumia kila hoja iwezavyo, na Isabelle mwenyewe alilia na kusihi kuruhusiwa kurudi, lakini Agnes alisimama imara. Kama unavyoweza kufikiria, Isabelle mwenye miaka 16 alihisi ni kama maisha yake yameharibiwa.

Isabelle Hoggan ni bibi yangu mkubwa, na ninashukuru zaidi kwa ushuhuda na imani iliyoangaza kwa nuru kali katika moyo wa mama yake, ambao haukumruhusu kubadilisha ushirika wa binti yake katika Kanisa kwa ajili ya ahadi ya kidunia. Leo, mamia ya wale wa uzao wake ambao wanafurahia baraka za ushirika katika Kanisa ni wafadhiliwa wa imani ya kina wa Agnes na uongofu kwa injili.

Marafiki vijana, tunaishi katika nyakati za hatari, na maamuzi ambayo unatakiwa kufanya kila siku, au hata kila saa, yana athari ya milele. Maamuzi unayofanya katika maisha yako ya kila siku yataamua yale yatakayokutokea baadaye. Kama bado hauna ushuhuda thabiti na imani kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni ufalme wa Mungu duniani, sasa ndio wakati wa kufanya kifaacho ili kupata imani hiyo. Kuchelewa kuweka bidii inayohitajika ili kupata aina hiyo ya imani inaweza kuwa hatari kwa nafsi yako.

Uongofu wa kweli ni zaidi ya kuwa tu na maarifa ya kanuni za injili na ina maana hata zaidi kuliko tu kuwa na ushuhuda wa kanuni hizo. Inawezekana kuwa na ushuhuda wa injili bila kuiishi. Kuongoka kwa kweli kunamaanisha tunatumia kile tunaamini na kukiruhusu kuleta “mabadiliko makuu ndani yetu, au mioyoni yetu.”3 Katika kijitabu Kweli kwa Imani, tunajifunza kwamba “uongofu ni utaratibu, siyo tukio. Unakuwa mwongofu kama matokeo ya ... juhudi za haki za kumfuata Mwokozi.”4 Inagharimu muda, juhudi, na kazi. Bibi yangu mkubwa alikuwa na imani imara kwamba injili ilikuwa muhimu zaidi kwa ajili ya watoto wake kuliko yote ambayo dunia ingetoa katika kwa njia ya utajiri na faraja kwa sababu alijitolea, kuvumilia, na kuishi injili. Uongofu wake ulikuja kwa njia ya kuishi kanuni za injili na kujitolea kwa ajili yao.

Ni lazima tupitia mchakato huo kama tunataka kupata aina hiyo ya msimamo. Mwokozi alifundisha, “Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kama mimi nanena kwa nafsi yangu tu.”5 Wakati mwingine sisi hujaribu kufanya kinyume. Kwa mfano, tunaweza kuchukua njia hii: Nitafurahia kuishi amri ya zaka, lakini kwanza nahitaji kujua kwamba ni kweli. Labda hata tunaomba ili kupata ushuhuda wa amri ya zaka na kutumaini Bwana atatubariki na ushuhuda huo hata kabla ya kujaza risiti ya zaka. Haifanyi kazi kwa njia hiyo. Bwana anatutarajia kutumia imani. Ni lazima tulipe zaka kamili mfululizo ili kupata ushahidi wa zaka. Utaratibu huo huo unatumika kwa kanuni zote za injili iwe ni sheria ya usafi, kanuni ya maadili, Neno la Hekima, au sheria ya mfungo.

Napenda kushiriki mfano wa jinsi kuishi kanuni kunatusaidia kuwa waongofu kwa kanuni hiyo. Nilikuwa mwanamke kijana katika miaka ya 60 na msichana pekee wa WSM katika shule yangu ya upili. Ilikuwa nyakati ya mapinduzi iliokumbwa na upinzani wa maadili ya jadi, matumizi ya madawa, na mawazo ya “kufanya kitu chochote ukipendacho.” Wengi wa rika yangu walikuwa watu wazuri lakini waliipata kuwa rahisi kupatikana katika msisimko wa maadili haya mpya, ambayo kwa kweli yalikuwa tu uasherati wa zamani. Wazazi wangu na walimu walinisisitizia thamani ya kuchunga mwili wangu kwa heshima, kuweka nia ya wazi, na zaidi ya yote, kujifunza kuamini katika amri ya Bwana. Nilifanya uamuzi kuepuka hali ambapo nilijua pombe itapatikana na kukaa mbali na tumbaku na madawa ya kulevya. Hii mara nyingi ilimaanisha sikujumuishwa katika sherehe, na nilifanya miada mara chache. Matumizi ya madawa yaliendelea kuongezeka zaidi na zaidi miongoni mwa vijana, na hatari hazikujulikana vilivyo kama leo. Wengi wa rika yangu baadaye waliteseka uharibifu wa kudumu kutoka kwa madawa ya kubadili akili au kupatikana katika ulevi mkubwa. Nilishukuru kwa kufundishwa kuishi Neno la Hekima katika nyumba yangu, na nikapata ushuhuda wa kina wa kanuni hiyo ya injili nilipofanya imani na kuiishi. Hisia nzuri iliyonijia kwa kuishi kanuni ya kweli ya injili ilikuwa Roho wa Roho Mtakatifu ikithibitisha kwamba kanuni ilikuwa kweli. Hapo ndipo uongofu wa kweli unaanza kufanyika.

Nabii Moroni, katika Kitabu cha Mormoni, alifundisha, “Ninataka kuonyesha ulimwengu kwamba imani ni vitu ambavyo vinatumainiwa na havionekani; kwa hivyo, msishindane kwa sababu hamwoni, kwani hamtapata ushahidi wowote mpaka baada ya majaribu ya imani yenu.”6 Katika dunia yetu ambapo furaha ya papo hapo ndio matarajio, mara nyingi tunakuwa na hatia ya kutarajia malipo bila ya kuyafanyia kazi. Naamini Moroni anatuambia kwamba lazima tufanye kazi kwanza na kufanya imani kwa kuishi injili, ndipo tutakapopokea ushahidi kwamba ni kweli. Uongofu wa kweli hutokea unapoendelea kutenda juu ya mafundisho unayojua kuwa ni kweli na kuweka amri, siku baada ya siku, mwezi baada ya mwezi.

Huu ni wakati mtukufu wa kuwa kijana katika Kanisa. Wewe ni wa kwanza kushiriki katika mtaala wa vijana wa Come, Follow Me, ambao unayo kama mojawapo wa madhumuni yake makuu uongofu wako kwa injili ya Yesu Kristo. Ni vyema kukumbuka kwamba haijalishi jinsi wazazi wako na viongozi walivyo na ushawishi, “una wajibu wa msingi kwa ajili ya uongofu wako mwenyewe. Hakuna mtu anayeweza kuongoka kwa ajili yako, na hakuna mtu anayeweza kukulazimisha kuongoka.”7Uongofu hufanyika tunapotia bidii kuhusu kusema sala zetu, kusoma maandiko yetu, kuhudhuria kanisa, na kuwa wastahiki kushiriki katika maagizo ya hekalu. Uongofu huja tunapotenda juu ya kanuni ya haki tuyojifunza katika nyumba zetu na katika darasa. Uongofu huja tunapoishi maisha safi na wema na kufurahia uenzi wa Roho Mtakatifu, Uongofu huja tunapoelewa Upatanisho wa Yesu Kristo, kumkiri Yeye kama Mwokozi na Mkombozi wetu, na kuruhusu Upatanisho kufanyika katika maisha yetu.

Uongofu wako binafsi utakusaidia unapojiandaa kufanya maagano hekaluni, kutumikia misheni, na kuanzisha nyumba yako mwenyewe ya baadaye. Unapoongoka, utakuwa na hamu ya kushiriki na wengine ulichojifunza, na tumaini lako na uwezo wa kushuhudia kwa wengine kwa imani na nguvu utaongezeka. Hamu hii ya kushiriki injili na wengine na tumaini la kushuhudia ni matokeo ya asili ya uongofu wa kweli. Mwokozi alifundisha Petro, “Nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.”8

Kumbuka Yoshua, nabii-shujaa? Hakuwa ​​tu mwongofu mwenyewe, lakini alifanya kazi bila kuchoka hadi mwisho wa maisha yake ili kuleta watoto wa Israeli kwa Mungu. Tunasoma katika Agano la Kale: “Nao Israeli wakamtumikia Bwana siku zote za Yoshua.”9 Mtu aliyeona uongofu wa kweli hutumia nguvu ya Upatanisho na hupokea wokovu kwa nafsi yake mwenyewe, kisha hufikia kutoa ushawishi wa nguvu juu ya wale wote wanaomjua.

Kuishi injili na kusimama katika maeneo matakatifu daima haipendezi wala si rahisi, lakini nashuhudia kwamba inastahili! Bwana alimshauri Emma Smith “kuyaweka kando mambo ya ulimwengu huu, na kuyatafuta mambo ya ulimwengu ulio bora.”10 Nashuku hatuwezi kuanza kufikiria jinsi “mambo hayo dunia yalivyo bora”!

Nashuhudia kwamba tuna Baba wa Mbinguni mwenye upendo ambaye hamu Yake kuu ni kusaidia na kutubariki katika juhudi zetu za kuishi Injili na kuwa waongofu. Alisema wazi kwamba lengo Lake kuu na kazi ni “kutokufa kwetu na uzima wa milele.”11 Anataka kutuleta nyumbani kwa uwepo Wake. Nashuhudia kwamba tunapotenda juu ya mafundisho ya injili na kuyaweka katika mazoezi ya kila siku, tutakuwa waongofu na tutakuwa njia ya kufanikisha mema mengi katika familia zetu na katika ulimwengu. Tuweze sote kubarikiwa katika jitihada zetu za kila siku ili kufikia lengo hilo ndilo ombi langu katika jina la Yesu Kristo, amina.